Kizazi kipya na wasomi wapya

Ndugu Mhariri,

ELIMU ni nyenzo muhimu katika kumkomboa mwanadamu katika nyanja zote za kimaisha. Elimu si tu kuingia darasani na kusoma vitabu bali ni kuwa na upeo mpana wa kuchanganua mambo yanayotokea katika jamii. Elimu makini na sahihi ni lazima imfanye mhitimu kuenzi tamaduni nzuri zilizopo katika jamii inayomzunguka. Msomi ni mtu anayepaswa kuigwa kwa matendo yake yenye hekima katika jamii.

Katika nchi yetu wasomi wengi “hawajisomi” na baadhi yao wamekuwa wakiishi mithili ya wanyama kwa kutotumia elimu yao katika kudadisi mambo. Ni watu wasiofuata na kuheshimu utamaduni wa kitanzania badala yake, wanasujudia utamaduni wa kigeni usiokuwa na manufaa kwa wanajamii. Mimi niko chuo kikuu nina ushahidi na haya ninayoeleza.

Kitambo nilifikiri kwamba elimu ingekuwa silaha nzuri sana kwa Mtanzania kujikomboa kifikra za kiutamaduni, lakini wapi. Elimu ndio imekuwa chombo cha kumfanya msomi kutojitambua kabisa. Leo hii wasomi wengi hasa wa vyuo vikuu baada ya kupata elimu, sasa wamepata nafasi ya kutembea nusu uchi kwa madaha.

Wamepata nafasi ya kuchubua ngozi kwa mikorogo mikali ili kufanana na mzungu, wamepata nafasi ya kuzungumza kwa kubana sauti kama manawali wa Ubelgiji na kuishi kwa utamaduni wa nchi za magharibi. Huyu ndiye msomi wetu wa leo hajitambui, hajithamini na wala hajielewi. Si wote wako hivyo la hasha! Wapo wengine wanaotambua umuhimu wao katika jamii na kujiheshimu kama wasomi.

Niliwahi kuandika makala mbili katika moja ya magazeti nchini Desemba, mwaka 2010, chini ya kichwa cha habari “hawa ndio wasomi wetu wa leo” na “kama huu ni uongo ukweli ni upi” nikijaribu kueleza hisia zangu juu ya mmomonyoko mkubwa wa maadili miongoni mwa wanazuoni wetu, baada ya kupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu.

Katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya wanachuo waliopata kusoma makala zile walinishambulia kwa matusi na kunikejeli kwa madai ya kupotosha umma na kujenga mitazamo hasi dhidi ya wasomi wetu. Nilifikiri kuwa nimekosea lakini leo hii nimejiridhisha kwa uchunguzi niliofanya na kukiri kuwa wengi wa wasomi wetu ni chachu ya mmomonyoko wa maadili  katika jamii zetu.

Mbali na hapo wengi wao ni wavivu wa kufikiri. Ni wasomi ambao wanapenda kusoma habari nyepesi katika magazeti ya udaku badala ya kutafuta habari muhimu ambazo ni za uhakika. Ni wavivu wa kusoma majarida na vitabu lakini badala yake wamewekeza bidii katika kusikiliza muziki hata kama hakuna ujumbe wa msingi kwao.

Sikatazi kusikiliza muziki bali tujitahidi kupembua na kudadisi mambo ya msingi. Hata mimi napenda kusikiliza muziki pale ninapochoka lakini wengi hatuko hivyo.  Waangalie vijana wanaosoma katika taasisi mbalimbali za elimu wengi wao wanawaza kujilimbikizia mali pindi wanapopata nafasi nyeti za kazi au utawala waanze kula mpaka waote vitambi.

Wanawaza kuwa wezi wa mali ya umma na kuwa mafisadi hata kabla hawajapata fursa hizo maridhawa. Sasa wakipata itakuwaje? Kwa nchi kama hii yenye wananchi masikini, kama kila msomi atawaza kujilimbikizia mali kamwe hatutafikia maendeleo. Uzalendo kwa baadhi ya wanazuoni umetoweka kabisa. Maendeleo dhaifu katika nchi yetu ni matokeo ya Watanzania hasa wasomi kutanguliza maslahi yao binafsi kuliko ya jamii kwa ujumla.

Wasomi wengi wamekuwa bingwa wa kushabikia starehe hasa wale wa vyuo vikuu. Ukiyaeleza haya utaonekana adui wa umma. Lakini wale wenye utashi na walio makini watakubali ukweli huu usiopingika. Ndugu mhariri,naomba ieleweke kuwa barua hii haijumlishi wanazuoni wote bali ni wale wenye tabia niliyotaja hapo juu.

Kwa kuhitimisha, nafikiri kuna umuhimu wa kutilia mkazo suala la utamaduni na maadili bora katika ngazi zote za elimu ili kujenga jamii bora yenye maadili na inayowajibika. Hii ni pamoja na kuanzisha somo la maadili ya jamii katika mitaala yetu ya elimu.

13 thoughts on “Kizazi kipya na wasomi wapya”

 1. JOHN MOSHI says:

  Ni kweli wengi wa wanavyuo wana tabia za ajabu sana mi ndio nipo mwaka wa kwanza yaani, kitabia vyuoni hapafai kabisa bora na kule A-level nilipo toka. Kwa hali hii wanaotusomesha wategemee kutuzika mara tu baada ya kumaliza shahada!

 2. Baraka Haule says:

  ni kweli kabisa,wengi wanafunzi wengi wakishafika vyuoni hujisahau kwamba wao ni kioo cha jamii badala yake matendo yao huwa ni mabovu kuliko  kuliko wale ambao hawajaenda shule,na hasa tabia za wasichana huwa ndio mbovu kupitiliza.

  Utakuta hata kama alikuwa anamchumba basi mchumba huyo atapata tabu na mwisho hufarakana. Masumivu huwa ni mengi sana kwa baadhi yao baada ya kutambua kwamba yale yalikuwa ni maisha ya mpito tu na siku moja itampasa arudi mtaani na kuchanganyika na wale aliowaacha huko.

 3. peter marwa says:

  Ni ukweli mtupu.Ni binadamu wachache wenye hulka ya kuukubali ukweli japo unauma. Wasomi Mkumbukeni Mungu.

 4. kijoji s.r says:

  kweli kaka wanavyuo wengi hawajitambui.            

 5. geofrey brighton says:

  Nampongeza huyo kijana msomi kwa kusema ukweli wa mambo ulivyo.Vijana wengi wamekuwa malimbukeni ndiyo maana hata wanapomaliza vyuo vikuu wanakosa namna ya kuanzisha chochote kulingana na taaluma zao.

 6. MLALA HUI says:

  WASOMI WANCHI YETU WAMEFELI KUPELEKA NCHI YETU MBELE WENGI WAO WAMEUNGANA NA WANASIASA KUANGAMIZA NCHI

 7. George Jared says:

  Ndugu Mhariri!

  Nchi hii kesi zipo nyingi zingine ufuatiliwa kwa karibu mfano. Serikali na madaktari,walimu  hutatuliwa mapema. Je ya wachimba madini wa waliokuwa Barrick Bulyanhulu mbona amtuabarishi kesi yamwaka  2007

  Hivi ni kwanini kesi zinazousu kazi zinachukua muda mrefu kutolewa hukumu wakati hayaitaji uchunguzi sana wa kipolisi yaani maswala ya kazi uwa wazi kabisa.

  Mfano. Ni kesi ya wafanyakazi wa mgodi wa Barrick Bulyanhulu wapatao 1350 ya waka 2007 mpaka hii leo hukumu haijatolewa na inasemekana watu wananeemeka na kesi hiyo kwa kufanya ichelewe.

  Naomba mwanahabari wa uchunguzi wa gazeti lako afatilie habari ya kesi hii kwa uongozi wa chama cha wafanyakazi wa migodi TAMICO na kuhudhuria kesi. Haiwezekani Barrick wachukue dhahabu na kuwanyanyasa wafanyakazi ili waogope kudai haki zao, kwa mtindo wa kuchelewesha kesi makusudi ili wengine waogpoe kudai haki.

  Mimi ni mmoja wa waathirika tangu mwaka 2007 mpaka leo naishi maisha ya shida sana.

  George Jared

  BUNDA

 8. ISSAYA GIDEON says:

  KEEP IT UP,ME NAKUKUBALI,ME SHUHUDA MWENZIO HAPO CHUONI.

 9. MAKURU says:

  NI KWELI KABISA BAADHI YA WASOMI WETU SUALA LA MAADILI HAWANA UNAWEZA WEZA KUKUTANA NA MTU UKAAMBIWA NI MWANACHUO UKASHANGAA KWA JINSI ALIVYOVAA, KIUKWELI LAZIMA WAJITAMBUE KUWA WAO NI MFANO KATIKA JAMII YETU.

   

   

 10. Simon Kishiwa says:

  Ni ukweli mtupu,sema bila kuchoka hata kama watachukia

 11. zakaria ramadhani mussa says:

  Nikweli kabisa tena bila kificho na atakaye kuchukia bac huyo nae nimmojawapo wa wavunjaji maadili ya Mtanzania thabiti,saizi kaka ktk vyuo wanafunzi wasiojitambua niwengi sana,Hujakosea kaka endelea kuturekebisha kwa nguvu zote,na Mungu atakusaidia.

 12. Msomaji wetu says:

  hapo hakuna ubishi baadhi ya wasomi wanashindwa kuonesha mabadiliko tuliyo yatarajia katika jamii

 13. misael kikoti says:

  ni kweli wasomi wengi wameshindwa kuonesha mfano stahili katika jamii kutokana na kuandaliwa kw maslai binafsi na si yo ya tanzania nzima

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *