Lukuvi tatua kero hizi za Mpigachapa Mkuu

NDUGU Mhariri, sisi ni watumishi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Mpigachapa Mkuu wa  Serikali. Kwa muda mrefu sasa, tumekuwa tukifanya kazi hadi muda wa ziada (overtime) lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, malipo yetu ya overtime ni chini ya kiwango kinachostahili.

Kiwango tunacholipwa ni kidogo kwa mujibu wa waraka wa posho za saa ya ziada za kazi na kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano kazini ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake.

Tumekwishafikisha malalamiko haya kwa wahusika ofisini lakini tumekuwa tukijibiwa eti hatustahili  kulipwa overtime kwa viwango husika kwa sababu hatuna elimu ya kutosha kulipwa posho kubwa.

Ndugu mhariri, kuhusu elimu miongoni mwetu ni kweli hapa kiwandani kwa Mpigachapa mkuu, elimu yetu ni darasa la saba. Lakini hata hivyo, hatuamini kwamba kwa kiwango chetu hicho cha elimu hatupaswi kulipa kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa kisheria.

Kama haya hayatoshi, tunalazimishwa kuja kazini siku za mwisho wa wiki na siku za sikukuu na kwa wanaoshindwa kufika kazini kwa siku hizo hupewa barua ili kujieleza kwa nini hawakufika kazini.

Hivyo basi, kutokana na kero hizi na nyingine ambazo si rahisi kuzieleza zote hapa, kupitia gazeti hili makini la Raia Mwema, tunamwomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Bunge na Uratibu, William Lukuvi, afanye ziara kiwandani na kuyapatia ufumbuzi matatizo haya.

Kero hapa kiwandani ni nyingi, kwa mfano, baadhi ya wafanyakazi wenzetu hasa wasichana wamekuwa wakilalamika na kudai kusumbuliwa ili hatimaye wajihusishe kimapenzi na mmoja wa watumishi waandamizi. Tunashauri madai haya kama yalivyo mengine, yafanyiwe kazi kwa kuchunguzwa ili ukweli ubainike.

Pia kuna madai kwamba usimamizi wa maduka ya vitabu vya serikali katika baadhi ya mikoa si wa kuridhisha na kasoro hii inadaiwa kutokana na utendaji mbovu wa bosi wetu.

Tunaelekea kuamini kwamba Katibu Mkuu wa wizara anapotoshwa na bosi wetu kwa sababu malalamiko mengi yamemfikia na hakuna hatua za kinidhamu wanazochukuliwa dhidi ya wahusika.

Tunawasilisha malalamiko yetu haya ili viongozi ngazi ya wizara wachukue hatua kwa sababu tunaamini, ofisi ya Mpigachapa mkuu wa Serikali, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni ofisi nyeti nchini, haipaswi kuhusishwa na tuhuma za namna hii.

Ni sisi wafanyakazi,
Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *