Mkuu wa Chuo DMI achunguzwe

SISI walimu na wafanyakazi wa Dar es Salaam Maritime Institute (DMI), tunashukuru na kuipongeza Serikali yetu inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kusikia kilio chetu na hatimaye kumng’oa madarakani aliyekuwa Mkuu wa Chuo, Shukuru Mkali.

Tukiwa kama Watanzania tumerudisha imani kwa Serikali yetu kwani imedhihirisha kuwa, Serikali ni sikivu na iko macho kulinda na kutetea maslahi ya taifa dhidi ya viongozi wabadhirifu na wasiokuwa waadilifu.

Pamoja na kuishukuru na kuipongeza Serikali yetu, tunashauri kwamba, kumuhamishia wizarani Shukuru Mkali haitoshi na badala yake, anapaswa kuwajibishwa zaidi kwa kukosa uadilifu na kwa matumizi mabaya ya madaraka yake.

Tunashauri Serikali iunde timu ya kumchunguza zaidi Mkali hasa mwenendo wake kiutendaji alipokuwa mkuu wa chuo na hasa tuhuma za ubadhirifu zinazomuandama hapa ofisini na kutokana na uchunguzi huo, achukuliwe hatua zaidi za kisheria.

Tunashauri hatua hiyo ya uchunguzi na hatua nyingine za kisheria dhidi yake ili iwe fundisho kwa watendaji wengine wenye mwenendo usioridhisha kimaadili katika kutimiza majukumu yao kwa niaba ya umma.

Uchunguzi huo ni vema ukaanza kwake tangu alipoingia madarakani Januari mosi, mwaka 2010 hadi siku alipong’olewa. Tunaishauri Serikali kuchunguza yafuatayo; mosi, uhalali wa malipo ya mishahara Sh. 900,000 isiyokatwa kodi wala makato ya michango ya NSSF, ambayo mkuu huyu wa chuo alikuwa akidaiwa kumpa Mwenyekiti wa Bodi, Meja Jenerali General Ligate Sande kila mwezi.

Madai ambayo Serikali hapa tunashauri ichunguwe ni kwamba, mwenyekiti huyo wa bodi amekuwa akilipwa fedha ili kumfumba macho na mdomo yeye na bodi yake wasiweze kuona au hata kukemea udhaifu wa kiuongozi na ubadhirifu wa fedha za umma uliokuwa ukifanywa na mkuu huyu wa Chuo.

Pili, ni kuchunguza uhalali wa malipo na matumizi ya teksi yaliyokuwa yakifanywa na mkuu huyu wa chuo wakati Serikali ilimpa gari aina ya Landcruiser Vx, pamoja na dereva.

Tatu, ukiukwaji wa sheria za manunuzi ikidaiwa kuwa mkuu huyu wa chuo alikuwa na Airline Agent wake maalumu aliyekuwa akikiuzia chuo tiketi za ndege kwa gharama kubwa mara mbili hadi tatu zaidi ya gharama za kawaida na kwamba, wakala huyo alipatikana bila kushindanishwa na mawakala wengine.

Jambo baya zaidi ni kwamba hata ofisa manunuzi wa chuo hakuwa amehusishwa katika mchakato mzima wa upatikanaji na ununuzi wa tiketi hizo za ndege. Katika hili mkuu huyu wa chuo ndiye anayetuhumiwa kuwa ofisa manunuzi.

Nne, uhalali wa matumizi ya fedha za umma uliokuwa ukifanywa na mkuu huyu wa chuo yeye binafsi katika kugharamia vifaa vya matumizi ya ofisi (stationeries ) uchunguzwe.

Tano, uhalali wa matumizi ya mamilioni ya fedha za umma zilizokuwa zikigharamia safari zake nje ya nchi na tija iliyotokana na safari hizo na hasa safari yake ya mwisho huko China iliyogharimu chuo zaidi ya milioni 100 kwake na msafara wake huku safari hiyo ikiwa ni feki na hivyo kuishia kufanya shopping huko China, nayo ichunguzwe.

Sita, ni kuchunguza uhalali wa matumizi ya fedha za hundi ya fungu maalumu la matumizi (OC) katika kuwalipa watumishi mishahara. Akaunti ya chuo ya fedha za kigeni (US Dollars and Euros) hasa kwa mradi wa Liferafts ambao hesabu ya mapato yake hakuna anayejua isipokuwa yeye mwenyewe, pia uchunguzi ufanyika.

Saba, ni kuchunguza halali wa mkuu huyu wa chuo kujilipa malipo ya ziada kila mwezi eti kama mhudumu (attendant) wa liferafts station ya chuo huku akijua ukweli kuwa yeye si mhudumu wa liferafts station ya chuo na wala hafanyi kazi hizo za ziada.

Mbaya zaidi alikuwa akidaiwa kutopitisha malipo yoyote kwa wahudumu wa liferafts station kama watakuwa hawajaweka jina lake kwa ajili ya malipo. Huu ni wizi mtupu kwa Serikali yetu.

Nane ni kuchunguza uhalali wa matumizi ya fedha za umma (za chuo) katika kulipa gharama za matengenezo ya viyoyozi nyumbani kwake. Tisa, kuchunguza uhalali wa matumizi ya fedha za umma uliokuwa ukifanywa kwake binafsi katika kununua vinywaji na vyakula kwa matumizi ya ofisini kwake na kwa wageni wake.

Tunaiomba Serikali ichunguze ushiriki wa wafanyakazi wenzetu hapa chuoni katika kufanikisha ubadhirifu wa fedha za umma uliokuwa ukifanywa na mkuu huyu wa chuo. Katika hili tunaiomba Serikali ichunguze ushiriki wa Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor) kwani haya yote yalifanyika akiwapo ofisini.

Pia tunaiomba Serikali ichunguze ushiriki wa ofisa manunuzi na ugavi wa chuo, Aretha Msungu kwani mkuu huyu wa chuo alikuwa akikiuka sheria za manunuzi huku yeye akiwepo na tulitegemea aisaidie Serikali katika hili lakini haikuwa hivyo.

Ni vema Serikali ichunguze namna walivyotumia nafasi zao kufanikisha uovu uliotokea dhidi ya mali za Serikali na wachukuliwe hatua za kisheria kama itabainika wamehusika kwa namna yoyote.

Mwisho tunaiomba Serikali ichunguze ushiriki ama ubia uliokuwapo kati ya mfanyakazi mwenzetu, Kauye Mageleja na mkuu huyu wa chuo hasa katika suala la uadilifu, ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi.

Mwenzetu huyu alikuwa ni kiungo muhimu katika kufanikisha ubadhirifu mkubwa uliofanywa na mkuu huyo wa chuo, ikiwamo madai ya unyanyasaji kwa wafanyakazi wenzake.

One thought on “Mkuu wa Chuo DMI achunguzwe”

  1. MUSA ABIL says:

    Ndugu mwandishi kilio changu ni kuondosha matatizo yanayo kabili chuo chetu cha DMI(DAR ES SALAAM MARITIME INSTITUTE),NDIO MAANA TUNAJITAHIDI KUTOA TAARIFA KWANI DUNIA YA LEO BILA ELIMU BORA KWA WANANCHI WAKO UJAFANYA KITU.TATIZO LA KWANZA NI MCHANGANYO WA MALIPO YA SCHOOL FEES AMBAZO LOAN BOARD WAMELIPA KWA WANAFUNZI WALIOANZA 2008/2009, NA KUMALIZA JANUARY 2012, LOAN BOARD ILITOA SHEET KWA KILA MWANAFUNZI PESA AMBAZO WAMEMLIPIA LAKINI KWA BAHATI MBAYA SANA DMI WENYEWE WANASEMA PESA WALIZOPATA NI KIASI KIDOGO AMBACHO AKITOSHELEZI KUTOKANA NA ASILIMIA YA MWANAFUNZI,PIA DMI WANASEMA WENYEWE HAWAWEZI KUTOA VYETI KWA MTU AMBAYE LOAN BOARD WAJAMMALIZIA SCHOOL FEES YAKE, SASA KWANZA MIMI SIAMINI KAMA LOAN BOARD WAJALETA HIZO PESA NA KWANINI WAJALETA DMI, HIVYO NDIO MAANA TUNAOMBA MSAADA WA TASISI YA KUZUIA RUSHWA KUTUSAIDIA HILI INAWEZEKANA HIZO PESA ZIMELIWA EITHER DMI OR LOAN BOARD KWANI KILA MWAKA BUNGE LINAPANGA BAJETI KWAAJILI YA MALIPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU, SASA TUNAOMBA IKULU ITUSAIDIE TUWEZE KUPATA VYETI VYETU ILI TUWEZE KUMUDU MAISHA MAPYA YA MITAANI  KWANI  UTUMISHI TAREHE 25 WAMETANGAZA KAZI LAKINI HAWATAKI HATA  KUTUMIA  TRANSCRIPT. SASA MIMI NAJIULIZA NITAWEZAJE KUMUDU MAISHA MAPYA ILI NIWEZE KUPATA KAZI AMBAYO NITATUMIA CHETI AMBACHO NIMEANGAIKIA MIAKA MITATU NANUSU,INAMAANISHA LOAN BOARD WASIPO LIPA HIZO PESA KATIKA SIKU ZINAZO KUJA HIVYO VYETI TUTAVISAHAU KWANI KILA MWANAFUNZI ANADAIWA SIO CHINI YA 800000 ZA LOAN BOARD, KWA MTU ALIYETOKA FAMILIA MASKINI NA PIA ANA KAZI HIZO PESA NI NYINGI SANA KWANI MAISHA YAMEPANDA SANA. MWISHO NAPENDA KUTOA ONGERA KWA WIZARA YA UCHUKUZI KUFANYA MABADILIKO YA UONGOZI PALE DMI ILA WAMESAHAU KUFANYA MABADILIKO MTU MMOJA TU CAPT. HATIBU KATANDULA, PALE SEHEMU YA KAZI ALIYOPO  CAPT KATANDULA AFAHI  KWANI  UDUMA YAKE KWA WATEJA WAKE NI MBOVU SANA,MCHANGANYIKO HUU WA PESA HIZI ZA MALIPO UMETOKANA NA UZEMBE NA UBABAISHAJI WAKE WA KAZI. TUNAOMBA MFANYE MABADILIKO SEHEMU HII PIA MFANYE UCHUNGUZI KWANI HATA NAFASI ZA KWENDA KUFANYA MAZOEZI YA MELI NCHI ZA NJE ANAFANYA KWA UTARATIBU USIOKUBALIKA NA SIO WAZI, NAWATAKIA KAZI NJEMA PIA TUNAWAAMINI SANA KWA KAZI ZENU NDIO MAANA TUNATOA TAARIFA KWA MANUFAHA YA NCHI YETU. T

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *