Nani akinusuru Chuo cha Ualimu Korogwe?

NDUGU Mhariri,

Sisi ni watumishi wazalendo katika Chuo cha Ualimu Korogwe, mkoani Tanga. Tunasikitishwa na uendeshaji mbovu wa chuo chetu.

Uongozi wa juu wa chuo umekuwa dhaifu katika kuchukua uamuzi wa kiutawala ili kulinda hadhi ya chuo hiki kitaifa na kimataifa. Tumejitahidi bila mafanikio kukabili uzembe wa kiuongozi chuoni hapa.

Juhudi zetu ni pamoja kuripoti katika mamkala husika, ikiwamo ngazi ya wizara. Tunaamini kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha za chuo, kuanzia fedha za michango, miradi ya chuo na hata zile zinazoletwa chuoni kutoka wizarani.

Wapo wenzetu waliodiriki kuhoji hadharani, kumuandikia nyaraka mbalimbali na hata kushauri uongozi wa juu wa chuo bila mafanikio. Maarifa
yote ya kiutaratibu na kikanuni yalifuatwa bila mafanikio na wengine ilibidi siku moja kumfungia mkuu wa chuo ofisini kama hatua ya kumshinikiza aondoe uozo chuoni.

Hatua zote hizo zimekuwa zikilenga kuwezesha mabadiliko ya kimfumo chuoni na kujibu hoja za msingi, ikiwamo kuitishwa kwa vikao vya ripoti za mapato na matumizi.

Athari za uongozi mbovu chuoni zimeanza kujitokeza ambazo ni pamoja na kuporomoka kwa kiwango cha taaluma chuoni. Kwa mfano, matokeo ya watahiniwa wa mtihani wa taifa kwa mwaka 2012 ni mabaya, zaidi ya watahiniwa 310 wanatakiwa kukariri masomo waliyofeli hapo mwakani wakati wenzao watakapokuwa wanafanya mtihani mingine, pia wapo wanachuo 67 waliofeli kabisa hivyo hawana sifa za kuwa walimu popote pale.

Gharama serikali inazoingia kumsomesha mwanachuo mmoja kwa miaka miwili si chini ya milioni sita (ukijumuisha mishahara ya watumishi, na gharama nyingine za uendeshaji).

Wakufunzi wamekuwa wakiomba vikao vya kujadili hali ya kitaaluma, kwa mfano, kujadili matokeo hayo mabovu lakini kutokana na maovu ya uongozi, imekuwa vigumu vikao hivyo kufanyika.

Tunaamini vikao haviitishwi kwa sababu uongozi utabanwa kuhusu mwenendo wake mbovu. Kero mbalimbali zimekithiri chuoni, kuanzia hali duni ya maktaba ambayo huchangiwa Sh. 10,000 na kila mwanachuo tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 hadi leo lakini hali ya jengo la maktaba si ya kuridhisha.

Hakuna vitabu vya kutosha maktaba, chumba cha maktaba kilichopo hali yake ni mbaya, maabara ya kompyuta si ya kuridhisha. Kuna madai kwamba fedha zinazotoka wizarani kwa ajili ya ukarabati zimekuwa zikitafunwa sambamba na fedha za michango ya Sh. 10,000 kila mwaka ya wanafunzi.

Mashine za kudurufu ni tatizo, wino kwa ajili ya mashine hizo hakuna na wanafunzi hujigharimia ili angalau kujitafutia elimu bora. Inafikia mahali hata barua za mkuu wa chuo zinakaa kwa karani wake zaidi ya wiki mbili bila kuchapwa kisa eti wino hakuna! Hii ni aibu kwa chuo kikubwa kama hiki.

Ndugu mhariri, chuo kina miradi na huduma kadhaa ambazo ni sehemu ya vyanzo vya mapato bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini. Baadhi ya vyanzo vya mapato vya chuo ni pamoja na fedha zinazotokana na huduma ya chakula kupitia mradi wa “Domestic Science” (DS).

Mradi huu unaendeshwa zaidi wakati wa kazi mbalimbali maalumu zinazofanyika eneo la chuo, kwa mfano shughuli za Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) au shughuli nyingine kama semina.

Mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa inayokiingizia chuo fedha nyingi lakini hali ya chuo haiendani na mamilioni ya shilingi yanayopatikana kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato.

Upo mradi wa mnara wa simu, mradi mdogo wa kantini ya chakula, mradi wa huduma ya mafunzo ya muda mfupi kwa wanafunzi wa sekondari maarufu kwa jina la TAI (Teachers Academic Initiatives) na wale wa elimu ya awali ambao nao unaingiza fedha. Tunaamini mapato ya miradi hii hayafanani na taarifa zilizopo na kwa kweli tunashangazwa na wakaguzi wa hesabu wanaofika chuo hapa na kuondoka kimya kimya bila kuwapo na ripoti kuhusu hali halisi.

Chuo chetu kimepoteza mvuto kwa sababu ya uongozi mbovu, miaka ya nyuma chuo kilikuwa kikipokea wanafunzi zaidi ya 1500 lakini leo hii hata 200 ni vigumu kuwapata. Wakati mwingine tunadhani ni njama zinazohusisha hata vyuo binafsi ili wanafunzi wakasome huko badala ya chuo hiki chenye sifa ya kipekee nchini.

Haturidhiki na mbinu zinazotumiwa na uongozi wa chuo katika kukabili matatizo haya kwa sababu uongozi ni sehemu ya matatizo haya.

Uongozi wenye tuhuma katika miradi ya chuo ukiwamo mradi wa majoho kwa ajili ya mahafali ya wanachuo haupaswi kuaminika kuongoza chuo cha kitaaluma, tena taaluma nyeti ya ualimu. Uongozi unaojihusisha na michango ya fedha za wanafunzi katika hali ya shaka kubwa haupaswi kuongoza chuo hiki.

13 thoughts on “Nani akinusuru Chuo cha Ualimu Korogwe?”

 1. koti says:

  Poleni sana, wafanyakazi wanafunzi na wananchi kwa ujumla, hii ndio Tanzania bwana, si ajabu kwamba uongozi uliopo unakula pamoja na wakubwa! maana naamini haya wanayajua kabla hayajafika kwa mhariri! hata hivyo jaribuni hata kufikiria suala la mgomo maana nchi hii bila ya njia hio hakuna atakaejali!

 2. john says:

  da kweli ufisadi sio kuwa katibu au waziri wa wizara fulani

 3. Mgeni A says:

  Enyi wandugu Poleni

  Kwani Wakaguzi wa Mahesabu na wa Masomo wanafanya nini? Kazi kwako CAG na Mkaguzi Mkuu wa Vyuo vya Ualimu. Vinginevyo yawezekana Vigogo (baadhi) huko Wizarani mna "Vituo" vyenu vya kujineemesha.. Huyi ni Korogwe Vipi Taasisi nyinginezo. Mola isaidie TZ ya Wasomi hawa..

 4. Msomaji wetu says:

  mkoani iringa bado hatujalipwa fedha za sensa

  napenda kutoa masikitiko yangu kwa watumishi kumi kutoka kila wilaya ambao tulichaguliwa kukagua madodoso ya sensa wilaya nzima kwa muda wa siku 15.lakini tulifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa na madodoso yote yakawa safi.LAKINI cha kusikitisha hadi sasa bado hatujalipwa na tunapewa ahadi za uongo kuanzia mwezi septemba hadi sasa.Namuomba Raisi kikwete na waziri mkuu mheshimiwa mizengo pinda ,mlifuatilie kwa umakini suala hili kwani linaitia aibu serikali.Ni sisi watumishi kumi kumi kutoka wilaya ya kilolo,iringa vijijini,njombe,makete,mufindi,na ludewa.

 5. musa says:

  Poleni sana wanachuo, lakini si huko tu hata makazini idara ya elimu ni ufisadi tu mfano wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya fedha za walimu zinachakachuliwa utadhani hakuna uongozi wa  juu.Hata ukipiga kelele utasakamwa na kusingiziwa mambo lukuki. But 2015 is nearly don't worrrrrrrrrrrrrrreeeeeee

 6. grace ngowi kutoka arusha says:

  mungu atusaidie jaman.yaan sisi tuliyopangiwa huko tunakosa hata hamu ya kuja kama mambo ni hayo.ila tusikate tamaa mungu yupo nasi

 7. joseph julius says:

  Kazi ipo xaiv kila kona ni uchakachuaji!

 8. Msomaji wetu says:

  NIMESIKITISHWA SANA NA HALI YA CHUO CHA KOROGWE MAANA MIE NI MIONGONI MWA WALIOSOMA HAPO TAFADHALI SERIKALI ITPIE JICHO MALALAMIKO HAYO

 9. Msomaji wetu says:

  SWALI KWANI ADA ZA WANACHUO ZINALIPWA KWENYE ACCOUNT YA NANI? MAANA WAKATI MIMI NASOMA HAPO KOROGWE ADA TULIWEKA KTK ACCOUNT YA MKUU WA CHUO NA KUNAWAKATI TULIKUWA NA SHIDA KUBWA YA MAJI TUKAHOJI MCHANGO WA WANACHUO ILI KUCHIMBIWA KISIMA PESA ZIMEFANYA NINI TUKAJIBIWA HAMUWEZI KUMUULIZA BABA YENU PESA UMEFANYIA NINI? HIVYO TATIZO NI KUANZIA MALIPO YA ADA NA MICHANGO KUPITIA KTK ACCOUNT YA MKUU WA CHUO. SERIKALI ILIANGALIE HILO KWA JICHO LA PILI

 10. Msomaji wetu says:

  YAANI KOROGWE MAISHA MAMBAYAA MIMI NILAINI KUNGEKUWA KUSOMA DIPLOMA TENA SIWEZI KWA MSOTO WA KOROGWE DUH

 11. Msomaji wetu says:

  hii hali inatishia sana msikate tamaa walimu endeleeni na mbinu mbalimbali za kunusuru chuo!ipo siku itawezekana!

 12. Msomaji wetu says:

  naomba serikili ifanye juhudi za ziada kunusuru hali hiyo la-sivyo chuo kirudishwe kwa wamiliki wa mwanzo ambao ni wamissionary wa ANGLICAN.Hata sisisi wazawa hatufurahishwi na hali hiyo.

 13. matokeo says:

  pata matokeo hapa matokeo. co 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *