Wahitimu ubaharia tunanyanyaswa

NDUGU Mhariri,

Tunaandika katika gazeti lako la Raia Mwema kutoa malalamiko yetu mimi pamoja na mabaharia wenzangu.

Kwa muda mrefu sasa, mabaharia tunaohitimu mafunzo katika Chuo cha Ubaharia cha Dar es Salaam  (Dar es Salaam Maritime Institute – DMI) tumekuwa tukipata wakati mgumu kupata vyeti vyetu.

Lakini si vyeti tu, bali pia imekuwa ni vigumu kupata seaman book (kitabu maalumu mfano wa hati ya kusafiria kwa mabaharia, ambacho hugongwa muhuri na kapteni wa meli kuthibitisha kumtambua kikazi mhusika).

 Vyeti vya uhitimu na seaman book ambayo ni sawa na leseni, vinapaswa kutolewa na Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri wa Maji na Nchi Kavu (SUMATRA), ofisi za Upanga, jijini Dar es Salaam.

Bila sababu za msingi, imekuwa ikitugharimu takriban mwaka mzima ili kupata nyaraka hizo muhimu kwetu. Kwa mfano, mwaka jana hawakutoa kabisa seaman book eti kwa kisingizio cha uchaguzi wa ubunge Igunga, wakidai mchapishaji wa seaman book hizo ndiye aliyekuwa na jukumu la kuchapa nyaraka za uchaguzi Igunga.

Sasa hakuna uchaguzi Igunga lakini wanaibua sababu nyingine eti hakuna mhuri, ukifika ofisini wanakuambia ujaze fomu na kulipa Sh. 15000, wanakwambia njoo baada ya wiki moja, ukirudi wanakwambia bado vyeti havijatiwa sahihi.

Ukirudi tena wanakwambia wahusika wapo kwenye kikao, ukirudi siku nyingine wanakwambia njoo wiki ijao ukirudi wanakuambia vitabu vimekosewa “chukua namba simu utupigie.

Ndugu mhariri, tatizo ni kwamba kwa sasa hiki ni chuo pekee nchini. Nenda rudi hizi zimekuwa ni usumbufu mkubwa kwa wanaotoka nje ya Dar es Salaam, wasio na makazi hapa jijini.

Hawa watu si tu wanatusababishia usumbufu lakini pia wanatukwamisha kuanza kazi za kibaharia ambazo ajira ni nyingi Ulaya. Kupitia gazeti hili, tunaomba mabosi wa ngazi za juu zaidi wachukue hatua kuondoa ubabaishaji huu.

Mwanafunzi mhitimu

3 thoughts on “Wahitimu ubaharia tunanyanyaswa”

  1. peter says:

    tena hawa watu wanaulasimu wa hali ya juu sana ni watu ambao hawafuati maadili ya kazi hawajari kama wako kazini mimi mpaka nimeamua kukiacha kitabu changu kwani safari ilikuwa isha wadia imenibidi nichukue kitabu cha bahamas hii yote ni kutokana na urasimu huu hawa wakubwa hapo sumatra hawajaliona hili kama vipi wawape nafasi wangine.

  2. Msomaji wetu says:

    Hadi sasa huo usumbufu upo???????

  3. Msomaji wetu says:

    mimi nimeacha hiyo 15000 na seamen book record yenyewe,ninatumia mikoba ya sauth africa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *