Loliondo pasua kichwa kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili, Mazingira

KAMATI ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira 'imepasuka' vipande kufuatia hatua ya baadhi ya  wajumbe wake  kutofautiana  kuhusu mgogoro wa ardhi katika pori tengefu la Loliondo wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha.

Sambamba na tofauti hizo wajumbe wa kamati hiyo pia warushiana maneno huku wakituhumiana kuwa kuna wenzao wamekula rushwa.

Wajumbe wa kamati hiyo walikuwa katika ziara ya kutembelea pori hilo wiki iliyopita na kufanya tathmini kuhusu mgogoro huo uliodumua kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhandisi Atashasta Nditie ambaye pia aliambatana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, wajumbe wa kamati hiyo walitembelea pori hilo  tengefu na kujionea uharibifu wa mazingira uliosababishwa  na uwingi wa mifugo katika eneo hilo.

Kiini cha Mgogoro

Mgogoro wa katika eneo la pori hilo tengefu lenye kilomita za mraba 4,000 ulianza tangu mwaka 1992 wakati wa uongozi wa serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi kugawa sehemu ya pori hilo kuwa kitalu cha uwindaji cha kampuni ya Ortello Business Cooperation (OBC) ya Falme za Kiarabu (UAE).

Sehemu iliyomegwa na kuwa kitalu cha uwindaji ilikuwa chini ya shirika la Wanyapori la Taifa wakati huo ikjulikana kama (Tawico) na iliendesha shughuli za utalii wa kiuwandaji na upigaji picha.

Hata hivyo, kampuni ya OBC imekuwa katika migogoro ya mara kwa mara na wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo hilo ambao wengi ni wafugaji wa jamii  ya kimasaai ambao wamekuwa wanaungwa mkono na mashirika lukuki ya hiari (NGOs) yanayofanya shughuli katika eneo hilo.

Aidha mgogoro huo pia unahusisha makampuni mengine ya wawekezaji ambayo hufanya shughuli za biahsara ya mahoteli, utafiti na upigaji picha katika eneo hilo hilo.

 Mgogoro ulizidi kushamiri zaidi kuanzia mwishoni mwa wamaka jana  baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na pendekezo la  kumega eneo la kilomita za mraba 1,500 kutoka eneo la kilomita za mraba 4,000 za pori tengefu la Loliondo ilikuwa pori la akiba (Game Reserve).

Eneo hilo kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa uhifadhi na utalii ndiyo chanzo cha mto Grumeti unaochangia asilimia 47.2 ya maji hifadhi ya taifa ya Serengeti na kustawisha asilimia 70 ya viumbe katika hifadhi hiyo.

Aidha eneo hilo pia linategemewa na mifugo na wananchi 783,701, serikali kupata mapato yake kupitia utalii wa picha na uwindaji, hoteli za kitalii na pia ni eneo la kuzaliana wanyama hasa nyumba na wanyama hao huanzia mfumo wa kuhama (Wildebeest Migration) ambao ni kivutio kwa watalii wengi.

Wananchi wanapinga mpango huo kwa maelezo kuwa kumegwa kwa eneo hilo kutasababisha watu zaidi ya 54,000, vijiji 14 na mifugo zaidi ya 700,000 kukosa makazi au kuhamishwa katika eneo hilo.

Wakati kamati hiyo ya Bunge ikitembelea eneo hilo, tayari kamati teule inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Mrisho Gambo kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, ilitarajiwa kurudi Loliondo Machi 14 (jana) kukamilisha mchakato wake na kupeleka mapendekezo kwa Waziri Mkuu kabla ya Machi 20.

Tofauti Kamati ya Bunge

Tofauti baina wajumbe wa kamati hiyo zilianza kujitoeza siku ya kwanza tu ya ziara hiyoMachi 6 baada ya msafara kusimamishwa na wananchi katika kijiji cha Arash ambapo katika hali isiyo kawaida wajumbe kadhaa wakiongozwa na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa walisimama kuwasikiliza.

 Ndassa akiungwa mkono na wajumbe Joseph Kasheku (Msukuma), Paulina Gekul, Dk. Godwin Mollel na Jabbir Kigoda walisema kama viongozi   wana kila sababu na haki ya kuwasikiliza wananchi hao hatua ambayo Mwenyekiti wa Kamati aliipinga.

“Kazi ya kamati si kufanya mikutano ya hadhara, kazi yetu ni kutembelea maeneo yote ambayo kuna uaharibifu wa mazingira na kufanya tathmini  yake na baadaye kufanya majumuisho na kutoa mapendekezo yatakayosadia Serikali kufanya maamuzi,” alisema mwenyekiti huyo.

Aidha wajumbe hao waliendelea kutofatiana pia wakati wa kusikiliza pande zinazohusika na mgogoro huo katika mkutano wa ndani uliofanyika mjini Karatu ambapo wajumbe hao waliendelea “kurushiana vijembe”.

Akizungumza na Raia Mwema mara baada ya kikao hicho, mmoja wajumbe, Dk. Godwin Mollel ambaye ni Mbunge jimbo la Siha (Chadema), alipinga hatua ya mwenyekiti huyo kuwanyima huru wa kutoa mawazo yao.

“Kama mnavyoona hata nyie waandishi wa habari, Mwenyekiti hatoi fursa ya sisi kusikilizwa na ameegemea upande moja na hii maana yake ni kwamba kuna ajenda maalumu inataka kupitishwa na sisi tutumike kama rubber stamp,” alisema Dk. Mollel.

Mjumbe huyo aliongeza: "Kabla ya ziara hii tuliambiwa kwamba, kuna mifugo kutoka nchi jirani na matrekta yamevamia eneo hili la pori tengefu lakini tumefanya ziara hapa siku nzima hakuna matrekta wala mifugo zaidi ya wenyeji wachache tuliowakuta hapa. Kuna upotoshaji mwingi.”

Naye Mjumbe mwingine ambaye ni mbunge wa jimbo  la Babati Mjini, Paulina Gekul, alidai kuwa wajumbe wa Kamati hiyo wameshawishiwa na kupotoshwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,  Profesa Jumanne Maghembe ili kumsadia kulinda maslahi yake katika mpango wa kugawa ardhi hiyo.

“Siku tulipoanza ziara asubuhi yake, Waziri alikuja kwetu  kusema wafugaji wamehamisha mifugo yao na matrekta usiku…..Waziri alikuwa anasema uongo tu hakuna mifugo wala matrekta yaliyohamishwam” alidai mjumbe huyo.

Aliongeza kuwa kuhusu Mwenyekiti kuegemea upande mmoja katika mgogoro huo kwamba alionyesha chuki za wazi dhidi ya wajumbe waliokuwa wanataka kutetea maslahi ya wananchi walio wengi.

“Waziri atueleze baada ya eneo kutengwa wananchi hawa 54,000 na hii mifugo 700,000 wanahamishiwa wapi? Na tuelezwe kampuni ya OBC itafanya shughuli zake za uwindaji katika kitalu kipi? aliohoji mbunge huyo.

Kwa upande wake, Mbunge Joseph Kasheku (Msukuma) alisema kutokana na maadili ya chama chake atakwenda kutoa maoni yake katika kikao cha majumuisho kitakachofanyika mjini Dodoma baadaye.

“Mimi ni mbunge na mwenyekiti wa chama cha CCM Mkoa wa Geita kwah iyo nitasubiri muda muafaka wa kufanya majumuisho tuone kama Mwenyekiti ataendelea kutufanyia ubabe wake,”alisema Mbunge huyo machachari.

Tuhuma za Rushwa

Wajumbe wa Kamati hiyo pia walituhumiana kuwa kuna wanaotumiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na makampuni kadhaa ya wawekezaji ili kutoa maoni na mapendekezo yatakayosadia na kushinikiza maamuzi ya serikali.

Mwenyekiti wa Kamati, Nditie, aliimbia Raia Mwema kuwa tuhuma hizo ni nzito na kimetia doa kamati yake ambayo anaamini kuwa imeundwa na wabunge wenye uweledi na watu wanaominika katika jamii.

“Hilo sitaki kulizungumzia sana ni tuhuma nzito, jambo moja nataka kuliweka wazi ni kwamba tofauti zilizojitokeza ni hisia za wajumbe moja moja binafsi  ambalo ni jambo  la kawaida, ” alisema.

Aliongeza kuwa ana imani kubwa kwamba wajumbe wote watotoa maoni yao na mapendekezo yao wakati wa majumuisho ili kuisadia serikali kutatua mgogoro huo kwa njia sahihi.

Hata hivyo, Gekul alipinga tuhuma hizo za rushwa na kubainisha kuwa kinachofanyika ni kuwachafua majina yao baada ya kukosa hoja za msingi dhidi yao.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi ya kutuchunguza basi, hapo tutawajua waliowekewa fedha kwenye akaunti zao za benki na kama ni sisi basi pia itafahamika,” alisema mbunge huyo.

Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi alisema kamati hiyo kama chombo cha Bunge na wananchi kinaowajibu wa kuisadia serikali kwa kutoa mapendekezo yenye tija kwa sekta utalii na uhifadhi kwa faida ya Tanzania.

Kwa upande wake Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha (CCM), akizungumza kwa njia ya simu na Raia Mwema  alifafanua kuwa kwa tathmini iliyofanyika iwapo kilomita hizo za mraba 1,500 zitageuzwa kuwa Game Reserve, maamuzi hayo yataleta athari za moja kwa moja kwa wananchi wake.

Ole Nasha ambaye ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alisema miongoni mwa athari hizo ni tarafa ya Loliondo yenye vijiji 14  kupoteza zaidi asilimia 90 ya ardhi yake kwa ajili ya Game Reserve.

“Naomba nizungume kwa niaba yangu kama Mbunge na kwa niaba ya wananchi wa Ngorongoro kuwa hakuna anayepinga mpango wa kutatua mgogoro huu wa muda mrefu ila tungependa njia za kidiplomasia zaidi zitumike kwa malsahi mapana ya nchi yetu,” alisema ole Nasha.

Alisema iwapo mpango huo utatekelezwa, wananchi wanaokadiriwa kufikia 54,000 wanaoishi katika vijiji hivyo 14 watakosa maji kutokana na vyanzo vingi kuwa eneo hilo, na vijiji vitapoteza mapato yatokanayo na utalii.

“Lakini pia mpango huo utaongeza migogoro ya ardhi kati ya wananchi wa tarafa za Loliondo (wafugaji) na Sale (wakulima) na pia utaleta matatizo kwa Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro kwa maana wafugaji wengi watakaondolewa wanaweza  kuhamishia mifugo yao huko,” aliongeza.

Mbunge huyo aliongeza: "Kwasasa tusubiri mapendekezo ya kamati teule ila ushauri wangu ni kwamba  tutumie busara katika jambo hili. Kama hoja ni kuokoa Ikolojia ya Serengeti binafsi naamni kuwa kuna njia nyingi za kufanya hivyo kwa kuwatumia wataalamu wetu.”

One thought on “Loliondo pasua kichwa kwa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili, Mazingira”

  1. EMANUEL says:

    Napenda kumpongeza mwandishi wa makala hii kwa kujaribu kupata maoni ya wadau mbalimbali lakini makala hii imekosa kutoa mawazo ya wananchi moja kwa moja pamoja na kuwa ilihusu mpasuko wa Kamati ya Bunge lakini wananchi pia walikuwa na maoni ya kusema juu ya kamati hiyo ya Bunge. Sipendi kuonekana kama napinga kamati lakini napenda kutoa maoni yangu kuwa, mwonekano wa kamati hiyo ulikuwa tofauti na uhalisi wa kuundwa kwake kama kamati ya Bunge. Kamati ilikuwa inaonekana kama inafanya kazi ya Wizara ya maliasili na Utalii ambayo ni watuhumiwa wa kupora ardhi ya vijiji. Kamati ilipaswa kwenda yenyewe na kufanya kazi na viongozi wa wilaya na Mkoa badala na wizara ambayo wangewakilishwa tu na waakilishi. Ilivyoonekana, Waziri Maghembe alionekana akiongoza kamati na kueleza mawazo ya wizara pekee, alimudu kushawishi kamati kwamba wao, wizara wapo sahihi. ilionekana kamati inafanya kazi ya wizara badala ya kazi ya kibunge. vilevile kushindwa kuwasikiliza walalamikaji, wananchi na kusikiliza upande mmoja ilikuwa moja ya mapungufu ya kamati hiyo. Pamoja na hayo, ninacho ona mimi ni  kuwa, eneo hilo ni eneo la matumizi mseto maana yake kuwa ni vijiji na pori tengefu na zote zipo kwa mujibu wa sheria. Lakini mchakato unaoitwa kuwa ni wa kutatua mgogoro, unakuwa wa kuegemea upande mmoja. Vijiji havina hata taarifa ya kinachoendelea. Hawakuwahi kupata taarifa rasmi ya nini serikali inafanya. Huenda hili linafanyika kwa makusudi kabisa au kwa kusaulika lakini sheria ya usimamizi wa ardhi ya vijiji bila shaka inakiukwa. Kimsingi Halmashauri za vijiji ndivyo vyombo vilivyona mamlaka ya usimamizi wa ardhi ya kijiji na Mikutano Mikuu ndio vyombo vya maamuzi hivyo kuvipuuzia hivi vyombo vya kisheria ni kukiuka sheria na suluhu la mgogoro huo hauwezi kufikiwa. Kamati pia pamoja na kutembelea kujionea na kujifunza juu ya eneo hilo lakini pia walipaswa kuheshimu mamlaka ya vijiji vinavyosimamia eneo hilo kwa upande mmoja badala ya kusikiliza wizara ya maliasili pekee ambao ni upande wa pili wa mgogoro. Vilevile kuwaingiza wawekezaji katika mchakato ni hofu kubwa kuwa haya hayafanyiki kwa manufaa ya umma wala nchi bali kwa manufaa ya hao wawekezaji. Hii naona kunyima uhalali mchakato huu wa ardhi wa kumega kilometa za mraba 1500. Vilevile, haijafanyika tathimini yakinifu kujua madhara ya kimazingira na kijamii ambayo vijiji vitaathirika kutokana na ardhi yao kumegwa. Kiukweli ardhi hii ndio ardhi pekee ndio inayotegemewa na vijiji kwa malisho ya mifugo yao. Kinachosemwa kilometa za mraba 2500 ambao hubaki kuwa ya vijiji kiuhalisia haibaki kwa ajili ya malisho bali ni eneo ambalo tayari linamatumizi kikamilifu. Mfano. eneo hili ni pamoja na mji wa LOLIONDO, misitu ya Loliondo, maeneo ya kilimo na Tarafa nzima ya Sale inayoundwa pia na eneo la Ziwa Natron. Hivyo kimahesabu eneo pekee linalobaki kwa wafugaji ni chini ya kilometa za mraba 200. Naomab kuwakilisha maoni yangu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *