Lowassa aitia Chadema majaribuni

HATUA ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kutangaza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa Kenya umekiweka majaribuni chama chake, gazeti hili linafahamu.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Lowassa alitangaza hadharani kwamba yeye atamuunga mkono Kenyatta; Rais wa sasa wa Kenya, kwenye uchaguzi wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika Agosti mwaka huu.

Wakati Lowassa akienda hadharani na kutangaza hilo, Chadema imesema hadi sasa haijaamua imuunge mkono nani katika uchaguzi huo na kwamba uamuzi wa Waziri Mkuu huyo mstaafu ni wa binafsi.

Akizungumza na Raia Mwema hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, alisema kwa sasa chama chao kinafuatilia kwa karibu kinachoendelea Kenya na kwamba hawajaamua wamuunge mkono nani katika uchaguzi huo.

“Jambo la kumuunga mkono mgombea ni la chama na mimi kama Katibu Mkuu sikumbuki kama chama kimewahi hata kujadili tu kwamba kitamuunga mkono nani.

“Ninachojua ni kwamba tunafuatilia kwa karibu sana kila kinachoendelea nchini Kenya na kama hatimaye tutaona umuhimu wa kutangaza tunamuunga mkono nani, tutafanya hivyo. Ila kwa sasa bado,” alisema Mashinji.

Alisema amesikia kwamba Lowassa ametangaza kumuunga mkono Kenyatta lakini huo ni uamuzi binafsi wa mbunge huyo wa zamani wa Monduli kutokana na uhusiano wake binafsi na Uhuru na kwamba chama chao hakihusiki na msimamo huo.

Pamoja na maneno hayo ya Mashinji, Raia Mwema linafahamu kwamba suala la Lowassa kutangaza kumuunga mkono Kenyatta limekiweka chama hicho majaribuni; kwa sababu ya si wanachama wote wa Chadema wanamuunga mkono mgombea huyo.

Katika chaguzi zilizopita, Chadema ilikuwa ikimuunga mkono mgombea wa muungano wa wanasiasa wa upinzani, maarufu kama NASA, Raila Odinga, ambaye kimataifa anajulikana kama mpinzani mashuhuri zaidi nchini Kenya.

Baadhi ya wanasiasa wa Chadema wanahusisha itikadi na maoni yao moja kwa moja na Raila kuliko Uhuru ambaye hajawahi kufanya siasa za maana za upinzani.

Mmoja wa wabunge mashuhuri wa Chadema aliyezungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma, alisema kama Chadema itafuata alichosema Lowassa itaonekana “anawaburuza” na ikisema haimuungi mkono itaonekana kuna tofauti kati yao na mgombea wao huyo wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“ Nadhani kuna bumbuwazi. Hakuna ambaye alitaraji Lowassa angesema aliyoyasema hadharani. Wakubwa wana hali ngumu; ama watangaze kumtosa Lowassa na kuleta picha isiyofaa kwa umma au kumuunga mkono na kuonekana chama kinamfuata mtu. Haya ni majaribu,” alisema mbunge huyo.

Gazeti hili linafahamu kwamba baadhi ya wana Chadema wanamuunga mkono Lowassa kwa sababu wanaamini Raila aliwasaliti kwa kuonyesha kumuunga mkono Magufuli wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka juzi hapa nchini.

Pamoja na kuwapo kwa ushindani mkubwa katika uchaguzi huo, Raila alikwenda hadharani na kudai kwamba angefurahi Magufuli ashinde kwa sababu ni rafiki yake.

Kauli yake hiyo haikupokewa vema na wana Chadema walioona kauli hiyo kama ni usaliti kwao kwa vile siku zote wamekuwa wakimuunga mkono katika siasa za Kenya, pasipo kujali anashindana na nani.

“ Ngoja nikwambie, tunafahamu Raila ana urafiki na Magufuli na hivyo anaweza kumsaidia kwenye kampeni. Kitakuwa kitu cha ajabu kama sisi na Magufuli tutakuwa upande mmoja kwenye uchaguzi wa Kenya,” kilisema chanzo kingine cha gazeti hili.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita nchini Kenya wa mwaka 2012, Magufuli alikwenda kumpigia kampeni Raila kwenye uchaguzi huo, ingawa CCM haikuwa imetangaza kumuunga mkono mgombea yoyote kabla ya uchaguzi huo .

Katika mahojiano yake na idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) mwishoni mwa mwezi uliopita, Lowassa alitoa sababu tatu za msingi za kwanini aliamua kutangaza jambo hilo hadharani.

“Kwanza, huu ni wakati wenyewe kwa sababu kule (Kenya) ndiyo sasa wanafanya kura ya maoni kuchagua wagombea. Pili ni kwamba namuamini mgombea mwenyewe (Uhuru) na tatu nilitaka sauti yangu isikike,” alisema Lowassa aliyesema pia kwamba Uhuru anawafaa Wakenya kwa sababu rekodi yake ya utendaji wake ni nzuri.

Kwa mara ya kwanza, Lowassa alitangaza kumuunga mkono Kenyatta wakati alipokuwa akizungumza na wageni kutoka Jamhuri ya Kenya wakiongozwa na wabunge 13, Madiwani, Machifu na Maleigwanan  waliomtembelea kijijini kwake Ngarash, Monduli mwishoni mwa mwezi uliopita.

"Mimi naamini Uhuru Kenyatta anao uwezo mkubwa wa kuwaunganisha vema wananchi wa Kenya na Watanzania. “Naahidi  ukifika muda muafaka tutaungana naye kumsaidia katika kampeni zake. Natamka wazi na dunia yote ijue kuanzia sasa kwamba sisi tunampenda Kenyatta na yeye anajua kama tunampenda, kwa hiyo tunamuunga mkono tukiamini kabisa ana uwezo wa kuunganisha wananchi wetu,” alisema Lowassa.

2 thoughts on “Lowassa aitia Chadema majaribuni”

  1. Hansi Madinga says:

    Binafsi sioni tatizo kwa Mhe: Lowassa kumuunga Uhuru Kenyata! Na vile vile unaweza kuwa ni uamuzi wake binafsi usiokihusisha chama chake, kwahiyo sioni kama kuna tatizo lolote hapo! 

  2. Juma Makuri says:

    Msiomjua Lowasa in sawa na wasiomjua Uhuru Kenyatta. Wote ni  wasaliti wa ASILI zao. Uhuru ni  mwana KANU kajivua gamba tu. Na Lowasa ni mwana CCM naye kajivua kamba tu. Kujivua gamba sio kupoteza ukali wa sumu. Hawa wote wana uchu wa madaraka sio uzalendo wa nchi zao. Lowasa kama alikula mkate wa bibi atashindwa kula mkate wa babu? CHADEMA kuweni makini na MTU huyu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *