Lowassa, mwendapole asiyejikwaa kuelekea 2020

WIKI tatu zilizopita nimekuwa nikiandika mfululizo wa makala ninazozitambulisha kama “Miezi 20 baada ya mahojiano na Magufuli” yaani miezi 20 baada ya kufanyika mahojiano kati yangu na Dk. John Magufuli, Septemba 15, 2015 akiwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nikilenga kutathmini safari yake kuanzia kampeni hadi Ikulu, akiongoza taifa kwa takriban mwaka mmoja na nusu sasa.

Katika makala zilizotangulia nilieleza kuhusu Magufuli na majeruhi wanaotokana na utawala wake huu, namna anavyoweza kukwepa kuzidi kujisababishia madonda ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020. Kuna makosa ya kiutawala yamekuwa yakifanyika kiasi cha kuzua matukio yanayofifisha mwendelezo wa uhalali wa kisiasa wa Magufuli na kumwacha akibaki Magufuli mwenye uhalali wa madaraka kwa mujibu wa sheria, yaani urais wenye ushawishi hafifu wa kisiasa.

Ni kweli, kuna wakati tena katika mazingira mahsusi, nguvu za madaraka zinaimarisha nguvu za kisiasa na hivyo kuimarisha ushawishi wa kisiasa wa mhusika lakini vile vile inaweza kuwa kinyume chake, kwamba unaweza kutumia nguvu za madaraka (hard power vs soft power) kiasi cha kumomonyoa uhalali wa kisiasa mbele ya jamii.

Kwa mfano, hivi karibuni, Rais Magufuli ameondoa watumishi wenye vyeti vyenye utata – ametumia madaraka yake vizuri ya urais, lakini katika tukio hilo hilo, hapakuwa na ulazima wa kuwaita wahusika “majizi” kwa kuwa wapo wanaodai kuonewa na watakwenda mahakamani. Je, mahakama ikiwapa ushindi nani atawasafisha dhidi ya kauli (ya hadharani) ya “majizi”? Ni dhahiri, katika mazingira haya, uhalali (ushawishi) wa kisiasa unaweza kuporomoka.

Bahati mbaya sana, baadhi ya viongozi wanaomsaidia Magufuli nao wameiga mfumo huu wa ‘kufyatua’ kauli zenye majivuno ya madaraka. Tumesikia majuzi bungeni, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akimweleza Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga, kwamba anaweza kuondoka katika Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa mbunge huyo amehoji kuhusu kusuasua kwa utekelezaji wa mradi wa maji jimboni kwake, ingawa naye (Kitwanga) hakupaswa kutoa kauli ya vitisho kwamba atahamasisha wananchi waharibu miundombimu ya mradi wa maji iliyokwishakamilika. Lwenge ni kama anaamini ndiye mwenyeji zaidi katika CCM kuliko Kitwanga, ni sawa na ile kauli ya “nimechukua fomu ya urais mwenyewe”.

Kwa ujumla, mazingira hayo ndiyo niliyoyatumia kujadili kwa ufupi katika wiki mbili zilizopita kuhusu Tundu Lissu, mmoja wa majeruhi wa utawala huu, majeruhi ambaye anafaidika kutokana na makosa ya kiuongozi ya baadhi ya wakubwa.

Niliahidi makala inayofuata nitamzungumzia Edward Lowassa, mwanasiasa aliyeacha kivuli katika Chama cha Mapinduzi (CCM) na ambaye, kwa kiasi kikubwa, anayo nafasi kubwa ya kujinufaisha na makosa ya utawala wa Magufuli. Kimsingi, ukichunguza sana, kuna mazingira fulani ambayo katikati ya kilele cha mafanikio ya Magufuli, kuna faida kwa Lowassa. Hili nitafanunua baadaye.

Kwa nini Edward Lowassa?

Unaweza kujiuliza kwa nini Edward Lowassa awe katika orodha ya majeruhi wa kisiasa wa utawala huu wa Magufuli? Majibu yake; kwanza, anazo kura zaidi ya milioni sita (6,072,848) kati ya kura zaidi ya milioni nane (8,882,935) za mshindi wa urais mwaka 2015. Yaani Lowassa bado anaishi katika mtaji wa asilimia 39.9 za waliopiga kura mwaka 2015 na Magufuli anaishi katika mtaji wa asilimia 58.46 za waliopiga kura mwaka 2015, tofauti kati yao ni asilimia 18.56 tu.

Takwimu ni kama kioo, hazidanganyi. Kwa vyovyote vile, makosa au ufanisi wa Magufuli lazima vihusishwe na takwimu hizo za 2015. Kila jambo zuri analofanya Magufuli kama kiongozi lazima liakisi asilimia 58.46 za matokeo ya kura za mwaka 2015 na kila kosa la kiutawala nalo liakisi takwimu hizo hizo, hasa kwa kuzingatia sayansi ya takwimu.

Kwa hiyo Lowassa si mwanasiasa wa kubezwa kutoka katika orodha ya wagombea urais wa mwaka 2015. Ni miongoni mwa wanasiasa wenye mtaji wa kura katika maisha ya utawala huu, kama ilivyokuwa kwa Dk. Wilbroad Slaa katika awamu ya mwisho ya utawala wa Jakaya Kikwete au Maalim Seif na Dk. Ali Mohamed Shein kwa Zanzibar katika awamu iliyopita ya serikali ya umoja wa kimataifa.

Magufuli na utata wa Lowassa

Lowassa ni majeruhi mzoefu wa kisiasa. Alipokuwa mwanachama wa CCM, safu ya uongozi wa juu Chadema iliongoza mashambulizi hadharani dhidi yake. Alipojiunga Chadema, mashambulizi dhidi yake yamekuwa chini ya uratibu wa CCM, wana-Chadema wakigeuka watetezi wakuu. Ni mwanasiasa wa aina yake, kwa kweli anapaswa kuandikiwa kitabu cha maisha yake ya kisiasa.

Mashambulizi dhidi ya Lowassa, miaka yote, yamekuwa yakimhusisha na ufisadi, na utawala huu wa Magufuli unasifika kukabiliana na ufisadi. Mantiki iliyopo ni rahisi tu, endapo Rais Magufuli atakabiliana na ufisadi kikamilifu katika miaka yake hii iliyosalia madarakani kabla ya 2020 bila Lowassa kufikishwa mahakamani, ni dhahiri kwamba, jina lake litakuwa limesafishika. Watu makini watajiuliza, imekuwaje mtu anayetuhumiwa na chama tawala, asifikishwe mahakamani na serikali kinara katika kukabili ufisadi? Maana yake ni kwamba, siasa za ufisadi wa Lowassa zitakuwa hazihitajiki jukwaani 2020 miongoni mwa watu makini.

Kwa hiyo, sifa za Magufuli kukabiliana na ufisadi bila Lowassa kufikishwa mahakamani zitamnufaisha Lowassa huyo huyo katika jukwaa la kampeni 2020 kama atagombea urais. Kwamba ajenda kuu dhidi yake katika uchaguzi wa 2015 itakuwa imekwishakufa kwa kuwa ‘jemedari’ wa kukabili ufisadi (Magufuli) naye hakuona sababu ya kumfikisha mahakamani, ni mtu safi katika eneo hilo mahsusi. 

Kutoka miezi 20 kuelekea 2020

Kama nilivyoeleza awali, nimekuwa nikimjadili Magufuli katika kipindi cha miezi 20 baada ya kufanya naye mahojiano na sasa, tutazame miezi hiyo 20 kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020, kati ya Magufuli na Lowassa (kama wote watakutana katika kuwania urais).

Kimsingi, kuanzia sasa kuelekea 2020 Magufuli hapaswi tena kuendeleza siasa zake za kulaumu waliomtangulia, kila mara amesikika akisema “…hii ndio Tanzania…hapa ndipo tulipofika” akionesha namna waliomtangulia walivyovuruga nchi. Ingawa hataji majina wala kuweka bayana ni utawala gani hasa katika miaka takriban 40 ya CCM madarakani anaoulenga katika mashambulizi yake hayo, lakini ni kweli kwamba Lowassa na Magufuli ni sehemu ya makosa ama ufanisi wa tawala zilizopita, angalau kuanzia Awamu ya Pili ya mzee Ali Hassan Mwinyi. Kwa hiyo, wote wanapaswa kufanya siasa za “kuganga yajayo” si yaliyopita kwa wote ni sehemu ya yaliyopita.

Lowassa ndiye mkongwe zaidi serikalini kuliko Magufuli. Wakati Magufuli akiwa mwajiriwa wa Kiwanda cha Nyanza Cooperative Union Ltd kama mkemia (mwaka 1989 hadi 1995), Lowassa alikwishahudumia ngazi kadhaa za kiserikali.

Alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) Arusha (1989 – 1990), wakati Magufuli bado akiwa mkemia wa kiwanda cha Nyanza, Lowassa akawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (akishughulikia masuala ya mahakama na Bunge – 1990 – 1993). Wakati bado Magufuli akiwa mkemia, Lowassa pia akawa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi 1993-1995).

Na wakati Magufuli anateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi katika awamu ya kwanza ya Benjamin Mkapa, Lowassa akawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira na Umasikini (1997 – 2000)

Kwa hiyo, kila mara Magufuli anapolaumu tawala zilizopita, yeye pamoja na Lowassa ni sehemu ya tawala hizo (angalau kuanzia wakati wa Mwinyi), tofauti ama unafuu wanaoupata ni kwamba hawakuwa katika madaraka ya juu (urais) ingawa pia walikuwa wakishiriki katika vikao vya juu zaidi kitaifa ikiwamo vikao vya baraza la mawaziri.

Mwendelezo wa Magufuli kurekebisha makosa ya tawala za nyuma na kutumia fursa hiyo ya marekebisho kama kete ya kisiasa hautamsaidia kuelekea 2020. Magufuli anapaswa kurekebisha makosa ya waliomtangulia bila masimango kwa kuwa naye akiondoka, atakuwa ameacha makosa kutokana na ukweli kwamba naye si malaika wa kisiasa. Ukweli ni kwamba, Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa busara, mzee Mwinyi, Mkapa na Kikwete kuvumilia baadhi ya kauli za hadharani za Magufuli yule waliyesimama naye jukwaani kuzindua kampeni zake pale Jangwani, Agosti 23, 2015.

Anapaswa kurekebisha kasoro hizo kimya kimya kwa kuwa yeye pamoja na Lowassa ni sehemu ya tawala zilizopita na kwa hiyo, kwake, huo si mtaji wa mkubwa wa kisiasa. Kama nilivyoeleza awali, kuna uwezekano mkubwa siasa za vita dhidi ya ufisadi zikafutika 2020, na hata siasa za ukosoaji wa tawala zilizopita zisiwe na nafasi wakati huo. Swali ni moja tu, nini kitatawala siasa za 2020? Jibu ni dhahiri, uchumi. Je, mfumo wa uchumi umelindwa katika misingi ya kulinda ajira zilizokuwapo wakati Magufuli anaingia madarakani, na hata kuzalisha ajira mpya? Uchumi ndio siasa kuu ya 2020, katika hili, wakati Magufuli akivuja jasho kujinusuru, Lowassa ni sawa na mwendapole anayepaswa kuhakikisha hajikwai kabla 2020 na kwa hiyo bado ataendelea kuwa majeruhi wa kisiasa wa utawala huu.

Wiki ijayo tutajadili urais wa Magufuli kwa kuwahusisha Mwalimu Julius Nyerere, mzee Ali Hassan Mwinyi, Mkapa na Kikwete, katika kile kinachoitwa mviringo wa ushawishi (sphere of influence au spherical influence) kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *