Lwakatare utata

WINGU limeendelea kutanda kuhusu mkanda wa video wenye picha ya Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Bukoba Mjini, kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Wilfred Lwakatare.

Wingu la sasa linahusisha taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zinaendelea ya kuwa operesheni ya kusaka watuhumiwa zaidi katika sakata hilo imeshika kasi, ikiwa ni matokeo ya mahojiano yaliyoendeshwa kati ya maofisa wa polisi na Lwakatare, pamoja na mwenzake, Ludovick Rwezaura.

Swali kubwa sasa ni je, nani wengine wataingizwa katika orodha ya watuhumiwa wa vitendo dhidi ya baadhi ya watu, akiwamo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, aliyetekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya kiasi cha kupoteza jicho lake moja.

Wingu hilo linazidi kutanda katika wakati ambao Lwakatare amefikishwa mahakamani akishitakiwa kwa makosa manne, likiwamo la kula njama ya kutenda kosa la jinai la kutoa sumu kwa nia ya kumdhuru Dennis Msacky, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, njama ambazo wanadaiwa kuzipanga eneo la King’ong’o, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Shitaka jingine la pili linalomkabili Lwakatare na mwenzake, Ludovick Rwezaura ni kula njama ya kufanya kosa la jinai kinyume cha kifungu cha 24 cha Sheria dhidi ya Ugaidi. Na tatu ni kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi, kinyume cha kifungu cha 5 (a) cha sheria namba 21 inayopinga ugaidi, wakati shitaka la nne dhidi yao ni kudaiwa kuhamasisha vitendo vya ugaidi.

“Baada ya mahojiano na Lwakatare kuna masuala ya msingi ambayo ni kama yameelekeza polisi kuendelea na msako wa baadhi ya watuhumiwa katika matukio haya ya utekaji na utesaji. Unaweza kushangazwa na majina makubwa ya watu wengine wanaoweza kunaswa,” anaeleza mmoja wa maofisa wa polisi aliyezungumza na mwandishi wetu kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, inadaiwa ya kwamba, baada ya mahojiano na Lwakatare ndipo polisi walipobaini umuhimu wa kumsaka Ludovick Rwezaura na kwamba, wapo watuhumiwa wengine watatu wanasakwa na polisi katika mazingira ya usiri mkubwa.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa taarifa hizo kutoka ndani ya Jeshi la Polisi bado haijawekwa wazi kama wengine watakaokamatwa watafunguliwa mashitaka au watatumika kama mashahidi wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo dhidi ya Lwakatare na mwenzake, Ludovick.

Taarifa zilizovuja siku moja kabla ya Lwakatare kufikishwa mahakamani zinadai ya kwamba, yapo baadhi ya mambo ambayo Lwakatare aliyakana na kutoyatambua ambayo yamejionyesha katika picha ya video iliyopachikwa kwenye mtandao wa jamii forum, wiki iliyopita lakini pia, kwa upande mwingine, inadaiwa kuna ambayo yaliyomo kwenye video hiyo kuwa alikiri kuyatambua. Gazeti hili linashindwa kufichua yapi aliyakana Lwakatare na yapi aliyatambua kutokana na suala hilo kufikishwa mahakamani tayari.

Lwakatare alifikishwa mahakamani Jumatatu wiki hii na kunyimwa dhamana na hadi jana Jumanne tunakwenda mitamboni, bado dhamana ilikuwa haijapatikana, huku mawakili wa pande zote wakiendelea kupambana kisheria ili ama apate dhamana hiyo au anyimwe.

Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka unaongozwa na Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza na upande wa utetezi unawahusisha mawakili, Peter Kibatala, Tundu Lissu, Profesa Abdalah Safari na Nyaronyo Kicheere.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *