Makala
Maana ya matokeo Arumeru Mashariki
Zitto Kabwe
Toleo la 233
4 Apr 2012
  • Barabara ya Arusha-Moshi sasa ni liberated zone

MACHI 11, mwaka huu, nikiwa ndani ya ndege natokea Arumeru kuzindua kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki kwenda Kirumba, Mwanza kuzindua kampeni za udiwani katika kata ya Kirumba, niliandika makala kuhusu nini kitaamua mshindi katika uchaguzi ule.

Nilianza makala yangu ile kwa kuandika; "Uchaguzi wa Ubunge Arumeru Mashariki ni kipimo cha namna wananchi mnavyoridhika na watawala, namna mnavyoridhika na mgawo wa ardhi na namna mnavyoridhika na mgawanyo wa maji katika wilaya yenu".

Haya maneno ilikuwa ni nukuu ya sehemu ya hotuba niliyotoa wakati namkaribisha Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuzindua rasmi kampeni zetu.

Ardhi ilikuwa ajenda kubwa sana. Washindani wetu wa CCM wakaona hatari ya hoja ya ardhi na kuanza kutoa ahadi mbalimbali za kumaliza kero ya ardhi. Hawakuaminika.

Wananchi walisema, hawa wamemaliza miaka 50 bila kutatua kero hii, watawezaje kupata suluhisho sasa. Wakakataa. Hawakuichagua CCM na badala yake wakamchagua kwa kura nyingi sana Joshua Nassari, kijana wa miaka 26 tu kuwa Mbunge wa Jimbo lao.

Katika makala ile nilieleza wazi kwamba; "Uchaguzi wa Arumeru ni uchaguzi kati ya kuwa na ardhi au kuendelea kutokuwa nayo. Ni uchaguzi muhimu kwa watu wa Meru. Wasio na ardhi watamchagua mgombea atakayesimamia mgawo wa ardhi unaozingatia haki. Mgombea huyo ni mgombea wa CHADEMA Joshua Nassari. Sasa Nassari lazima aibebe ajenda ardhi. Hana namna ni lazima awe sauti ya wananchi masikini waliofukarishwa na mfumo mbovu wa kugawa ardhi ulioanzishwa wakati wa ukoloni na kuendelezwa chini ya uongozi wa CCM.

Ushindi wa CHADEMA katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki ni ishara ya dhahiri kabisa kwamba siku za CCM kuongoza taifa letu zinahesabika. Ukilinganisha nguvu ya rasilimali watu na fedha ambayo CCM waliiweka huko Meru kulinganisha na CHADEMA, ni dhahiri kabisa kuwa fedha si kigezo cha kushinda uchaguzi. Wananchi sasa wanataka masuala yao yashughulikiwe. Hii pia imejionyesha katika chaguzi za madiwani.

CCM imepoteza nusu ya viti vya udiwani vilivyokuwa vinagombewa. Kata za Lizaboni - Songea, Kiwira - Mbeya na Kirumba - Mwanza zote zimeenda CHADEMA. Kata ya Msambweni Tanga imeenda CUF. CCM walipata kata katika Wilaya ya Bagamoyo, Bariadi na Temeke. Pia walipata kata katika Manispaa ya Dodoma.

Huu ni uchaguzi wa kwanza wa madiwani ambao CCM imepoteza nusu ya viti vilivyokuwa vinagombewa tangu mfumo wa vyama vingi uanze. Arumeru imekuwa jimbo la kwanza CCM kulipoteza kwa chama cha upinzani tangu mwaka 1997, ambapo CCM walipoteza Jimbo la Magu kwa chama cha UDP.

Kwa CHADEMA, hili ni jimbo la kwanza kulichukua kutoka CCM katika uchaguzi mdogo tangu ianzishwe mwaka 1992. Itakumbukwa kwamba mwaka 2008, CHADEMA ilishinda Jimbo la Tarime kwa kulirejesha maana lilikuwa chini yake kabla ya kifo cha Chacha Wangwe.

Hivyo ni dhahiri kabisa kwamba siku za CCM kuwa madarakani zinahesabika. Ushindi wa Arumeru na udiwani katika kata mbalimbali umeleta mageuzi makubwa ya kisaikolojia kwa wananchi kuliko hata ushindi wa Tarime.

Ni wazi kabisa kuwa ushindi huu utafuatiwa na mikutano wa kunadi chama katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Kusini na ile ya Magharibi ambako CHADEMA haijafanya operesheni.

Kushindwa kwa CCM Arumeru pia kutaleta mpasuko zaidi ndani ya CCM na kuunganisha nguvu za wanasiasa ndani ya CHADEMA. Wakati CCM itakuwa inanyoosheana vidole kutafuta mchawi na hata wengine kufurahia kushindwa kwao (wakiamini ni kushindwa kwa mmoja wa mahasimu wao), CHADEMA kitakuwa kinashikana mikono na kuimarisha mshikamano ili hatimaye kuchukua dola ifikapo mwaka 2015.

Jambo moja la dhahiri baada ya uchaguzi wa Arumeru ni kwamba ukipanda basi kutoka Moshi kwenda Arusha, utakuwa ukipita katika ngome ya CHADEMA.

Ni ngome ya CHADEMA kuanzia Moshi mjini, Hai, Arumeru Mashariki na Arusha Mjini. Kwa waliomsoma Rais Yoweri Museveni katika kitabu chake cha Sowing the Mustered seed, akitumia njia za Frelimo katika ukombozi, eneo hili sasa ni Liberated Zone, yaani ukanda uliokombolewa. CHADEMA mshikamano daima.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Zitto Kabwe
+255-756809535
http://www.zittokabwe.com

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa kambi ya Upinzani Bungeni.

Maoni ya Wasomaji

Ni kweli kabisa siku njema huonekana kuanzia asubuhi, tumefurahiswa sana na mabadliko ya kweli ya fikra za wa Tanzania. Kwa muda mrefu tumekuwa waoga kufanya maamuzi ya kweli eti tu kwa kisingizio cha kutishia amani ya nchi, hii imekuwa ni silaha ya CCM, katika kampeni zao, na sasa wananchi tuna akili ya kutafakari na kutoa maamuzi sahihi bila shinikizo la mtu yoyote. Bila kigugumizi HUU NI MWISHO WA CCM. VIVA CHADEMA, VIVA ARUMERU
 

Nadhani sasa ni wakati mwafaka wa kuangalia na kutafuta mbinu mbalimbali kwa ajili ya 2015. Tunaweza tukatumia mtandao kukusanya michango kwa wapenda mageuzi wote sio tu nchini hata nje ya nchi kama alivyofanya BARAKA OBAMA (Nguvu ya Umma), tukaandaa jopo la "voluntters" kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao sasa. Wanafunzi wa vyuo na wale waliokwisha maliza wanaweza kuwa walimu wazuri sana wa kuelemisha umma ambao wengi wapo pamoja nasi.
 
NOMBA TUANZE SASA NA SI 2015
 
PEOPLES POWER
 
 

hongera nassari kwa ushindi huo pia hongera na madiwan wote wa chadema mwanza mbeya,songea kwa ushindi huo moto huu wa mageuzi usizimike mpaka 2015 wananchi tumechoka na ccm

Pia na kanda ya kati inahitaji ukombozi kwani pamesahaulika kabisa, haiwezekani iwe kanda ya kaskazini na sehemu nyingine wapate ukombozi ilihali viongozi wa chadema mnasahau maeneo mengine

Zitto, mfano wako kutoka kwa Museveni ni urahisishaji wa mambo and it also an impertinent example. kubadilisha watawala ni rahisi kuliko ukombozi wa kweli. Historia ya Afrika inatutaka tuwe makini zaidi

Toa maoni yako