Mabadiliko katika usalama wa taifa ni ya msingi kuwa na taifa salama

NCHI yoyote ambayo ina idara ya usalama wa taifa ambayo inalegalega, nchi hiyo inakuwa katika hatari ya utawala wake kuyumba.

Idara ya Usalama wa Taifa (intelligence service) ya nchi yeyote ndicho chombo kikuu cha nchi kujilinda. Kuweza kuelewa Idara ya Usalama na umuhimu wake ni sawa na kujaribu kuelewa mfumo wa kinga mwilini (immune system).

Mwanadamu ameumbwa akiwa na kinga ya asili mwilini na kinga hii hufanya kazi wakati wote hata kama mtu hajui ipo. Ni kinga hii inatusaidia kupigana na magonjwa na maambukizi ambayo mengine hatujui tumeyapata.

Kinga ya mwili hufanya kazi kwa namna ya ajabu sana kiasi kwamba inapodhoofika basi mwili huweza kushambuliwa na hata magonjwa madogo madogo ambayo vinginevyo yasingekuwa na matatizo.

Mfumo huu wa kinga mwilini hufanya kazi kwa kuhusisha viungo, na michakato mbalimbali ikishirikisha chembechembe mbalimbali za mwili ili kuhakikisha kuwa mwili unakuwa na kinga wakati wowote. Ili mfumo huu ufanye kazi basi unatakiwa uweze kutambua mara moja aina nyingi ya vitu visivyotakiwa mwilini ili uweze kuvishughulikia.

Vitu vishambuliavyo mwili (pathogens) vinakuja katika aina mbalimbali na vingine vina uwezo wa kujibadili badili ili visiweze kugunduliwa na kinga ya mwili.

Hata hivyo, mwili wa mwanadamu nao umetengeneza mifumo na una uwezo wa kutengeneza mifumo ya kutambua vijidudu hivyo hata vikijibadili namna gani.

Wakati mwingine mfumo huu unakuwa na matatizo yake na unaweza hata kusababisha kushambulia chembe nzuri za mwili na kusababisha magonjwa.

Lakini kuna wakati mfumo wa kinga ya mwili unaweza kushambuliwa kiasi kwamba hauwezi kujirudisha katika hali ya kawaida. Katika hali hii mtu anajikuta anaugua na anapokwenda hospitali basi anapewa dawa za aina mbalimbali na hata kubadilishiwa chakula ili kuupa mwili kile kinachoitwa “boost” ya kuupa nguvu. Dawa na tiba za aina mbili zimegunduliwa ili kusaidia mwili kupambana na magonjwa na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Hata hivyo, mwili unapopoteza uwezo wa kujilinda kabisa basi unakuwa wazi kushambuliwa na kila aina ya magonjwa. Hali ya Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) ni ugonjwa mkubwa zaidi ambao unatishia wanadamu kwani mtu anayepoteza kinga mwilini anakuwa ni mtu asiye na ulinzi.

Hivyo, magonjwa nyemelezi (opportunistic diseases) na magonjwa mengine yanaweza kumvamia mtu na kumsababishia ugonjwa wa UKIMWI. Hadi hivi sasa ugonjwa huu hauna tiba.

Lakini, upo mchanganyiko wa madawa ambayo mtu anaweza kuyatumia kuupa mwili nguvu ya kupambana na magonjwa na mtu akitumia madawa hayo inavyopaswa na kwa wakati wote anaotakiwa basi anaweza kuupa mwili wake nguvu ya kupambana na magonjwa madogomadogo. Na akiwa katika madawa haya anaweza kutumia dawa za magonjwa nyemelezi na kuyashinda.

Usalama wa Taifa basi ni kitu cha namna hiyo. Taifa halitakiwi hata kidogo kuwa na Ukosefu wa Kinga za Nchi (UKINCHI) yaani hali ya taifa kukosa mfumo wa kiinteligensia ambao unafanya kazi ipasavyo, kwa wakati na kwa ukamilifu wake.

Baadhi ya mambo ambayo yanaendelea sasa nchini yanatudokeza tu kuwa kuna hali fulani hivi ya tatizo katika idara hii kiasi kwamba hata tunaogopa kuzungumzia au tunafikiria kuzungumzia ni uhalifu. Matokeo yake, wapo watu mitaani wanapita na kujitambulisha kuwa ni ‘watu wa usalama wa taifa” na wengine tunafikiria tunawajua kwa jinsi wanavyofanya mambo – yote yakiwa ni kinyume cha sheria ya idara hiyo.

Ni kutokana na hili na mengine mengi ambayo tumeyashuhudia miaka hii michache naamini ipo haja ya haraka ya kubadilisha muundo na mfumo wa idara hii ili kuitengeneza kuweza kukabiliana na changamoto za intelijensia katika taifa ambalo linajaribu kutengeneza mfumo wa kisasa wa maisha na kiuchumi.

Haja hii inatokana na ukweli mwingine kuwa tunaishi katika dunia mpya kabisa yenye changamoto ambazo miaka 10 tu nyuma hatuwa tunazifikiria.

Nikiongezea katika makala zangu za nyuma naweza kusema kuwa baadhi ya mabadiliko yanayohitajika tena kwa haraka kwenye taasisi hii ni haya yafuatayo:

Mkuu wa Idara ni lazima asailiwe na kupitishwa na Bunge

Kwa haraka nasikia mtu anasema “tusubiri Katiba Mpya”. Suala hili haliitaji Katiba Mpya; linahitaji mabadiliko katika sheria ya sasa. Kwa vile chombo hiki kinagusa kwa namna ya pekee maisha ya kila Mtanzania, kila taasisi na hata kugusa mahusiano yetu na mataifa ya nje hatuna jinsi isipokuwa kuhakikisha yule anayeteuliwa kuongoza taasisi hii anaelewa changamoto zinazotukabili na tuweze kuelewa misimamo yake mbalimbali.

Njia ya uhakika ya kufanya hivi ni kuhakikisha kuwa mtu anayeteuliwa na Rais kuongoza idara hii ni lazima asailiwe na kuthibitishwa na Bunge kwa kupigiwa kura kwanza kwenye Kamati husika na pia kwenye Bunge zima. Hili ni badiliko la kwanza na la msingi.

Idara yapaswa igawanywe

Mojawapo ya matatizo ambayo nayaona – kwa maoni yangu- ni kuwa idara hii imepewa majukumu makubwa lakini haijapewa muundo wa kukabiliana na majukumu hiyo.

Kwa mfano, baadhi ya vitu vinavyofanyika kama sehemu ya idara za ndani (departments) za TISS yangepaswa kuwa taasisi zinazojitegemea zikiwa na uongozi wake. Lakini kubwa zaidi ni ile haja ya kutengeneza kazi za ujasusi wa ndani na ujasusi wa nje ya nchi.

Mfano mzuri hapa ni mfumo wa Marekani au hata Uingereza na baadhi ya nchi zina taasisi zinazoshughulikia upepelezi na ujasusi wa ndani na vile vile taasisi zinazoshughulikia ujasusi na upepelezi wa nje.

Marekani ina taasisi kama CIA, NSA, FBI wakati Uingereza ina M16 na taasisi nyingine. Israeli ina taasisi kama Mossad (ya ujasusi wa nje) na Shin Bet, Nigeria ina National Intelligence Agency (ya nje) na State Security Services yenye kushughulikia mambo ya ndani.

Sasa hivi ukiangalia utaona kuwa pamoja na TISS taasisi nyingine zinazoshughulikia na upelelezi ni CID (chini ya Polisi ambayo inashughulika na upelelezi wa makosa ya jinai – si taasisi ya intelijensia) na Idara ya Intelijensia ya Jeshi (Military Intelligence).

Kuna uwezekano pia ipo taasisi nyingine ambayo haijatangazwa rasmi ambayo nayo inafanya kazi nchini – hili lisitushangaze. Hii tunaweza kuiita ‘Secret Service”.

Idara zote hizi hazina mfumo unaozisimamia kwa pamoja au ambao unalazimisha zifanye kazi kwa pamoja. Kwa bahati mbaya ni taasisi moja tu ambayo mkubwa wake anajulikana na imeundwa kisheria – TISS.

Ni muhimu kutenganisha na kuunda taasisi nyingine ambazo zitaongozwa kisheria kufuatana na mahitaji ya taifa.

Kugawanywa huku ni kwa ajili ya kufanya kazi kwa urahisi, kwa haraka na kwa weledi.

Watumishi wa Idara wafanye kazi kwa utaratibu unaoeleweka

Niliandika wiki kadhaa zilizopita kuwa baadhi ya watendaji wakuu wa idara ya TISS sasa hivi wameshapitisha muda wao wa kustaafu lakini bado wanaendelea na ajira.

Wengine tunadokezwa wanajaribu kila wawezalo waendelee kidogo hata kwa mkataba kwani hawako tayari kuachilia kazi. Na wengine japo wamepitisha muda wao wa utumishi wa umma wanaendelea kufanya kazi bila barua rasmi ya Rais ya kuwapa muda wa nyongeza.

Kuna watumishi karibu wa tano wa ngazi za juu ambao wanaendelea na ajira licha ya kupita muda wao wa utumishi serikalini. Hili si jambo jema, ni kuidhoofisha Idara kwani kunasababisha minong’ono isiyo ya lazima lakini pia inazuia watu wengine kupanda ngazi.

Ni muhimu watendaji wake wawajibishwe

Mojawapo ya mambo ambayo binafsi naamini yanahitajika ni kuhakikishwa kuwa watendaji wa idara hii wanawajibishwa ama na chombo kilichowateua au wanalazimishwa kuwajibishwa na wanasiasa.

Wengi mnaweza kukumbuka jinsi Mkurugenzi wa CIA huko Marekani alivyolazimika kujiuzulu baada ya mahusiano yake na mapenzi na mwandishi wa kitabu cha maisha yake ulipokuja kujulikana. Hakukuwa na uhalifu wowote lakini kashfa ile ilikuwa ni kubwa na haikujali utumishi wake wote uliotukuka jeshini – namzungumzia Jenerali Petreaus.

Kashfa kadhaa nchini zingetosha kuwawajibisha wakubwa kadhaa ndani ya Idara wanaodaiwa wamepitisha muda wa utumishi.

Kwa maoni yangu kati ya kashfa zote ni ile ya ndege ya kijeshi kuweza kuingia nchini usiku wa manane, kuchukua wanyama na kuondoka nao na hadi sasa hakuna kurudishwa huku idara ikiwa imelala usingizi. Huu ni Ukosefu wa Kinga Nchini!

Kashfa nyingine zinaweza kuwa ni nyongeza tu lakini ukweli ni kuwa kama lilivyo jeshi la polisi idara hii nayo inahitaji mabadiliko ya haraka.

Hata hivyo nitakuwa najidanganya nikisema kuwa naamini serikali ya CCM inaweza kufanyia mabadiliko idara hii; haiwezi. Kwa sababu moja kubwa inanufaika na udhaifu uliopo.

NI matumaini yangu kuwa kipo chama na watu ambao wanajua wanatakiwa kufanya nini endapo watashika madaraka ili hatimaye nchi yetu iwe na mfumo wa idara ya kijasusi ambao umeundwa kisheria, unazingatia maslahi ya taifa, unaheshimu haki za msingi za raia na za binadamu na ambao utendaji wake uko chini ya viongozi wa kiraia.

Tusubiri tuone.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *