Mabadiliko ya tabianchi ‘yavuruga’ wakulima mikoa ya Nyanda za Juu

Mbeya
Watumia sayansi, elimu ya jadi kukabili changamoto za tabianchi
Baadhi wahitaji mbegu za muda mfupi, wengine warejea mbegu za asili
Kilimo Uyole waja na mbegu zinazohimili ukame.

MIAKA ya hivi karibuni imekuwa michungu kwa wakulima wengi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, maarufu kwa “The big four,” pamoja na zao lao muhimu la mahindi.

Ni mikoa ambayo inatoa mchango mkubwa katika uzalishaji mazao ya chakula nchini. Pamoja na mahindi, yapo mazao kama mpunga, maharage, viazi mviringo na viazi vitamu, mboga mboga kama vile kabichi na hata mazao ya mafuta kama ufuta, alizeti na mawese.

Veremund Mfuse, kutoka katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ni miongoni mwa wakulima wenye kuonja machungu ya ukame unaoathiri uzalishaji wa zao la mahindi na mpunga wilayani humo.

Katika kipindi hiki ambacho nchi na dunia kwa ujumla imo katika mahangaiko kutokana na ongezeko la joto, mkulima huyu kutoka wilayani Mbarali amekuwa akishuhudia kushuka kwa uwezo wake wa uzalishaji mahindi, tatizo analosema linawakabili wakulima wote mkoani humo.

“Changamoto yetu kubwa wilayani Mbarali ni ukame, kuna upungufu mkubwa wa maji, mvua hazina uhakika tena, kipindi cha mvua kimepungua, kimekuwa kifupi, mpunga ulikauka kabla ya kukomaa, wengi hawakufikia malengo, tunavuna kidogo sana,” anasema Mfuse katika mahojiano yake na mwandishi wa makala haya.

Gulzar Sabir wa Rujewa wilayani Mbarali, naye anakubaliana na Mfuse kuhusu athari za ukame zinazowakabili wakulima wa mahindi na mpunga wilayani humo, anasema kuwahi kukatika kwa mvua kumeathiri sana kilimo cha mazao hayo mawili.

“Tatizo la mahindi hivi sasa huku Mbarali ni mvua, zinakatika mapema kwa hiyo mahindi yanakauka kabla ya kukomaa au hata kubeba, mbegu za muda mfupi ni nzuri zaidi, mvua zinapokatika mahindi yanakuwa tayari yamekomaa,” anasema Gulzar.

Katika kukabiliana na tatizo hilo la ukame, ambalo wataalamu wanasema linatokana na mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya wakulima wanatumia mbegu mpya za mahindi (hybrids), zenye kuhimili ukame, huku wengine wakifanya majaribio kurudi kwenye mbegu za asili.

Mbegu mpya za mahindi zenye kukomaa haraka

Mtafiti wa mazao kutoka Taasisi ya Kilimo ya Utafiti Uyole, Anold Mushongi amefanikiwa kutayarisha aina kadhaa za mbegu za mahindi zenye kutumia maji kidogo, zinazostawi kwenye udongo wenye rutuba kiasi na zenye kuhimili magonjwa.

Kwa mujibu wa Mushongi, uwezo wa mbegu hizo alizozizalisha ni mkubwa zaidi hususan katika hali ya ukame, ikilinganishwa na zile za wenyeji, kwamba zinatoa mavuno makubwa zaidi; kati ya tani nane hadi kumi kwa hekta moja wakati zile za wenyeji ni tani zisizozidi mbili kwa hekta.

Mbegu  hizo mpya zinakomaa katika kipindi cha siku kati ya 125 hadi 130, hii ikiwa ni chini ya takribani wiki tatu, kwa siku zinazohitajika mbegu za kawaida za mahindi kukomaa.

Mfuse, kwa upande wake, anasema aina hiyo ya mbegu za mahindi zinazotumia siku chache zaidi kukomaa ndizo hasa anazozihitaji kwa sasa.

“Mbegu zinazochukua siku nyingi kukomaa ni hasara (kwa hali ya hivi sasa). Tunahitaji mbegu zenye kuchukua muda mfupi zaidi kukomaa, ili kwamba pale mvua zinapokatika na mahindi yanakuwa yamekomaa,” anasema Mfuse.

Hivi sasa aina nne za mbegu hizo mpya, hybrids, ambazo zinaelezwa kufaa zaidi kwenye uwanda wa juu, zinalimwa katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma na Rukwa, ambayo iko kati ya meta 800 hadi 2,200 kutoka usawa wa bahari.

Mahindi ni zao kuu la chakula kikuu nchini, na takwimu za taasisi hiyo ya utafiti ya kilimo, zinaonyesha kuwa takribani asilimia 85 ya Watanzania wanategemea mahindi kwa chakula au kuishi.

Nusu ya mahindi yanayozalishwa nchini, kwa mujibu wa taarifa za taasisi hiyo ya utafiti, hutoka katika mikoa hiyo ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma, iliyoko katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na inafahamika kama “nation’s bread basket.”

Inaelezwa zaidi kuwa mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini inachangia takribani asilimia 90 ya mahindi yote yanayohifadhiwa na Hifadhi ya Taifa ya Nafaka (National Strategic Grain Reserve).

Katika miaka ya nyuma mikoa hiyo ilipata mavuno makubwa ya mahindi, tofauti na hivi sasa mavuno yameshuka kutokana na ukame, mvua zisizo za uhakika na kuongezeka kwa magonjwa ya mazao.

“Inaonekana mabadiliko ya tabianchi yanasababisha ongezeko la joto, hali inayosababisha kuibuka kwa insect pests, aina mpya za magonjwa kama vile maize streak fungus, magugu kama vile striga au kiduha kwa Kiswahili, yanayostawi maeneo ambayo udongo umepungukiwa nitrogen, haya yote yanaathiri sana mazao,” anasema Mushongi.

Hata hivyo, wakulima wanatambua pia kwamba tatizo la matumizi mabaya ya ardhi limechangia katika kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mathalani, Mfuse anasema kwamba uteketezaji wa miti ya asili kwa ajili ya kutengenezea mkaa, ufungaji unaozidi uwezo wa malisho, na kilimo cha kwenye mabwawa, kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji wakati wa kiangazi, kwamba ni shughuli zilizokuza tatizo la ukosefu wa maji.

Mbegu za asili katika kilimo

Wakati hatua zote zinazochukuliwa kukiwezesha kilimo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, zimeweka mkazo zaidi katika sayansi ya kisasa, baadhi ya wakulima katika mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini, hivi sasa wameona umuhimu wa kutumia mbegu za mahindi za asili, ambazo wanasema zinakabiliana vema zaidi na hali ya maeneo yao.

Miongoni mwa wakulima hao Leneth Motto, kutoka Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, ambaye anasema pamoja na wakulima kuendelea kupanda mbegu za hybrid kutoka nchini Kenya, bado wanapendelea zaidi mbegu zao za mahindi za asili ambazo hutumika zaidi kwa ajili ya chakula na zile za hybrid hupanda zaidi kwa ajili ya biashara.

“Mbegu za asili mahindi yake ni mazito, na yanakomaa mapema, ni mazuri kwa chakula, yanatoa unga mwingi ikilinganishwa na yale ya hybrid,” anasema Motto na kuongeza,

“Haya mahindi ya hybrid ni mazuri kwa kuuza, mahindi yake matamu, marefu, ukila ni laini, hybrid bei iko juu ukiuza mabichi, lakini yakikauka ni mepesi, yana pumba nyingi, ya asili ni rahisi tunatunza wenyewe na yanastahimili mabadiliko ya hali ya hewa.”

Kwa mujibu wa mama huyo mkulima, Taasisi hiyo ya Utafiti wa Kilimo Uyole inawasaidia kukabiliana na matatizo mbalimbali ya kilimo kutokana na tafiti zao.

Matokeo ya utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo, inayojishughulisha na utafiti, ikiwa na makao yake nchini Uingereza, yanabainisha kwamba elimu ya jadi kuhusu mbegu inaweka mwongozo wenye manufaa kwenye kilimo kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika ukanda wa Pwani nchini Kenya, mathalani, watafiti walibaini kuwa wakulima wengi wameamua kuzirudia mbegu zao za asili za mahindi, ambazo zimethibitika kuwa ni ngumu na bora zaidi katika kuhimili hali ya hewa isiyotabirika na magonjwa yapatikanayo kwenye maeneo yao.

Wakulima kutoka eneo hilo nchini Kenya wanapendelea zaidi mbegu zao za asili kuliko zile za kisasa kwa sababu ni rahisi, wanazipata kwa urahisi zaidi na ambazo wanasaidia miongoni mwao hapo kijijini na vijiji vya jirani.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya utafiti, watunga sera wanaonekana kutothamini jinsi elimu ya asili, kwa karne nyingi tu sasa, ilivyoweza kuzisaidia jamii za asili kukabiliana na ongezeko la joto pamoja na kubadilika kwa mazingira wanamoishi.

Hata hivyo, Mushongi anaamini kwamba, changamoto kuu inayokabili Tanzania katika suala la uzalishaji chakula nchini hivi sasa ni jinsi ya kuongea tija katika mazao ya kilimo, kwani kadiri idadi ya watu inavyongezeka na tabianchi inazidi kutotabilika.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.