Mabenki na taasisi za fedha zijitazame

KATIKA mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais John Magufuli, aligusia kidogo kuhusu matatizo yanayozikumba baadhi ya benki hapa nchini hivi sasa.

Kwa ufupi, Rais alieleza namna baadhi ya benki na taasisi nyingine zilivyokuwa zikifanya biashara katika namna ambayo sasa imeziletea matatizo.

Benki zimekutwa na matatizo ya namna mbili; mosi kufanya biashara kwa kutegemea fedha za serikali na pili kukopesha watu ambao hawana sifa za kukopeshwa. Wanasiasa wametajwa kuwa katika kundi hili.

Mapema kabisa, tuseme kwamba wanasiasa nao wanastahili mikopo. Kwa namna yoyote ile, hatudhani kwamba Rais Magufuli alimaanisha wanasiasa wasipewe mikopo.

Lakini, tunaamini kwamba baada ya maelezo yale ya Rais, benki sasa zitatimiza majukumu yake kwa weledi wa kiwango cha juu.

Badala ya kuangalia serikali na wanasiasa, tunaamini kwamba benki za Tanzania sasa zitaanza kubuni njia mpya zitakazowafanya wakulima, wafugaji na wajasiriamali wachanga waweze kupata mikopo hiyo.

Ni kweli kwamba benki zilitengeneza faida kubwa kwa kufanya biashara na serikali. Kimantiki, benki hizo hazikuwa na sababu ya kuhangaika na Watanzania masikini wakati fedha za serikali zipo.

Ni muhimu sana macho na masikio ya benki zetu yakaelekezwa kwa Watanzania walio wengi; mmoja mmoja na kwa kupitia vikundi vyao vya kuwawezesha kiuchumi.

Ni kwa namna hiyo pekee, ndipo Watanzania wataanza kuona faida ya kuwa na benki zaidi ya 50 katika nchi yao. Benki hizi zinatakiwa, kwanza kabisa, kuwasaidia wananchi walio chini.

Kama Tanzania itakuwa na watu wengi wenye uwezo wa kukopesheka, maana yake ni kuwa benki zitakuwa zimetengeneza idadi kubwa ya watu inaoweza kufanya nao biashara.

Ikifikia wakati huo, benki zetu hazitakuwa tena na sababu ya kutegemea fedha za dezo za serikali kujiendesha kwa faida.  Bila shaka, huo ndiyo utakuwa wakati ambapo gurudumu la maendeleo la nchi yetu litakuwa limepiga hatua nzuri.

Hili linawezekana kama benki zetu zitaamua kufanya uamuzi huu mapema iwezekanavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *