Mabingwa wafichua ‘kemikali’ hatari

WAKATI bado kukiwa na hali ya kutothibitishwa kitabibu Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameathirika kiafya kwa kupewa sumu au la, taarifa za awali zinabainisha kuwapo kwa ‘kitu’ kwenye ute ute (bone marrow) ndani ya mifupa yake, chenye uwezo wa kuzalisha kemikali zinazoshambulia chembe hai za ngozi, Raia Mwema, limeelezwa.

Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizotufikia kutoka vyanzo mbalimbali vya habari hospitalini Apollo, India, awali alipofikishwa nchini humo, jopo la madaktari bingwa walifanya uchunguzi na kubaini ‘kitu’ hicho kwenye ute ute ndani ya mifupa yake.

Hata hivyo, taarifa hizo zinabainisha kuwa baada ya kufanya utafiti wa kina, madaktari hao ambao miongoni mwao ni mabingwa wa kutafiti kemikali, walifanikiwa kubuni chembe nyingine za kudhibiti kemikali (kitu) zilizobainika ndani ya ute ute huo.

“Katika hali ya kushangaza, baada ya kubaini kuwapo kwa kemikali ndani ya ute ute wake na jopo la maprofesa ambao ni madaktari bingwa kufanikiwa kubuni namna ya kudhibiti hicho kilichogundulika, walishtushwa kemikali hizo kuwa na uwezo wa kuendelea kujizalisha na kuendelea kushambulia ngozi yake,” kinaeleza chanzo chetu cha habari kutoka hospitalini Apollo, nchini India ambako Dk. Mwakyembe alikwenda kutibiwa kwa mara ya kwanza.

“Kwa hiyo, walianza kazi ya kupambana na kemikali hizo zisiweze kuendelea kujizalisha na walipoona dalili za kufanikiwa walimruhusu kurejea Dar es Salaam, lakini wamechukua kemikali hizo kwa ajili ya uchunguzi zaidi. Sasa ni majopo ya kitabibu yanayokusanya maprofesa kadhaa ndiyo wanaoendelea na uchunguzi wa kina kubaini ni kemikali za aina gani, zimeingizwa vipi mwilini mwake.”

“Na sasa amekuja hapa India kwa ajili pia ya kuangaliwa maendeleo yake. je, kemikali zile zimefanikiwa kuangamizwa kama bado zimepungua kwa kiasi gani au bado zina uwezo wa kuendelea kujizalisha kama ilivyokuwa awali? Kwa hiyo, uchunguzi bado haujakamilika,” kinaeleza chanzo hicho chetu cha habari kutoka Apollo.

Kwa upande mwingine, mara baada ya kurejea kutoka India kwa mara ya kwanza alikokwenda kutibiwa, mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kuona baadhi ya picha za hali ya Dk. Mwakyembe na namna ngozi yake ilivyokuwa imeathirika, mwili ukiwa umevimba na ngozi kuchanika na kuwa kavu na ngumu na yenye magamba mithili ya ngozi ya mamba.

Ni wakati huo ambao, Dk. Mwakyembe mwenyewe alipata kumdokeza mwandishi wetu kwamba; “Hali ilikuwa mbaya sana alipokuwa India kwa matibabu kwa mara ya kwanza.”

Lakini kwa upande mwingine, wataalamu wengine wa kemia na baiolojia nchini kwa nyakati tofauti bila kutaka majina yao yaandikwe gazeti kutokana na namna suala la Dk. Mwakyembe linavyozungumziwa na viongozi wa taasisi nyeti nchini, wameelezea uwezekano wa kurutubishwa kwa kemikali za namna hiyo ili kushambulia baadhi ya chembe hai katika mwili wa binadamu na hatimaye kusababisha kifo cha mhusika na baadaye, kifo hicho kuaminika kimetokana na ugonjwa fulani.

Katika hatua nyingine, taarifa za “internet” zinabainisha kuwa kemikali za namna hiyo huweza kutengenezwa na wakemia sambamba na wanabaiolojia kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwadhuru watu mashuhuri kwa malengo mbalimbali.

Kazi za ute-ute (bone marrow) mwilini

Kazi kubwa ya ute uliopo ndani ya mfupa wa mwanadamu (bone marrow) ambao humo ndimo inaelezwa kuwa kemikali zinazomdhuru Dk. Mwakyembe zilipo, ni kuzalisha aina tofauti za chembe hai za damu ambazo ni muhimu kwa afya ya mwanadamu kwa ujumla.

Kuna aina mbili za ute huo katika mifupa ya mwanadamu ambazo ni kwanza; ute wa njano (yellow bone marrow) ambao umesheheni kiwango kikubwa cha chembe hai zenye mafuta (fat cells).

Lakini aina ya pili ni  ute mwekundu (red bone marrow) ambao hujumuisha chembe nyingine hai muhimu katika uzalishaji wa chembe damu mpya (new blood cells).

Kazi ya chembe damu na ute-ute

Ute mwekundu ndani ya mfupa (red bone marrow) na hasa katika mifupa mikubwa wajibu au kazi yake ya msingi ni uzalishaji wa shehena ya chembe damu hai mpya.

Ute ute huo unatajwa kujihifadhi katika mifupa ya mwanadamu hususan katika maeneo matano ya aina ya mifupa.

Mifupa hiyo ni; mosi, mifupa ya mkono (arm bones), pili; mifupa ya kifuani (breastbone); tatu, mifupa ya miguu (leg bones); nne, mifupa ya mbavu (ribs) na tano, uti wa mgongo (spine)

Kwa upande wa Dk. Mwakyembe, picha za mionzo zilizopata kuonwa na mmoja wa watu wake wa karibuni akiwa katika matibabu India zinadaiwa kuonyesha mifupa iliyoanza kuathiriwa kwa kuwa na alama za awali tofauti na mingine ni ya mifupa ya mikono kuelekea mifupa ya kifuani, na kwa hiyo, kama ni kitu (sumu?) kilichokuwapo kwenye ute wa mifupa yake basi kiliingia ,inawezekana kupitia viganja vya mikono yake na kupenya kwenye ute ndani ya mifupa ya mikono.

Dk. Mwakyembe na DCI Manumba

Kama vile mtu ambaye amekerwa na namna Jeshi la Polisi, kupitia kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, Dk. Mwakyembe Februari 18, wiki iliyopita, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kujibu kile kilichoelezwa na Manumba kuhusu afya yake.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, DCI alieleza bayana kwamba Dk. Mwakyembe hajalishwa sumu na kwamba kinachomsumbua ni ugonjwa wa ngozi tu, maelezo ambayo yamepingwa na Dk. Mwakyembe mwenyewe akisema kinachomsumbua bado hakijawekwa bayana na jopo la madaktari bingwa wanaomtibu India.

Taarifa hiyo ya Mwakyembe ilieleza : “Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.

“Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika barua  hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika). Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:

 1. Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya “wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo, nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
 2. Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza.
 3. Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia mikoa mingine!
 4. Ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.

Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe.  Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi? Si ni polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru,  wamekuwa wakikerwa na tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili lichunguzwe kwa kina?

Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti/kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!

Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.

Tuendelee kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

 

20 thoughts on “Mabingwa wafichua ‘kemikali’ hatari”

 1. Jackson Ringo says:

  Tatizo la nchi yetu kuwapa nafasi viongozi ambao hawana historia nzuri ya utendaji, pia huenda tatizo hili linasababishwa na katiba ya nchi yetu ambayo inatoa madaraka ya mtu mmoja kumteuwa kiongozi kushika nyazifa kubwa kitaifa bila kuwepo jopo la kuchunguza uwezo na dhamira ya kweli ya utendaji wa mhusika kwa mwenendo takriban miaka mitano  au kumi ya utendaji. Nashauri kuwepo na jopo la kuwahoji na kuwatathimi viongozi wanaochaguliwa na mamlaka ya juu ili kuondoa undugu, kulipana fadhila au kuendeleza rushwa kwa anaye chagua au kuchaguliwa.

 2. Robert Ndilla says:

  Hali na taarifa hii inatisha.

  Nchi hii tumwamini nani?Pole sana Mwakyembe,

 3. malika says:

  nimelia sana kwa hii habari masikini waziri mwakiembe hizi ni habari tukizisikia na kuziona kwenye michezo ya james bond 007 matumizi ya sumu kwa kijasusi kuuwa na njia ziko nyingi za kufikisha sumu inapotakiwa kuondosha mpinzani .pole sana nimesikia kuna kundi la mafia wa kigeni ambao kwa bei poa wanaweza kuingiza sumu yoyote kwa mwenye kuihitaji .inatisha na kusit\iktisha .mungu atakusaidia kutambua tatizo ni mwanzo wa ushindi.pole sana tutazidi kukuombea uzima  na afya njema

 4. mina says:

  hii ni hatari kwa nchi yetu. Pole sana Dr Mwakyembe,

  Njaa za watu wachache zinamaliza watu wenye mchango mkubwa kwa Taifa. Polisi ndiyo inashiriki kunagamiza Taifa. Time will tell na inaelekea ujambazi aliojitahidi kuukomesha RAis Kikwete alipoingia madarakani uliokuwa unaongozwa na mapolisi wenyewe umeanza kurudi. Tusipochukua hatua haraka tutarudi kule kule ambapo hata majumbani kwetu ja,mabazi atakuja na document anakwambia achia hii nyumba ni yangu.

 5. mwasakafyuka says:

  walochomfanyia Mwakyembe ni kitu kibaya sana hasa kwa wanadamu wa leo walioelimika,waliostaarabika na waliopevuka kiakili,lakini wajue nguvu ya MUNGU ni kubwa kuliko nguvu zote,na wajue MWAKYEMBE atatangulia lakini vita yake aliyoianzisha haitokwisha kamwe,yaani ndio kwanza mapambano yanaendelea.ALUTA CONTINUA.

 6. Joesoef P says:

  Pole sana Mheshimiwa Mwakyembe; tunamwomba mwenyezi Mungu azidi kukuimarisha na wale wote wanaokutibu waweze kupata ufumbuzi wa kuzuia virutubisho vya sumu kwenye ute ute mwilini mwako. Wapo wanadamu wanaofanya kazi kama kikundi au genge; lakini wakumbuke kuwa mwisho wa maisha yao hapa duniani hawatakusanyika kama kikundi au genge ili kuwajibika kwa matendo yao …

 7. Raymond shoo. Shinyanga. says:

  POLE BABA, POLE SANA MZEE WETU. Tunajua haya yote ni kuwa unatupigania watanzania na Tanzania kwa ujumla. Usife moyo na wala usikate tamaa, watanzania wote tuko pamoja nawe bega kwa bega kuukataa ufisadi, unyonyaji, uonevu,ugandamizwaji, ubepari na umaskini unaondelea hapa tanzania kwa sasa, tunakuombea Mwenyenzi Mungu akupe nguvu na ukapate kupona mapema Amen!!

 8. kanakanfumu says:

  Kimsingi,  hii ya Polisi ni hujuma dhidi ya wapinga ufisadi.

  Sijapata kuona polisi wazembe kama wa nchi yetu hii,hususani katika zama zetu hizi za'Chukua Chako Mapema. Ni aibu iliyoje kwa polisi kusubiri wapelekewa ushahidi mezani kama vile mlevi alivyo baa anasubiri kuletewa bia alizomwagiza baamedi.

  ni polisi hawahawa ambao wanapigiwa simu na raia kwamba kuna tukio la uharifu,lakini wao kwa makusudi wanajichelewesha kufika eneo la tukio hadi majambazi yanapoondoka ndiyo polisi nao wanafika na mikwara mbuzi.Katika hali hiyo haihitaji kupiga ramli kujua kuwa polisi nao ni wezi na inawezekana michoro hiyo ya matukio ya ujambazi wanaijua fika.

  ndiyo polisi wetu hao,Mwakyembe

 9. Malenga says:

  Mwakyembe kimsingi anavuna alichopanda. Maana kama siyo yeye na jopo lake waliochunguza Richmond kuficha ukweli juu ya nani walikuwa nyuma ya Richmond, haya yasingempata. Kwanza tungekuwa na serikali safi saa nyingine ikiongozwa na rais safi badala ya huyu mzururaji na kibaka wa kawaida. Hivyo basi Mwakyembe ajutie uroho wake wa kupewa cheo alicho nacho ambacho kimetumika kummaliza. Nadhani hili ni somo tosha kwa wengine wanaotumia nafasi zao kwa ajili mambo binafsi.

 10. Ralph says:

  Baada ya kufichua sakata la Richmond na kuonyesha udhaifu wa serikali, alikosea sana kukubali uwaziri wa serikali dhaifu ile ile! Pole sana Mwakyembe historia ndio imejiandika hivyo!

 11. Makongorosi says:

  Hali hii inatia uchunngu na kusikitisha sana, maana tulizoea kuona wenye fedha wakitumia z fedha zao kuangamiza masikini sasa ninajiuliza kama wameweza kumdhulu kigogo je sisi kina kajamba nani itakuwaje?

 12. Waltera Samuel Mairo says:

  Mwakyembe Hatokufa bali ataishi, sawa na neno la Mungu linasema. Wenye hil naye ndio watakaotangulia hasa wale wahujumu uchumi wa nchi hii, wanafikiri kwamba Mungu hawaoni wanalofanya; They will pay it kwa machozi no matter what and when!!! God bless Africa, bless Tanzania. Mungu mponye mtumishi wako Mwakyembe naye ataponyeka, muokoe naye ataokoka maana wewe ndiwe sifa zake in Jesus name. Jeremia 17:14

 13. Mussa omary ngogo says:

  Pole Mh Inaniuma sana kama nchi imefika wakati watu wakweli  hawatakiwi si nchi tena.

 14. Makotso Salia says:

  Hizo ni taarifa za kiinteligensia! Maskini polisi wanafanya kazi kama ya mpiga ramli? Iko wapi intelligentia hapo? Hivi intelligentia nini? Je watumishi hawa ni Intelligence kweli au ? Natafakari nashindwa kupata majibu!

 15. Emmanuel Sipiteck Olenjoro says:

  Pole sana Muheshimiwa,Dr.Mwakyembe kwa maradhi mabaya yanayo kuundama,na mungu akuponye.Ila shida yangu inakuja kwako,kwamba watu wanatoa information bila kuchunguza utafiti wakiscience.Je wewe unaposema vyombo vya habari vinatumwa au kushinikizwa na mafisidi,Huo ni ushahidi wakiscience pia au ni Tuhuma zakisiasa? au nizile fitina zawanasiasa uchwara? mimi sioni mantiki ya mtu anayeshindwa kuelekea kwenye utatuzi wa tatizo lake,nabadala yake anaelezea mambo yasio na msingi.Maana hatuitaji mlolongo wamatatizo.Tunaitaji kinachokusibu.

   

 16. Mutalemwa> says:

  Hivi kweli Tanzania tunahitaji kuuwa wasomi wetu eti kwasababu wamesema ukweli????? Kwanini tufanye hivyo jamani?  I envision Tanzania full of Zombies and illiterates who cannot critique, question or ask anything that is not going well. Hatukupaswa kumpa sumu Dk. Mwakyembe. that is the brain of Tanzania Kikwete ingilia kati. Bunge lako litaishia kujazwa na watu wenye Diplomas in cookery, among others na hawajui kinachoendelea. Kazi yao ni kutafuta sumu na kuuwa wasomi ambao wangesaidia Tanzania japo kupunguza umaskini kwa kuwafichua mafisadi.

  Mimi nilikuwa Police. watu niliojiunga nao karibu nusu hawakuwa na certificates za kwaruhusu wajiunge na Jeshi hilo.

  Where is the integrity of such an important pillar of the state??? Jeshi la police raia watauawa wataisha. watoa sumu watawageukia nanyi mtauwawa tu. Sumu haichagui mzee mwema.  Pole sana my brother mwakyembe. Kama mission aliyokupa muumba wako ya kuiokoa Tanzania toka mikonono mwa Mafisadi hujaikamilisha, hakuna atakaye kuua. watakutesa tu ila utaishi utimize kazi iliyo kuleta Duniani!!!!!!!

 17. Buhembo says:

  Hii Ni Hatari Lakini Mungu Ni Mkubwa Na katika kuonyesha Utakatifu wake kwa waja wake Haya yote yatakuja julikana kma mchezo wa Kuigiza.Pole Mr Mwakyembe Mungu yungali nawe, Na hakika Kwa Dhamra Yako Utaja Shinda Majkaribu Haya.

 18. mwita says:

  kama mwlimu mwakyembe kafanyiwa hivi na jeshi la polisi,  je hawa jamaa wakistaafu wataishi wapi, pale watakapokuwa hawana mamlaka katika jeshi hili wanalolingia. Tunasubiriana ngamani kama wao sasa hivi wako mwambani. Hakika hatutasahau  utesaji huu, tukipata nafasi tutafanya yale yaliyofanywa kwa NICOLAI SHEUSESCO wa ROMANIA

  Mambo hadharani tu, mpaka wabaya wajifunze, na kushuhudia kwa macho.labda waue ukoo wote

 19. Seif Athmani says:

  Kweli sisi wanainchi tunasikitishwa sana kwa afya ya mtetezi wetu Dr. Mwakyembe.Mimi nilidhani kwa maelezo haya RAISI angechukua hatua ya kuwafukuza wote waliotajwa kuhusika au kutomtendea haki Dr.Mwakyembe akianzia na IGP  Saidi Mwema na DCI.

  Na jeshi la polisi lote lingepanguliwa upya kwani mpaka sasa naona kuna hatari bado ya kumuwinda Dr.Mwakyembe.RAISI tunaomba uingilie kati kwani bado tunamuhitaji sanasana Dr.Mwakyembe ambaye ndiye  mkombozi wa sisi walala hoi.

 20. James says:

  inashangaza sana taifa letu limegeuka kuwa kitu cha ajabu, what are we killing each other for? injustice or justice? Kizazi hiki kinachochipuka leo kina namna moja tu ya kukiangamiza, si kwa vita ya mwilini bali rohoni. Jambo la kwanza la msingi ni kuhakikisha tunawang'oa viongozi feki wa dini (imposters) kabla hatujachukua hatua nyingine. Maana kama serikali yetu tunapoipa taarifa za uhalifu wakati wao ndio waharifu inabakia sehemu moja tu salama ya kuwashitaki ni kwa yule anaewapa uhai yaani MUNGU. hii inaweza kuonekana ni upuuzi kabisa lakini vita inayopiganwa bila kushika mtutu. na vita kali ambayo hakuna wa kuiamua isipokuwa walioianzisha. Nilisikia juzi tu kiongozi mkubwa wa nchi anatamba bila aibu, maana hatutakiwi kujivunia upuuzi, bali mema, anatamba eti CCM hakuna wa kuing'oa, KWELI? unaamini hilo? Muamal Gaddaf na utajili wote aliokua nao na ukuu wa ngome yake nani aliamini atakua kaburini leo. Labda kama raia mwema niseme hivi tuna wimbi la wachungaji na mapadre na maaskofu ambao pia ni mawakala wa serikali, pia lipo wimbi la mashehe ambao kiukweli si mashehe bali vibaraka wa mafisadi serikalini wapo katikati yetu kutuchimba mawazo yetu na kuifanya shughuli nzima ya haki kuwa ndoto. Hawa tunahitaji wote kuwatoa sadaka kwa shetani kwa unafiki wao, pili tunahitaji wapambanaji waaminifu watakao simama kidete kuhakikisha viongozi wote tulio wachagua kwa mapenzi yetu juu yao na wakatupa ahadi moto moto ikiwa hawazitimizi kama kufa na wafe, wote! tena hili tulifanye kwa machozi na kilio kwa kumaanisha. Hali ilipokuwa mbaya katika nchi ya misri wakati wana wa israel wakiwa utumwa hakukuwa na msaada kwao zaidi ya Mungu, Watanzania tunaonekana wote mataahira wa akili, mkianza jambo wanapitisha makombora mitaani ili kuwatisha muogope vita! hatuna haja kujifunza kutumia mtutu, tunaweza kuwagombanisha na alie waumba na kuwapa uhai huyo anajua vema namna ya kuwanyamazisha gafla wakiwa vitandani mwao kama wanavyofanya wao kwa kila mtetezi wa haki kama Dr. Mwakyembe, nimalizie kwa kusema Harrison Mwakyembe alitaka kushonwa tu mdomo lakini Mungu amempa nafasi amalizie alipoishia, na atafanikiwa hakika. maana tutakubeba mabegani mwetu kwa maombi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *