Machinga Mwanza wajibu bajeti ya serikali

WAFANYABIASHARA ndogo ndogo (machinga) mkoani Mwanza wameipongeza serikali kutokana na hatua ya kuwatambua rasmi wakiahidi kuiunga mkono katika kufanikisha bajeti yake kwa mwaka 2017/2018.

Katika hatua za mapato na maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali za bajeti yake ya Sh trilioni 31.7 kwa mwaka 2017/2018, serikali imeeleza kuwatambua rasmi wafanyabiashara ndogondogo wasio rasmi na wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.

Hao ni pamoja na mama lishe, wauza mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga na matunda ambapo serikali imeahidi kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazofanya.

Wakizungumzia hatua hiyo katika mahojiano na Raia Mwema jijini Mwanza mwishoni mwa wiki iliyopita, machinga hao wameishukuru serikali chini ya Rais Dk. John Magufuli na kuahidi kuipatia ushirikiano katika juhudi za kuinua uchumi nchini.

Pia wamempongeza Mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Stanslaus Mabula, wakiamini amechangia hatua hiyo ya serikali kwa kuwasilisha mahitaji yao bungeni.

“Tunaishukuru serikali kwa hatua hiyo ya kututambua kuwa sisi pia tunachangia mapato yake,” amesema Katibu Mtendaji Mkuu wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Moshi Maketa.

“Hatua hiyo ya serikali kututambua rasmi itatuhamasisha kuiunga mkono katika ukusanyaji kodi kupitia bidhaa tunazonunua madukani,” ameongeza.

Katibu wa Kamati ya Maafa ya Muungano wa Machinga mkoani hapa, Mazinge Hussein, amesema hatua ya serikali kuwatambua rasmi itawawezesha kufanya shughuli zao kwa uhuru na amani.

“Lakini pia hatua hiyo itaiondolea serikali matumizi ya fedha yasiyo ya lazima ya kugharimia operesheni za kuwaondoa machinga mijini.

“Tunaamini hatua hiyo ya serikali itazifanya taasisi za kifedha kurejesha imani na kuendelea kutukopesha fedha za mitaji ya biashara zetu,” ameongeza Hussein.

Katibu wa Kamati ya Ulinzi ya Muungano huo, Maulid Rashid, amesema hatua hiyo imedhihirisha dhamira nzuri ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli ya kutetea wananchi wa hali ya chini.

“Kimsingi bajeti hiyo ya serikali inatia moyo na kuonesha malengo chanya ya kuwaboreshea machinga maeneo ya kufanyia biashara. Tunaiahidi serikali kwamba tuko tayari kuijenga Tanzania ya viwanda,” amesema Rashid.

Nao mama lishe katika maeneo mbalimbali likiwamo la Sahara jijini Mwanza, Pamela Mushi, Angel Michael, Rose Bubele na Rukia Kennedy, wanaamini kwamba hatua ya kutambuliwa rasmi serikalini imewafungulia mlango wa mafanikio ya kiuchumi.

“Tutaoinesha serikali fadhila zetu kwa kuiunga mkono katika shughuli za maendeleo kuanzia kwa mbunge wetu, Mabula,” amesema Pamela.

“Tunaishukuru serikali kututambua rasmi kwani kazi zetu za mama lishe zinatusaidia kujipatia riziki ya kujikimu na familia zetu,” amesema Angel.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo, ameishukuru serikali akisema hatua hiyo imetimiza shauku ya muda mrefu ya machinga ya kuomba fursa ya kutambuliwa rasmi serikalini.

“Kwa hatua hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli na wasaidizi wake imeingia kwenye historia muhimu ya machinga,” amesema Tembo na kuendelea:

“Kutokana na hatua hiyo, ninatoa wito kwa machinga wote kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli na serikali yetu katika kuleta maendeleo ya jamii na taifa letu.

“Tunaamini hatua ya serikali ya kututambua rasmi itatekelezwa sambamba na kutuboreshea majengo na maeneo ya kufanyia biashara zetu.

“Kwa upande mwingine, tunavishukuru na kuvipongeza vyombo vya habari kwani vimechangia kutimia kwa ndoto hii ya machinga kutambuliwa rasmi serikalini.

“Pia tunamshukuru kwa namna ya pekee mbunge wetu, Mabula, kwani amekuwa karibu na sisi muda wote na tunaamini mafanikio haya ya machinga kutambuliwa rasmi serikalini yana mkono wake kutokana na kuwasilisha mawazo yetu bungeni.”

Kumwombea dua Rais 

Wakati huo huo, machinga jijini Mwanza wameahidi kuandaa hafla ya kumwombea dua Rais Magufuli kabla ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Hatuna kitu cha maana cha kulipa fadhila za Rais Magufuli, badala yake tunaandaa dua maalum ya kumwombea afya njema na maisha marefu,” amesema Tembo.

“Pia katika dua hiyo tutamwomba Mungu amjaalie Rais wetu John Magufuli mafanikio ya kuendeleza uongozi uliotukuka kwa Watanzania,” amesema Pamela Mushi.

Kumbukumbu muhimu

Jiji la Mwanza linakadiriwa kuwa na machinga zaidi ya 20,000. Desemba 3, mwaka jana wengi wao walivunjiwa meza zao na kushinikizwa kuhamia maeneo mbalimbali nje ya jiji, shughuli ambayo ilitekelezwa na vyombo vya dola, hususan askari polisi kwa ushirikiano na mgambo wa jiji.

Machinga waliokumbwa na hatua hiyo ni waliokuwa wakifanya biashara katika maeneo ya katikati ya jiji la Mwanza kama Makoroboi, Stendi ya Tanganyika, Dampo, Darajani, Sahara na barabarani.

Kuanzia siku ya utekelezaji wa amri ya kuhamishwa katikati ya jiji, machinga hawakuonekana kwenye maeneo yasiyoruhusiwa licha ya viongozi wao kutangaza awali kwamba hawataondoka.

Maduka mengi hayakufunguliwa katikati ya jiji kwa siku mbili mfululizo, yaani Desemba 3 na 4, mwaka jana kutokana na hofu ya kuzuka vurugu kati ya machinga na vyombo vya dola.

Karibu machinga wote walitekeleza amri hiyo ya serikali ya kuondoka katikati ya jiji bila shuruti hali inayosemekana iliokoa matumizi makubwa ya fedha, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya kukabiliana na ambao wangekaidi.

Hata hivyo, siku chache baadaye Rais Magufuli baada ya kusikia manung’uniko ya machinga hao aliagiza warejeshwe katikati ya jiji kuendelea na biashara zao hadi watakapoandaliwa maeneo rafiki ya kuendeshea shughuli zao hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *