UENDESHAJI wa shughuli za mandari (picnic) katika sehemu za wazi, kama vile ufukwe wa bahari, humruhusu kila mshiriki kufanya anachotaka, anavyotaka na katika muda anaotaka yeye; tena bila hofu ya kuhojiwa na mtu yeyote.
Lakini hivyo sivyo mambo yanavyopaswa kuwa katika uendeshaji wa taasisi rasmi. Katika taasisi rasmi kama vile TANESCO, TTCL, CRDB, TANGO, Bunge, Wizara za serikali, Mawakala wa Serikali, na Ikulu ya nchi, shughuli za kila siku huendeshwa, na lazima ziendeshwe, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazowawezesha watu kujua kesho patatokea nini. Hivi ndivyo kanuni ya utawala wa sheria inavyotamka.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba kanuni ya utawala wa sheria haizingatiwi mara zote na Ikulu ya Tanzania. Na kibaya zaidi, jambo hili linaruhusiwa kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na bunge letu.
Yaani; katika Tanzania ya leo, Rais anayo madaraka makubwa sana kiasi kwamba anaweza kufanya uamuzi wa kuajiri na kutimua mtumishi wa umma bila kutoa sababu yoyote na bila uwezekano wa kuhojiwa na chombo chochote hapa nchini. Na kama kuna mtu ambaye haamini maneno haya, hebu autazame ushahidi ufuatao:
Madaraka ya Rais wa Tanzania Juu ya Watumishi wa Umma
Kulingana na Katiba ya Tanzania (1977) katika ibara ya 34 (4), 35(1) na 36(1) mamlaka ya Serikali ya Tanzania yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe au kwa njia ya Rais kutoa kasma ya madaraka yake kwa watu wengine ambao ni watumishi wa umma, ambapo watumishi hawa watatekeleza kazi zao kwa niaba ya Rais.
Kwa kuzingatia vifungu hivi vya Katiba, mwaka 2002 Bunge la Tanzania lilitunga Sheria ya Kuratibu Ajira na Mahusiano ya Kazini Kwenye Sekta ya Umma (Public Service Act No. 8 of 2002).
Na yafuatayo ni maudhui ya sheria hii ambayo, kwa namna moja au nyingine, yanaruhusu kukiukwa kwa kanuni ya utawala wa sheria katika sekta ya umma:
Awali ya yote, Rais anayo mamlaka ya kuteua Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni Mkuu wa watumishi wa umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri (ib. 4 (1)); anayo mamlaka ya kuteua, kupandisha cheo, kusitisha mkataba wa ajira, kubatilisha uteuzi, kuhamisha na kutimua wafanyakazi wafuatao:
Mkuu wa watumishi wa umma, Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu wa Baraza la Mawaziri, Makatibu wakuu wa Wizara mbalimbali na wasaidizi wao, Wakuu wa Taasisi ambazo ni Mawakala wa Serikali, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, na Mabalozi (ib. 5 (1) (a-c)).
Pia, Rais anayo mamlaka ya kuteua idadi nyingine yoyote ya watumishi wa umma kujaza nafasi ambazo zinatambuliwa kwa mujibu wa sheria ya bunge. (ib. 5 (3)); anayo mamlaka ya kuteua wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma, na mwenyekiti wa tume hii. (ib. 9(1); na anayo mamlaka ya kuwaondoa wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma ofisini. (ib. 9 (7) (b) & 9 (10)).
Vile vile, Rais anayo mamlaka ya kumteua Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma (ib. 14 (1), anayo mamlaka ya kuanzisha kurugenzi, idara, vitengo, vijitengo na kamati mbalimbali za Tume ya Utumishi wa Umma. (ib. 15 (2)), na anayo mamlaka ya kuidhinisha ripoti ya mwaka ya Tume ya Utumishi wa Umma ichapwe au kuwekwa wazi katika mchakato wowote wa kisheria (ib. 17).
Kadhalika, Rais, kwa mujibu wa kanuni na taratibu maalum, anayo mamlaka ya kutoa kasma ya madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya 36 ya Katiba ya nchi (ib. 21(1) (a), anayo mamlaka ya kutoa kasma ya madaraka yake kwa mtumishi yeyote wa umma au ofisi yoyote ya umma (ib. 21 (b), na anayo mamlaka ya kutoa idhini kwa Tume au mtumishi yeyote wa umma ambaye tayari anayo kasma ya madaraka toka kwa rais, kusimamia shughuli za watumishi wa umma ambao rais anayo mamlaka juu yao (ib. 21(2)).
Aidha, Rais anayo mamlaka ya kumwondoa mtumishi yeyote wa umma kutoka katika utumishi wa umma katika Jamhuri ya Tanzania endapo rais anaona kwamba kufanya hivyo kunalinda maslahi ya umma (ib. 24 (1), anayo mamlaka ya kutoa amri ya kumtaka mtumishi wa umma aandike barua ya kustaafu au amri ya kuitaka mamlaka husika kumfukuza kazi mtumishi yeyote wa umma (ib. 25(2) (a) & (b)); na anayo mamlaka ya kuthibitisha, kubadilisha, na kubatilisha uamuzi wowote uliofanywa mamlaka ya kinidhamu dhidi ya mtumishi wa umma; na anao uamuzi wa mwisho kuhusu rufaa zote zinazohusu watumishi wa umma zitakazomfikia (ib. 25 (1) (a) & (d)).
Lakini sio hivyo tu. Kwa mujibu wa sheria ya ajira katika utumishi wa umma, Rais pia, kwa mujibu wa kanuni na taratibu maalumu, anayo mamlaka ya kusikiliza rufaa za kesi zingine mbali na zile zilizotajwa katika kifungu cha 23 (ib. 25 (e), na anayo mamlaka yasiyoweza kuhojiwa na mtu yeyote au chombo chochote pale anapofanya maamuzi kwa mujibu wa ibara ya 36 ya Katiba ya Tanzania 1977 (ib. 32 (2) (a-b).
Ubaya wa madaraka makubwa mikononi mwa Rais wa nchi
Hayo ndiyo madaraka yaliyo mikononi mwa Rais wa Tanzania. Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba wapiga kura ndio waajiri wakuu katika nchi, ambapo rais ni mwajiriwa mmojawapo, inafuata kimantiki kwamba; wapiga kura wanayo haki ya kuhoji maamuzi na matendo ya mtumishi wa umma yeyote, na rais akiwemo.
Uzoefu wangu kama mhadhiri katika masuala yanayohusu “Usarifu wa Biashara” (Business Administration) na “Mawasiliano Sanifu” (Technical Communication), unanifundisha kwamba; nchi yoyote iwayo, na Tanzania ikiwemo, inaongozwa kwa kuzingatia utaratibu rasmi katika mipaka ya “muundo wa uongozi” (Organizational Structure) uliopo kwa mujibu wa sheria halali.
Muundo wa uongozi hufafanua nani anafanya nini, nani anaripoti kwa nani, na taratibu rasmi za kazi. Kimsingi, muundo huu huwa ni matokeo ya mchakato wa kubainisha na kutofautisha kazi zitakazofanywa, kufafanua na kutoa kasma ya majukumu na madaraka, na kuweka kanuni za mahusiano kwa ajili ya kuwawezesha watu kufanya kazi kama kikundi na kwa kasi ili kufanikisha malengo ya pamoja (organizing process).
Kwa ujumla, mchakato wa kusuka muundo wa uongozi hutoa majawabu kwa maswali sita yafuatayo:
Swali la kwanza linahusu “mgawanyo wa majukumu” (“work specialization” or “work differentiation” or “division of labor”) nalo ni hili: Ni kwa kiasi gani na kwa kuzingatia kanuni gani kazi zimegawanywa katika kurugenzi, idara, vitengo na vijitengo tofauti?
Swali la pili linahusu “mnyororo wa kasma ya madaraka na majukumu” (“chain of delegated responsibilities and authorities” or “chain of command”) nalo ni hili: Nani anayetoa kasma ya majukumu na madaraka kwa yupi?
Katika kujibu swali hili, majibu manne tofauti huweza kutolewa. Kama mkuu wa nchi anapokea kasma ya madaraka moja kwa moja toka kwa mungu, basi, huo ni mfumo wa kifalme.
Kama mkuu wa nchi anapokea kasma ya madaraka kutoka kwa wananchi katika namna ambayo inamfanya yeye kuwa kitovu cha mfumo wa utawala, huo ni mfumo wa kirais (“presidential system of democracy”).
Kama mkuu wa nchi anapokea kasma ya madaraka kutoka kwa wananchi katika namna ambayo inalifanya bunge kuwa kitovu cha mfumo wa utawala, huo ni mfumo wa kibunge (“parliamentary system of democracy”).
Na kama mkuu wa nchi anapokea kasma ya madaraka kutoka kwa wananchi katika namna ambayo inazifanya mahakama kuwa kitovu cha mfumo wa utawala, huo ni mfumo mwingine.
Swali la tatu linahusu “jukwaa la uwajibikaji” (“forum of accountability”) kwa kwa kila mwajiriwa nalo ni: Liko wapi jukwaa la uwajibikaji kwa kila mwajiriwa?
Katika kujibu swali hili, majibu mawili tofauti yanawezekana. Kwanza yule aliyetoa kasma ya madaraka anaweza kuwa ndiye jukwaa la uwajibikaji. Na pili, yule aliyetoa kasma ya madaraka anaweza pia kuwa ameteua jukwaa la uwajibikaji pia kwa niaba yake.
Swali la nne linahusu “wigo wa madaraka” (“span of control”) aliyo nayo kiongozi, nalo ni: Ni watu wangapi wanaoripoti kwa bosi mmoja?
Swali la tano linahusu “vitovu vya maamuzi” (“centers of decision-making authority”) nalo ni: Vitovu vya uamuzi katika taasisi vimejikita wapi?
Na swali la sita linahusu “urasimu” (“formalization”), kwa maana ya wingi wa sera, sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza maamuzi na matendo ya waajiriwa nalo ni: Kuna urasimu kwa kiasi gani katika taasisi?
Hitimisho na mapendekezo kwa wapiga kura
Kutokana na yaliyosemwa hapo juu kuhusu mchakato wa kufuma muundo wa uongozi, ni wazi kwamba Tanzania sio dola ya kifalme. Kwa hiyo, madaraka ya rais yanatoka kwa umma.
Na hii maana yake ni kwamba rais ni mwajiriwa anayepaswa kutoa taarifa ya utekelezaji kwa mabosi wake (wapiga kura) ama kwao moja kwa moja au kwenye majukwaa ya uwajibikaji yaliyoteuliwa na wapiga kura.
Hivyo sio sahihi kusema kwamba utekelezaji wa madaraka ya rais, kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha Katiba ya nchi, haupaswi kuhojiwa na yeyote.
Pia, ni wazi kwamba wigo wa madaraka ya rais ni mpana sana kama ambavyo muundo wa uongozi wa nchi ni mrefu sana; kiasi kwamba hawezi kumudu vizuri kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya watu anaowateua.
Mwaka 2005 Rais aliahidi kuzipitia na kuziboresha sheria zote zinazopingana na kanuni za utawala bora. Ibara ya ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 inathibitisha kauli hii.
Hivyo, katika kampeni zitakazoanza hivi karibuni, nawahimiza wapiga kura wote kumwuliza Rais Kikwete aeleze ni kwa nini hajaifanyia marekebisho Sheria ya Ajira za Watumishi wa Umma, na kwa kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kupitia sanduku la kura kwa sababu ya uzorotefu huo.
Lakini si hivyo tu. Pia vyama baki vya ushindani yafaa vikaulizwa viseme vina mikakati gani ya kuondoa kasoro hii katika Sheria ya Ajira za Watumishi wa Umma.
Ni lazima vyama vya siasa vitueleze muundo wa uongozi wa nchi vitakaouzingatia mara baada ya Uchaguzi wa Oktoba iwapo kitashinda uchaguzi.
Toa maoni yako