MJADALA mkubwa duniani ni kuhusu kiongozi aliyetawala Libya kwa miaka 42, Muammar Gaddafi. Kiongozi huyu aliyeuwawa siku chache zilizopita huko Sirte, chini Libya, yapo mengi yanayojadiliwa juu yake ikiwamo mabishano kama alistahili kuuawa jinsi ilivyofanyika juma lililopita.
Upo upande unaoamini kuwa, kwa jinsi inavyosadikiwa kuwa ameifanyia mambo makubwa ya kimaendeleo nchi yake, hakustahili kulipwa fadhila kwa kuuawa namna ile; huku hoja kubwa ya upande huu ikichagizwa na madai kuwa kuangushwa kwa utawala wa Gaddafi na hadi kuuawa kwake kumefanywa kwa malengo ya kunufaisha nchi za magharibi kama Marekani na washirika wake.
Kwamba, kwa mwamvuli wa majeshi ya NATO yaliyoingia Libya kuwasaidia ‘waasi’ ili kuipata ‘demokrasia’, kulikuwa na cha ziada kinachotafutwa. Cha ziada hiki ni utajiri wa mafuta iliopo Libya. Kumtoa Gaddafi kunaweka njia rahisi ya kuweza kunufaika na mafuta haya.
Ipo hoja nyingine inayoshutumu vikali maamuzi haya yote ya kuung’oa utawala wa Gaddafi hadi kumuua. Kwamba haya yote ni kinyume na sheria za kimataifa na haki na uhuru wa ndani wa nchi yoyote duniani. Walio na maamuzi ya ama kumtoa kiongozi wao na kumuweka mtu mwingine madarakani ni wananchi wa nchi husika.
Hata mauaji yake yalivyofanyika yanapingwa vikali. Kwa mtindo uleule aliouawa Osama Bin Laden, ndivyo vivyo hivyo wauaji wa Gaddafi walivyofanya; wamehukumu na kutekeleza hukumu wao wenyewe. Hii ni dhihaka kwa utawala wa sheria. Ni dhihaka kwa wale wote wanaojidai kusimamia haki ya mtu kutokuwa na hatia mpaka pale mahakama itapojiridhisha na kudhihirisha hivyo.
Mmojawapo ya wanaopinga namna mauaji ya Gaddafi yalivyofanyika ni Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin ambae katika ziara yake ya kiserikali nchini Dermark katika siku za hivi karibuni amekuwa akiuliza swali kuwa “ni nani hasa aliwapa ruhusa majeshi ya NATO kumuua Gaddafi?”
Na ndio maana, kama kuna ushahidi wa kiongozi kukiuka haki za binadamu akiwa madarakani kama vile kufanya mauaji ya raia, kuna mahakama kama vile ile ya uhalifu ya kimataifa (ICC), The Hague, nchini Uholanzi ambazo ni sehemu muafaka kupelekwa.
Lakini upo upande unaoendelea kuuunga mkono matukio haya yote: kuanzia uamuzi wa wababe wachache wa dunia kuamua kuingia Libya kwa hoja ya ‘kuwasaidia wa-Libya kumtoa Gaddafi hadi madarakani na hadi kumuua. Wanaotetea hili wanasema hapakuwa na njia nyingine zaidi ya hizo zilizotumika kumwondoa dikteta aliyejiimarisha kwa muda mrefu, huku akiwapoteza wapinzani wake’.
Kufuatana na mitazamo hii miwili tofauti, dunia imegawanyika. Mgawanyiko huu umezikumba pia nchi za Umoja wa Afrika (AU) tangu wakati ule waasi walipoanza kusaidiwa na majeshi ya Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO). Hata hivyo, kilicho dhahiri ni kuwa nchi hizi zimekuwa zikitoa misimamo yake juu ya jambo hilo ama kwa kujifichaficha au kwa kuamua kukaa kimya na kunung’unika pembeni.
Ni kwa sababu hii, ndipo tumeshuhudia, nchi kadhaa, ikiwemo Tanzania kwa kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakipiga kelele sasa baada ya Gaddafi kuuawa. Membe amenukuliwa na vyombo vya habari akilaani vikali namna Gaddafi alivyouawa. Na kwa maneno mengine, Membe pia ameonesha kutounga mkono matukio haya yote yalivyofanyika dhidi ya Gaddafi.
Yapo maswali yanayoulizwa juu ya maamuzi kama haya ya kutoa misimamo baada ya matukio kutokea. Kwamba hii inadhihirisha uoga uliowajaa viongozi wengi kwa kushindwa kujipambanua mapema katika kile wanachokiamini. Uoga huu unatokana na ama kunufaika kwa namna moja au nyingine kutokana na utawala mbovu wa hao ambao wanatakiwa wawakemee.
Sababu nyininge ya kukaa kimya na kusubiria hatua za mwisho ndipo viongozi wetu waongee (mathalani mpaka pale Gaddafi alipouawa), ni kuhofia hali walizo nazo watawala hawa. Mfano, kama ni kuwakemea viongozi wanaofanya madudu ya kuminya demokrasia, inakuwa vigumu kwasababu wengi wa viongozi wanakuwa na matendo yaleyale;
Viongozi hawa wanakuwa na kigugumizi cha kukemea maovu ya viongozi wenzao kama ule mfano ulio katika Biblia pale Wayahudi waliomkamata mwanamke mmoja kwa kosa la uzinzi, walipompeleka kwa Bwana Yesu wakimjaribu kama ataridhia apewe adhabu ya kosa hilo kwa mujibu wa sheria za Kiyahudi, yaani kupigwa mawe. Tunasimuliwa kuwa Yesu aliwaambiakuwa ‘asiye na dhambi na awe wa kwanza kumtupia jiwe mwanamke huyo.’ Hata hivyo kilammoja aliondoka zake, ikiwa dhahiri kuwa hakuna aliyekuwa msafi (asiye na dhambi).
Tukiachana na mitazamo inayoendeleza ubishi juu ya yaliyofanyika dhidi ya Gaddafi, ukweli na uhalisia unaobakia ni kuwa: zama za Gaddafi zimekwisha; lakini wapo viongozi walio mithili ya Gaddafi. Na swali linabaki kuwa je, ni nani atafuata baada ya Gaddafi? Au kwa maneno mengine, baada ya somo hili la Gaddafi, kuna hatua gani wananchi wa nchi mbalimbali za dunia, hasa Afrika, watawachukulia viongozi walio mithili ya Gaddafi?
Wakati nikitafakari kuhusu maswali haya siku chache zilizopita katika juma ambalo Gaddafi aliuawa, kuna Rais mmojawapo wa nchi za katikati ya bara la Afrika akawa amekuja kuitembelea Afrika Kusini. Yaliyojadiliwa kuhusu Rais huyu, ambayo yalifunua zaidi uelewa wangu kuhusu kiongozi huyu wa nchi yenye eneo la kilometa za mraba zipatazo 28,000 tu yalinishtua.
Ieleweke kuwa, lengo langu hapa si kupendekeza kuwa huyu ni mmojawapo ya watu wanaopaswa kuchukuliwa hatua kama zilizochukuliwa dhidi ya Gaddafi. Lengo langu ni kushirikisha namna viongozi wetu na matendo yao yanavyoweza kuwa ni ya kutisha na kuwa dhahiri kinyume na misingi ya kawaida ya kiuongozi.
Huyu si mwingine, bali ni Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Guinea ya Ikweta. Wakati akijitapa kuwa nchi yake ina utajiri mkubwa wa mafuta, hata kufikia hatua ya kuialika Afrika Kusini kufanya biashara nayo kwa kwenda kuchuma na kufaidi utajiri huo nchini kwake, Rais huyu amekuwa akishutumiwa vikali na wanaharakati kama mmojawapo ya viongozi wanaoongoza kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Huku nchi yake ikiwa imefikia uwezo wa kukusanya mapato yafikiayo dola za kimarekani bilioni 4 kwa mwaka, chanzo kikuu kikiwa utajiri wa mafuta, wanaofaidi matunda haya ni watu wachache. Asilimia kubwa ya wananchi wake ni masikini. Takwimu za hivi karibuni (Julai, 2011), zinaonesha kuwa Guinea ya Ikweta ina idadi ya watu wapatao 668,225.
Kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya kutetea haki za binadamu, Human Rights Watch, mtu mmoja kati ya watu watatu nchini Guinea ya Ikweta hufariki kabla ya kufikisha miaka 40. Lakini kwa mujibu wa orodha ya mwaka 2006 ya jarida la Forbes-jarida litoalo mara kwa mara orodha ya watu matajiri zaidi duniani, Rais Obiang ni wa nane kwa utajiri kati ya viongozi matajiri duniani; akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola za kimarekani milioni 600.
Kama ilivyokuwa kwa Rais Hosni Mubarak wa Misri na Muammar Gaddafi wa Libya, Rais Obiang aliingia madarakani mwaka 1979 baada ya kumpindua anayetajwa kuwa Dikteta mwingine wa nchi hiyo Rais Fransisco Macias Nguema. Inakadiriwa kuwa, zaidi ya watu 100,000 waliokuwa wapinzani wa utawala wa Dikteta Nguema waliuawa au kukimbilia uhamishoni.
Haid hivi sasa Rais Obiang amekuwa madarakani kwa miaka zaidi ya 32; inaelezewa pia kuwa amekuwa akimshrikisha na kumrithisha utajiri wake mwanae wa kiume Teodorin, ambaye inadaiwa anamwandaa kurithi kiti chake hicho cha Urais.
Teodorin, pamoja na kuwa waziri wa kilimo katika serikali ya baba yake, akipata mshahara wa dola za kimarekani 5000 kwa mwezi (karibia shillingi za kitanzania milioni 8), anadaiwa kuwa mfujaji mzuri wa fedha kwa kununua na kumiliki magari mengi ya kifahari, majumba kadhaa likiwemo mojawapo lililo Paris, Ufaransa. Pia anadaiwa kufuja fedha kwa ‘tafrija’ na kuwafurahisha marafiki zake sehemu nyingi duniani.
Lakini kilichowahi kushtua zaidi ulimwengu kuhusu Rais Obiang ni madai yaliyotolewa na mpinzani wake mkubwa wa kisiasa, Severo Moto, mwezi Machi mwaka 2004 kuwa Rais Obiang ni mla watu (cannibal), na kuwa ‘huwa anawala maadui zake wa kisiasa anapowaua”.
Madai hayo yaliyotolewa na Moto alipokuwa akihojiwa na Radio moja nchini Uhispania hayajawahi kukanushwa na serikali ya Obiang;Moto alilisitiza kuwa asingeweza kurejea Guinea ya Ikweta kwani angeuawa pia, akidai kuwa Kamishina mmoja wa jeshi la polisi nchini humo aliuawa na kuwa alizikwa bila ya baadhi ya sehemu zake za siri pamoja na ubongo.
Rais Obiang hata hivyo amefanya jaribio la kujisafisha kwa jamii ya kimataifa dhidi ya shutuma hizi; ambazo pia ziliwahi kutolewa dhidi ya dikteta wa Uganda Idi Amini Dada kuwa nae alikuwa akila nyama za watu. Rais Obiang alitoa ‘ofa’ kwa Taasisi ya Elimu ya Umoja wa Mataifa (Unesco) ianzishe tuzo ya utafiti wa sayansi ya Uhai kwa jina lake; Obiang alikuwa amehiari kutoa dola za kimarekani milioni 3 kudhamini tuzo hii. Hata hivyo Unesco imekataa ‘ofa’ hii.
Rais Jacob Zuma wa nchini hapa ‘ameiponda’ Unesco kwa kukataa udhamini huu, huku akiita uamuzi huo ni wa kiupendeleo. Kwa mujibu wa Zuma uamuzi wa Unesco unadhihirsha jinsi dunia ilivyo na upendeleo, labda angekuwa Rais mwingine-mfano asiye wa Afrika kama Obiang, ‘ofa’ hiyo ingekubaliwa.
Hii ndio misimamo ya viongozi wetu. Leo hii Zuma anamtetea Obiang kuhusu ofa yake kwa Unesco; lakini anasahau kuhoji ni kwa kiasi gani wananchi masikini katika nchi tajiri ya Guinea ya Ikweta wanafaidika vipi na utajiri wa rasilimali ya mafuta yaliyo nchini kwao.
Zuma alipaswa kumshauri Rais Obiang kuwa badala ya ofa hiyo kuelekezwa Unesco kwa sasa, ingehakikisha kwanza wananchi wa Guinea ya Ikweta wanapata huduma za kijamii kwa maendeleo yao; na si kama ilivyo sasa ambapo wanaonufaika na utajiri uliopo nchini humo ni walio wachache.
Hawa ndio aina ya viongozi tulionao. Wanaothamini kupata sifa zaidi kimataifa na kwingineko kwa matendo kama hayo ya kutoa ‘ofa’ au kuzawadiwa tuzo wao wenyewe; lakini wananchi wanaowaongoza wakiendelea kutaabika katika lindi la umasikini.
Tulianzia na mjadala wa Gaddafi; tujiulize viongozi wetu wengine katika nchi zetu wana usafi kiasi kuweza kushutumu au kukemea matendo maovu ya viongozi wenzao. Au ndio wanasubiri wengine watolewe madarakani au hata kuuawa kama Gaddafi, ndipo wanapaza sauti zao ‘kuchomoza’ misimamo yao!
Toa maoni yako