Makala
Madini yetu, damu zetu!
Paul Dotto
Afrika Kusini
Toleo la 189
8 Jun 2011

MOJA ya filamu maarufu kuhusu Afrika zilizotoka miaka ya hivi karibuni ni ile inayoitwa Blood Diamonds. Filamu hii imeakisi maisha na hali ilivyokuwa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone mwaka 1996-1996; huku wahusika  wakuu katika mgogoro wakiwa waasi na serikali (jeshi) ya nchi hiyo. Filamu hiyo inasisimua, na ni kielelezo cha matatizo na migogoro mingi katika nchi zetu za Afrika.

Matatizo hayo ambayo waathirika wake wakubwa ni wananchi wa kawaida waliozungukwa na umasikini wa kutupwa ni matokeo ya uchu wa madaraka, ubinafsi na unafiki wa baadhi ya, ama wananchi mmoja mmoja au watawala wa nchi hizi.

Nchi za dunia ya kwanza kwa namna moja ama nyingine pia zimekuwa chanzo cha matatizo haya yanayowakumba Waafrika waliofanywa wahanga wa mifumo mingi iliyo duni.

Filamu hii ikiwa na matukio mengine yanayosononesha sana ikiwemo lile la askari waasi kuwakata mikono wananchi katika vijiji ili wasipige kura katika uchaguzi, imebeba jina la ‘almasi za damu’.

Jina hili linaelezewa kusadifu jinsi almasi zinazochimbwa maeneo mbalimbali ya (vilipokuwa) vita katika Afrika ili kufadhili migogoro au mapigano kwa upande mmoja; huku zikitajirisha ‘mabwana wa vita’ na makampuni yanayoendesha biashara ya almasi duniani kwa upande mwingine.

Lakini kubwa zaidi linalooneshwa wazi wazi na kwa namna isiyo wazi kwa pamoja katika filamu hii, ni thamani ya maisha au uhai wa mwanadamu ulivyodhalilishwa kama kitu kisicho na maana yoyote ikilinganishwa na utajiri, madaraka na hadhi binafsi (status).

Huku matukio mengi yakiwa yamemzunguka mmojawapo wa wahusika wakuu wa filamu, kijana mvuvi Solomon Vandy (Djimon Hounsou), baada ya kutekwa na waasi na kunusurika kukatwa mikono, anapelekwa kunako sehemu waasi wanaposimamia uchimbaji wa almasi na kuziuza kwa wateja wao wakubwa - wengi kutoka nchi za Ulaya na Afrika Kusini.

Bahati ya mtende inamwangukia tena Solomon baada ya eneo alipo kuvamiwa na majeshi ya serikali na kuwakamata waasi na mateka wao (kina Solomon).

Solomon anafanikiwa kwa siri kuhifadhi kwa kukichimbia ardhini ‘kidonge’ kikubwa cha almasi ya zambarau wakati waasi wakipambana na jeshi la serikali.

Kitendo hicho anakiona kiongozi wa waasi, Kapteni Poison ambaye anapiga kelele kuhusu hilo wakati anapelekwa korokoroni, lakini Solomoni anakana.

Hata hivyo; kijana Mzungu mzaliwa wa Zimbabwe, ambaye ni agenti maarufu wa biashara hiyo ya madini kwenda nchi mbalimbali, Danny Archer (Leonardo DiCaprio) aliyekamatwa kwa kusafirisha kwa njia haramu madini hayo kwenda Liberia, anaposikia ukelele wa Kapteni Poison, anapamga mkakati wa kumtoa Solomon ili akamwoneshe almasi hiyo.

Ni kwa kufanikiwa kumtoa Solomon ndipo makubaliano yanakuwa kwamba Solomon atampeleka Archer almasi hiyo ilipo, huku Solomon akiahidiwa na Archer kupelekwa na kukutanishwa na familia yake waliyopotezana nayo baada ya kijiji chake kuvamiwa na waasi (huku mwanae ambaye hajafikia hata umri wa miaka 16 akifanywa askari na waasi).

Ni hii safari ya Solomon na Archer-iliyotawaliwa na nia na madhumuni mawili tofauti kabisa kati ya wawili hawa (thamani ya maisha dhidi ya thamani ya almasi), tunadhihirishiwa vifo vya mamia na maelfu ya wananchi, mateso, taabu na madhara mengine lukuki kama matokeo ya vita hivyo.

Si nia yangu kuelezea kila tukio la filamu hiyo kwa kina. Nia yangu ni kutumia mfano huu kufananisha na hali halisi ambayo inatukumba katika nchi zetu kwa sababu tu ya baraka ya utajiri wa raslimali; hasa ya madini tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Nautumia mfano huu si kwa muktadha wa vita kama ilivyokuwa Sierra Leone. Hatuna vita juu ya madini, lakini mwenendo wa mambo katika maeneo ya madini nchini kwetu, na hata katika nchi za jirani yamekuwa na harufu na picha za damu. Nitaeleza.

Chukulia tukio la Nyamongo wilayani Tarime wiki chache zilizopita ambapo wananchi watano waliuawa kwa madai ya kuvamia mgodi. Hii si mara ya kwanza tunasikia kuhusu matukio yanayofanana na hili.

Kwa kipindi kirefu sasa imekuwa ni kawaida kusikia, ama watu wameuawa, au kuna vurugu kati ya wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi na walinzi, polisi au wawekezaji wenyewe katika migodi ya Mererani, Mwadui/Maganzo, Buzwagi, North Mara, Isanga (Nzega) na kwingineko.

Kama hiyo haitoshi, hali kama hizi za ‘damu kumwagika’ zinaendana na matukio mengine kama wakazi na wawekezaji kutambuana kwa utambulisho (identities) za kiadui.

Tumesikia majina mengi kama wanayobatizwa wananchi wa maeneo haya kama vile ‘wachimbaji haramu’, ‘wavamizi’, majambazi’  na mengine mengi.

Kwa mfano, wananchi hasa vijana wanaoishi karibu eneo la machimbo ya Mwadui katika maeneo kama Maganzo (wanaotuhumiwa kuwa huwa wanavamia eneo hilo kusaka almasi), wanaitwa ‘Wahabeshi’.

Uhabeshi ni  Ethiopia; hivyo kwa tafsiri ya haraka haraka hawa wanaitwa hivi ikiwa na maana ni ‘wavamizi haramu’. Wamebatizwa jina la nchi nyingine; hivyo ni kama wakimbizi katika nchi yao wenyewe.

Kwa upande mwingine, ukiwasikiliza wakazi wa maeneo hayo nao wana namna zao za kuwaita wawekezaji majina mbalimbali. Utasikia majina kama ‘makaburu’, ‘wanyonyaji’, ’wezi’, na mengine mengi yenye maana hasi na yanayotambulisha hisia ama za hasira au kutopendezwa na wawekezaji hao.

Tukiweka pembeni masuala ya nani ni jambazi au sio jambazi katika matukio kama haya, tunakubaliana katika suala moja: Madini na baadhi ya raslimali zingine tulizonazo zimekuwa si za manufaa yanayotarajiwa; bali zimegeuka kuwa shubiri na balaa kubwa kwa wananchi.

Hali ya kutoridhishwa na mwenendo wa mambo inajidhihirisha wazi kutokana na matukio hayo ya watu kuuawa, mahusiano ya uadui yaliyopo kati ya wawekezaji na wakazi wanaozunguka migodi hii, na hata sauti nyingi za wanasiasa na viongozi wenye nia njema, wanaharakati na hata waandishi.

Kama hali itaendelea kuachwa hivi hivi, kuna bomu tunalifuga ambalo kuja kulipuka kwake itabaki kuwa ni majuto yetu. Lakini swali kubwa ni kuwa tumefikaje hadi hapa tulipo?

Mosi, tunafahamu kuwa kwa muda mrefu sheria ambazo tumekuwa nazo, hasa sheria ya madini, ndio zimekuwa chanzo kikubwa cha masahibu haya yote.

Pamoja na Sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 kuongeza kiwango cha asilimia ya mrahaba kwa serikali toka kwa wawekezaji, masuala yanayohusu mahusiano ya wakazi wa maeneo ya migodi na hata stahiki wanazohitaji wakazi hawa yameachwa yanaelea hivi hivi.

Ikumbukwe kwamba imekuwa ikielezwa kuwa Tume ya Bomani iliyotoa mapendekezo mengi juu ya kuboresha sekta ya madini, mengi kati ya hayo imesemwa kuwa yaliingizwa kwenye sheria hiyo mpya ya madini.

Hata hivyo, kama ambavyo aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari Mkurugenzi wa Taasisi ya HAKIARDHI, Aman Mhinda, mojawapo ya mapendekezo muhimu ambayo sheria haikuyazingatia ni lile la kuanzishwa kwa chombo maalumu au mahakama maalumu kushughulikia migogoro iliyopo katika maeneo ya migodini au palipo na madini.

Si kwamba matatizo kama haya kati ya wawekezaji wa madini na wakazi wa maeneo husika yanatokea hapa kwetu tu. Hata nchi nyingine za Afrika ambazo sekta ya madini ni kubwa kumekuwa na masuala ya kufanana na hili, lakini suala linalopigiwa kelele likiwa hili hili la namna ambavyo wananchi wananufaika na sekta ya madini nchini kwao.

Hapa Afrika Kusini (kwa mfano) kumekuwa na mjadala mkubwa tangu mwaka jana kufuatia kauli ya Rais wa Jumuiya ya Vijana ya ANC, Julius Malema, kuwa anaamini ili wananchi wa Afrika Kusini wanufaike na madini, suluhisho ni kutaifisha sekta ya madini (nationalisation).

Kwamba kuwepo na kampuni moja kubwa la kitaifa ambalo ndilo litasimamia shughuli zote na kuhakikisha makampuni ya wawekezaji, hasa wa nje, kwa mujibu wake, “hayaibi utajiri wa wananchi wa Afrika Kusini”.

Mkakati kama huu ambao Malema anasema atapigania ili siku moja ufanyiwe kazi na serikali, unatajwa kuwa ni hatari kwani waweza kuifanya sekta ya madini kuyumba kutokana na ukweli kuwa serikali haiwezi kuwa na wataalamu wengi na nyenzo za kutosha kuendesha sekata kubwa kama hiyo.

Ingawaje wataalamu wa mipango ya maendeleo wanasema hoja na mkakati wa Malema ni mgumu kutekelezeka, anachokizungumza kinatokana na ukweli ulio mchungu na dhahiri.

Ukweli huu ni kuwa suala la wananchi kutonufaika na utajiri wa madini katika nchi zao barani Afrika ni ugonjwa mkubwa ambao utafutwaji wa dawa yake yaonekana kutotiliwa maanani inavyopaswa.

Ni viongozi wachache wanaokiri kuhusu tatizo hili, kama alivyofanya Rais wa Zambia Rupia Banda mapema mwezi Aprili mwaka huu wakati  akizindua mgodi wa Kalumbira nchini humo.

Banda alisema wazi kuwa serikali yake inatambua kuwa ‘haipati manufaa yanayostahili na kutosheleza’ kama inavyopaswa kutoka kwenye sekta ya madini nchini humo.

Pamoja na matatizo ya kisheria ya kanuni ambazo zinaweza kutambulisha stahili ya wakazi wanaozunguka migodi yao, kama vile kutoa baadhi ya huduma za kijamii, tatizo la pili ni viongozi waandamizi katika ngazi za chini katika maeneo hayo.

Kuna malalamiko mengi kwamba viongozi wa ngazi za vijiji, kata hata wilaya, badala ya kuwa wasuluhishi wa migogoro katika maeneo hayo, wamekuwa ndio wanaoikuza na kuilea migogoro kwa kuegemea upande mmoja (hasa wa upande wawekezaji).

Ni kitu cha kushangaza kwamba katika maeneo ya kandokando ya migodi ambayo nimewahi kufika ya Mpwapwa, Nzega na Maganzo, malalamiko ya wakazi dhidi ya viongozi wa ngazi hizo yanafanana.

Shutuma hizi zinaambatana na madai kuwa viongozi hao hunufaika wao binafsi kwa rushwa na bakshishi zingine kutoka kwa wawekezaji, na hivyo kuwategemea kutatua migogoro katika hali iliyo ya usawa inakuwa ni vigumu.

Kingine ambacho kimetufikisha Tanzania kwenye madini yetu kuwa na uhusiano mkubwa na ‘damu’, ni huu ujasiri hatari wa hawa wanaoitwa walinzi katika migodi hii na hata polisi.

Ni jambo la kusikitisha na kushangaza kuwa suluhisho lililopo katika migogoro hii imekuwa ni mtutu wa bunduki, bila kujali kuwa kila binadamu ana haki ya kuishi. Na kama ni wahalifu, kwa nini kusitumike utaratibu wa kisheria wa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo husika vya sheria?

Tumefika hapa tulipo, mahali ambapo thamani ya uhai wa binadamu haina maana zaidi ya kulinda maslahi ya wachache wanaovuna raslimali zilizopo.

Lakini mbaya zaidi uzalendo wetu kwa nchi yetu, kwa manufaa yetu na ya vizazi vijavyo, utakuwa wa kuhojiwa iwapo tutayafanya haya yanayotokea kuwa ni mambo ya kawaida!

Hizi ni changamoto kubwa ambazo hazipaswi kupigwa kalenda katika kuzishughulikia.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Paul Dotto
dkuhenga@gmail.com
+27-837249156, +255-755172570

Toa maoni yako