Makala
Madiwani 10 wa CHADEMA wawekwa kitimoto Arusha
Paul Sarwatt
Arusha
Toleo la 193
6 Jul 2011
  • Ni wale waliosaini mwafaka na CCM
  • Wahenyeshwa na kamati ya Marando na Dk. Kitila
  • Ripoti kuwasilishwa Kamati Kuu CHADEMA

HATMA  ya mgogoro baina ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Manispaa ya Arusha na uongozi wa juu wa chama hicho kuhusu muafaka  uliofikiwa wa uchaguzi wa nafasi ya umeya wa mji wa Arusha, sasa, itaamuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho baada ya kamati ya watu wanne kumaliza kazi ya kuwahiji madiwani hao.

Muafaka baina ya madiwani hao wa CHADEMA na wale wa  Chama Cha Mapinduzi kuhusu mgogoro  wa uchaguzi  nafasi ya umeya wa Jiji la Arusha ulifikiwa Juni 20 baada ya pande zote mbili kukubaliana kugawana madaraka.

Katika makubaliano hayo, ambayo baadaye yalitiwa saini na pande zote mbili, nafasi ya umeya imebakia kwa meya wa sasa, Gaudence Lyimo (CCM);  huku CHADEMA  “wakipozwa”  kwa  kupewa nafasi ya unaibu meya kwa muda wa miaka mine, nafasi ambayo tayari Diwani wa Kimandolu, Estomih Mallah, ameshatangazwa kuijaza.

Hata hivyo, muafaka huo ulipingwa na uongozi wa juu wa CHADEMA ambao ulisema kwamba haukushirikishwa katika majadiliano na wala haukutoa Baraka zake kwa kile kilichokubaliwa; hatua ambayo pia ilifuatiwa na  Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godless Lema, kuupinga hadharani muafaka huo.

Kufuatia malumbano baina ya madiwani wa CHADEMA na viongozi wa chama chao katika vyombo vya habari, uongozi wa kitaifa wa chama hicho uliunda kamati ya wanne ambayo iliwahoji madiwani wote 10;  lengo likiwa ni  kuisaidia Kamati Kuu ya chama kufanya uamuzi sahihi kuhusu mvutano huo.

Madiwani hao waliohojiwa Ijumaa iliyopita  katika hoteli ya Bristol, iliyopo eneo la Kaloleni, mjini Arusha. Kamati hiyo iliongozwa na mwanasheria wa CHADEMA, Mabare Marando.

Wajumbe wengine wa tume hiyo ni Esther Daffi ambaye pia ni mwanasheria, Lazaro Massay ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, na Dk. Kitila Mkumbo ambaye anatajwa kama   mshauri wa CHADEMA kuhusu masuala ya siasa.

Taarifa zilizolifikia Raia Mwema  kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa kwa upande wao madiwani waliohojiwa wameweka msimamo wa pamoja  kuwa wako tayari kuwajibishwa na chama lakini hawatabadili maamuzi waliyofikia kuhusu muafaka uliofikiwa baina yao na CCM.

Mtoa taarifa  kutoka ndani ya chama hicho  (jina linahifadhiwa) alieleza kuwa kimsingi kulikuwa na mawasiliano ya kutosha baina ya uongozi wa chama kuanzia ngazi ya wilaya na mkoa, na kila mara walikuwa wanapeana taarifa za mazungumzo ya muafaka uliokuwa ukisimamiwa na wajumbe watano kutoka kila chama chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond  Mushi.

Aidha, imeelezwa kuwa madiwani wote waliohojiwa na tume hiyo waliweka wazi kuwa hawako tayari kuburuzwa na Mbunge wao, Godbless Lema, ambaye amekuwa wanadai kuwa amekuwa akionyesha dharau za wazi dhidi yao.

Madiwani pia waliulalamikia uongozi wa wilaya kuwa ndiyo chanzo cha kuzorota kwa mawasiliano baina yao na uongozi wa Taifa katika siku za mwisho kabla ya kutiwa saini kwa muafaka kutokana na kile kinachodaiwa kuwa viongozi wa wilaya,  chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Derek Magoma, umeshindwa kutimiza majukumu yake.

Mmoja  wa madiwani  waliohojiwa, ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alithibitisha madiwani kuweka msimamo wa pamoja kuwa hawako tayari kurudi nyuma katika maamuzi waliyofikia kuhusu muafaka kwa kuwa wananchi hawezi kuwaelewa iwapo watabadili msimamo wao.

“Sisi tunawajibu wa kusimamia maendeleo ya  wananchi katika kata zetu; kwa hiyo mgogoro kuhusu nafasi ya umeya ambao ulisababisha madiwani wa CHADEMA kususia shughuli za Halmashauri, ulikuwa na athari za moja kwa moja kwetu; huku wananchi wakituhoji kuhusu ahadi mbalimbali tulizotoa wakati wa kampeni”, alisema mmoja  wa madiwani hao.

Diwani huyo aliongeza kuwa pamoja na viongozi wa wilaya na mkoa kuarifiwa   juu ya hatua mbalimbali  zilizofikiwa kabla ya kusainiwa kwa  muafaka,  baadhi yao, pamoja na Mbunge Lema, wamekuwa wanawapotosha viongozi wa kitaifa wa chama chao  ambao wamejenga picha kuw madiwani ndio tatizo.

“Mheshimiwa mbunge  hatoi nafasi kwa watu wengine kutoa mawazo yao katika kila jambo. Anataka wote tufuate mawazo yake; hata kama si sahihi. Tuko katika siasa, na lazima mbunge atambue na kuheshimu  mawazo ya watu wengine; vinginevyo ni udikteta ambao hatutakubaliana nao”, alisema.

“Muafaka ulifikiwa ni sawa na mtoto aliyezaliwa ambaye kisayansi haiwezekani akarudishwa tumboni kwa mama yake. Na kwa mantiki hiyo, sisi tunasema tumeafikiana, na sasa tuanze kutekeleza yale ambayo wananchi wanataraji kutoka kwetu”, alieleza diwani huyo.

“Kwa upande wetu tulichogundua ni kuwa hatua ya kupinga uchaguzi wa meya wa Arusha, na baadaye maandamano ya Januari 5 ambayo yalisababisha vifo vya watu watatu, haikuwa na mashiko, na chama ngazi ya taifa hakikufanya uchambuzi wa kina  baada  ya kupokea taarifa za viongozi wa wilaya na mkoa”, aliongeza kusema diwani mwingine.

Diwani huyo anaeleza kuwa baadhi ya viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa walikuwa wanatoa taarifa za kuwapotosha viongozi wa wa kitaifa ambao walijenga picha kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kufikia muafaka uliosainiwa.

Akizungumzia  hatua ya madiwani hao kuhojiwa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, alithibitisha kuwa timu ya Marando tayari imemaliza kazi hiyo, na kwamba anatarajia kuipokea rasmi ripoti yao   kabla ya mwisho wa wiki hii.

“Mahojiano yamekamilika, na taarifa hiyo itawasilishwa kwangu muda wowote  kabla ya kumalizika kwa wiki hii. Taarifa nilizopata ni kwamba mahojiano yalifanyika kwa kuzingatia taratibu zetu kichama”, alisema.

Katibu huyo wa CHADEMA alisema baada ya kupokea taarifa na mapendekezo ya kamati hiyo, yeye kama Katibu Mkuu atayawasilisha kwa Kamati Kuu ya chama itakayokutana muda wowote baada ya kukamilika kwa kazi ya kupitia mapendekezo.

 Dk. Slaa alisema Kamati  Kuu ndiyo itakayoamua juu ya mgogoro huo, na hiyo itafanyika baada ya kupitia kwa makini mapendekezo ya kamati iliyoundwa.

“Kwa sasa  natoa wito kwa wanachama na wapenzi wa chama chetu kuwa na subira na kutoa nafasi kwa vyombo vya chama kutimiza wajibu wao, lakini suala hili litamalizwa katika njia ya kidemokrasia; kwani ndicho chama chetu kinachoisimamia na kuamini”, alisema.

Dk. Slaa aliongeza kuwa chama hicho kiko makini katika kushughulikia masuala ya msingi na hawawezi kufanya maamuzi ya kukurupuka ambayo hayatakuwa na maslahi kwa chama na wanachama wake.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini  (CHADEMA),  Godbless Lema,  alikanusha madai yaliyotolewa dhidi yake kuwa amekuwa sehemu ya matatizo yaliyotokea Arusha, na kwamba hatoi nafasi kwa  viongozi wengine, wakiwemo madiwani, kutoa mawazo yao.

“Huo ni upotoshaji wa mambo. Sijawahi kupinga mawazo ya kiongozi yeyote ndani ya chama kama ni mawazo chanya na yenye nia njema katika masuala tunayopigania  kila siku. Ieleweke wazi kuwa katika siasa kutofautiana mawazo ni jambo la kawaida. Kwa hiyo, siwezi kupinga michango ya kimawazo ya watu wengine”, alisema Lema.

Lema aliweka wazi kuwa mgogoro baina yake na madiwani unatokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu na kile walichokuwa wanakipinga awali kama chama kuhusu uchaguzi wa meya wa Arusha.

“Kama chama lengo letu halikuwa  nafasi ya unaibu meya; bali tulilalamikia hatua ya kukiukwa kwa  taratibu za uchaguzi wa nafasi, na hatukuwahi kusema tuna ugomvi binafsi na meya aliyechaguliwa; bali tulisema taratibu zilizomwingiza madarakani zilikuwa si sahihi”, alisema.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa mkoani hapa wanaeleza kuwa  CHADEMA, ambacho kinajaribu kujenga taswira yake mbele ya jamii kama chama kikuu cha Upinzani  baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, kinaweza kuathiriwa na mgogoro huo  kisiasa katika mkoa wa Arusha ambako kina wafuasi wengi.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako