Maendeleo hayaji kwa kulalamika

TUMEBHATIKA kuuona mwaka mpya wa 2017. Ni mwaka mpya na ni jambo la kheri na lililo jema kuuanza kwa kumshukuru Allah kwa kutuwezesha kuuona.

Shukrani zangu za pekee ziwaendee wale wote wanaofuatilia safu hii kwa kunitia moyo ili nisichoke kuandika hali kadhalika kwa kunisaidia kwa kunipa maoni yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kunikosoa kama njia mojawapo ya kunifanya nijiulize maswali mengi zaidi kuhusu ninachoandika. Akhsanteni kwa kuniwezesha kuandika na kujadiliana nanyi.

Wakati nikitoa shukrani hizo ni jambo jema kujipanga upya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunajadiliana na kushauriana kwa lengo la kupata muafaka katika mjadala kuhusu mustakabali wa taifa na ni njia ipi iliyo sahihi ya kuinua ustawi wa watu wetu.

Hakuna ajuaye yote, na kwa maana hiyo, kila siku tupo katika darasa kubwa kupitia mijadala mbalimbali inayoendelea hapa nchini kuhusu mustakabali wa taifa letu.

Ninaamini kila Mtanzania anatambua kwa haitawezekana kupiga hatua yoyote ya maana ya maendeleo kama hakutakuwa na ushiriki mpana sana wa wananchi wote katika mjadala wa njia gani ya kupita ili tufikie pale tunapotaka kufika.

Maendeleo hayaletwi kwa sera na sheria tu. Haiwezekani kupata maendeleo kwa maazimio, sera na sheria tu bila ya uelewa wa pamoja na kwa hakika makubaliano ya kile ambacho tunakihitaji au tunatamani kukipata.

Ushiriki wa wananchi wengi katika mijadala mbalimbali kuhusu mustakabali wa maisha yao kama taifa ni muhimu sana kama kweli tunayo dhamira ya kweli ya kutaka kuyapata hayo maendeleo tunayoyazungumzia.

Aidha, hayo maendeleo yanayozungumziwa ni lazima yapate ufafanuzi na kuwapo na makubaliano ya pamoja na tafsiri inayoeleweka kuhusu dhana yenyewe hiyo ya maendeleo.

Ni vigezo gani vinavyotumika kuelezea maendeleo? Ni kitu au vitu gani vikiwapo katika nchi yetu tunasema kuna maendeleo? Vigezo gani vinaweza kutumika katika ngazi ya kijiji kupima maendeleo? Je, maendeleo ya kaya moja moja yanapimwa kwa kutumia vigezo gani?

Nimewahi kuandika katika safu hii kwamba ni vigumu sana kutamba kwamba Tanzania ipo katika dunia ya leo ambayo inadaiwa kuwa ni kama kijiji. Dhana ya dunia kuwa kijiji imetokana na hatua kubwa sana iliyopigwa katika mawasiliano.

Yaani kinachomaanishwa ni kwamba kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano hivi sasa mtu aliyepo katika kijiji cha Wamasai kule Ngorongoro anaweza kuwasiliana kirahisi kabisa na rafiki yake wa Marekani aliyekutana naye katika Kreta kwa bahati nasibu tu.

Hivi sasa anaweza si tu kuongea naye kwa simu bali anaweza kumuona naye akamuona na kujiridhisha kwamba huyo mtu ndiye na yu hai kwani anamuona katika video. Hiyo ndiyo dunia ya sasa.

Si tu kwamba watu wawili wanaweza kuonana na kuzungumza, bali hata kundi la watu walio sehemu mbalimbali duniani, yaani mmoja akawa yupo Santiago, Chile mwingine Ontario, Canada na mwingine Abu Dhabi na wakaunganishwa na mwingine aliye Australia na wakaonana na kuongea na hatimaye kufikia muafaka wa mjadala bila ya kutumia gharama kubwa sana. Ndiyo dunia ya sasa. Yaani dunia ambayo watu wanaweza kuwasiliana mithili ya mawasiliano katika kijiji.

Lakini ni muhali sana kudai kwamba sisi tupo katika dunia hiyo. Ukweli ni kwamba bado nchi yetu ni dunia ya zamani. Na jambo ambalo linatukwaza kama nilivyowahi kusema ni kwamba hatuna miundombinu ya kutuingiza katika kijiji hicho kikubwa kinachoitwa dunia.

Watanzania wengi hatuna anwani. Ni anwani ndiyo inayotuingiza katika kijiji kiitwacho dunia. Hatuna anwani ya kutuwezesha kutambuliwa tunapoishi na kwa kutokana na udhaifu huo ni vigumu kuwa mwanachama wa hicho kijiji kiitwacho dunia.

Mmasai anayepigiwa simu na swahiba yake aliyepo Marekani hawezi kujitambulisha kwa mfumo wa kisasa kwa sababu mfumo huo wa anwani za makazi bado haujasambaa kote nchini japo ulizinduliwa kwa mbwembwe nyingi miaka kadhaa iliyopita. Hadi leo sehemu kubwa ya nchi yetu haina anwani.

Mwaka jana ulikuwa wa kwanza wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli. Kwa walio wengi ulikuwa ni mwaka wa kuona ni mwelekeo gani serikali hiyo mpya itachukua katika kuujenga uchumi na kuinua ustawi wa Watanzania.

Kwa walio wengi ulikuwa ni mwaka mgumu. Hadi tunauaga mwaka kulikuwa na maoni mchanganyiko kuhusu mwelekeo wa utendaji wa serikali. Ugumu wa maisha katika mwaka uliopita umejadiliwa katika hadhira mbalimbali kuanzia za kisomi zilizojaa wanazuoni hadi za vilabu vya pombe huko vijijini.

Wapo waliohisi kwamba ndio walioumia zaidi kutokana na staili ya utawala ya kiongozi mkuu wa nchi kutokana na jinsi alivyoamua kumulika katika sekta zote muhimu katika ustawi wa taifa letu.

Uchumi wetu ulitikisika kwa sababu kadhaa lakini moja ambalo ni la wazi kabisa ni kwamba kumekuwapo jitihada za makusudi kabisa za Rais Magufuli za kuhakikisha kwamba anapambana na ubadhirifu wa mali ya umma. Hili la kupambana na ubadhirifu ni pamoja na kuhakikisha kwamba ufisadi unakomeshwa katika sura zake zote.

Katika kuonyesha kwa umma dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi kumekuwapo na mtikisiko mkubwa katika asasi kama Mamlaka ya Bandari ambayo ni muhimili mkuu katika uchumi kwani biashara ya ndani na nje ya nchi hutegemea kwa kiasi kikubwa utendaji katika bandari zetu zote.

Bandari ni muhimu kwa sababu ndiyo mlango mkuu wa kusafirisha kuingiza nchini na pia kutoa kutoka nchini kwenda nje bidhaa mbalimbali. Ukiukwaji wowote wa sheria, kanuni na taratibu katika bandari zetu ni pigo kubwa sana katika uchumi wetu.

Safisha safisha aliyoianzisha Rais Magufuli ni ngumu sana na ndiyo sababu imekuwa na mwangwi mkubwa sana.

Tumeuanza mwaka mpya ambao bila shaka utakuwa na changamoto nyingi sana. Changamoto zilizopo si za Rais Magufuli na mawaziri wake tu hizi ni changamoto zetu wote.

Ni wajibu wetu kushiriki katika mjadala mpana wa kitaifa wa mustakabali wa taifa letu. Hatuna budi kujiridhisha kwa pamoja kwamba tunasafiri pamoja kufika kule tunakotaka.

Tusipokuwa pamoja ni wazi kwamba tutaishia kuwa ni watu wa kulaumiana na kulalamikiana na hiyo haitatufikisha katika maendeleo tunayoyataka.

Endapo tuna dhamira ya kweli ya kujiletea maendeleo yetu wenyewe ni lazima tukubaliane kukubaliana na kutofautiana kwa nia njema na lengo moja la kujiletea hayo maendeleo.

Tuuanze mwaka mpya kwa kuwa na azimio la pamoja la kujiletea maendeleo bila ya kuwa watu wa kulalamika na kukata tamaa.

Nawatakia kila la kheri katika mwaka mpya wa 2017!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *