Maendeleo yatatokana na uthubutu, tafakuri

MAKALA hii, na nyingine chache zitakazofuata, ni muendelezo wa makala ya wiki jana iliyohusu kile ambacho Profesa Chachage Seithy Chachage alichokiita “collective imbecilization.”

Nimekwisha kuieleza dhana hii kama ule mchakato wa kuwafanya watu wengi wawe ni wapumbavu, wajinga, mazuzu, mazezeta, mafala kwa pamoja. Nguvu ya uzuzu wao inakuwa imejengeka kwa idadi kubwa ya watu hao, na tusisahau ule msemo kwamba tusiwapuuze watu wapumbavu wanapokuwa wengi.

Katika kujenga na kuimarisha “collective imbecilization” zipo asasi zinazosaidia mchakato huo. Asasi hizo ni zile ambazo siku zote zinahusika na kukuza na kuendeleza mitazamo ya jamii na ambazo hujenga misingi ya hulka, tafakuri, weledi na maadili miongoni mwa wanajamii.

Asasi hizo zinaweza kuwa zinashirikiana katika kufanya kazi hiyo. Kwa mfano asasi ya familia, ambayo ni ya msingi kabisa katika jamii yoyote ile, na asasi nyingine kama mifumo rasmi ya elimu, mifumo ya utawala, mifumo ya sheria na mahakama, asasi za itikadi za imani za kidini, mifumo ya uzalishaji, vyombo vya utawala, mifumo ya siasa, asasi za upashanaji wa habari, vyombo vya burudani na starehe …. zote ni asasi zinazoshirikiana kujenga jamii ya aina fulani.

Kusema hivyo haiwezi kuwa na maana kwamba asasi hizo hukubaliana moja kwa moja juu ya mitazamo inayotakiwa ndani ya jamii, kwa sababu mara nyingi huwa zikitofautiana na zikikinzana na kuvutana kuhusu mambo muhimu ndani ya jamii, na mara nyingi kazi ya kutafuta mwafaka inakuwa nzito sana na kuifanya jamii ipoteze uwezo wa kusonga mbele kwa kasi ambayo baadhi ya wanajamii na asasi zao wangependelea.

Baina ya wale wanaotaka kupiga hatua za kasi kuelekea kwenye maendeleo (progressive) na wale wanaoshikilia na kung’ang’ania mafundisho na makatazo ya kimapokeo (traditional) hutokea misuguano ya siku zote, na hii haiwezi kuisha alimradi jamii inaendelea kuishi pamoja.

Hutokea mrengo fulani ukawa na nguvu kuliko mirengo mingine kutokana na msukumo wa kisiasa, kiuchumi au kiutamaduni, na watu wanaweza kuona kama vile mabadiliko makubwa yanatokea ndani ya jamii, lakini mabadiliko hayo yakaja kubainika kwamba yalikuwa ni kiini-macho na wala hayakuwa na mashiko katika jamii. Mengine yanaweza kubainika kwamba yalikuwa endelevu na yakadumu kwa muda mrefu, na wakati mwingine yakawa ndiyo yenye athari za kudumu kwa vizazi kadhaa vijavyo.

Katika kujadili michakato, misukumo na mikondo hii, bila shaka hatuwezi hata kidogo kusahau kwamba jamii yetu inaishi katika dunia ambayo imeingiliana katika mambo mengi, na kwamba mambo yanayotokea kwingine duniani yanatuathiri pia, na si rahisi kufunga milango na madirisha ya jamii yetu ili kuikinga na athari za mambo yanayotokea ughaibuni.

Katika kujadili masuala yote haya nitajitahidi kuchokoza mjadala ambao usuli wake (background) utakuwa historia fupi ya nchi yetu na nchi nyingine tunazopakana nazo katika bara letu kwani historia zetu zinafanana na wakati mwingine zimekuwa zikiingiliana. Inawezekana pia kwamba mustakabali wetu ni wa pamoja. Matatizo mengi tunayosumbuliwa nayo yanawasumbua na wengine wengi ndani ya Afrika.

Msingi wa matatizo yetu kufanana ni kwamba miaka ipatayo hamsini tu iliyopita tulikuwa pamoja kama Waafrika chini ya himaya za ukoloni zilizotugandamiza kiasi cha kupoteza utu wetu na kupoteza uwezo wa kufikiri sawa sawa. Kabla ya ukoloni, bila shaka tunajua, nchi zetu zilikuwa ni mahali pa watu waliotuzidi akili kuja kukamata na kusafirisha watu wa kwenda kuwatumikia watu wengine bila utashi wao na bila ujira.

Madhara ya kisaikolojia tuliyoachwa nayo kutokana na utumwa na ukoloni yanaelekea kutoondoka. Ni kama vile utumwa na ukoloni vimetuachia ulemavu wa akili unaotufanya tusiweze kufikiri sisi wenyewe, na sisi wenyewe sasa tunafanya kila kitu kuzuia watu wasifikiri. Hali inayojitokeza ni kwamba sote tumeathirika na utumwa na ukoloni, halafu sasa tunajiwekea sisi wenyewe mazingira ya kuendeleza hizo hizo athari za utumwa na ukoloni katika mazingira ya leo.

Ili mabwana zetu waliotuteka wafanikiwe, ilibidi tufanywe kupoteza uwezo wa kusaili yale tuliyokuwa tukifanyiwa na tukiamrishwa kufanya. Hiyo peke yake, baada ya karne kadhaa, ilikwisha kutufanya mazuzu. Hii ni kutokana na mantiki kwamba nyenzo isiyotumika hudhoofika, ikapata kutu, ikavia, ikadumaa. Akili isyotumika ni vivyo hivyo, itavia, itaota magugu, itapata kutu.

Sasa, badala ya kusaidiana kujikomboa dhidi ya akili butu hii, sisi wenyewe tunataka kuendeleza ubutu huo kwa kumzuia kila anayetaka kufikiri angalau kidogo asiweze kufikiri hata hiyo kidogo. Kilicho kibaya zaidi ni kwamba hata hao wanaowazuia wengine kufikiri hawaelekei kwamba wao angalau wanajaribu kufikiri ili waweze kuwafikiria hao waliowazuia wasifikiri. Iwapo wanaowazuia wenzao wasifikiri wao wenyewe hawafikiri, ni nani atafikiri kwa niaba ya hao wote wasiofikiri?

Kwa kuwa tumefanikiwa kupunguza kiwango cha tafakuri, tumekuwa watu wa kughilibiwa na kila aina ya matapeli, iwe ni katika siasa, iwe ni katika biashara, iwe ni katika imani za dini. Kila mahali, wengi wa hao wanaofanikisha shughuli zao ni matapeli. Wanafanikiwa kwa sababu wamegundua kwamba watu walio wengi ni mazuzu ambao hawajazoea kuzisumbua akili zao kwa kuuliza maswali, na hali hiyo inaibua fursa kem kem za biashara za utapeli.

Nitatoa mifano kadhaa inayoonyesha ni jinsi gani tulivyoendelea kujishusha katika shughuli ya tafakuri hadi tumefikia hatua ya kuwa kama tumekubali kwamba, tunapojilinganisha na wenzetu waliotuzunguka, ubora wetu ni gredi ya tatu au ya nne.

Hakuna jamii inayoweza kupiga hatua madhubuti za maendeleo iwapo watu wake wanajidharau wenyewe kila wakijilinganisha na watu wa jamii nyingine. Ni sharti la kwanza kabisa kwamba jamii ijiamini na iwafunze watoto wake kujiamini pale jamii husika inapotaka kufanya mambo makubwa  ya kimaendeleo. Hivyo ndivyo jamii zilizoiteka dunia zilivyofanya: Warumi wa kale. Waajemi, Wayunani, Wamongoli, Waturuki, Wahispania, Wareno, Waingereza.

Vijiinchi kama Ureno na Uingereza ni vijiinchi vidogo kabisa. Zote mbili zikichanganywa pamoja zinaweza kumezwa na mkoa mmoja wa Tanganyika. Umaarufu na utajiri wa nchi hizo ulitokana na kuwa na watu, hasa vijana wake, waliokuwa na uthubutu wa kufikiria mambo ambayo mara nyingi hayakuwa yanaonekana kama  yanayowezekana.

Huo ndio uthubutu tunaohitaji, siyo tu ili tuweze kufanya mambo makubwa ya kuishangaza dunia, bali hata kuweza kuendelea kuwapo kama jamii huru kwa maana ya “survival”. Bila hiyo tunajiweka katika nafasi ya kuweza kuchukuliwa utumwani kwa mara nyingine au kuwekwa chini ya himaya ya wale wanaotumia akili zao wakati sisi tumekataa kutumia zetu.

Hatutaweza kujenga uchumi wa viwanda bila watu wanaofikiri. Hatutaweza kuinua uchumi wetu wa kilimo, ambao ndio msingi wa kweli wa kuanza kufikiria uchumi wa viwanda bila kuwa na kada kubwa ya Watanzania wanaosumbua bongo zao kufikiri hata mambo yasiyofikirika, mambo yaliyo nje ya uwezo wa kufikiri wa watu wengi.

Haiwezekani kuwa na maendeleo ya viwanda kama watoto wa nchi hii bado wanakwenda shule ambazo zina “matundu” matatu ya choo kwa ajili ya watoto 500. Ni mambo mengi ambayo hayawezi yakafanyika kama watu wetu hawajajipatia uhuru wa kufikiri, na kutokana na huo uhuru, wakawa na uhuru wa kubadilishana mawazo na fikra miongoni mwao wenyewe, na baina yao na jamii za dunia nzima.

3 thoughts on “Maendeleo yatatokana na uthubutu, tafakuri”

 1. Paul John Mhozya says:

  Enzi hizo na mpaka leo ni kuwepo kwa shida ndiko kulizaa watu kufikiri. Kuna aina mbili za shida na namna ya fikra za kuzitanzua. Kuna nadhari za jumla kuhusu matatizo yanayohusu maisha na vitu vinavyomzunguka mwanadamu. Isaac Newton amesifika kwa kuandika nadharia ya mwendo F=ma. Alifikiri sana hadi kuandika ndharia hii, hakuwa na shida, alikuwa akila na kushiba. Ukiingia kwenye tabia za makundi fikra zinazaa falsafa. Nyerere alishuhudia unyonyaji na kuibiwa haki za lazima kama rasilimali na na matunda ya nguvu za mtu. Kutanzua hili akaanzisha falsafa ya ujamaa na kujitegemea, pia alikaa na kufikiri sana. Hili ndiyo kuundi la kwanza, la nadharia na falsafa.

  Kundi la pili ni la vitendo, pia tunaweza kuligawa katika makundi mawili, nadharia kwa vitendo (functional literacy) na ufundi. Mkulima au mfugaji hukutano na changamoto nyingi ambazo huzikabili kwa kubadilisha mbinu. Lazima awe mkali wa kufikiri ili kufahamu mbinu mpya ipi itamsaidia kukabili changamoto fulani. Enzi za ujima Mwingereza alikuwa anatengeneneza nyuzi kwa (nduti) ya kuzungusha kwenye paja. Akatokea mtu akafikiri kama hataweza kutoa nyuzi nyingi zaidi akiunganisha (nduti) nyingi zinazozungushwa na paja moja? Huyu alikwa fundi au mhandisi.

  Nilivyomwelewa Jenerali Ulimwengu anazungumzia fikra za kifalsafa tu. Na hao anataka waanze kufikiri kwa kuwa walishakuwa mazuzu ni mchanganyiko wa wanafikra niliowataja. Si wote wanaweza kuwa wanafalsafa kwa sababu kila kundi lina mwelekeo wake. Kasoro aliyoileta yeye Jenerali Ulimwengu ni kukandamiza wana falsafa na kulazimisha wananadharia na wahandisi wamtengenezee falsafa anazozitarajia, haiwezekani. Matokeo yake yeye mwenyewe Jenerali Ulimwengu kageuka mwanafalsafa lakini mwenye upeo wa mzunguko usiokuwa na msaada katika jamii wa aina ya " We are poor because we are poor". Acheni magugu yabane mzao, yatakaposhamiri na kujiangamiza menyewe ndipo mpande mbegu njema za mazao yenu. Ikichukua karne poleni!

 2. Ali Said says:

  Sir,

  Mambo yote uliyotaja hapa juu ni ya kweli.

  Elimu bora  ni muhimu kabisa katika ku lift a country into the path of development.

  Naishi hapa England,na few years ago I watched a news-story here  iliyomuonesha msichana mdogo wa miaka 14 akitembea 14 miles everyday (7 miles to and from) kwenda shule mkoani morogoro,halfu akifika shule,the resourses available pale shuleni were very scarce.

  Huyu msichana kutembea 14 miles a day to go school ,50 years after independence…nillilia..bila elimu taifa litabaki duni katika kila maana ya hilo neno..duni in every sphere..

  Secondly,lazima watu wawe na utaifa lakini in the right way,yaani watu hasa kama ulivyosema juu ,vijana wawe ambituos kibinafsi kugundua/anzisha projects ambazo siyo tu zitawafaidi binafsi bali anaweka nia kuwa hata jamii yake nayo itafaidika..hii ndio something missing kwa waafrika,ni wachache sana wanafikiria jamii yake bali matumbo yetu tu..

  Hapa juzi,mama mmoja hapa England ambaye alifariki majuzi,usia wake umefunguliwa na ..ameacha mali yake yote kwa jamii,ikiwa ni pesa pamoja na kisiwa kilichopo katika Lake District hapa England,ambayo ni sehemu maarufu ya Holidays..nikumbushe kaka yangu lini ulisikia tajiri anaachia mali yake kwa yatima wanaoomba omba mababarani africa…

  Wewe ni mtu decent,mwenye uchungu wa kutaka jamii yako itoke katika umaskini na ujinga.nakujua toka enzi za 1970s,keep it up kaka yangu..africa needs more people like you….

   

 3. Donasian M.B says:

  Upembuzi mzuri, kwa jamii yetu iliyoamu kujikwamisha. Ila ukisema watu wamezuiwa wasifikiri mimi najiuliza ni kwanini ukubali kuzuiwa kufikiri? Chuo cha dar kimekuepo kitambo xana…iweje na hao wahitimu wake wakubali kuzuiwa kufikiri? Hapa naona kutofikiri kwetu ni "voluntarily"

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *