Magufuli aingizwa vitani

RAIS John Pombe Magufuli ameelezwa kuingizwa katika vita ambayo haina sababu baada ya uamuzi wa vikao vya juu vya CCM vilivyokutana mkoani Dodoma wiki iliyopita, Raia Mwema limeelezwa.

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), iliwavua uanachama baadhi ya viongozi wa chama hicho, kuwaonya wengine na kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wale walioitwa wasaliti wa chama hicho.

Hata hivyo, baadhi ya waliokumbwa na hatua hizo wamedai kwamba Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ameingizwa katika vita ambayo hakuwa na sababu nayo.

“ Unajua kwanini Rais Magufuli alipata nafasi ya kuwa mgombea urais wa CCM mwaka juzi (2015)? Ni kwa sababu alikuwa na rekodi nzuri lakini pia hakuwa na makundi.

“ Makundi yalimalizika baada ya uchaguzi ule wa ndani ya chama. Ndiyo maana baadhi ya waliochukuliwa hatua walishiriki kwa hali na mali kuhakikisha CCM inashinda kwenye uchaguzi ule.

“Watu hawakuwa na shida na Magufuli. Watu hawana mpango wa kumsaliti Magufuli. Yale yalikuwa ni mambo ya uchaguzi na yalishapita. Huu sasa ni mgogoro mwingine ambao haukuwa na sababu,” alisema mmoja wa wana CCM aliyefukuzwa na NEC wiki iliyopita.

Katika historia yake ya takribani miaka 50, CCM imewahi kufukuza wanachama wake kwa wingi walau mara mbili; ya kwanza ikiwa ni mwaka 1968 wakati TANU (mtangulizi wa CCM) ilipowafukuza viongozi walioonekana kupingana na Azimio la Arusha na mwaka 1988 wakati ilipowafukuza akina Maalim Seif Shariff Hamad.

Katika mara zote hizo mbili, mwisho wa hatua hiyo ilikuwa ni kutengeneza kada ya wapinzani ambao ingawa bado hawajaitoa madarakani CCM, ndiyo wapinzani wakuu wa chama hicho hadi sasa.

Viongozi wa CCM waliofukuzwa uanachama wa chama hicho ni wenyeviti wa mikoa minne wa chama hicho ambao ni Jesca Msambatavangu wa Iringa, Ramadhan Madabida wa Dar es Salaam, Erasto Kwilasa wa Shinyanga na Christopher Sanya wa Mara. Mwingine aliyekumbwa na kadhia hiyo ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT),  Taifa, Sophia Simba.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke, alipewa onyo kali na kuvuliwa wadhifa wake huo.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu Taifa waliofukuzwa ni pamoja na Ali Sumaye wa Wilaya ya Babati Mjini na Mathias Erasto Manga wa Wilaya ya Arumeru huku Mjumbe wa Kamati Kuu, Emmanuel Nchimbi akipewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi.

Kwa mujibu wa Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole, wote waliochukuliwa hatua hizo walifanya usaliti dhidi ya chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Inafahamika kwamba wote waliochukuliwa hatua walikuwa katika kambi ya Edward Lowassa wakati akiwania kupitishwa na CCM kuwa mgombea wake wa urais kwenye uchaguzi huo.

Karibu viongozi wote waliofukuzwa uanachama hawajazungumza hadharani na vyombo vya habari lakini Raia Mwema limeambiwa takribani wote wameshtushwa na hatua hiyo ingawa taarifa zilivuja walau wiki moja kabla kuwa watavuliwa nyadhifa zao.

“Chukulia mfano wangu. Ni kweli nilimuunga mkono Lowassa wakati huo. Lakini mara baada ya chama kutangaza kumkata, mimi nilipiga kampeni Magufuli apitishwe. Na aliposhinda, nikapiga kampeni ili amshinde Lowassa (akiwa mgombea wa upinzani nafasi ya urais).

“ Kwangu mimi, historia yangu na Lowassa iliisha baada ya yeye kuhamia upinzani. Lakini kwa hatua hii, inaonekana sikufanya lolote na kwa kweli nimesikitika sana,” alisema mmoja wa viongozi waliofukuzwa kwa masharti ya kutotaka kutaja majina yake.

Ni kiongozi huyo ndiye aliyeliambia gazeti hili kwamba hakuna uamuzi wa pamoja uliopangwa kufikiwa nao kwa sababu hakukuwa na mawasiliano kabla na hawakujua kama hatua watakayochukuliwa ndiyo hii.

Raia Mwema limeambiwa kwamba wote waliofukuzwa na kuchukuliwa hatua nyingine za kinidhamu walifanyiwa hivyo baada ya kuchunguzwa kwa takribani miaka miwili na Kamati ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.

Kwanini wamefukuzwa, kwanini wamepona?

Nchimbi, Sophia na Kimbisa walikuwa pamoja kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kukata jina la Lowassa miongoni mwa waliokuwa wakiwania urais kupitia chama hicho.

Hata hivyo, Sophia amefukuzwa kabisa wakati Nchimbi amepewa onyo na kutakiwa kuomba radhi huku Kimbisa akiwa amesamehewa makosa yake.

Raia Mwema limeambiwa kwamba kamati hiyo ya Mangula ilibaini kuwa wakati Nchimbi na Kimbisa walibadilika na kushiriki kikamilifu katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Sophia hakufanya hivyo.

Gazeti limeambiwa kwamba si tu kwamba Sophia hakushiriki kikamilifu kwenye kampeni hizo lakini kuna ushahidi wa yeye kuwa na mawasiliano yanayotia shaka na vyama vya upinzani vilivyounda Ukawa wakati huo.

“Ripoti ya Kamati ya Maadili iliweka bayana namna Sophia alivyokisaliti chama wakati huo. Baada ya ukweli kuwekwa hadharani, wajumbe wa NEC hawakuwa na namna zaidi ya kukubali afukuzwe uanachama.

“Hali ilikuwa hivyo kwa Msambatavangu wa Iringa. Kuna watu walitaka kumtetea lakini zilionyeshwa picha za yeye kushiriki kwenye kikao cha CCM siku moja na siku hiyo kushiriki kikao kingine cha Ukawa. Baada ya hapo hakukuwa na msalia mtume,” gazeti hili limeelezwa na kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Nchimbi alipewa kazi ya kuunganisha vijana wa CCM na wale walio kwenye vyuo vikuu ili kusaka ushindi na ilielezwa kazi yake ilikuwa nzuri. Kwa sababu hiyo, wajumbe wa NEC waliomba kwamba Nchimbi asifukuzwe bali apewe onyo.

Kwa Kimbisa, gazeti hili limeelezwa kwamba kwanza aliwahi kuomba radhi huko nyuma kutokana na tukio hilo la kupinga uamuzi wa Kamati Kuu, lakini kilichomwokoa zaidi ni namna CCM ilivyoshinda vema katika mkoa wa Dodoma ambako yeye ni Mwenyekiti wa Mkoa.

“Dar es Salaam kwa Madabida, CCM ilifanya vibaya sana . Ilipoteza majimbo ya Kinondoni, Ubungo, Kawe na Kibamba. Na ilionekana yeye hakufanya jitihada za maana kuokoa chama chake.

“ Lakini kwa Kimbisa kule Dodoma, CCM ilishinda majimbo yote. Wapinzani hawakuambulia kitu. Kama Kimbisa angekuwa amecheza faulo kama za Dar, CCM ingeshindwa na upinzani. Hapo ndipo alipookoka,” Raia Mwema limeambiwa.

Kwa ujumla, wenyeviti wote na wajumbe wa NEC waliovuliwa nyadhifa zao au kuadhibiwa wanatoka katika maeneo ambako CCM hakikufanya vema.

Bashe, Malima na Msukuma

Mojawapo ya tukio lililokuwa sehemu ya mkutano huo ilikuwa ni kuwekwa ndani kwa wabunge wawili wa CCM; Hussein Bashe na Joseph Rusheku (Msukuma) pamoja na mjumbe wa NEC, Adam Malima.

Raia Mwema limeelezwa kwamba vyombo vya usalama vya CCM vilielezwa kwamba wanachama hao watatu walikuwa na mipango ya kuvuruga vikao hivyo na ndiyo sababu wakakamatwa.

Hata hivyo, kinyume cha taarifa za awali kwamba wanasiasa hao walikuwa na kiasi kikubwa cha fedha walichotaka kukitumia kuvuruga vikao hivyo, hakuna aliyekutwa na ushahidi wa kuthibitisha.

“ Ndiyo maana nakwambia, kuna watu wanataka kumharibia Magufuli. Wanataka kumgombanisha na watu ambao wanamuunga mkono. Mambo ya Lowassa yameisha. Tujenge CCM ya Magufuli, mmoja wa watu walio karibu na viongozi hao aliliambia Raia Mwema juzi Jumatatu.

Akizungumzia matukio ya vikao hivyo, msemaji wa zamani wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema hatua zilizochukuliwa na chama chake ni sahihi, zimekuja kwa wakati.

 “Uamuzi wa NEC ( Halmashauri Kuu) ni sehemu ya mabadiliko yatakayokiwezesha Chama kuwa na wanachama waadilifu na si mara ya kwanza kwa CCM kufukuza wanachama wake wa ngazi za juu ukiukwaji wa maadili na utovu wa nidhamu.

“Hili la kufukuza, kutoa onyo kali kuvuliwa uongozi ni utaratibu wa chama chochote cha siasa kwamba lazima tufike mahali mtakase safu ya uongozi  ili kupata uongozi utakaotoa matumaini kwa wanachama na wananchi,” alisema.

Akizungumza kwa mifano, Sendeka alisema CCM kimewahi kufukuza wanachama wake huko nyuma, mwaka 1988, ambapo kilimfukuza uanachama Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu pamoja na NEC pamoja na wenzake saba wakiwemo mawaziri kwa kukiuka maadili ya chama na kimeendelea kuwa imara hivyo hilo si jambo geni kwa CCM kufikia maamuzi magumu.

Mazingira ya mabadiliko ndani ya Chama yanayopunguza wingi wa wa vikao vya Chama huku muundo ukibaki uleule isipokuwa idadi ya wajumbe. Mfano Kamati kuu itapungua kutoa 34 hadi 24, Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi 163 huku Mkutano Mkuu ukipungua kutoka 2,380 hadi 1,706 tu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisisitiza kuwa mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho ni jambo la kawaida na kwamba yalianza tangu muda mrefu na kwamba wapinzani wao walifikia hatua ya kukopa sera yao wakidhani ni jambo jipya.

Alisema CCM ni chama kikubwa na kina misingi yake iliyojengwa madhubuti katika kuwatumikia wananchi wanyonge na ndio maana bado inaaminika na kupewa kura nyingi za urais, ubunge udiwani na serikali za mitaa.

“Mabadiliko haya ni ya kawaida kabisa, na tutazidi kuwa imara zaidi, hakuna wa kuiyumbisha CCM. Chama hiki kitaendelea kubaki imara na wananchi wanatuamini na wanatuelewa,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *