Magufuli apingwa

UAMUZI wa Rais John Magufuli kufuta Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), umekosolewa na wataalamu wa mipango miji huku wakieleza kuwa itaigharimu nchi kwa siku zijazo kwa kuwa umelenga zaidi maslahi ya kisiasa na si uhalisia.

Wakizungumza na Raia Mwema kwa nyakati tofauti muda mfupi baada ya tangazo la rais, baadhi ya wataalamu hao wamesema ni ukweli kwamba wananchi wa Dodoma wamekuwa wakilalamikia CDA lakini ni kwa sababu ya uzembe wa serikali na maslahi ya kisiasa tofauti na kazi kubwa iliyofanywa na mamlaka hiyo katika mazingira magumu tangu ilipoanzishwa.

“CDA ilianzishwa kwa lengo la kuhamisha serikali kwenda Dodoma, sasa rais ametangaza kuhamisha serikali, wajanja wakamuwahi kumpa taarifa za uchonganishi ili wafaidike na ardhi maana wanajua CDA haiyumbi kwenye kufuata sheria. Kama ilikuwa ni lazima kufanya uamuzi huu, ni heri Rais angefanya hivi mwaka 2020 baada ya yeye kuwa amehamia.

“Sasa tusubiri tsunami ya vurugu. Hatuwezi kuona athari za uamuzi huo wa Rais leo au kesho lakini baada ya miaka mitano tutaikumbuka CDA na serikali itaingia gharama kubwa bila sababu za msingi,” alisema mmoja ya wahandisi wa mamlaka hiyo ambaye aliomba asitajwe jina kutokana na nafasi yake kikazi kwa sasa.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya CDA zinaeleza kuwa wakati tangazo hilo linatolewa na Rais,  tayari wafanyakazi walikwishajua kila kitu kwa kuwa kumekuwa na taarifa za wanasiasa waliokuwa wakieleza kuwa ni lazima wafutwe kwa kuwa wanakalia ardhi badala ya kuiachia na kutoa kipaumbele kwao katika ugawaji.

“Ili upate ubunge Dodoma ni lazima uiseme vibaya CDA na kusema kweli hata sisi wafanyakazi tulikwishakatishwa tamaa sana na maneno ya hapa na pale. Huwezi kuamini kwa mara ya mwisho tulipewa fedha na serikali mwaka 2015 na sasa tunajiendesha wenyewe. Lakini kila siku hakuna kizuri kinachofanywa na mamlaka hii licha ya mji wa Dodoma kujengwa kwa mpangilio kwa asilimia 75 na ndio mji pekee Tanzania uliojengwa kwa kuzingatia sheria namba nane ya mipango miji ya mwaka 2007,” alisema mtaalamu huyo.

Mmoja wa Watanzania wanaoifahamu vema CDA tangu kuanzishwa kwake, alilieleza gazeti hili kwamba uamuzi huo wa Rais unamaanisha kwamba sasa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kupitia Baraza lake la Madiwani itakuwa na uwezo wa kugawa ardhi inavyotaka na muda si mrefu mji huo hautakuwa tofauti na majiji mengine yaliyopo nchini.

Alisema pamoja na matatizo yote yanayoelezwa kuwapo CDA, bado mji huo ulikuwa umepangika kuliko yote mingine nchini; kwa kuwa mamlaka hiyo iko makini katika kuhakikisha kila kinachofanyika kinaendana na mpango uliokuwepo.

“ Zamani Dodoma hii ilikuwa kama jangwa kabisa. Hii miti ambayo sasa unaiona mjini ni matunda ya wataalamu wa CDA. Bila ya mamlaka hiyo, utaanza kuona Dodoma nayo inakuwa na maeneo kama Manzese Dar es Salaam ambayo usingeweza kuyaona kupitia CDA,” alisema.

Alisema CDA ilikuwa na ufanisi kwenye miaka ya nyuma kwa sababu ilikuwa ikisimamiwa na Ikulu yenyewe, huku bodi yake ikiundwa na mawaziri sita –wawili kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wanne wa Serikali ya Muungano. Pia, Waziri aliyehusika na Wizara ya Ustawishaji Makao Makuu alikuwa na bodi ya ushauri iliyokuwa na wataalamu kutoka Australia, Mexico, Canada na Marekani.

Mmoja wa washauri hao alikuwa ni Sir John Overall, raia wa Australia aliyepewa kazi ya kuugeuza mji wa Canberra nchini kwake kutoka mji uliokuwa katikati ya pori na kuwa mji wa kuvutia.

Mipango iliyoachwa mezani CDA

Wakati mamlaka hiyo ikivunjwa wiki hii, kulikuwa na mambo makubwa matano yaliyokuwa yakishughulikiwa na chombo hicho katika juhudi za kufanikisha serikali kuhamia Dodoma na kuhakikisha mji huo unajengwa kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za mipango miji.

Mojawapo ya mipango hiyo ni kupima viwanja 20,000 vya makazi, biashara na maeneo ya huduma za kijamii, kukamilisha kazi ya kulipa fidia eneo la ujenzi wa bandari kavu katika eneo la Ihumwa ambapo tayari mamlaka hiyo imepata orodha ya wanaostahili kulipwa na kufanya tathmini ya fidia.

Kazi nyingine ni kukamilisha mpango wa kuingiza viwanja vyote katika mfumo mpya wa kisasa maarufu kama Land Rent Management System (LRMS), mfumo mpya wa kuhudumia wateja kwa haraka, matumizi ya taarifa za kijiografia unaotumika katika usanifu wa majengo, mipango mijini na matumizi bora ya ardhi pamoja na mfumo mpya wa usimamizi wa ukusanyaji mapato.

CDA ilianzishwa mwaka 1973 kwa tangazo la Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere na kuanza kazi rasmi mwaka 1976 baada ya kukamilika kwa Mpango Kabambe. Hata hivyo, hadi mwaka 2007 CDA haikuwa na orodha ya viwanja vyake hali iliyosababisha mamlaka hiyo kuanza kupitia upya kazi zake na hadi sasa viwanja vinavyotambuliwa rasmi na mamlaka hiyo ni 56,000.

Mpango wa Ujenzi wa Mji Mkuu (Master Plan) wa CDA ulikuwa katika hatua za mwisho wakati Rais Magufuli alipotangaza kuhamisha serikali kwenda Dodoma, lakini baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhamia mjini humo serikali iliunda kamati maalumu ya kupitia upya mpango huo.

Wajumbe wa kamati hiyo walisafirishwa kwenda nje ya nchi kujifunza jinsi ya kupanga miji  -jambo linalolalamikiwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwa mambo waliyojifunza ni sawa na yale yaliyokuwa yakipangwa na CDA katika mpango mpya wa mwaka 2010.

Raia Mwema linafahamu kwamba hadi wakati Magufuli akitoa tangazo hilo jipya, CDA ina wafanyakazi wa kada mbalimbali 276, ina vifaa vyote vya ujenzi, nyumba kadhaa na vitendea kazi mbalimbali.

Wakati hayo yakiendelea, wabunge kadhaa hususani wa mkoani Dodoma wamempongeza Magufuli kwa kuchukua hatua hiyo na kuweka wazi kuwa imekuja kwa wakati mwafaka kwa maslahi ya wananchi walio wengi.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, Felister Bura, alisema kwa muda mrefu wananchi wa Dodoma wamekuwa wakiilalamikia CDA kuvunja nyumba zao na kuchukua ardhi bila kuwalipa fidia.

Amewatoa hofu wananchi ambao tayari wamelipia viwanja lakini hawajapatiwa viwanja kuwa na amani kwa kuwa haki zao zitalindwa kupitia Manispaa ya Dodoma. Naye Mbunge wa Vwawa,  Japhet Asunga, ameungana na Bura na kueleza kuwa serikali ina lengo zuri  kuivunja CDA kwa kuwa ilikuwa inasababisha mgongano kwa kukinzana na sheria za serikali za mitaa hivyo kuleta kero.

Kwa upande wake, Mbunge wa Busega,  Dk. Raphael Chegeni, alisema uamuzi wa rais kuivunja CDA ulitegemewa na wengi kwa kuwa haikuwa na viwango na ilikuwa ikizuia wawekezaji kutokana na kutoa hatimiliki ya ardhi kwa muda wa miaka 33 badala ya 99.

 “Sura ya nchi imechukuliwa na Dodoma baada ya kutangazwa kuwa Makao Makuu ya nchi na hivyo haina budi kuruhusu wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza,  CDA haikuruhusu  wawekezaji kuwekeza kutokana na ardhi yote kuwa mali ya CDA  hivyo kuwatia hofu wawekezaji,” alisema Chegeni.

Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema mamlaka hiyo imekuwa kikwazo kwa muda mrefu kutokana na kumiliki ardhi ya Dodoma bila ya kuwa na watu na kuongeza kuwa hakuna sheria iliyounda CDA bali ni tamko lililotolewa na serikali tu.

Kwa upande wake Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigalla, amesema rais ana maono yake na kuna mahali anataka kuifikisha Dodoma kama makao makuu ya nchi kwamba amezingatia ndoto zake kuufanya kuwa Jiji.

One thought on “Magufuli apingwa”

  1. Massanda O'Mtima Massanda says:

    Kama kutoka 1976 hadi 2007 walikuwa bado hawajawa na orodha ya viwanja vilivyopimwa, basi ina maana kwamba hawakutenda kazi zao inavyopaswa.

    Juu ya hayo, raisi amesema wataalam wa CDA watahamishiwa Manisipaa na sehemu zingine kulingana na utalaam wao ikiwa na maana kwamba bado utalaam wao utakuwa na nafasi ya kuuweka mji wa Dodoma katika hali iliyokusudiwa.

    Aidha, miji / majiji yaliyorejelewa na watalaam hao wa iliyokuwa CDA kwamba imekaa shaglabagla, inadhihirisha jinsi watalaam wetu wasivyowajibika kiweledi na hivyo kufanya miji / majiji yetu yawe kama yalivyo.

     

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *