‘Magufuli atakataa ushauri’

Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki aliyeko kwenye matibabu ya majeraha ya risasi Ubelgiji ameliambia Raia Mwema Jumatano kwamba haamini kama Rais Dk. John Magufuli anaweza kupokea ushauri wake.

Ameeleza msimamo wake huo katika mahojiano yake kwa njia ya mawasiliano ya simu kutokea nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu, baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi kadhaa, Septemba mwaka jana.

“Ungekuwa mshauri wa Rais katika awamu hii, ungeshauri nini kuhusu hali ya kisiasa, uchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla?” liliuliza swali la gazeti hili kwa Tundu Lissu.

Katika kujibu, Lissu alisema; “Kwa kadiri ninavyomfahamu Rais John Magufuli, sidhani kama ningeweza kuwa mshauri wake au hata kama angeweza kukubali ushauri wangu. Na wala asingekuwa anakosea.”

Akaendelea kueleza; “Katiba ya Tanzania imetamka wazi, tangu mwaka 1962 kwamba Rais hawajibiki kufuata ushauri wa mtu yeyote katika utekelezaji wa majukumu yake kama Rais. Ukiwa na Katiba ya aina hiyo, na ukiwa na Rais wa aina ya Magufuli, basi Mungu atusaidie.”

Lissu, katika mahojiano hayo alizungumzia pia masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

TLS na ofisi ya AG

Lissu alizungumzia baadhi ya masuala yanayoendelea kati ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Dk. Adelardus Kilangi, na hasa madai ya kutengenezea kanuni kwa TLS.

“AG hana mamlaka kisheria kutengeneza kanuni za aina yoyote kwa TLS. Mamlaka hayo kwa mujibu wa sheria ya TLS ni ya governing council (baraza la uongozi) na wanachama wetu kupitia mkutano mkuu wa wanachama. Na wala hakuna masharti yoyote kwenye sheria mama kwamba kanuni za TLS zinatakiwa kuwa ‘gazetted’ (kutangazwa katika gazeti la serikali). Walioamua kwamba kanuni za uchaguzi wa TLS zilizopitishwa kihalali na governing council zipelekwe kwa AG kwa ajili ya kuwa ‘gazetted’ walifanya hivyo kinyume cha matakwa ya sheria mama.

“AG ametaja vifungu vingi vya sheria ili kuhalalisha alichokifanya. Hakuna kifungu chochote kwenye sheria kinachompa mamlaka hayo. Kwa mujibu wa sheria mama ya TLS na sheria za kimataifa tulizoziridhia, mawakala na wanataaluma ya sheria wanatakiwa kuwa huru dhidi ya kuingiliwa na serikali.

Alizungumzia pia athari zinazoweza kujitokeza endapo uamuzi wa AG utaachwa kama ulivyo akisema:

“Ukiachia mbali kwamba kitendo cha AG kinakiuka sheria za nchi yetu, kuachia uamuzi huo uendelee ni kuhalalisha serikali kuingilia masuala ya TLS na uendeshaji wa taaluma ya sheria. Hali hiyo ikiruhusiwa basi itakuwa na athari kubwa na ya moja kwa moja kwa haki za wananchi. Mawakili wataanza kuogopa kuwakilisha wananchi kwenye kesi ambazo serikali inaziona zina masilahi au athari za kisiasa.”

Alizungumzia pia kuhusu sahihi iliyopo kwenye kanuni za uchaguzi wa TLS, akisema sahihi iliyopo kwenye kanuni za uchaguzi si yake na wala haijaweka kwa ridhaa yake.

“Mimi sijasaini nyaraka yoyote kutoka Sekretarieti ya TLS tangu Septemba mwaka 2017 nilipopigwa risasi na kujeruhiwa vibaya. Nasikia kuna watu wanaosema sahihi yangu iliwekwa kwa maagizo ya governing council ya TLS. Kama ni hivyo basi huo ni uthibitisho mwingine kwamba hiyo si sahihi yangu bali iliyowekwa na mtu mwingine kwa maagizo ya watu wengine. Wangekuwa wanataka kufanya mambo kihalali wangeniletea hizo nyaraka kwa DHL nikazisaini na kuzirudisha kwa njia hiyo hiyo.

“Au wangeniuliza kwanza ili niwape ridhaa ya kutumia sahihi kwenye nyaraka hizo. Hilo nalo hawakufanya. Kwa hiyo, kanuni hizo hata wazitetee namna gani ni batili, ukiachilia mbali yaliyoingizwa ndani na AG,” alisema Lissu ambaye anamaliza muda wake wa urais TLS mwezi ujao, Aprili, 2018.

Ndege za serikali

Lissu pia alizungumzia kuhusu ndege za serikali (bombardier Q400-Dash8) zinazoendelea kusubiriwa ‘kuwasili’ nchini.

Ikumbukwe kuwa Lissu ndiye aliyekuwa mmoja wa wanasiasa wa kwanza kueleza hadharani kwamba ndege hizo aina ya Bombardier zimeshikiliwa nje ya nchi na mdai mmoja wa serikali, ambaye ni kampuni ya Stirling Civil Engineering iliyokuwa imevunjiwa mkataba wake kabla ya muda, mkataba wa ujenzi wa barabara kuanzia eneo la Wazo Hill, Dar es Salaam hadi Bagamoyo mkoani Pwani.

Katika hilo, Lissu alisema; “Suala la msingi ni kwamba tunadaiwa fedha nyingi na mali za nchi zimekamatwa kwa sababu ya tabia ya kupuuza masharti ya kisheria kwenye mikataba ambayo serikali inaingia na watu au taasisi za ndani na nje ya nchi.

“Bombardier imekamatwa kwa sababu aliyekuwa Waziri wa Ujenzi alifanya makosa (wakati wa kuifukuza kampuni hiyo ya ujenzi). Kwa sababu ya makosa yake, tulishitakiwa na kushindwa kesi. Baada ya kushindwa kesi, hatukulipa deni la wadai wetu kitendo kilichosababisha ndege yetu kukamatwa.

“Hata kama ndege hiyo itaachiwa tutakuwa tumeingia hasara ya aina mbili; kwanza tutakuwa tumeilipia ndege pesa nyingi kuliko thamani yake halisi wakati tunainunua.

“Pili, ndege hiyo ilipaswa kuletwa nchini tangu Julai mwaka jana (2017), lakini mpaka sasa haijaletwa. Katika wakati ambao inaletwa, tutakuwa tumeingia hasara ya kutokuitumia kwa takribani mwaka mzima au zaidi.”

Kauli za Rais Magufuli

Lissu alipata fursa pia ya kueleza kuhusu kauli za Rais John Magufuli, ambaye hivi karibuni aliwataka Watanzania wamuamini, kwamba wana “Rais jiwe kwelikweli” asiyetishwa wala kutishika, na hata akienda mbinguni Mungu akamchague (kwa kuwa alikuwa kiongozi mzuri) anaweza kuongoza malaika.

“Baada ya miaka miwili, Rais Magufuli amethibitisha jinsi ambavyo kuna kasoro katika uongozi. Hali ya kisiasa nchini imeharibika kuliko kipindi kingine chochote tangu uhuru. Kuna watu wana hofu. Kuna mabavu na uonevu.

Siasa jimboni kwake

Lissu alizungumzia baadhi ya matukio katika Jimbo ambalo yeye ni mbunge, Jimbo la Singida Kaskazini, hasa tukio la hivi karibuni la mbunge mwingine kutoka Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, kutoa zawadi ya vitanda katika Jimbo la Singida Mashariki (chini ya Lissu).

“Kuhusu zawadi ya mheshimiwa Kingu jimboni kwangu hiyo ni siasa ya kijinga sana. Wilaya ya Ikungi ina hospitali chache sana zenye uwezo wa kulaza wagonjwa. Kubwa kati ya hizo ni hospitali mbili za Kanisa Katoliki, Makyungu nilikozaliwa mimi na Puma, na sidhani kama zina tatizo la vitanda vya wagonjwa.

“Zilizobaki ni vituo vya afya vya serikali ambavyo havina uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya 10 kila kimoja kwa wakati mmoja.

“Kimojawapo ni Kituo cha Afya Ikungi jimboni kwangu ambacho kwa taarifa zangu hakijapelekewa kitanda hata kimoja kwa sababu hakina tatizo la vitanda. Sasa hivyo vitanda 72 vinavyosemwa vimepelekwa jimboni kwangu na mheshimiwa huyu viko wapi kama si siasa za kijinga tu?

“Hata kama angepeleka jimboni kwake asingepata mahali pa kuviweka kwa sababu vituo vya afya vya Ihanja na Sepuka havina uwezo wa vitanda vingi vya namna hiyo. Ninayafahamu maeneo hayo sana.

Kuhusu maandamano je?

Kuhusu kuwapo kwa kauli za viongozi mbalimbali juu ya kufanyika kwa maandamano hapo Aprili 26, mwaka huu, Lissu alisema; “Kuhusu maandamano ya Aprili 26, msimamo wangu kwa wale wanaotoa vitisho vya kuua watu au vitendo viovu, ni kwamba kama maandamano yangekuwa jambo baya kiasi hiki kwa nini yameruhusiwa kwenye Katiba na sheria za Tanzania? “Ina maana wale wanaCCM waliopitisha Katiba na sheria za kuruhusu maandamano walikuwa na kasoro kifikra?

Lissu amekuwa akiendelea na matibabu nchini Ubelgiji kutokana na majeraha ya risasi alizopigwa Septemba 7, 2017 majira ya saa saba mchana.

Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Dodoma Area D. Baada ya kupata matibabu ya awali, Lissu alisafirishwa hadi jijini Nairobi kwa matibabu zaidi, na baada ya hapo, alisafirishwa kwenda Ubelgiji.

Kati ya watu waliosikitishwa na shambulizi hilo la Lissu ni pamoja na Rais Magufuli ambaye baada ya tukio hilo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa twitter, akilaani vikali tukio husika.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyeshikiliwa na vyombo vya dola akituhumiwa kuhusika katika shambulizi hilo, licha ya familia ya Lissu, na Tundu Lissu mwenyewe kuiomba serikali kupitia ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) kuruhusu wapelelezi wa kimataifa kuchunguza tukio hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *