Makala
KESI YA LEMA
Majaji wana chanjo ya kutotumiwa kisiasa?
Msomaji Raia
Toleo la 234
11 Apr 2012

KESI ya kupinga matokeo ya uchaguzi jimboni Arusha Mjini imekwisha. Uchaguzi wa mbunge Godbless Lema umetenguliwa na sasa yuko nje ya jengo la Bunge.

Jaji Gabriel Rwakibarila alitoa hukumu hiyo wiki iliyopita na kuacha gumzo kubwa linaloendelea kujadiliwa nchi nzima. Kwa kuwa kesi imekwisha, naamini ni ruksa kwa yeyote kujadili anavyoweza.

Yako masuala kadhaa yanayovutia kusikiliza yakijadiliwa. Nami napenda nijadili baadhi yake kwa lengo la kupanua mjadala huu.

Kimsingi, nimesikia ubunge wa Lema umebatilishwa kwa sababu ya vitendo vyake vya kumkashifu mgombea mwenzake katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010. Kwa watu wenye msimamo huu, wanamwona Lema  kuwa ajilaumu mwenyewe kwa kukosa staha dhidi ya mwenzake na kutamka maneno yaliyomdhalilisha na kumpunguzia utu wake mbele ya jamii. Kwao hawa, Jaji Rwakibarila amemtumia Lema kummaliza Lema, yaani Lema alimpatia Jaji silaha ya kutumia kummaliza kisiasa.

Lipo kundi jingine linaloona Jaji amekuwa mwanasiasa kuliko Lema na Batilda Buriani. Hukumu ya Jaji imejikita zaidi katika makosa ya kashfa dhidi ya Batilda Buriani. Ili kuthibitisha makosa haya ni ama Batilda angefika mahakamani kama mlalamikaji au kama shahidi. Yote mawili hayakutokea. Badala yake wawakilishi watatu wa Batilda wakafika kulalamika kuwa Batilda amekashfiwa. Kitendo hiki kinaonekana kama kasoro inayotumiwa na wanaomlalamikia Jaji Rwakibalira.

Lipo kundi jingine kubwa linalotetea upekee, uhuru na utakatifu wa mhimili wa Mahakama. Kwamba, mahakama zetu ziko huru, ni za pekee na takatifu katika uwanja wa utoaji haki.

Wanamtaka Lema na chama, kuheshimu maamuzi ya Mahakama na kama hawajaridhika wakate rufaa katika ngazi nyingine ya mhimili ule ule ulio wa pekee, huru na mtakatifu. Watetezi wa uhuru wa Mahakama, wanasisitiza kuwa mizengwe ya kisiasa, fitna za kisiasa na mikakati ya kimaslahi, viko nje kabisa ya uzio wa Mahakama.

Hawa wanatutaka tujilazimishe kuamini kuwa majaji na mahakimu hawasomi magazeti, hawasikilizi radio, hawaendi misibani, hawana mahusiano na wanasiasa kiasi cha kuguswa mistakabali yao kisiasa, na kamwe hawana huruma wala upendeleo dhidi ya wale wanaowateua kuingia katika mhimili huo.

Kesi ya Lema kwa upana wake ilibua masuala mengi sana. Wale wanaolazimika kunusa mkono wa wanasiasa nyuma ya hukumu ya Jaji wana kila sababu za kufanya hivyo. Kwa maneno mazito zaidi ningesema, wamelazimishwa pasipo kutaka kwao, kuamini kuwa kuna mkono mzito wa wanasiasa.

Ushahidi wa karibuni ni pale Ikulu yetu kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilipokanusha vikali ndani ya saa chache, tuhuma zilizorushwa na Lema dhidi ya Ikulu kuwa ilikuwa imehusika na uandaaji wa hukumu hiyo.

Kwa kuwa imezoeleka kuwa Kurugenzi hiyo ikisema suala fulani ni kweli linakuwa ni kinyume chake, na ikisema ni uongo inakuwa inamaanisha ni kweli, basi kanusho la Ikulu lilithibitisha pasipo shaka wasiwasi huo wa baadhi ya watu.

Sambamba na uzoefu huo dhidi ya Kurugenzi ya Mawasiliano, upo ukweli mwingine kuwa Kurugenzi hiyo imekuwa kimya sana au kuchelewa sana kutoa ufafanuzi wa masuala mengine makubwa. Kwa hili la Lema, ilijitokeza ndani ya saa machache na kwa kutumia maneno ambayo uchaguzi wake uliacha shaka kubwa kama taarifa ile iliandaliwa Ikulu yetu.

Kesi ya Lema iliigusa Ikulu pale Jaji wa awali alipokataliwa kwa madai kuwa alikuwa na maslahi hasi dhidi ya CHADEMA kutokana na chama hicho kutuhumu baadhi ya wateule katika wizi wa fedha kutoka Benki Kuu. Mnyororo ulichorwa na Lema kuonyesha uhusika wa jaji huyo na baada ya mvutano mfupi lakini mkali, Jaji huyo alijitoa.

Pamoja na kwamba ni haki ya mshitakiwa kumkataa jaji, lakini kitendo cha kumkataa jaji kwa sababu za kisiasa, kiliacha doa kubwa katika mustakabali wa kesi hiyo. Jaji kutuhumiwa kuwa na maslahi ya kisiasa, ni sawa na mke wa Kaisari kutuhumiwa uzinzi.

Baadaye kesi ya Lema iliibua masuala mengine ya wanasiasa wakubwa. Mara Batilda ana mimba ya mkubwa mmoja nje ya ndoa; mara Batilda ni Al-Qaeda; mara uchaguzi utarudiwa wakati kesi ikiwa inaendelea!

Kwa maoni yangu, madai ya mimba ile ilileta balaa katika kesi ya Lema. Si tu kuwa madai yale yangeweza kuleta balaa katika ndoa ya Batilda, bali kuikanusha au kuithibitisha kungedai Batilda na mzito huyo wafike mahakamani kutoa maelezo ya ziada.

Je, kutofanyika kwa hilo kwaweza kuwa ndiyo chanzo cha watu kujadili na kuhoji uhalali wa hukumu hii? Je, madai ya mimba nje ya ndoa ndicho chanzo cha kubadili kesi kutoka ile ya uchaguzi na kuwa kesi ya kashfa? Iwavyo na iwe, mimba ile imeleta balaa kubwa katika historia ya utoaji haki hapa nchini.

Mpaka hapa ni sahihi pia kuhoji ikiwa majaji wetu wako salama na michezo ya kisiasa. Hawa ni watu muhimu katika wajibu wa kutoa haki, je, wanayo chanjo ya kuwazuia kupata ugonjwa unaoitwa siasa?

Kama wanayo mbona hawa wao wenyewe wanatuhumiana na kuitana majina ya bandia. Wako majaji wanaoitwa “M-serikali”, “Wa system”, wa  “Voda Fasta”, “Wa Ikulu” na “wa awamu ya nne”.

Ubaguzi huu ikiwa unaonekana wazi wazi katika mahusiano ya majaji wenyewe, ni wazi basi makundi haya yatakuwa yanajitahidi kuhakikisha kuwa utambulisho wa kundi lao unadumishwa kwa njia yoyote.

Mchezo wa majaji hawa ni mauti ya Watanzania wanaotarajiwa kupata haki katika Mahakama zao wanazolipia kodi kwa jasho na damu.

Uwepo wa makundi maslahi miongoni mwa majaji, ni uthibitisho kuwa siasa inatumika katika uteuzi wao na vigezo vingine visivyofahamika wazi. Ikiwa vigezo hivyo vipo, ni wazi kuwa vinatumika kushawishi maamuzi na hukumu za majaji hao. Ni balaa kwa Watanzania kukaa na kuamini kuwa majaji wetu wana kinga za kuwazuia kuwa wanasiasa katika mawazo na maamuzi yao.

Mfumo wao wa uteuzi na mazingira yao ya kufanya kazi, vinategemea ama fadhila za wanasiasa au maamuzi ya kisiasa, ya moja kwa moja, au yale ya kupitia kwa Jaji Mkuu.

Tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa wakiwalazimisha mahakimu kuwanyima dhamana watuhumiwa; tumeshuhudia ma-DC na ma RC wakiiomba mahakimu fulani wahamishwe kwa sababu ni kikwazo kwa maslahi ya wanasiasa fulani.

Tumeshuhudia mahakimu wakifichwa na kutoroshwa ili wasiweke sahihi fomu za wagombea wa vyama fulani wakati wa uchaguzi; tumemsikia Jaji Mkuu wa sasa akilalamika kuwa uhuru wa Mahakama haupo kwa sababu wakuu wa wilaya na mikoa ni wajumbe wa kamati za nidhamu za mahakimu.

Tumemsikia mara kadhaa Jaji Mkuu aliyepita na huyu wa sasa, wakilalamika kuwa kukosekana kwa bajeti ya kutosha ya kuendesha Mahakama kunainyima uhuru Mahakama.

Tumewasikia wasajiri wa mahakama zetu wakilalamika wanavyohangaishwa na vijana wadogo kule Hazina, wakiwalazimisha watoe chochote ili kupitishiwa mafungu ya Mahakama.

Tumeshuhudia jaji mstaafu aliyekuwa mgonjwa akihitaji kwenda nje kwa matibabu, akilazimika kushinda kwenye benchi la Hazina kubembeleza ili fungu litoke aende matibabu. Tumeshuhudia jaji fulani akipatiwa maslahi yake kwa haraka kwa sababu wakati wa ujaji wake alikuwa mzuri sana kwa wanasiasa.

Hata kama inaweza kudaiwa kuwa majaji wetu hawaingiliwi na wanasiasa kwa njia ya wazi, tukubaliane kimsingi kuwa, kuwaingilia majaji kwa njia ya kificho ni hatari zaidi kuliko wangeiliwa kwa uwazi na kila mtu akajua.

Kwa hili la Lema, Serikali imetuandalia mazingira ya kutoiamini Mahakama kwa sababu, Lema tangu achaguliwe kuwa mbunge, amefanywa kuwa tatizo kubwa kuliko matatizo mengine yanayolikabili Taifa letu.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Msomaji Raia
msomajiraia@yahoo.co.uk

Maoni ya Wasomaji

Msomaji Raia. I always read your articles with a lot of admiration. Your article is nothing less than the position whether we like it or not. If there are   doubting Thomases, let them do a research and prove Msomaji raia wrong.
Cheers 

The truth is Mahakama zetu haziko huru, wanasiasa wanaziongoza na kuzishurutisha......hata hivyo tuendelee kuziamini ili tupate nafasi ya kufanya marekebisho...na kubwa ni kwa majaji kutoteuliwa na Raisi wachaguane miongoni mwao nakuthibitishwa na chombo husika

Msomaji raia, nafarijika kwa kuwa unachokiandika ni ukweli wa yule anayeishi Tanzania. Ukiona wachache wanataka watu waamini kwamba mahakama zetu ziko huru, basi jua kwamba aidha hawajawahi kufika huko, au hawasumbui bongo zao....mfano ni kesi ya mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mtikila.
Another nice peace of narration from Mosomaji Raia Mwema,
Asante sana kwa makala murua!

Ni sawa na mke wa Kaisari kutuhumiwa uzinzi. kweli nime ipenda hii Nukuuu, Mwl. Julias aliwahi kusema katika uhai wake kwamba CCM sio mzazi wake wa kike (yaani Mama yangu). Kwa maana kwamba CCM Ita Tawala lakini mwisho wa siku Tanzania kwanza. Maana yake ni kwamba Angeweza kutoka CCM nakujiunga na chama chochote kile cha Siasa au hata kama Angekuwa sisim hawezi kuamini kila kinacho tendwa na CCM.
Lakini maamuzi ya Jaji huyu anafikiri nje ya CCM hakuna maisha, Ni aibu na Fedheha kubwa sana kwa msomi kama huyu. Sababu anazidi kuichimbia kaburi CCM.
Sipendi kuamini Jaji huyu kama amesoma kwa kodi za watanzania walio Ambiwa na Julias, wafunge Mikanda ili yeye aweze kwenda shule, kama kweli alikwenda shule kwa kodi za Babu na Bibi yangu pale Chiulu na kule Nyambiti au Itumbili pale Magu, hangeweza kutumia Ushahidi wa mtu ambaye hakuwa Mgombea nakuamini kuwa kilicho ongolewa ni sawa.
 Hakika tutahukumiwa kwa Matendo yetu, na chochote kile tunacho kifanya, lazima tuogope Mungu, Tusije kutuhukumiwa. Hivi huyu Jaji anasali kweli? Sitaki kuamini kama anaweza kunyonga haki kwa kiwango hiki.
Hebu tusifike sehemu tusianze kuitwa oooh huyu wasisiemu ohhh huyu wa Systerm na majina kama hayo lakini kiukweli wacha waende.
 aaa Inauma si kwamba, Lema hana hatia, la hasha...!
 lakini Angalau hiyo hukumu Ingekuwa na Mashiko yenye maana.
               Ni hayo inauma saaaaana.

Ni ajabu, hawa walioshitaki sijawahi kuwasikia kwenye harakati zozote za haki za binadamu tangu kabla na baada ya mfumo huu wa vyama vingi kuanzishwa. Kuna kashfa nyingi za wazi na pia kunyimwa kwa haki kumetapakaa nchi nzima, ikiwemo kunyanyasa wajane, yatima, albino nk. Kina Mama Nkya, Bisimba na wengine wanajulikana kwa kupigania haki kwa yeyote yule, ilikuwaje hawa wakahuzunika kusikia maneno ya kashfa na ubaguzi kwa ya Lema tu ilhali mambo haya yapo na hatujawasikia kuwemo kwenye harakati kama hizo. Sina maana kuwa kama ni kweli wasilalamike lakini ni lazima mtu unayeweza kuchukua hatua kama hiyo lazima uonyeshe uhalisia wako na si kuramba makombo kwa sababu ya ufukara wako iwe kimawazo ama kiuchumi. Mbunge wa Mtera ametukana kule Arumeru Mashariki, jamaa hawa watamfungulia mashtaka? Wao kichowauma ni kwa huyo tu waliyempenda isipokuwa kwa wengina haiwaumi? Nadhani huu ni upungufu wa fikra. Ni aibu.

Toa maoni yako