Mamia washindwa kuuza hisa zao DSE

Afisa Mtendaji wa DSE Moremi Marwa

Mamia ya wawekezaji kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wanashindwa kuuza hisa zao kutokana na kukosekana kwa wanunuzi, hasa kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka, ambapo wanunuzi wengi wanakabiliwa na mahitaji mengine ya kifedha.

Ripoti za soko la hisa kwa wiki jana zilionyesha kwamba, kulikuwepo na idadi kubwa ya hisa zilizohitaji kuuzwa, ikilinganishwa na idadi idadi ya mahitaji ya hisa kwa wawekezaji wanaotaka kununua.

Raia Mwema imebaini kwamba wawekezaji wengi hivi sasa wanakimbilia hisa za kampuni ya soko (DSE) ambayo iliorodheshwa mwezi Juni mwaka jana, na kampuni nyingine zikiwemo ya bia Tanzania (TBL), Kampuni ya Sigara (TCC), Twiga Cement na TOL Gases ndizo zilizoambulia wawekezaji wiki jana.

Ripoti zimeonyesha kwamba, wawekezaji kwenye kampuni zote zilizoorodheshwa ndani ya nchi ndio wanaouza hisa zao nyingi kwa sasa, huku idadi ya wanunuaji wakiwa ni wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Kampuni zilizoongoza kwa wingi wa hisa sokoni kwa ajili ya kuuzwa kwa wiki jana ni benki za CRDB, NMB na DCB.  Wawekezaji wa CRDB ndio waliokuwa wakiongoza kwa kuuza hisa kwa wingi katika kipindi hicho, lakini muitikio wa wanunuaji ulikuwa mdogo.

Katika mnada wa Jumatano wiki jana zaidi ya hisa milioni 1.3 zilipelekwa sokoni na wawekezaji wa kampuni mbalimbali za ndani, lakini hadi mwisho wa mnada ni hisa  10,000 tu ndizo zilipata maombi ya kununuliwa.

Siku za Jumatatu na Jumanne ya wiki jana, idadi ya hisa zilizotakiwa kuuzwa nazo zilikuwa ni zaidi ya milioni 2 kila siku lakini mahitaji ya wanunuzi hayakuvuka hisa  30,000 .

Kwa siku za Alhamisi na Ijumaa hali iliendelea kama siku za mwanzo za wiki ambapo mamia ya wawekezaji walijaribu kuuza hisa zao kwenye soko bila mafanikio.

Ripoti za DSE zinaonyesha kwamba kwa siku hizo mbili za mwisho, jumla ya shilingi bilioni 6 zilipatikana kutokana na biashara ya hisa, lakini idadi kubwa ya wauzaji na wanunuaji hisa walikuwa ni wawekezaji kutoka nje.

Hata hivyo, kwa siku ya mwisho wa wiki, wawekezaji kutoka ndani ya nchi walianza kurejea kwani hadi mwisho wa siku, wawekezaji hao waliongeza ushiriki wao hadi kufikia asilimia 9 ya hisa zilizonunuliwa na asilimia 37 ya hisa zilizouzwa.

Hata hivyo, katika kipindi cha wiki jana, hakukuwa na mwekezaji yeyote mwenye hisa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye masoko ya nje ya Nairobi na London aliyeziweka sokoni kwa ajili ya kuuza na hakukuwa na mahitaji yoyote ya hisa za kampuni hizo kwa wiki nzima.

Kampuni zilizoorodheshwa DSE kutokea soko la Nairobi ni Jubilee Holdings, Kenya Airways, Nation media Group, KCB Limited, Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL) na Uchumi Supermarkets. Kampuni ya Acacia iliorodheshwa awali kwenye soko la hisa la London, Uingereza.

Shirika la ndege la Precision nalo lilikumbwa na mdororo wa biashara katika kipindi hicho, kwani kwa siku mbili za mwanzo wa wiki hisa 10,500 ziliwekwa sokoni kwa ajili ya kuuzwa lakini hazikufanikiwa kupata mnununuzi.

Kampuni ya bia ya Tanzania (TBL) ndiyo iliyoongoza kwa kuchangia mapato mengi ya mauzo ya hisa katika kipindi cha wiki jana kwani kwa siku tatu za mwanzo, biashara ya hisa zake ilikusanya shilingi zaidi ya bilioni 7.

Kampuni nyingine zilizofanya vizuri wiki jana kwa kuwa na mauzo makubwa ni Kampuni ya Sigara (TCC),  Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE),  Kampuni inayotoa huduma za usafiri wa anga ya Swissport Tanzania na benki ya CRDB.

Kwenye uchambuzi wake, Tanzania Securities Limited, madalali wa soko, ilisema kwamba soko linakabiliwa na upungufu wa ukwasi kwani wawekezaji wengi waliotegemewa kuchangamsha soko wanakabiliwa na mahitaji ya kifedha kwa hiyo isingekuwa rahisi soko kuwa na mabadilishano mengi ya hisa.

Ripoti za kila siku za DSE kwa wiki jana zilionyesha kwamba idadi ya wawekezaji kutoka nje ya nchi imeendelea kuongezeka, huku idadi ya wawekezaji wa ndani ikiongezeka kwa kiwango kidogo sana.

Katika kipindi cha mwanzo wa wiki, asilimia 71 ya mapato ya manunuzi ya hisa ilichangiwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi na idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia asilimia 99 mwishoni mwa wiki.

Kabla ya mwaka 2012, wawekezaji kutoka nje ya nchi walikuwa wamewekewa ukomo wa kununua hisa DSE, lakini sasa zuio hilo lilindolewa mwaka 2015 na sasa wanaweza kununua idadi yoyote ya hisa wanazotaka.

Mauzo ya hisa miongoni mwa wawekezaji wa ndani nayo imepungua kutoka asilimia 100 mwanzoni mwa wiki jana hadi kufikia asilimia chini ya tatu mwishoni mwa wiki.

Hii inaonyesha kwamba wawekezaji wengi waliouza hisa nyingi kipindi cha wiki jana ni wale kutoka nje ya nchi na wawekezaji wengi walionununua hisa zaidi wanatoka nje ya nchi.

Madalali wa soko la hisa wanasema kwamba, wawekezaji kutoka nje ya nchi ndio wanaochangia kwa kiwango kikubwa cha biashara ya hisa DSE, hasa kwa pande zote mbili za uuzaji na ununuaji.

Wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi wanapendelea sana kampuni za benki, bia na saruji, kwani ndizo kampuni zinazoonekana kufanya vizuri kwenye soko la hisa la Dar es Salaam ama masoko mengine duniani.

Kwa mujibu wa ripoti za DSE, mtaji  wa jumla wa soko nao umepungua hadi kufikia shilingi trilioni 18.6 mwishoni mwa wiki jana kutoka shilingi trilioni 20.1 za wiki ya kwanza ya Januari mwaka jana.

Mtaji wa kampuni za ndani nao umepungua hadi kufikia shilingi trilioni 7.5 mwishoni mwa wiki jana, kutoka shilingi trilioni 7.7 Desemba 30 na shilingi trilioni 9.0 zilizorekodiwa mwoshini mwa Januari mwaka jana.

Viashiria vya soko, ikiwemo kile cha jumla (DSEI), cha kampuni za ndani (TSI),  cha viwanda (AI) na kile cha huduma (CS) vilishuka katika kipindi cha kuanzia Desemba 30 hadi mwishoni wa wiki jana.

Hata hivyo,katika kipindi hicho hicho kiashiria cha benki, fedha na uwekezaji (BI) kiliongezeka kidogo hadi kufikia pointi 2,762.82 mwishoni mwa wiki jana kutoka pointi  2,761.26 za wiki iliyoishia Desemba 30 mwaka jana.

Hatua hii inakuja wakati soko la hisa likitarajiwa kupata bidhaa zingine katika robo ya kwanza ya mwaka huu baada ya kampuni za simu kuagizwa kuwa zihakikishe zinaorodhesha hisa zao.

Kampuni ya Vodacom Tanzania tayari imeshapeleka maombi kwenye Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMSA) kwa ajili ya kuuza asilimia 25 ya hisa zake huku wakilenga kukusanya shilingi bilioni 500.

Kampuni za Tigo na Airtel nazo tayari zimeshatangaza kuanza mchakato wa kuuza hisa zao kwenye soko la hisa la Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka huu.

Kampuni za simu Tanzania zinalazimika kuuza na kuorodhesha hisa zao kwenye DSE kutokana na matakwa ya sheria ya mawasiliano na posta ya mwaka 2010 ambayo imeweka suala hili kama lazima.

Hata hivyo, mwisho wa kuuza na kurodhesha hisa zao ilikuwa ni Desemba mwaka jana, lakini kutokana na ucheleweshwaji, sasa inatarajiwa kwamba taratibu zote zitakamilika katika robo ya kwanza ya mwaka huu inayoishia Machi.

Pamoja na kuuza hisa zao wakati huu ambao soko bado linakabiliwa na upungufu wa ukwasi, wachambuzi wa masuala ya hisa na mitaji wanasema kwamba bila usaidizi wa wawekezaji wa ndani kuna wasiwasi mkubwa iwapo watanzania wataweza kuzinunua zote za kampuni za simu.

Serikali inasema inatarajia kampuni 89 za mawasiliano na simu zinazofanya biashara Tanzania kuwasilisha maombi ya kuuza hisa za awali. Hata hivyo, ni kampuni tatu tu za simu ndizo zilizowasilisha maombi yao mamlaya ya masoko ya mitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *