Marekani yaishutumu Iran kwa uchokozi wakati wasiwasi wa nyuklia ukizidi

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson ameishutumu Iran kwa uchokozi wenye nia ya kuzua machafuko huko Mashariki ya Kati na kuhujumu maslahi ya nchi yake katika ukanda huo.

‘Iran isiyodhibitiwa inaweza kufuata njia ile ile iliyopitia Korea Kaskazini na kuufanya ulimwengu wote kuifuata,” Tillerson alisema.

Rais Donald Trump mapema jana alitoa amri ya kupitiwa upya kwa makubaliano ya kinyuklia baina ya nchi yake na Iran ambayo yalifikiwa wakati wa utawala wa Rais Barack Obama.

Hata hivyo, Marekani anakiri kwamba Tehran imekuwa ikitekeleza makubaliano hayo ya mwaka 2015.

Iran hadi sasa haijatoa matamshi yoyote juu ya kile kinachoendelea.

Nchi hiyo imekuwa ikakana mara kwa mara shutuma za nchi za Magharibi kwamba iliwahi kutaka kuunda silaha za kinyuklia.

Jumanne wiki hii, Washington iliishutumu Korea Kaskazini kwa vitendo vyake vya kichokozi,’baada ya Pyongyang kufanya jaribio lililoshindwa la makombora mwisho wa wiki iliyopita.

Korea Kaskazini ilidai kwamba inaweza kuwa inafanya majaribio ya makombora kila wiki, na ikaonya “vita kamili” iwapo Marekani itachukua hatua zozote za kijeshi.

Marekani inafanya nini kuhusu Iran?

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano wiki hii, Tillerson alisema kwamba mchanganuo ambao aliueleza katika barua yake kwenda kwenye bunge la Congress, utaangalia sera ya Marekani kuelekea kwa Iran – ikijumuisha pamoja na mambo mengine jinsi Tehran inavyotekeleza makubaliano ya nyuklia lakini pia vitendo vyake huko Mashariki ya Kati.

“Iran ni taifa linaloongoza ulimwenguni kwa kuunga mkono shughuli za kigaidi na inahusika katika kuchochea migogoro kadhaa na kuhujumu maslahhi ya Marekani katika mataifa kama Syria, Yemen, Iraki na Lebanon, na kuendelea kuunga mkono mashambulizi dhidi ya Israel."

Kama sehemu ya orodha kubwa ya mabadiliko, alikosoa uhusika wa Iran katika mgogoro wa nchini Syria na kuendelea kumuunga mkono Rais Bashar al-Assad.

Mapema Waziri huyo wa Mambo ya Nje alikiri kwamba Iran imekuwa ikitekeleza masharti ya makubaliano ya mwaka 2015. Lakini alisema kwamba “tamaa ya nyuklia” imebaki kuwa ni hatari kubwa dhidi ya amani na usalama wa kimataifa.

Makubaliano ya kinyuklia ya Iran ni nini?

Makubaliano ya kihistoria ya mwaka 2015 yalishuhudia vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Iran vikiondolewa baada ya Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki yaani International Atomic Energy Agency (IAEA) kuthibitisha kwamba Tehran imeacha shughuli zake za kinyuklia.

Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kudhibiti shughuli za Iran katika vinu vya kinyuklia.

Barack Obama alidai kwamba makubaliano hayo, baina ya Iran na mataifa sita makubwa duniani yakiwemo China, Urusi na Uingereza, ni njia sahihi ya kuizuia Iran kumiliki silaha za kinyuklia.

Lakini Rais Trump alielezea makubaliano hayo kama ni mabaya zaidi katika historia.

Iran inasema kwamba mpango wake wa kinyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani na kwamba itaendelea na mpango wake wa kuunda makombora.

Kwa namna gani msimamo wa Marekani umebadilika?

Ulipokuwa unatangaza mtazamo mpya kwenye sera kuelekea kwa Iran, utawala wa Trump bado haujatupilia mbali makubaliano hayo ya kinyuklia.

Lakini Rex Tillerson amekuwa karibu na hilo kwa kusema kwamba makubaliano hayo hayana maana yoyote kuendelea nayo, hata kama anakubali kwamba yamekuwa yanafanya kazi.

Wiki hii waziri huyo alilitaarifu bunge la Congress kwamba Tehran imekuwa inatimiza wajibu wake katika makubaliano hayo kwa kupunguza shughuli zake za kinyuklia ili kuondolewa kwa vikwazo dhidi yake, jambo ambalo anapaswa kuthibitisha kila baada ya siku 90.

Rais wa zamani Barack Obama anakubaliana na ukweli kwamba Iran inasaidia sana vitendo vya kigaidi, kwamba inaunga mkono vikundi ambavyo vimekuwa vikihujumu maslahi ya Marekani katika ukanda huo, kwamba ni adui mkubwa wa Israel na majaribio yake ya makombora ya masafa marefu yanapingana na marufuku ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Lakini Obama aliweka masuala hayo pembeni na  makubaliano ya nyuklia, jambo ambalo lingekuwa ni gumu kufikiwa iwapo masuala yote yangejumuishwa pamoja jkatika meza ya majadiliano.

Tillerson, kwa upande mwingine, anasema mtazamo huo ulikuwa ni kosa na kuongeza mtazamo mpya utaangalia hatari zote ambazo zinasababishwa na Iran.

Hili lina uhusiano gani na Korea Kaskazini?

Rais Donald Trump amezidisha shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini, ambayo imekuwa ikiongeza kasi ya majaribio ya silaha za kinyuklia pamoja na makombora, pamoja na kuwepo kwa marufuku ya Umoja wa Mataifa.

Lengo la Korea Kaskazini ni kutaka kuwa na uwezo wa kuweka bomu la kinyuklia katika kombora la masafa marefu lenye uwezo kwa kufika mahali popote duniani, ikiwemo Marekani.

Trumo amesema kwamba hilo halitoweza kutokea, na “njia zote zipo mezani” katika kukabiliana na Pyongyang.

Jumatano hii, Tillerson alirudia mtazamo wa utawala wa Trump kwamba zama za uvumilivu zimeshindwa.

Na alisema kwamba Marekani ilikuwa inataka kubadili mwelekeo kabla Iran haijafuata njia iliyochukuliwa na Korea Kaskazini.

Hata hivyo, Iran inasema kwamba ina haki ya kutumia nguvu za kinyuklia – na kusisitiza kwamba mpango wake wa kinyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *