Mateso ya Kibanda

WALATINI wanamsemo mashuhuri; docendo discimus yaani kwa kadiri tunavyopata fursa ya kufundisha ndivyo nasi tunavyojifunza (by teaching, we learn) hapa Tanzania tumerahisisha msemo huo kwa tafsiri…kuona ni kujifunza au tembea uone.

Docendo discimus ndiyo wito (motto) katika vyuo vikuu kadhaa vikubwa na maarufu duniani, kuanzia Chuo Kikuu Cherepovets, kilichopo Urusi; Stranmillis kilichoko Belfast – Ireland ya Kaskazini; Chuo Kikuu cha Chichester kilichopo Magharibi ya Sussex – England; Chuo Kikuu cha Central Washington na Chuo Kikuu Polotsk – Belarus.

Tanzania, kama taifa tupo katika zama mpya. Zama za kuwapo kwa makundi ya kupanga na kutekeleza matukio ya kuteka, kutesa na kujeruhi baadhi ya wanajamii, hasa wanajamii wanaoaminika kuwa kero kwa baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara au watu mashuhuri.

Tupo kwenye zama za ugaidi na magaidi, sambamba na utekelezaji wa sheria dhidi ya ugaidi unaopigiwa chapuo na nchi za Magharibi hasa Marekani. Waandishi wa habari (baadhi) ni kati ya walengwa wa mipango hii ya magaidi.

Hali ya wasiwasi imegubika baadhi ya waandishi wa habari na hasa wale wanaoaminika kufanya kazi yao kwa weledi, weledi ambao kwa wengine ndiyo kiini cha waandishi hao kushughulikiwa.

Ingawa Katiba na sheria nyingine za nchi zinawahakikishia usalama dhidi ya vitisho vya ugaidi na magaidi wa ndani ya nchi, bado vyombo vya ulinzi na usalama kwa sehemu kubwa vimekuwa vikishindwa kung’amua mapema mipango hiyo ya kudhuru wanahabari na mfano mmojawapo ni unyama dhidi ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Absalom Kibanda.

Tayari Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, amepoteza jicho lake moja kutokana na unyama aliofanyiwa na bila shaka, mwili wake utadumu katika makovu ya majeraha. Hali hii inasikitisha katika tasnia ya habari na si ya kuvumilika.

Jicho la Kibanda limepotea kutokana na matokeo ya kazi yake, kwa namna fulani sawa na mwandishi wa habari wa gazeti la Sunday Times, Marie Colvin. Tofauti iliyopo (wote wamepoteza jicho moja moja) ni kwamba, wakati Kibanda amepoteza jicho akiwa ndani ya nchi yake yenye amani, Marie Colvin alipoteza jicho lake akiwa kazini tena katika uwanja wa vita. Ndiyo, kila mmoja amepoteza jicho lake; wote ni wanahabari na wote kazi yao inalenga umma.

Marie Colvin, ni mwanahabari mzaliwa wa Marekani lakini akiwa anafanyia kazi gazeti la Sunday Times la Uingereza, ni mwandishi mashuhuri duniani.

Mwanamama huyu mwenye umri wa miaka 55, alipoteza jicho lake mwaka 2001 akiwa kazini huko Sri Lanka, akiripoti kuhusu vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Askari walirusha bomu ambalo baada ya kulipuka lilimjeruhi Marie na kusababisha apoteze jicho lake moja.

Lakini Kibanda kwa upande wake, alikuwa ndani ya nchi yake yenye amani akitokea kazini kwake kurejea nyumbani. Akatekwa, kuteswa na kujeruhiwa katika nchi hiyo ya amani, isiyokuwa na makundi ya wazi ya waasi.

Tukirejea kidogo kwa Marie Colvin; Februari 22, mwaka huu aliuawa kutokana na shambulizi la mizinga kutoka kwa majeshi ya nchi ya Syria, walipokuwa wakishambulia waasi wa nchi hiyo.

Mara ya mwisho kabla ya kuuawa, Marie Colvin alituma habari ya kusikitisha kuhusu wanawake na watoto 300, waliokuwa wamekwama katika kifusi cha jengo, kwa wiki mbili bila msaada.

Na katika hali ya kusikitisha alieleza namna ambavyo alishuhudia mtoto wa wiki mbili akiwa na majeraha makubwa alivyokuwa akikata roho taratibu mbele ya macho yake.

Marie hakujua naye atauawa siku chache zijazo katika shambulizi la mizinga ya kijeshi licha ya uzoefu wake kama mwandishi katika kuripoti migogoro mbalimbali ya kivita, kuanzia Chechnya, Kosovo, Sierra Leone hadi Libya.

Lakini si yeye tu, waandishi wengi wa habari duniani wamewahi kupoteza maisha wakati wakiwa kazini kwenye maeneo ya kivita (war zone). Kwa hiyo, kuna mambo mawili ya kuzingatia; kwanza ni mwandishi kupata misukosuko inayoweza kutafsiriwa kama ajali kazini kwa mfano wanapokuwa uwanja wa vita.

Pili, kuna unyama dhidi ya waandishi wa habari kwa malengo maalumu ya kibinafsi. Alichofanyiwa Kibanda ni unyama na si ajali kazini.

Kwa kuzingatia haya, si busara hata kidogo kuruhusu Tanzania iwe tishio kwa waandishi wa habari eti kwa sababu ya matakwa binafsi ya kikundi fulani cha watu. Haiwezekani waandishi wa habari Tanzania wafanye kazi mithili ya watu walioko kwenye uwanja wa vita.

Tanzania hakuna mazingira ya vita na wala Tanzania si uwanja wa vita. Majeshi yetu hayako katika mapambano dhidi ya waasi. Nimesikia baadhi wanahoji mitaani, mbona kuna watu wengi wanafanyiwa ukatili wa kutisha na maisha yanakwenda kimya kimya?

Majibu yangu kwao ni kwamba, shambulizi dhidi ya mwandishi wa habari ni shambulizi dhidi ya ustawi wa jamii. Ni shambulizi dhidi ya juhudi za kuokoa wenye shida.

Tafakari kazi iliyofanywa na Marie Colvin wa Sunday Times kabla ya kuuawa kwake. Aliripoti kuhusu madhila ya watu 300 waliokwama kwenye kifusi cha jengo lililoangushwa kwa silaha nzito za kijeshi, dunia ilifahamu kuhusu suala hilo na hatua zilichukuliwa, ingawa Marie baadaye alipoteza maisha.

Hii maana yake, waandishi wa habari wanafanya kazi ya jamii kwa matakwa ya taaluma yao. Ni watumishi wa jamii kitaaluma, si adui wa jamii. Jamii inapaswa kuwalinda wanahabari. Hawa ni rafiki wa jamii na si maadui (journalists are friends not foes)

Tafakari, hadi Marie anapoteza jicho lake mwaka 2001 akiwa Sri Lanka kuripoti vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, kazi yake iliokoa maisha ya raia wangapi? Je, kazi yake hiyo ilikuwa kwa manufaa yake binafsi au kwa manufaa ya raia wa Sri Lanka na dunia kwa ujumla? Kama ni kwa manufaa binafsi na familia yake; je, manufaa hayo yanalingana na thamani ya jicho lake?

Kwa hiyo, kama wanavyosema Walatini desendo discimus, nasi tunapaswa kujifunza pia, jamii ya Watanzania bila kujali itikadi au misimamo ya vyama vyao inapaswa kuunga mkono kupinga unyama dhidi ya wanahabari kwa sababu wanahabari wapo kwa ajili ya ustawi wa jamii husika.

Yapo mazingira ya ajali kazini kwa upande wa waandishi wa habari kwa mfano yaliyomkuta Marie Colvin kuanzia kule Sri Lanka (2001) alipopoteza jicho lake na kisha huko Syria alikofariki dunia kwa shambulizi la kijeshi, kote huko ni maeneo ya vita, wanasema vita wakati mwingine haina macho.

Lakini tofauti na yaliyomkuta Kibanda. Hakuwa kwenye uwanja wa vita na wala kitendo alichofanyiwa si ajali kazini bali ni unyama uliolenga kupandikisha vitisho dhidi ya ustawi wa tasnia ya habari nchini. Kwa Watanzania wote, desendo discimus.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *