Mauzo ya hisa yashuka DSE

Mauzo ya hisa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) yalishuka hadi kufikia shilingi milioni 511 wiki iliyopita kutoka shilingi milioni 787 za wiki ya awali.

Hata hivyo, pamoja na kushuka kwa kiasi cha mauzo, idadi ya hisa zilizonunuliwa katika kipindi cha wiki jana kwa mujibu wa ripoti za DSE, ziliongezeka hadi kufikia hisa 530,000 wiki jana kutoka hisa 460,000 za wiki ya awali.

Ripoti za DSE zimeonyesha kwamba katika kipindi chote hicho cha wiki, idadi ya wawekezaji wa ndani ilikuwa kubwa kuliko wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa pande zote mbili za kununua na kuuza.

Wachambuzi wa masoko ya hisa na mitaji wanasema kwamba, kupungua kwa biashara ya hisa kwenye DSE imesababishwa na kuhama kwa wawekezaji ambao sasa wanakimbilia kwenye hati fungani.

Katika mnada wa hati fungani uliofanyika Januari 25 mwaka huu, kiasi cha shilingi bilioni 387 zilikusanywa kutoka kwa wawekezaji mbalimbali, ikiwa ni zaidi ya shilingi bilioni 139.5 zilizotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Wengi wa wawekezaji wanakimbilia kwenye hati fungani na amana za serikali kwa kuwa ni sehemu isiyo na hatari za kibiashara na viwango vyake vya riba vinavutia zaidi.

Meneja wa Masoko na bidhaa za DSE Patrick Mususa alisema mwanzoni mwa wiki hii kwamba japokuwa mauzo yameshuka, ukubwa wa mtaji kwa kampuni zote zilizoorodheshwa ndani na nje ya nchi uliongezeka  hadi shilingi trilioni 19.1 wiki jana kutoka shilingi trilioni 18.7 za wiki ya awali.

Kampuni zilizoongoza kwa mauzo ya hisa kwa wiki jana ni Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo hisa zake zilikuwa ni asilimia 57 ya mauzo ya soko ikifuatiwa na  DSE iliyokuwa na asilimia 23.2 na CRDB ilifuatia kwa asilimia 13.3 ya hisa zote zilizofanyiwa biashara.

Mususa alisema kuongezeka kwa mtaji wa soko katika kipindi cha wiki jana ni matokeo ya kuongezeka kwa bei ya hisa za Acacia kwa asilimia 6, KCB kwa asilimia 5 na EABL kwa asilimia 1.3.

Ripoti hiyo imeonyesha kwamba japokuwa bei ya hisa za DSE ziliongezeka kwa shilingi 20 kwa hisa, mtaji wa soko kwa kampuni za ndani ulibakia kwenye kiwango kile kile cha shilingi trilioni 7.5.

Katika siku ya kwanza ya wiki jana, kiasi cha shilingi milioni 54 zilipatikana kwenye mauzo ya hisa, ambapo asilimia 96.88 ya kiwango hicho kwa upande wa ununuzi ilitokana na wawekezaji wa ndani.

Ripoti ya siku ilionyesha kwamba, asilimia 96.88 ya mauzo ya hisa pia yalifanywa na wawekezaji wa ndani ya nchi, hali inayoonyesha kuadimika kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Kwa siku ya Jumanne, biashara iliendelea kufanywa na wawekezaji wa ndani kwani ripoti zilionyesha kwamba asilimia 100 ya hisa zilizonunuliwa na kuuzwa zilikuwa ni za wawekezaji wa ndani ya nchi.

Kwa siku hiyo, kiasi cha shilingi milioni 47.39 zilipatikana na zote zilitoka kwa wawekezaji wa ndani ya nchi.

Siku ya Jumatano kiasi cha shilingi milioni 36.33 zilipatikana kwenye mauzo ya hisa ambapo asilimia 100 ya hisa zilizonunuliwa na asilimia 100 ya hisa zilizouzwa zilikuwa za wawekezaji wa ndani.

Hata hivyo, siku ya Alhamisi ya wiki jana, kulikuwepo na kurejea kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi kwani ripoti zinaonyesha kwamba asilimia 88.15 ya manunuzi na asilimia 32.31 ya mauzo yalifanywa na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Katika mnada wa siku hiyo, kiasi cha shilingi milioni 309.53 zilipatikana kwenye biashara ya hisa huku asilimia 88.15 ambazo ni shilingi milioni 272.85 zilitokana na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Katika siku hiyo, ushiriki wa wawekezaji wa ndani kwa upande wa mauzo ulikuwa ni asilimia 67.69 ya mauzo yote, hali inayoonyesha kwamba bado idadi kubwa ya wawekezaji wanaouza hisa zao kuwa watanzania.

Madalali wa soko wanasema kwamba wawekezaji kutoka nje ya nchi ndio hasa wanachangamsha soko la hisa, na biashara takriban asilimia 80 na zaidi inafanywa na wawekezaji hao.

Katika siku ya kufunga wiki, kiasi cha shilingi milioni 63.54 zilipatikana kwenye mauzo ya hisa ambapo asilimia 98.56 ya thamani hiyo ilitoka kwa wawekezaji kutoka nje.

Ushiriki wa wawekezaji wa ndani kwa mujibu wa ripoti hiyo kwa siku ya mwisho wa wiki ulikuwa ni asilimia 100 ya hisa zote zilizouzwa na asilimia 1.46 ya hisa zote zilizonunuliwa.

Katika kipindi cha wiki jana, kiashiria cha jumla cha kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko (DSEI) kilipanda kwa pointi 45 hadi pointi 2,192 kutoka pointi 2,147 za wiki ya awali.

Hatua hii ilitokana na kuongezeka kwa bei ya hisa za DSE, KCB, Uchumi Supermarkets, Acacia, EABL na NMG katika kipindi cha kufunga wiki hiyo.

Hata hivyo, kiashiria cha kampuni za ndani (TSI) kwa wiki iliyopita kwa mujibu wa ripoti za DSE kilibakia pale pale kwenye pointi3,550.

Viashiria vya sekta za viwanda (AI), Huduma za benki na kifedha (BI) na kile cha huduma za biashara (CS) kwa wiki jana vilibakia kama wiki ya awali kutokana na kutobadilika kwa bei ya hisa.

Kwa upande wa hati fungani, mauzo yake yalipanda kwa asilimia 54 kutoka hati fungani zenye thamani ya shilingi bilioni 15.7 hadi shilingi bilioni 24.2.

Katika kipindi hicho, hati fungani tisa zenye thamani ya shilingi bilioni 24.2 ziliuzwa na kununuliwa kwa wiki iliyoishia Januari 27 mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchambuzi wa soko iliyotolewa juzi na Tanzania Securities Limited, madalali wa soko na washauri wa uwekezaji, Benki ya NMB ndiyo iliyofanya vizuri mwaka jana kwa upande wa bei ya hisa.

Kwenye ripoti hiyo, bei ya hisa za NMB ziliongezeka kwa asilimia 10 hadi kufikia shilingi 2,750 Desemba 21 mwaka jana kutoka shilingi 2,500 za Januari Mosi mwaka jana.

Kampuni nyingine zilizofanya vizuri kwa upande wa upandaji wa bei ya hisa katika kipindi cha kuanzia Januari Mosi mwaka jana hadi Desemba 21 ni TOL Gases kwa asilimia 5.26 na benki ya Mkombozi ambayo hisa zake ziliongezeka kwa asilimia 2.

Katika kipindi hicho, bei ya hisa za Simba ilishuka kwa asilimia 40 kutoka shilingi 2,670 za Januari 1 mwaka jana hadi shilingi 1,600 za Desemba 21 mwaka jana.

Kampuni nyingine ambazo bei ya hisa zilishuka katika kipindi cha mwaka jana ni CRDB kwa asilimia 37.5, DCB kwa asilimia 29.82, TCC kwa asilimia 27.90 na Mwalimu Commercial Bank kwa asilimia 21.81.

Bei ya hisa za Swissport ilipungua kwa asilimia 14.17 hadi shilingi 5,450 Desemba mwaka jana kutoka shilingi 7,350 za mwezi Januari mwaka jana huku bei ya hisa za TBL zikishuka kwa asilimia 18.9 kwa kipindi hicho.

Hata hivyo, ripoti ya TSL imeonyesha kwamba viashiria vyote vya soko ikiwemo cha jumla (DSEI) na TSI vyote vilipungua kipindi hicho kutokana na kutoongezeka kwa bei ya hisa kwa kampuni nyingi katika soko.

Kwa upande wa kampuni zilizoorodheshwa kutoka nje ya nchi, bei yao ya hisa haikupanda wala kupungua katika kipindi hicho  kilichofanyiwa tathmini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *