Mbowe afungua kesi dhidi ya Makonda

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa kukiuka sheria na taratibu katika kushughulikia watuhumiwa wa biashara za dawa za kulevya nchini.

Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freemana Mbowe, pasipo kutaja tarehe ya kesi, alisema majaji waliopangiwa katika kesi hiyo inayokusudiwa kusikilizwa Februari 21 ni pamoja na Jaji Sakiety Kihiyo, Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Khaday.

Mbowe aliongeza kusema kwamba Chadema inakubaliana kabisa na inaunga mkono mapambano dhidi ya uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya lakini staili anayoitumia Makonda inawafanya watuhumiwa kuukimbia mkono wa sheria.

 “Sisi Chadema tunakubaliana na kabisa na mapambano dhidi ya waingizaji na watumiaji wa dawa za kulevya nchini lakini kwa staili ambayo Makonda anaitumia ni kuwaandaa wafanyabiashara wanaotuhumiwa kuukimbia mkono wa sheria”alisema Mbowe

 “Kupinga kwetu utaratibu wa kutaja majina ya watu hadharani pasipo vielelezo kutamsaidia Makonda na mamlaka nyingine kufuata sheria katika kushughulikia suala hilo kama ilivyofanyika hivi karibuni,” alisema Mbowe

Akikabidhi ripoti hiyo yenye majina 92 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya yakiwemo majina ya watoto wa viongozi kwenye uongozi wa serikali ya Awamu ya Pili, Tatu na Nne, Makonda alisema kwamba yeye (Makonda) na Kamishna wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Simon Sirro, waliamua kutaja majina hadharani kwa kuwa biashara ilifanyika hadharani.

 “Majina 97 yanawahitaji watu wa Interpol (Mtandao wa Kimataifa wa Polisi) waweze kuvuka nje ya mipaka yetu kwa ajili ya kushughulikia baadhi ya watuhumiwa waliopo kwenye orodha,”alisema Makonda.

Vita ya kupambana na uingizwaji na utumiaji wa dawa za kulevya ilitangazwa hivi karibuni na Makonda (Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam) huku wafanyabiashara, viongozi wa dini na wanasiasa akiwemo Mbowe wakitajwa hadharani kwamba miongoni mwa watuhumiwa.

2 thoughts on “Mbowe afungua kesi dhidi ya Makonda”

  1. Ngulu F.S says:

    Ana haki ya kufikiria alivyofikiri na kuamua kumfungulia mashtaka Makonda. Binafsi nashawishika kuamini Makonda anazo sababu za msingi kwa kufanya aliyoyafanya katika jitihada za kudhibiti janga la madawa ya kulevya nchini. Nashindwa kuamini kuwa amekurupuka tu!.Ila subira yavuta kheri. Sheria ni msumeno. Tuone hii mechi itakavyochezwa na vyombo vya sheria. 

  2. Erick Cleophas says:

    Walishafanyiwa uchunguzi kama miaka kumi iliyopita, biashara hii ilikuwa ikifanyika hadhalani kwenye mahotel yao na wao wanafahamu , kwanini hawajaieleza serikali nani wanfanyia biashara chafu kwenye mahotel yao? kwa kifupi hapo utaona kuwa uenda nao ni washiriki wa biashara hiyo tena kwa kificho kwa sababu biashara hiyo inalipa na wao walikuwa wakifurahia maisha kila kukicha na muda wote walikuwa na uwezo wa kuitishia serikali kwa nguvuya fedha za dawa zakulevya. Taifa haliwezi kuendeshwa na mtandao wa kimafia hata siku moja. Tuungane vita hii ni takatifu na adui ni dhaifu ni vitisho tuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *