Habari
Meya Mbeya adaiwa kulazimisha safari ya China
Felix Mwakyembe
Mbeya
Toleo la 221
11 Jan 2012
Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas  Kapunga

SAFARI ya Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga nchini China mwaka 2009 imezidi kugubikwa na utata kutokana na kuwapo kwa barua zinazopingana kutoka kwa wenyeji wake nchini humo na wakala wa safari hiyo hapa nchini.

Wakati pande hizo mbili zikitofautiana, uongozi wa jiji hilo umekana kuhusika  na gharama ya safari ya meya huyo nchini China hivyo hoja iliyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuendelea kujitokeza katika kila mkutano wa Baraza la Halmashauri ya Jiji hilo, madiwani wakiendelea kumbana meya wao ili alitolee maelezo sakata hilo naye akikwepa.

Barua ya mwaliko wa viongozi hao haiweki wazi kuhusu kugharamia nauli yao, lakini barua ya ufafanuzi inakanusha na kusisitiza yalikuwa ni makosa ya uchapaji.

Aprili mwaka 2009 Meya Kapunga na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati huo, John Mwakipesile walifanya ziara nchini China kwa mwaliko wa kampuni ya AMEC ya nchini humo, safari ambayo imezua mzozo ndani ya Jiji la Mbeya baada ya Mkaguzi wa Hesabu kubaini jiji hilo kugharamia safari hiyo kinyume cha taratibu za fedha.

Barua ya mwaliko yenye kumbukumbu namba AMEC/INV/TZ2009001, ambayo hata hivyo haina tarehe wala sahihi ya Meneja Mkuu bali jina lake tu, ilitumwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile ikimwalika yeye na Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga.

Barua hiyo ya Meneja Mkuu, Wang Guoqing inaonyesha kuwa viongozi hao walialikwa na Kampuni ya Changzhou Machinery and Equipment Imp & Exp. Co. Ltd (AMEC) yenye makao yake Changzhou, katika Jimbo la Jiangsu nchini China.

Hata hivyo, mwaliko huo haukuweka wazi suala la nauli ya viongozi hao kwenda na kurudi nchini humo,  bali unazungumzia gharama za waalikwa hao watakapokuwa nchini China.

“Tulipia gharama zenu zote mtakapokuwa hapa China,” inasema sehemu ya barua hiyo inayozungumzia gharama za viongozi hao wawili katika safari yao hiyo ya nchini humo.

Barua ya ufafanuzi kuhusu sakata hilo, ya Oktoba 21, mwaka jana, ikiwa haina jina la meneja mkuu bali sahihi yake na kutumia karatasi isiyo na nembo ya kampuni kama ile ya mwaliko, inasisitiza kwamba kampuni hiyo haikuwanunulia tiketi ya safari hiyo ya kwenda nchini China na kwamba ilikuwa ni makosa ya uchapaji katika barua yao ya mwaliko ambayo hata hivyo, haizungumzii suala la nauli.

Kwa mujibu wa barua hiyo, kampuni hiyo ya haihusiki kuwagharamia nauli ya kwenda nchini humo, bali lilikuwa jukumu la ofisi zao, ambazo kwa upande wa Jiji la Mbeya uongozi unakana kuhusika.

Katika hali ya kushangaza, Paul Mwakajumba alimwandikia barua, isiyo rasmi, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kupitia kwa Mweka Hazina wa jiji hilo, akidai kwamba awali kampuni hiyo ya nchini China ndiyo ilikuwa ilipie ghrama za tiketi kwa ajili ya viongozi hao wawili, lakini hadi tarehe ya barua hiyo, Oktoba 20, mwaka jana walikuwa hawajalipa.

Mwakajumba, katika barua yake aliyoiandika kwenye karatasi za barua za kawaida na isiyo katika karatasi rasmi za kampuni wala mhuri wa kampuni,  amejitambulisha kama anatoka katika Kampuni ya East Africa Trade House. Co Ltd ambao ndio waratibu wa safari hiyo iliyofanyika Mei, 2009.

“Tulialikwa na Kampuni ya AMMEC-HINA; kampuni hiyo awali ilikuwa ilipie gharama za tiketi kwa ajili ya waheshimiwa hao, lakini mpaka leo hii ninapokuandikia bado kampuni hiyo haijalipa hata senti, naendelea kuwasiliana nao na jibu la mwisho nitalolipata nitaijulisha ofisi yako,” anasema Mwakajumba katika barua yake hiyo.

Barua hiyo ya Mwakajumba iliandikwa Oktoba 20, 2011 na siku iliyofuata, Oktoba 21 kampuni hiyo ya nchini China iliandika barua, ikitoa ufafanuzi unaokanusha kuhusika na gharama za nauli ya viongozi hao.

Wakati mawasiliano ya barua kati ya kampuni hiyo ya AMEC na wakala kwenda Jiji la Mbeya yakifanyika, baadhi ya viongozi wa jiji hilo waliokuwapo wakati wa sakata hilo wanamshangaa Meya Kapunga kuendelea kung’ang’ania ofisi ilipe wakati ukweli wa safari yake anaufahamu kwamba jiji halikuhusika.

“Yeye angekubali alipe, anajua alichokifanya sio kizuri,” anasema mmoja wa maofisa wa jiji hilo wenye kulifahamu kwa ukaribu sakata hilo.

Viongozi hao wa jiji wanaenda mbali zaidi wakibainisha chanzo cha mzozo kuhusu matumizi ya fedha kwa ajili ya nauli ya meya huyo kwenda China kuwa ni hatua yake ya kulazimisha safari ambayo haikumhusu.

“Safari haikuwa yake, alilazimisha na wenzetu kama hakuwemo katika orodha ya walioalikwa hawawezi kuchakachua wakakulipia,” anasema ofisa mmoja wa jiji hilo, jina linahifadhiwa.

Mei, mwaka 2009 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mwakipesile na Meya wa Jiji la Mbeya, Kapunga walienda China kwa mwaliko wa Kampuni ya AMEC inayojishughulisha pamoja na utengezaji wa mitambo ikiwamo matrekta ambapo kwa safari yao ilihusu zaidi mradi wa matrekta.

Barua ya mwaliko inabainisha madhumuni ya safari hiyo kuwa ni mradi wa kuyatangaza matrekta ya kampuni hiyo kwa manufaa ya wakulima nchini.

Hata hivyo, safari hiyo imezua mgogoro ndani ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, baada ya kuwapo kwa hoja ya Mkaguzi wa Serikali kuhusu fedha, zaidi ya shilingi milioni tano, zilizochotwa kutoka jiji kwa ajili ya nauli ya Meya Kapunga kwenda China bila maelezo yanayojitosheleza.

Hoja hiyo inashikiwa ‘bango’ na baadhi ya madiwani wa jiji hilo wakisimamia hoja kwamba akiwa kiongozi wa juu ameshiriki katika matumizi mabaya ya fedha za jiji.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Felix Mwakyembe
fkyembe@gmail.com
+255-713290487

Toa maoni yako