Mfalme akitinga utupu hadharani, ni uhaini kutosema yuko uchi

HAIKUWA kwa bahati mbaya wala kutotarajiwa, bali kwa stahiki yake na haki; pale mheshimiwa Mikogo Mingi, mwana wa Mfalme Mingi Mikwara, aliposhika kiti cha ufalme kumrithi baba yake aliyeitwa na Mungu katikati ya mwezi Machi mwaka huo. Mfalme huyo kijana ambaye kabla ya hapo hakujisumbua kufuatilia wala kujifunza staili ya utawala bora kutoka kwa baba yake kwa umri wake wote wa miongo mitatu; alipania kufanya makubwa kwa mkupuo na kwa mkurupuko kuleta mapinduzi katika nyanja za uchumi na uhusiano wa kimataifa. 

Sherehe za kutawazwa zilikuwa baridi kwa sababu familia na raia kwa ujumla walikuwa bado na majonzi kwa kuondokewa na mfalme wao kipenzi; zilikosa shamrashamra na umwagaji sifa alizotamani mfalme huyo mpya.

Ili kuhakikisha madoido hayo hayavuki nje ya upya wa madaraka yake, aliagiza ifanyike sherehe ya kitaifa kuadhimisha mwaka mmoja wa utawala wake, siku aliyotaka kutoka ndani ya suti mpya na ya kipekee ambayo haikupata kuvaliwa na watawala waliomtangulia, kuashiria “mageuzi” nchini.

Aliagiza mafundi nguli wa kushona suti kutoka ng’ambo kuja nchini ambao walijipiga kifua kumshonea suti yenye kuonwa na wenye busara na hekima pekee na si kina “Yahe mie”, mafukara wa fikira, wavivu wa kufikiri na malofa.

Hatimaye mafundi hao wa kigeni walitaarifu kukamilika kwa suti siku moja kabla ya siku ya sherehe.  Na siku hiyo ya vionjo, katikati ya mzizimo wa sherehe, mafundi walimvua nguo chumbani na kumvisha “suti” (hewa) mpya iliyodhaniwa kuweza kuonwa na wenye busara na hekima pekee, wakati ukweli alibakia uchi wa mnyama akiamini amevishwa suti.

Akatoka nje kwa mbwembwe na makeke amepanda farasi, “mtupu kwa utupu wa kuzaliwa” akipungia mikono umati uliofika kumshangilia katika suti yake ya kipekee.

Wajumbe wa Baraza la Mawaziri walishindana kwa mbinu za kumwaga sifa na kusifia; huyu akimwita “jembe” mwingine akimwita “kiboko yao”, na sifa nyingine lukuki; kila mmoja akidai kubaini vionjo tofauti katika suti hiyo ambavyo mwenzake hakuviona. Wakajisifia kukidhi matakwa ya mfalme kwa pendekezo lao la kupata kampuni ya kigeni kuja kushona suti hiyo nchini na kuwekeza teknolojia mpya.

Washauri wa Ikulu walitunga na kuimba mashairi kusifia rangi na jinsi suti hiyo ilivyotulia, huku wanahistoria wakitweta kwa machapisho juu ya upekee wa suti hiyo. Wanasheria wa Ikulu, wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wao walihemka kuandaa Hati za Makabidhiano na Hati za haki ya Umiliki Mali/Nguo mpya ya Mfalme.

Wachumi waliandika “Mpango Uchumi” juu ya bidhaa hizi za kipekee (suti na tai) chini ya ushirikiano wa sayansi na teknolojia na wa ki-viwanda na wenzao wa nchini kama njia ya kueneza teknolojia kwa wenyeji.

Magazeti ya Serikali na binafsi yenye kudhibitiwa, yalitangaza tukio hilo kwa vichwa vya habari vikubwa na kwa wino wa kuangaza:  “SUTI ILIYOSHONWA KWA AJILI YETU NA KWA MAZINGIRA YETU. SUTI ILIYOSHONWA NYUMBANI KUTOKA NG’AMBO. SUTI YA KITAIFA – SUTI MAKINI KWA VIWANDA VYA NDANI….”; lingine likasema, “Bila Mfalme Mikogo Mingi, Ufalme utayumba”.

Wahariri waliandika tahariri nzito nzito kuwataka wananchi kuiga viwango vya juu vya kimataifa vilivyooneshwa na mafundi wa suti ya mfalme.

Viongozi wa dini walisifia udugu wa kibinadamu uliooneshwa kati ya wageni na raia katika ushonaji wa suti ya mfalme; wakaomba Mungu abariki juhudi nyingine nyingi zenye mwelekeo huo.

Nao wanasiasa walitoana jasho kwa kukinzana na kugombana juu ya mantiki kisiasa, kwa mfalme kuvaa suti ya aina ya pekee siku hiyo, na waligawanyika vikali kuhusu maudhui ya kisiasa na mfumo wa serikali uliowakilishwa na suti mpya ya mfalme. Wakati wote huo, wananchi walikauka koo kwa kushangilia kila kionjo cha kufikirika cha suti hiyo, lakini wakijua ukweli kwamba Mfalme wao alikuwa uchi.

Kisha ghafla, katikati ya sauti chovu za wasifia suti ya Mfalme; ikasikika sauti ya mtoto mdogo mgongoni mwa mama yake ikisema kwa kupiga kelele: “Mama! Mama, tazama, mfalme yuko uchi, mfalme yuko uchi!”.

Mama yake alijitahidi kumnyamazisha kwa kumfinya; lakini mtoto aliendelea kupiga kelele kusema kilichokuwa dhahiri kwa kila mtu: “Lakini mfalme yuko uchi; kweli, yuko uchi”.

Hapo, kana kwamba macho ya waliokuwa wakishangilia suti yaliondolewa utando, kila mmoja alianza “kuona” na kusema cha kweli alichokuwa akiona tangu mwanzo lakini hawakudiriki kusema ukweli kwa hofu ya kuitwa ya kuitwa wasio na busara.

Kuona hivyo, Baraza la Mawaziri, kwa kunong’ona na mafundi wa kigeni wa suti ya mfalme, likaazimia kuwa, kila mtoto na kila mtu mzima ambaye hakuweza kuiona suti ya Mfalme, afanyiwe (tiba) upasuaji wa macho yake kwa gharama zake.

Hadithi hii ya karne ya 19 na mwandishi Christian Anderson ambayo imerejewa pia kwa mazingira yetu na mwana riwaya nguli barani Afrika, raia wa Kenya,  Ngungi wa Thiong’o katika kitabu chake “Ngugi Detained”, ina mengi ya mfano kwa yanayojitokeza katika nchi nyingi barani Afrika, ikiwamo Tanzania dhidi ya uhuru wa mawazo, uhuru wa kujieleza na namna tabaka la watawala linavyoweza kuminya uhuru huo na kupindisha ukweli kwa aibu ya taifa.

Ukimwacha mfalme mwenyewe, ambaye kwa “upofu”, mbwembwe na uchu wa sifa na kujikweza, alikubali kudanganywa na “mafundi” kutoka ng’ambo; wengine wote walijua kuwa mfalme alikuwa uchi; Taifa likalazimika  kugharamia suti isiyokuwepo; huku wasaidizi wake, kwa nidhamu ya woga, unafiki na kujipendekeza, wakitetea wasichoamini, kwamba mfalme alipendeza ndani ya suti mpya isiyokuwepo; mfalme akaridhika kudanganywa.

Kwa nidhamu ya woga na kujipendekeza, wasaidizi wa mfalme, kwa kushirikiana na ubeberu wa kimataifa, waliamua kushika nyundo ya chuma dhidi ya wananchi waliouona ukweli, kwa kuwatisha kuwang’oa macho kwa gharama zao (kizuizini) ili mradi tu kuwaziba mdomo.

Nao mumiani wa kimataifa, kwa ukimya wa raia waliodhibitiwa walizidi kutafuna rasilimali za taifa bila kufuta midomo kwa kisingizio cha “uwekezaji” na ushirikiano wa kimataifa na bila hofu ya kuhojiwa.

Na vivyo hivyo kwa vyombo vya habari vilivyobanwa na kudhibitiwa; kwamba havikuweza kuandika kwa uhuru kuisemea jamii iliyofungwa mdomo, wala dhidi ya maovu ya kijamii ila kusifia vituko vya mfalme aliyekuwa uchi kadamnasini, huku uchumi ukiendelea kuporwa na tabaka la wachache kwa mikataba ya suti ya kilaghai iliyofungua “uwekezaji” hewa nchini.

Inawezekana mfalme, kwa dhamiri, dhamira na kwa hulka, alikuwa na nia njema kwa nchi yake; lakini kwa tabia ya makeke na kupenda makuu, aliingiza nchi bila kufahamu, kwenye mikataba ya kinyonyaji, uwekezaji usiojali, uhusiano na wa kimataifa na ukoloni mamboleo.  Kwa dhamira yake hiyo njema iliyofichika, tunaweza kumsamehe asining’inizwe.

Na vipi Baraza la Mawaziri? Kazi ya baraza ilikuwa ni kumshauri mfalme kwa yote yahusuyo sera za uchumi na siasa kwa manufaa ya nchi.  Kwa yote aliyofanya mfalme hasidi kwa taifa, kwa kuelewa au kutoelewa, baraza haliwezi kusamehewa kwa kushindwa kutekeleza jukumu lake la ushauri na kwa kunyamazia matokeo yake bila kuhusishwa na uhaini na usaliti kwa taifa.

Lakini hapa kuna mkanganyiko:  baraza lingefanyaje kama, pamoja na jukumu lake la kushauri, lilinyamazishwa na mfalme asiyeambilika kwa madai kuwa halazimiki kupokea ushauri kutoka kwa mtu yeyote katika kutekeleza majukumu ya nchi; baraza likafyata mkia kwa hofu ya kuitwa “wasaliti” dhidi yake”?

Usaliti ni kwa mtu kujiengua na kwenda kinyume na yale yaliyokubaliwa kwa pamoja huku yeye huyo akiwa ameshiriki katika makubaliano.  Usaliti ni kujiweka kando au kuwachomea nguru washirika wako kwa lengo la kutifua mipango yao (yenu) au kuwaangamiza.

Kunyamazia kwa nidhamu ya woga vituko vya mfalme akiuza uhuru na uchumi wa nchi kwa wageni kwa mikataba ya kilaghai na kujidhalilisha, hakukuwa usaliti, unafiki na uzandiki pekee, bali pia kilikuwa kitendo cha usaliti kwa taifa uliopitiliza kiwango cha uhaini na kwa baraza hilo la mawaziri kuasi kiapo chao cha madaraka.

Baraza lilipaswa kumshauri mfalme kwa uwazi na ukweli; na kama angeonekana kuwa ngangari, lilipaswa kujiuzuru kuonesha dhamiri njema kwa nchi na kwa wananchi.

Na wananchi waliofika kushangilia suti ya mfalme wakijua alikuwa uchi, je, nao waning’inizwe kwa usaliti?. Hapana. Hawa ni “bendera hufuata upepo” wanaotumiwa na tabaka la watawala wabovu kujenga “Pepo ya Mabwege” kwa kushangilia kila litokalo midomoni mwa tabaka la watawala, jema au baya bila kujali athari kwa nchi. Je, haikusemwa kwamba, “Kwenye msafara wa mamba na kenge wamo”?.

Kwa wahariri wa vyombo vya habari kuingizwa katika sakata hili, kwa kusifia “mradi” wa mfalme kwa vichwa vya habari na tahariri pana na kwa wino wa kuangaza, walisaliti jamii na taaluma yao ya kuandika ukweli na kuimulikia jamii njia katika safari ya kuyasaka maendeleo; waliatamia udhalimu na dhuluma iliyoinyemelea jamii.

Tunasema, Mwandishi wa habari na tasnia ya habari kwa ujumla na kwa wajibu wake usiohojika, ndiyo macho, masikio, pua na mdomo wa jamii, mwenye kazi, wajibu na majukumu sawa na umuhimu wa viungo hivyo katika mwili wa binadamu.

Na ili mwandishi aweze kutekeleza vyema majukumu yake, anatakiwa kuwa juu ya jamii kimaono na kifikra, awe mjuzi, jasiri na mwerevu kama nyoka, lakini mpole kama Hua (ndege).

Mwandishi si ofisa uhusiano wa mfumo wowote wa utawala na wa wafalme, bali ni mchambuzi wa mema na mabaya kwa lengo la kuielekeza jamii njia salama ya kupita. Wala mwandishi wa habari haandiki kumfurahisha au kumjenga mtu; bali anaandika kujenga na kutetea jamii bora na imara; kuelimisha, kuonya na kuelekeza.

Na hapa ndipo ulipo mgongano kati ya wanahabari na wafalme wenye kupenda kusifiwa hata kwa mapungufu yao. Wakati kwa mwanahabari, utekelezaji wa majukumu ya kawaida ya wafalme unaweza kuwa si habari ila mapungufu yao; katika hilo, wafalme wanataka kusifiwa na kukwezwa kwa maandishi mapana na kwa wino wa kuangaza ili watambuliwe kama tabaka.

Kwa mwandishi, mbwa kuuma binadamu si habari (kwa kuwa ni jambo la kawaida na lenye kutarajiwa), lakini kwa binadamu kuuma mbwa ni habari kubwa. Vivyo hivyo, kwa machinga kukata mauno akicheza “kiduku” stendi kuu ya mabasi Ubungo si habari; lakini ni habari kubwa kwa Mkuu wa Mkoa kufanya hivyo mahali hapo.

Wanahabari wasikubali kusaliti taaluma zao kwa kukubali kuwa maafisa uhusiano wa wafalme na kuacha nchi ikigwaya gizani.  Nao wafalme waheshimu taaluma na taasisi za kitaaluma kama ambavyo nao wangetaka raia waheshimu taaluma ya wafalme ya kutawala kwa haki na kidemokrasia.

Hapa kwetu, operesheni ya macho kwa vyombo vya habari kwa kukataa kusifia suti ya mfalme imefanyika kwa njia nyingi, ikiwamo ya kuvituhumu kwa makosa ya “uchochezi” chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu. Wakati haya yakiendelea, nchi kama Uingereza, zilikwishafuta Sheria zinazohusu makosa ya “uchochezi” na “habari za uongo” (False News Offences) tangu mwaka 1887.

Na mwaka 1997, Mahakama ya Rufaa (Supreme Court) ya Uganda ilionesha njia, kwamba, katika habari hakuna uchochezi wala uongo, kwani kile ambacho kinaweza kuonekana uongo leo, kesho kinaweza kugeuka kuwa ndio ukweli wenyewe.

Katika Kesi ya Charles Onyango – Obbo na mwingine, dhidi ya Serikali ya Uganda, mhariri huyo wa gazeti la “The Monitor” aliiomba Mahakama kutamka kama Serikali ilikuwa na mamlaka na haki ya kudhibiti uhuru wa habari chini ya kifungu cha 50 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code) ya Uganda (Tanzania vifungu 50 na 55) kwa kisingizio cha kulinda “maslahi ya umma”.

Katika kesi ya msingi kwenye Mahakama za chini, Obbo na mwenzake walishitakiwa kwa kuandika na kuchapisha habari: “RAIS KABILA AILIPA UGANDA KWA DHAHABU KAMA SHUKRANI KWA KUMSAIDIA KUMNG’OA MOBUTU”.

Mahakama hiyo ilisema: “…..kila mtu ana haki ya kutoa na kusambaza au kueneza mawazo yake”, na kwamba haki hiyo haiishii kupokea, kuhifadhi na kutoa aina kadhaa tu za mawazo, kama vile maoni sahihi, mawazo mazuri au taarifa za kweli; bali ni pamoja na kupokea, kuhifadhi, na kutoa mawazo, maoni na taarifa zote ambazo si lazima zionekane kuwa za kweli leo, kwani taarifa hizo hizo zinaweza kugeuka kuwa hivyo kesho”.

Huku ikibainisha kuwa msingi wa sheria hiyo ni Sheria za Kikoloni zenye chimbuko la miaka ya 1200 nchini Uingereza, Mahakama hiyo ilisema; Uganda kama nchi ya kidemokrasia, inapaswa kuheshimu misingi ya demokrasia kwa viwango vya kimataifa, na kwamba si sahihi kugeuza uchapishaji wa habari za uongo kuwa kosa la jinai la uchochezi, wakati Katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa juu ya Haki za binadamu (Bill of Rights) zinapingana na dhana hiyo, na kuongeza kwamba, ikitokea habari kuathiri mtu au taasisi, hatua sahihi ni kwa mhanga kufungua kesi ya madai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *