Mgogoro wa ushirika Moshi wapanda joto

Moshi, Kilimanjaro

MGOGORO ulioibuka katika Ushirika wa Mema na Mabaya unaoundwa na watumishi  wa Idara ya Kilimo na Mifugo katika Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro umepanuka zaidi baada ya wanachama kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kusitisha mara moja  makato ya fedha za michango katika mishahara yao.

Kufukuta kwa mgogoro katika chama hicho kuliripotiwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili katika toleo lake namba 479 la Oktoba 12, mwaka huu.

Ushirika huo ulianzishwa mwaka 1998 na watumishi wa Idara hiyo kwa malengo ya kusaidiana katika masuala mbalimbali  ya kijamii kama misiba, ugonjwa na pale mtumishi anapostaafu kazi.

Chama hicho kina wanachama zaidi ya 200 na kila mwanachama wa ushirika huo hukatwa shilingi 5,000 kama mchango wake kila mwezi katika mshahara wake.

Kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho mwanachama hupewa shilingi 500,000 iwapo atafiwa na ndugu wa karibu kama mume, mke, wazazi, mtoto  ili fedha hizo zisadie katika shughuli za mazishi.

Aidha,  kila mwanachama hupewa shilingi 50,000 pale atakapokuwa mgonjwa na kulazwa hospitali na shilingi 500,000, kila mwanachama anapostaafu kazi.

Hata hivyo, pamoja na makubaliano hayo kikatiba, taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa kuanzia mwaka jana viongozi wa chama hicho walisitisha utoaji fedha kwa wanachama wake bila kutoa maelezo ya kuridhisha.

Kusitisha makato

Katika barua ya Oktoba 24 mwaka huu kwenda kwa viongozi wa chama hicho na kunakiliwa  kwa  Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Moshi na Moshi Vijijini  wanachama hao wanataka kusitishwa kwa makato ya shilingi 5,000 katika mishahara yao haraka.

Barua hiyo imetiwa saini na Salvatory Mtui ambaye anabainisha kuwa anaungwa mkono na kundi kubwa la wanachama wanaopinga hatua ya uongozi wa chama kushindwa kufuata Katiba ya chama hicho.

“Kama wanachama hawapati fedha  pale wanapopata matatizo hatuoni tena sababu ya kukatwa  fedha katika mishahara yetu  kwa ajili ya michango isiyo na tija kwetu,” anaeleza Mtui.

“Kwa ukweli huo ni dhahiri kwamba mamlaka ya viongozi wa mema na mabaya ni mkutano mkuu peke yake na wala si kinyume chake,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Aliongeza kuwa kinachotokea ndani ushirika huo ni viongozi “kujibinafsishia”   chama hicho  na kuvunja Katiba ya chama kwa kujitwalia mamlaka ya kufanya maamuzi  bila mkutano mkuu wa chama.

“Mkutano mkuu ndiyo mamlaka ya juu au chombo cha juu kufanya maamuzi  na tangu mwaka jana haujafanyika na viongozi  wa chama hawaelezi sababu za kutofanyika kwa mkutano mkuu, na wanachama hawapati  fedha pale wanapokuwa na mamtatizo,” aliongeza Mtui.

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia simu Mtui aliithibitisha kuandika barua hiyo na kuongeza kuwa hali ilivyo sasa ndani ya chama hicho hakuna tena sababu ya kuoneana haya hivyo  viongozi wanapaswa kuitisha mkutano mkuu kujadilia matatizo ya chama na viongozi kuwajibika.

Naye mwanachama mwingine aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema  bado wasiwasi umetanda kuwa fedha za chama hicho zimetumiwa vibaya na viongozi wao na ndiyo sababu kubwa ya kukwepa kuitisha mkutano mkuu.

“Taarifa tulizo nazo ni kwamba baadhi ya viongozi wamebakiza miezi michache kustaafu kazi sasa usalama wa fedha zetu utakuwa shakani kwa sababu kiongozi anapostaafu si rahisi kupatikana tena,” alidai mwachama huyo.

Kauli ya Mwenyekiti

Akizungumza na gazeti hili kwa njia simu Mwenyekiti wa Ushirika huo Joyce Kessi alisema hababaishwi na wanachama wanaolalamika huku akiwawataja kama  “watu waoga”  na wasiojiamini.

“Kwanza kwanini mmeniandika katika gazeti lenu, mnanifahamu mimi? Unajua mimi ni nani? And your going to pay fo it,”alitishia Mwenyekiti huyo.

“Mara kwanza mlipondika nilikaa kimya  lakini  sasa naenda kuripoti kwa mwajiri wangu sasa hivi na pia naenda polisi kuwashitaki lazima mniombe radhi haraka sana au vinginevyo mtajuta mtajuta sana nitahakikisha nawashughulikia,” alidai Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo hata alipopewa nafasi ya kujibu hoja za walalamika hakuwa tayari kusikiliza zaidi ya kuendelea na vitisho dhidi ya mwandishi na gazeti hili.

“Hao wanachama walalamike na walalamike , na nyie endeleeni kuandika uongo dhidi yangu, nitahahakisha nakifungia hicho “kigazeti” chenu  haraka sana,”aliendelea kutishia Mwenyekiti huyo.

Juhudi za kuwapata Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Moshi na Moshi Vijijini hazikuweza kufanikiwa lakini moja wa maafisa wa ngazi za chini wa Manispaa ya Moshi aliimbia Raia Mwema kuwa suala la kusitisha makato ya fedha za wanachama liko nje ya uwezo wa Halmashauri hiyo.

Afisa huyo aliongeza kuwa ushirika huo una Katiba yake hivyo hakuna Halmashauri itakayokuwa na mamlaka ya kisheria ya kuingilia masuala ya ushirika huo ispokuwa wanachama watakavyoaamua kupitia vikao vya kikatiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *