Makala
Miaka 20 ya Vyama Vingi: Hasara kuliko faida
Andrew Bomani
Toleo la 248
11 Jul 2012

WIKI iliyopita ilitimia miaka 20 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Si kipindi cha kawaida. Kwa mtu aliyezaliwa mwaka 1992, sasa ana haki ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu.

Awali niseme kwamba katika makala za siku za nyuma, niliweka wazi jinsi ambavyo nilijikuta nikitafakari kwa kina juu ya mfumo wetu wa vyama vingi, kiasi cha kufikia msimamo kwamba kwa ujumla, suala la vyama vingi kwa maendeleo ya taifa, imekuwa hasara zaidi kuliko faida.

Nililazimika vile vile kufanya uchambuzi wa kina kuhusu Mwalimu Julius Nyerere kutokana na kwamba yeye alikuwa na nafasi kubwa mno kwenye mageuzi ya kisiasa nchini.

Hivi karibuni katika kuendelea kutafakari, nilijiuliza, hivi Mwalimu Nyerere kweli alikuwa anafikiri ni akina nani hasa, wangeweza kuwa wameanzisha hivyo vyama vya upinzani tokea mwanzo na kuwa na mafanikio makubwa?

Natoa ombi la dhati kupata majibu kutoka kwa wale wachache ambao kweli walikuwa wanaelewa kwa ufasaha fikra za Mwalimu. Nasema wachache maana wengi wanaojiweka sana kama watu wa Mwalimu si zaidi ya waigizaji au pretenders.

Kuweza kuelewa akina nani wangeweza kuanzisha hivyo vyama ni muhimu sana kutokana na kwamba hakukuwa na watu mashuhuri SANA katika harakati za mageuzi.

Na pengine hili halikuwa kwa bahati mbaya.

Tukichukua kwa haraka kielelezo cha nini Watanzania walichokuwa wanataka kisiasa, ile Tume ya Jaji Francis Nyalali iliweka wazi kwamba asilimia 80 ya wananchi walipendelea tuendelee na mfumo wa chama kimoja.

Inawezekana kweli kabisa asilimia hiyo ilikuwa si sahihi kiasi hicho lakini bado bila shaka angalau zaidi ya nusu walipendelea chama kimoja, ikiwa ni pamoja na kutaka mabadiliko ya maana ndani ya CCM. Ndiyo maana katika demokrasia kuna kanuni inayosema: "tuwaache walio wengi waamue wanachotaka na kuiacha kauli ya wachache". (Let the majority have their way and the minority their say).

Sasa kuweka kando maoni ya Watanzania wengi na kuungana haraka na asilimia ndogo katika suala kubwa mno la mfumo wa siasa haikuwa suluhu sahihi, na pengine ilikuwa ni kukaribisha matatizo mengine makubwa tu. Ilipaswa mageuzi ya kisiasa yafanyike kwa kasi ambayo ingepunguza athari mbalimbali.

Mfano mzuri wa athari ni kurejea mwezi Oktoba mwaka 1990, kabla ya Tume ya Nyalali kuanzishwa. Iliteuliwa kamati ya CCM ya Kushauri Juu ya Mageuzi, chini ya Waziri wa zamani wa Sheria, Bakari Mwapachu, na ambayo kama ilivyo kawaida Tanzania, taarifa hiyo haijulikani na viongozi wengi wa nchi.

Katika sehemu ya mwisho ya taarifa hiyo, kamati ilitahadharisha kuhusu umuhimu wa mageuzi makubwa ya kiuchumi. Nikinukuu sehemu ya kwanza: "Kuwapo kwa uchumi mzuri pia kunafanya hata vyama vitakavyoanzishwa kuwa vya kweli na si miradi ya viongozi na wanachama wake kupata njia ya kuendeleza maisha."

Sehemu ya pili ya taarifa kuhusu umuhimu wa mageuzi makubwa ya kiuchumi ilisema: "Vyama vitakavyoanzishwa vitakuwa na nafasi nzuri ya kuwa na wanachama watakaoendesha chama chao wenyewe bila kutegemea wafadhili wachache au misaada ya chini chini na ya vificho kutoka nje."

Ni jambo lililo wazi kwamba hili la kwanza na la pili ni tatizo kubwa sana. Nikianza na la kwanza, ni nadra sana kusikia hata kuhusu mikutano mikuu ya wanachama wa vyama kibao ili kutimiza sharti la msingi la kuchaguana.

Inawezekana hata ada za kila mwaka za chama hazilipwi. Na inaelekea kwamba viongozi wakuu wa nchi ndiyo wanaopendelea huu utitiri wa vyama ili kujigamba kwa wafadhili kwamba demokrasia imeshamiri Tanzania?

Kwa hili la pili, tumeshuhudia vyama vingine vikishutumiana vikali wakati mwingine kuhusu wafadhili wao. Ni imani yangu ya dhati kwamba ingekuwa jambo la kushangaza kutokana na kuingia kwenye mfumo mpya "kichwa kichwa" - licha ya Nyerere mwenyewe kutoa angalizo murua akiwa anastaafu Uenyekiti wa CCM, Agosti 1990 - kama kweli tungepata vyama kwa maana halisi ya vyama kwa muda mrefu.

Ni Mwalimu aliyetamka yafuatayo: "Si vema kuruka bila kuwa na hakika utaangukia wapi!" Ni lazima kuwepo na msingi imara katika kitu chochote kikubwa kama vile kujenga nyumba!

Nimepata kusoma mara kadhaa makala na hotuba zake za miaka ya nyuma, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, akiwatupia mpira Watanzania kwamba ni kama vile watu wa kutaka 'mabadiliko' bila kujitazama kwanza na kuviunga vyama vilivyopo kwa hali na mali. Kwa lugha nyingine, ni "armchair critics".

Nadiriki kusema Watanzania wengi tu si watu wa kuunga mkono kitu mara nyingi kwa kubahatisha. Mfano wa wazi kwa hili ni mwaka 1995 wakati Augustine Mrema alipogombea Urais na kupata kura nyingi. Watanzania wengi waliweza kwa sababu nzuri kumwona Mrema kama kiongozi wa watu. Ni bahati mbaya tu kwamba ilikuwa si rahisi kwa wengi kupata picha sahihi kilichokuwa kinamsukuma Mrema.

Kulionyesha hili, katika kitabu cha maisha cha Mwenyekiti mwanzilishi wa CHADEMA, Mzee Edwin Mtei, anaeleza kwamba CHADEMA kilituma ujumbe kuzungumza na Mrema kuhusu uwezekano wa kujiunga na chama hicho.

Masharti waliyopewa na Mrema ni kwamba CHADEMA kimteue kuwa mgombea urais na vile vile Mwenyekiti wa Taifa wa Chama.  CHADEMA kilikuwa tayari kumteua Mrema kuwa mgombea urais ila si Mwenyekiti kutokana na ulazima wa kikatiba wa kuitisha Mkutano Mkuu. Matokeo yake, Mrema alijiunga na NCCR Mageuzi na kupitishwa kuwa Mwenyekiti na mgombea Urais.

Sasa kweli yeye Mrema kutaka kukabidhiwa nafasi zote mbili haikuwa uchu wa madaraka? Na isitoshe, kwa upande wa CHADEMA pamoja na kutofanikiwa kumpata Mrema kuwa mwanachama halafu mgombea, kilimuunga mkono kwenye harakati za Urais kwa uelewa kwamba vyama hivyo vingeunda serikali ya mseto endapo wangeshinda.

Kwa maneno yake Mzee Mtei, mtu mmoja mkubwa ndani ya CCM alimwambia miaka michache baadaye kwamba tangu siku yeye Mtei alipotangaza kwamba CHADEMA kingemuunga mkono Mrema, alipoteza imani kwake. Na Mtei anasema akitazama nyuma, anakiri hilo lilikuwa kosa moja kubwa katika maisha.

Anaendelea kusema kwamba yalikuwa ni maoni ya wengi ndani ya chama chake ambayo alikuwa anajaribu kuheshimu lakini anasema alipaswa kuwa na nguvu kuupinga.

Hiki kitendo kilinipa picha jinsi ambavyo CHADEMA kilikuwa ni chama cha kubahatisha bahatisha. Na kutokana na jinsi ambavyo NCCR kilikuja kuvurugana hadi Mrema alihamia TLP na kufanikisha matakwa yake ya kuwa Mgombea Urais na mwenyekiti, lazima Watanzania wengi walivunjika nguvu kiasi fulani na upinzani.

Cha ajabu, mwaka 2000, ni kama CHADEMA hakikujifunza kutokana na 1995 maana tuliona ushirikiano kati yake na CUF kwa kumuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba. Kwa jinsi ambavyo leo hii vyama hivyo vinatupiana maneno mara kwa mara, huwezi kuamini vilikuwa pamoja hapo nyuma.Ni majuto tu!

Na juzi tu, Freeman Mbowe, alitangaza kwamba wamejifunza kutokana na kuchukua watu fulani kugombea vyeo fulani dakika za mwisho na kuleta usumbufu baadaye. Aliweka wazi safari ijayo hawataki 'makapi' ya CCM. Ni majuto mtindo mmoja!  

Katika mazingira haya, si vema kuwakosoa Watanzania. Siamini kwamba kama CHADEMA kingeonyesha umakini wa hali ya juu tokea zamani, wasingekosekana wafadhili wengi tu wa kufanana na MJ Sabodo.

Kwa kweli safari yao imekuwa na mapungufu makubwa kiasi cha hata waasisi wa chama hicho kama Mtei, hayati Bob Makani na hata Victor Kimesera, kushindwa kwenye kinyang'anyiro cha ubunge kwenye majimbo.

Hadi viongozi wakuu wote hawa wakwame sidhani kama ni suala la wananchi wenyewe kushindwa kuelewa ipasavyo! Vile vile, mwaka 2005, CHADEMA kilipomsimamisha Mbowe kama Mgombea Urais wake wa kwanza kabisa, kwenye jimbo lake la Hai alikokuwa Mbunge, kiti kilichukuliwa na CCM. 

Nafikiri haikuwa kwa bahati mbaya kwamba kutokana na matatizo mbalimbali yaliyokuwapo ndani ya vyama vingi, Nyerere alitamka kwamba 'upinzani wa kweli utatokana na CCM'. Lakini hili lilikuwa kama kujipinga kwa msimamo wake wa nyuma wa kutaka sana mageuzi kwa haraka.

Kuhitimisha, nimelazimika  kumtazama kiongozi mmoja mkubwa ndani ya CHADEMA ambaye pamoja na wenzake wachache, wameweza kufanya kazi nzuri sana miaka ya hivi karibuni na kuwapa Watanzania matumaini makubwa.

Huyu si mwingine bali ni Dk. Wilbroad Slaa. Yeye mpaka sasa amekuwa mwanachama wa CHADEMA kwa takriban miaka 17. Lakini kinachonisikitisha ni jinsi alivyojitoa CCM na kuingia CHADEMA baada tu ya kufanyika mizengwe kwenye kura za maoni jimboni Karatu 1995.

Hivi baada ya kuingia kwenye chama hicho endapo angekuta hicho chama hakitimizi matarajio yake, angehama tena na tena? Au hata kwenye uamuzi mzito wa CHADEMA kumuunga mkono Mrema na baadaye Lipumba, yeye Dk. Slaa alikubaliana kweli?

Kwa hali ya uwezo alioonyesha Dk. Slaa, binafsi naona alipaswa tu kuwa ameanzisha chama chake baada ya kutoswa. Ninaamini pia hicho chama kingekuwa kimepiga hatua kubwa hadi sasa.  

Kwa kweli, napata uchungu mkubwa jinsi ambavyo Tanzania ilikuwa inaonekana barani Afrika kama nchi yenye siasa za kuheshimika kwa muda mrefu, ila kufuatia kuingizwa kwenye mfumo wa vyama vingi miaka 20 sasa iliyopita, mambo ya kujivunia ni machache sana!

Yaani tumefikia mahali, aliyekuwa mstari wa mbele hata kudai mageuzi ya kisiasa na mwanzilishi wa NCCR, Mabere Marando, naye ametoka kwenye chama chake na kujiunga na CHADEMA.

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Andrew Bomani
+255-0784219535, +255-0715219535

Toa maoni yako