NI muhimu wakati kama huu ambao tunasherehekea miaka 50 ya kujitawala tukapitia historia ya kuendeleza kilimo na uchumi wetu Tanzania tangu uhuru hadi sasa.
Hii ni muhimu sasa, pengine kuliko kipindi chochote kile katika historia ya nchi hii kwa vile taifa hili linatimiza miaka 50 ya uhuru.
Tunatakiwa kujitathmini kwa kina ili kujua tumekosea wapi na tujipange vipi ili kukwepa makosa tuliyofanya huko nyuma na tunayofanya sasa. Nafanya hivyo kwa nia njema kabisa kwa lengo la kujenga nchi yangu ninayoipenda sana.
Vipofu wanaotafuta kofia nyeusi katika chumba chenye giza
Najua kuna watu watakaokerwa na tathmini hii, na hasa wale wanaopenda kusikia sifa tu bila kusikia upande wa pili wa shilingi. Wamejifungia ndani ya boksi wakitafuta majawabu ya kero za wananchi ambazo ziko nje ya boksi.
Ni sawa na vipofu wanaotafuta kofia nyeusi katika chumba chenye giza ambacho hata kofia yenyewe haimo. Wanatumia kila mbinu kuwaaminisha wananachi kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa sana kimaendeleo, na ili kuthibitisha hilo wanawahimiza walinganishe hali ya nchi ilivyokuwa mwaka 1961 wakati wakoloni wanaondoka na sasa waone kama ni sawa. Wakifungua boksi kidogo, wanajilinganisha, na mataifa mengine ya Afrika yanayotuzunguka.
Kwa haraka haraka wananchi wanaweza kushawishika na kuridhika kuwa nchi yetu imeendelea sana tangu tupate uhuru. Ukweli ambao wananchi hawaelezwi ni kwamba, tutoke ndani ya boksi kabisa, tuache tabia ya kujilinganishe na wachovu ambao hawana hata robo ya utajiri wa maliasili za Tanzania, tujilinganishe na walio mbele yetu.
Tusishindane na wachovu
Hata kwa ngazi ya mtu binafsi, ukitaka kuendelea usishindane na waliosawa na wewe au chini yako; shindana na waliojuu yako, la sivyo utabweteka. Kwanini tusichukue maamuzi magumu ya kujilinganisha na mataifa mengine ambayo tulikuwa ngazi moja ya maendeleo ya kiuchumi miaka ya hamsini na sitini, tuone wao wako wapi na sisi tuko wapi?
Kama kweli tunaendelea kwa kasi inayotakiwa, mbona Tanzania haijawahi kutoka katika nchi 20 masikini zaidi duniani tangu uhuru pamoja na kuwa nchi hii ina rasilimali nyingi ajabu?
Tujilinganishe na mataifa kama Malaysia, India, Indonesia, China, Singapore, Taiwan na Cambodia. Hapo sijataja Vietnam ambayo hata katika miaka ya 80 walikuwa bado nyuma yetu na sasa wako mbele yetu kwa maili nyingi sana.
Ukweli ulio wazi ni kwamba wakati wenzetu wanakimbia, sisi tunatembea kwa raha zetu kwa mateso makubwa ya wanyonge wa nchi hii.
Tukikwepa ukweli huu, na kuendelea kuwaaminisha watu kwamba nchi hii imepiga hatua sana kimaendeleo tutakuwa tunafanya usaliti dhidi ya umma wa Watanzania wanaotuamini na kututegemea kwa maendeleo yao na vizazi vyao.
Dhana nzima ninayoeleza hapa imejikita katika falsafa ya James Cameron, mwandishi na mwongozaji wa filamu maarufu za Terminator, Titanic, Aliens, na Judgment Day, ambaye alipata kusema “If you set your goals ridiculously high and it’s a failure, you will fail above everyone else’s success”. Kwa tafsiri isiyo rasmi anasema “Ukiweka malengo yako juu sana na ukashindwa; kushindwa kwako kutakuwa juu ya mafanikio ya wengi”.
Kwa ufafanuzi rahisi, mwanafalsafa huyu anatuhimiza daima kulenga mbali katika kila shughuli tuifanyayo. Mfano, mwanafunzi akilenga kupata diploma anaweza kuishia kuwa na cheti; akilenga kuwa na shahada anaweza kuishia kuwa na stashahada ; akilenga kuwa Rais anaweza kuishia kuwa waziri, n.k. ambayo tayari ni mafanikio makubwa.
Au tuseme mfanyabiashara, akilenga kuwa mjasriamali maarufu katika kata yake anaweza kuishia kuwa maarufu kijini kwake tu, lakini akilenga kuwa mjasriamali maarufu Tanzania anaweza kuishia kuwa maarufu katika mkoa wake, jambo ambalo ni mafanikio tayari. Au, tuseme mtu amelenga kujenga nyumba ya ghorofa na akaishia kujenga nyumba nzuri ya chini bado ni mafanikio.
Kwa mantiki hiyo hiyo, miaka hamsini ijayo Tanzania ikilenga kuwa kama Afria Kusini inaweza kuishia kuwa kama Kenya. Lakini ikilenga kuwa kama Marekani, inaweza kuishia kuwa kama Malaysia au Singapore, ambayo yatakuwa tayari ni mafanikio makubwa.
Kulenga mbali kuna maana kubwa sana katika saikolojia ya matumizi ya raslimali za mtu au nchi. Mtu binafsi akiwa na malengo mepesi ya maisha anaweza kudhani ana hela nyingi na hivyo kujikuta akitumia fedha yake ovyo kwenye ulevi na anasa nyingine. Lakini kama angekuwa na malengo makubwa, angegundua kwamba hana hela ya kuchezea.
Kama nchi ikijiwekea malenga makubwa italazimika kuwa makini sana katika kila senti inayopatikana, na haitakuwa na mchezo kwa yeyote anayekwamisha mipango kwa kutumbua fedha ya umma.
Kinyume chake, nchi isipokuwa na malengo ya juu sana inaweza kujikuta ikiwa na matumizi ya anasa kama matumizi ya magari ya kifahari, makongamano yasiyo na tija, kutokuwa na mfumo madhubuti wa kitaasisi wa kushughulikia wezi na wabadhirifu wa mali ya umma, na kujikita katika propaganda za kuwafanya wananchi waishi kwa matumaini kama tunavyoshuhudia hapa nchini.
Angalia aina na gharama ya magari ya Serikali; angalia madaraja ya ndege ambayo maofisa wa Serikali wanasafiria; au chunguza aina za samani zitumikazo katika maofisi ya Serikali, au angalia hatua zinazochukuliwa dhidi ya wabadhirifu wa mali/fedha za umma.
Kesi zinakaa mahakamani zaidi ya miaka mitano kwa kisingizio cha utawala wa sheria na haki za bianadamu. Yaani mwizi ndiye binandamu na ana haki zaidi kuliko umma ulioibiwa.
Tunashindwa nini kuwa na mahakama maalum ya kushughulikia kesi za namna hiyo? Ni mtumishi gani wa umma mwenye akili timamu anaweza kutishwa na adhabu za miaka mitatu au mitano wanazopewa wezi wa mali za umma?
Mfano, mtu akiiba bilioni moja akafungwa miaka mitatu (ambayo kihalisia ni kama mwaka mmoja na nusu), huo ni uwekezaji mzuri mno kwani asingeiba akakaa huru mwaka huo mmoja na nusu hangeweza kutengeneza hata robo ya robo ya hiyo fedha aliyoiba!
Ukichunguza mambo haya yote utagundua ni kwa jinsi gani viongozi wetu hawana haraka na nia ya dhati ya kuona Tanzania inahitimu kutoka katika lindi la umasikini kwa miaka ya hivi karibuni.
Tunacheza na nyani tutavuna mabua
Katika hali kama hiyo tutafanya makosa makubwa kama hatutajitathmini kwa kina tukitanguliza maslahi ya taifa, na badala yake tukaweka mbele unafiki na maslahi binafsi.
Tusisahau kwamba tuko hivi tulivyo, tukijivunia amani kwa sababu ya maamuzi magumu yaliyofanywa na waasisi wa taifa hili miaka 50 iliyopita. Kwa hiyo maamuzi yetu leo yataamua hali ya Watanzania miaka hamsini ijayo.
Tukiamua kutanguliza maslahi ya wawekezaji kwa faida ya muda mfupi, bila kusoma kwamba kuna hitoria ya ubepari, wajukuu na vitukuu vyetu watakuwa hawana cha kujivunia juu yetu, babu zao.
Ninapomalizia mfululizo wa historia ya kuendeleza kilimo nchini nitaweka bayana historia ya ubepari na kuonesha hatari inayolisubiri taifa hili iwapo tutaendekeza maamuzi mepesi mepesi juu ya mikakati ya mapinduzi ya kijani, na hasa suala la ardhi na mustakabari wa wakulima wadogo nchini.
Tunacheza na nyani tutavuna mabua. Babu zetu walidanganywa na zawadi ndogo ndogo kama shanga na mikufu, wakauza ardhi ya bara hili ambayo imekombolewa kwa damu nyingi; sisi tunadanganywa na 10% na ahadi kemkem za kututoa kwenye dimbwi la umasikini.
Izingatiwe kwamba watu hawali namba
Ziko njia nyingi ambazo mtu anayefanya tathmini kama hii anaweza kuwasilisha mada yake. Kwa mfano, anaweza kuchukua vigezo mbali mbali mfano idadi ya mabwana shamba, trekta, maksai, n.k. akalinganisha wakati wa uhuru na sasa miaka hamsini baadaye. Au akalinganisha kiasi cha mazao miaka ya nyuma na sasa, n.k. Wote watakuwa sahihi.
Mimi sitachukua njia hiyo kwani nafahamu wachambuzi wengi, ikiwemo Serikali watafanya hivyo, lakini waelewe kuwa hizo ni namba tu. Izingatiwe kwamba watu hawali namba na maneno matamu, mwisho wa siku kinatakiwa chakula kwenye sahani. Ninachojua ni kwamba bidii za kuendeleza kilimo Tanzania hazijafanikiwa.
Hivyo basi mimi nimechagua njia ya kuwakilisha historia hii kwa kuangalia kilichofanyika kuendeleza sekta ya kilimo kabla na baada ya uhuru. Na baadaye nitapendekeza kifanyike nini kuweka sekta ya kilimo katika njia sahihi kwa minajiri ya kufanya sekta hii itoa mchango madhubuti katika kuendeleza uchumi wa nchi hii, na kuzuia Kilimo Kwanza kisijegeuka kuwa Kilio Kwanza.
Wengi mtakuwa mnafahamu kwamba kwa kawaida historia huwa pana inavyosogelea wakati uliopo, na uwasilishaji wa mada hii hautaweza kukwepa hali hiyo.
Hali ya kilimo kabla ya uhuru
Historia ya kuendeleza sekta ya kilimo Tanzania ni ndefu. Lakini kama tutakavyoona baadaye, historia hii imegubikwa na kushindwa kwa mikakati mbalimbali ya kuendeleza kilimo, ingawaje kwa viwango tofauti kwa kila awamu ya uongozi.
Mwanzoni, kabla ya vita ya kwanza ya dunia kilimo cha Tanzania kilikuwa ni cha kijikimu. Baada ya vita ya kwanza ya dunia sura ya sekta ya kilimo ilibadilika. Kilimo cha kujikimu kilianza kuwa cha kibiashara na hasa baada ya kuanzishwa kwa mazao ya kibiashara kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.
Mazao kama chai, kahawa, pamba, tumbaku, pareto, katani na mbegu za mafuta yalishamili sana kipindi hicho. Pamoja na kwamba mengi ya mazao hayo yalilimwa na wakulima wadogo, uzalishaji uliongezeka kwa kasi ya kuridhisha.
Kasi hiyo ilitokana na msukumo mkubwa uliowekwa na Serikali ya kikoloni ili kuhakikisha inapatikana malighafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vya nchini kwao.
Awamu ya kwanza ya uongozi – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Kutoka mwaka 1961 mpaka mwaka 1965, kisiasa Tanzania ilifuata kipindi cha jamii huru/wazi na mfumo wa jamii shirikishi, au tuseme mfumo wa kibepari.
Mfumo huu ulimkera mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye mwaka 1967 alitangaza kuwa Tanzania ni nchi ya kijamaa (Rejea Azimio la Arusha), ambayo sera zake zilipinga kutumia mfumo wa soko huria kama njia ya kuboresha kilimo na ukuaji wa viwanda.
Kwa kifupi ubepari ulionekana ni unyonyaji kwa vile msingi wake mkuu ulikuwa kujilimbikizia faida kwa njia yoyote ile bila kujali masuala ya kijamii.
Serikali, ikiongozwa na nadharia za kisoshalist iliona ni busara kuingilia kati mfumo wa masoko katika sekta ya kilimo.
Vyama vya ushirika ambavyo hapo awali vilikuwa mali ya wanachama kwa kufuata misingi ya ushirika hasa katika mikoa ya Kilimanjaro na Ziwa Magharibi (Kagera) vilienezwa karibu nchi nzima chini ya mwavuli wa Azimio la Iringa la Siasa ni kilimo kwa lengo la kutoa msukumo katika suala zima la kilimo.
Vyama vya ushirika viligeuzwa njia ya kueneza usoshalist
Baadaye vyama hivi vipya viligeuzwa kuwa njia ya kueneza sera za kisoshalist. Ili kufanikisha malengo hayo ya kisiasa, viongozi wa vyama hivi waliteuliwa na Serikali. Matokeo yake urasimu, ubadhirifu, uongozi wa ovyo, na ufanisi duni vilitawala uendeshaji wake.
Utendaji mbovu wa taasisi hizi ulimaanisha bei ndogo kwa mkulima pamoja na mazao yao kununuliwa kwa mkopo. Hivyo vyama vya ushirika vilifutwa mwaka 1976 na nafasi yake kuchukuliwa na mashirika ya umma, yaliyopewa uhuru kamili wa kisheria wa kuwa wanunuzi, watunzaji, wasindikaji na wauzaji wa mazao.
Mfumo huu uliwezesha Serikali kupanga bei ya ununuzi kwa mazao yote makuu kwa lengo la kulinda maslahi ya wanyonge na hasa wakulima wadogo na walaji wa mijini.
Lakini muundo huu haukumaliza matatizo yaliyosababisha kuundwa kwake, na mwanzoni mwa miaka ya 1980, Serikali iliamua kurudisha tena vyama vya ushirika. Lakini hata baada ya kurudishwa havikuweza kuwa na nguvu kwa vile wanachama hawakuwa na uelewa wa kutosha juu ya misingi ya uendeshaji wa vyama vya ushirika, na isitoshe dunia ilikuwa inapitia mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Vijiji vya ujamaa
Ikumbukwe pia kwamba utekelezaji wa Azimio la Arusha ulienda sanjali na zoezi la kuanzisha vijiji vya ujamaa, ambapo Serikali ilihamisha watu kwa nguvu kuwapeleka katika makazi mapya.
Katika vijiji vya ujamaa, ardhi ilitakiwa kutumika kwa pamoja na uzalishaji kufanyika kijumuiya. Muasisi wa taifa hili alifikiri kuwa kwa kufanya wakulima kuishi pamoja wangenufaika kwa miundombinu ya kijamii kama vile shule, zahanati, maji, barabara, umeme, n.k.
Kwa kufanyakazi pamoja ilitarajiwa kwamba sekta ya kilimo ingeongezeka kwa kasi na kubadilisha maisha ya wakulima. Ingawaje hili lilioneka kuwa wazo zuri lakini wakulima wengi hawakupenda mpango huu hivyo ubishi na vipingamizi vilitawala katika kuacha mashamba yao ya awali na kuhamia makazi mapya. Mahali pengine kama Dodoma Serikali ililazimika kutumi nguvu za kijeshi.
Zoezi hili lilipoanza mwishoni mwa miaka ya 1960, kipindi hicho ni asilimia 5 tu ya wakazi wa vijijini waliishi katika makazi yanayoeleweka vijijini. Lakini kufikia mwaka 1975 sera ya ujamaa ilikuwa imeishalazimisha zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa vijijini kuishi katika makazi mapya.
Bei zilizopangwa chini ya mfumo wa ujamaa zilikuwa haziendani na bei halisi ya soko; zililenga kuwawezesha watu wa mijini kununua chakula kwa bei ndogo na kuleta faida zaidi katika mazao ya biashara.
Utaratibu huu ulionekana ni mzuri lakini kimsingi Serikali ilifanya makosa. Tafiti za kitaalamu zinaonyesha kwamba kilimo cha pamoja chini ya mfumo wa vijiji vya ujamaa kilichangia moja kwa moja kuporomoko kwa sekta ya kilimo. Mfano katika muongo wa 1970-1980 uzalishaji wa mazao ya biashara ulikuwa chini sana ikilinganishwa na miongo miwili iliyotangulia (1950-1970), ambapo sekta ya kilimo ilikuwa inakuwa kwa asilimia 6 kwa mwaka.
Matokeo yake wakulima walikatishwa tamaa na uzalishaji wa chakula ulipungua sana na kusababisha taifa kuagiza chakula kutoka nje. Mfano, kati ya mwaka 1973 na 1974, Tanzania iliagiza kutoka nje mahindi, mchele, na ngano yenye uzito wa tani 410,200, wakati uzalishaji ulikuwa tani 58,100 tu. Hiki kinakumbukwa kama kipindi cha njaa cha mwaka 1974/75.
kiasi cha chakula kilichoagizwa kutoka nje na kiasi kilichozalishwa ndani ya nchi kiliendelea kubadilika badilika mwaka mmoja hadi mwingine, kwa wastani wa tani 200,000 za nafaka kwa mwaka katika kipindi cha miaka ya 1970 na tani 300,000 mwanzoni mwa miaka ya 1980 kiliagizwa kutoka nje.
Kufuatia vita ya Tanzania na Uganda mwaka 1978/79 na kushindwa kwa mfumo wa kisoshalist duniani, hali ilizidi kuwa mbaya katika kipindi cha miaka ya 1980 ambapo usafirishaji wa mazao kwenda nje ya nchi ulikuwa ni pungufu kwa zaidi ya nusu kwa uzalishaji wa muongo uliotangulia.
Haya yote yanaweza kutafsiriwa kama kushindwa kwa sera za kuendeleza kilimo chini ya Serikali ya awamu ya kwanza.
Kanda za uzalishaji
Lakini jambo moja muhimu ni kwamba Serikali ilijiingiza kikamilifu katika maisha ya kila siku ya mkulima. Hivyo, pamoja na misukosuko mingi iliyoelezwa hapo juu mkulima alikuwa analindwa; mzigo mkubwa ulibebwa na Serikali kwa njia ya kutoa ruzuku mbalimbali.
Wale wote wenye umri kama wangu watakumbuka jinsi wakulima walivyokuwa wananufaika hasa kutokana na mazao ya kibiashara.
Mwalimu Nyerere, kwa kuona mbali, alihakikisha kila zao linakuwa na kiwanda cha kusindika, hivyo kufanya sekta ya kilimo kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya viwanda. Viwanda vya korosho, kahawa, pareto, pamba, nyizi, nguo, ngozi, tumbaku, n.k. vilianzishwa na kuajiri watu wengi sana.
Wakati naandika makala zangu za awali msomaji wangu aliwahi kunikumbusha hali ilivyokuwa kipindi hicho. Hapa nanukuu:
“Tuna viongozi wenye mawazo ya “Copy & Paste” wasiosimamia fikra zao, wanasubiri Bush aseme wao wa-copy bila kufikiri kesho atasema nini na itakuwaje akibadili fikra. Wameua viwanda ambavyo ilikuwa mbeleko ya kilimo na uchumi wa Watanzania kwa ujumla.
Mwalimu alilijua hili na kuanzisha viwanda ambavyo vilimwajiri mkulima moja kwa moja; Viwanda vya nguo, sigara, kahawa, chai, nyama, ngozi, viatu, mvinyo, mafuta ya kula, katani, NMC & Gapex n.k. Mwalimu aliweka kanda za uzalishaji mazao ili kujenga “kiburi” cha ushindani kikanda uliochambuliwa sanjari na fursa na hali ya hewa ya ukanda husika.
Ziko wapi the Big Four, iko wapi jeuri ya wasukuma kusema pamba ni dhahabu, Igembe Nsabo (jembe ni mali), Mji Kasoro bahari (kwa mantiki ya viwanda vilivyokuwepo Morogoro), mawese Kigoma, mkonge Tanga n.k.
Jiografia ya Tanzania shule za msingi tulijifunza pamoja na mambo mengine, “kanda” za Uzalishaji mazao. Tulisoma kilimo cha pamba - Shinyanga, miwa - Morogoro, mpunga - Kyela, kahawa (arabica na robusta) – Moshi na Bukoba, zabibu na karanga - Dodoma, na kadhalika, inasikitisha kwamba leo imekuwa ni hadithi na inawezekana na vitabu hivyo vimechomwa moto.
Haiingii akilini kwamba leo kuitwa mkulima ni “tusi” maana tunawasikia vijana kijiweni wakitoa matusi na kejeli kwa kuitana “we mkulima nini”? Wakimaanisha ni mtu asiye na mbele wala nyuma, mshamba na maana zingine zisizoleta staha kusikika kwa mwananchi anayejishughulisha na kazi ya kilimo. Nani katufikisha hapo?
Dk. Gabagambi umegusia namna viongozi wetu wanavyotamani maendeleo ya viwanda na miji ya nchi za magharibi. Hawajishughulishi kujua mchakato uliowafikisha wenzetu pale.
Hata hivyo kilimo kwao bado ni muhimili mkuu kwani walichokifanya ni ku-intensify kilimo kwa kuwawezesha wakulima wachache kuzalisha mazao ya kuwatosheleza watu wote na hivyo kuwasukuma wengine kwenye ajira za viwandani. Hatuwasikii wakiagiza chakula hawa, hivi viongozi wetu wanapotamani viwanda na miji ya wenzetu, hawajiulizi mahindi wanayokula yanalimwa viwandani? Misaada ya mahindi tunayoomba kwao inatoka wapi? Tunapohimiza viwanda wakulima wetu tumewafikisha level gani? The big four wako wapi? Na hivi viwanda wanavyohubiriwa ni vya kuzalisha kitu gani? Kama ni vyuma watakaofanyakazi huko watakula nini? Na hivyo vyuma tutamuuzia nani? kama ni Mtanzania kwa pesa ipi atanunua? Kama ni viwanda vya mazao yatokanayo na kilimo ni yepi hayo? Mbona vilivyokuwepo vilikufa tuna mbadala upi ambao utavikuza na kuviendeleza.
Mwalimu alisema, lengo la baadaye la viwanda mfano vya nguo ni kutengeneza nguo kutosheleza soko la ndani ambalo ni kubwa (Akinamama walijivunia kuvaa vitenge na Kanga za Urafiki, Mwatex, Mutex, nk) na kuuza nje nyuzi na si pamba ghafi.
Sina uhakika kama alikuwa anaeleweka kwa wasaidizi wake, ila nina uhakika hakuwa mchoyo kiasi hicho kutowaelekeza, mbona tunayasoma kwenye vitabu na hotuba zake? Yatosha tu kusema alipuuzwa kama leo wasivyopenda kusikia hotuba zake na kutukuza maandiko yake”.
Awamu ya pili ya Uongozi – Rais Ali Hassan Mwinyi
Serikali ya Awamu ya Pili ya uongozi chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, inakumbukwa kwa kuanzisha mfumo wa uchumi huria chini ya mwongozo wa IMF na Beki ya Dunia.
Serikali iliparamia uchumi huria kana kwamba kilikuwa kimegunduliwa kidonge cha maajabu chenye uwezo wa kutibu maradhi ya aina yoyote ya uchumi.
Kipindi hiki kilitawaliwa na Serikali kubana matumizi kwa kujiondoa ghafla na kikatili katika shughuli za moja kwa moja za uchumi. Matokeo yake miundombinu haikupewa kipaumbele, ajira zilisitishwa katika sekta zote na mtindo wa wananchi kuchangia huduma mbalimbali ulianzishwa.
Sekta ya kilimo iliathirika kwa njia nyingi zikiwemo upungufu mkubwa wa mabwana na mabibi shamba; kupunguzwa na hatimaye kufutwa kwa ruzuku kwenye pembejeo; vyama vya ushirika kukumbwa na madeni makubwa yaliyokuwa yakitolewa kisiasa kipindi cha nyuma na baadaye vyama vingi vya vilifirisika.
Bodi za mazao zilidorora; mashamba na viwanda vya usindikaji vya umma vilisimamisha uzalishaji na kukaa muda mrefu bila kufanyakazi vikisubiri ubinasfishaji na hivyo kuharibika. Vile vilivoendelea kuzalisha vilifanya hivyo kwa kukosa utaalamu na mitaji na hivyo kuzalisha kwa hadi asilimia 10% ya uwezo wake.
Hali hii iliendelea hadi katika miaka ya 1990 ambapo viwanda vingi vya nguo vilifungwa vikisubiri wanunuzi. Viwanda vikubwa vya nguo kama Ubungo Spinning Mill, Kiltex, Mwanza Textiles, Musoma Textiles, na Mbeya Textiles vilidorora kabisa na kuacha uzalishaji hata baada ya kubinafsishwa.
Utaratibu wa kuyapa mashirika ya umma wajibu wa kipekee (monopolistic power) wa kudhibiti uingizaji kutoka nje wa bidhaa tunazoweza kutengeneza wenyewe (imports) ulifutwa. Matokeo yake bidhaa za kila aina kutoka nje zilifurika soko la ndani.
Sekta ya nguo kwa mfano ilijaa nguo za mitumba kutoka nchi za Asia Mashariki, Ulaya na Marekani ambazo zilikuwa na ubora na bei nzuri zaidi kuliko zilizokuwa zinazalishwa ndani ya nchi.
Utaratibu huu uliendelea hadi kwenye awamu ya tatu ya uongozi ambapo kufikia mwaka 2002 uingizaji wa nguo za mitumba ulifikia asilimia 35.2 ya bidhaa zote zinazoingizwa nchini kutoka nje.
Pia kufuatia uchumi huria bei za pembejeo zilipaa hivyo wakulima kushindwa kuzimudu na kusababisha uzalishaji kushuka. Wakulima wadogo waliachwa kupambana na wafanyabiashara wakubwa katika kuuziana mazao. Matokeo yake ilikuwa ni bei kandamizi kwa wakulima wadogo.
Wadau mbalimbali wakiwemo wakulima walijiingiza katika vitendo vya udanganyifu. Wafanyabiashara walitumia madebe yaliyobondwa na mizani iliyochakachuliwa. Kwa upande wao wakulima walichanganya mazao na mchanga, au takataka nyingine – kwa njia ya kulipa kisasi - jino kwa jino!
Kufuatia kuparaganyika kwa sekta ya kilimo, benki nyingi ikiwemo CRDB iliyokuwa imeundwa mahsusi kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo iliipa kisogo mikopo ya kilimo, na hasa baada ya ubinafsishaji.
Kuacha viwanda hivi vife pengine ndilo kosa kubwa zaidi ambalo Tanzania ilifanya katika juhudi za kuendeleza kilimo nchini.
Ingefaa kuiga mfano wa nchi ya Vietnam ambayo iliyachukulia mageuzi ya kiuchumi kwa uangalifu mkubwa. Mageuzi hayo katika nchi ya Vietnam yalitawaliwa na mwendelezo wa misingi ya ki-socialist sambamba na ushiriki wa sekta binafsi.
Serikali haikubinafsisha mashirika yake ya umma. Badala yake iliruhusu sekta bianafsi kuanzisha viwanda vyake peke yake au kwa ubia na serikali. Kufuatia mageuzi hayo, sekta ya viwanda ilikua kwa kasi.
Viwanda vya Serikali na vya watu binafsi viliongezeka kwa kasi. Kwa mfano, uzalishaji wa nguo uliongezeka kwa asilimia 128.5 kati ya mwaka 1990 na 1997, na kwa kipindi hicho nguo za mitumba zilikuwa ni asilimia 0.07 tu ya bidhaa zinazoingizwa nchini humo (imports).
Awamu ya tatu ya uongozi – Rais Benjamin William Mkapa
Awamu ya Tatu, mwanzoni iliendeleza tabia ya kutelekeza kilimo, ingawaje kilimo kilifaidi kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
Lakini hali igeuka mwishoni mwa kipindi cha kwanza ambapo Serikali ilianzisha upya msukumo katika sekta ya kilimo iliyokuwa imetelekezwa katika muongo mmoja uliopita.
Kwa vile hapakuwepo na miongozo ya maana juu ya uendelezaji wa sekta ya kilimo, awamu hii ina sifa ya kuwa na utitiri wa sera na mipango mbalimbali ya kuendeleza sekta ya kilimo, chini ya Dira ya Taifa 2025 na MKUKUTA.
Mkakati maalum kwa sekta ya kilimo ulikuwa Agricultural Sector Development Strategy (ASDS) iliyokuwa chimbuko la program ya kuendeleza kilimo ijulikanayo kama Agricultural Sector Development Program (ASDP).
Baadhi ya sera na mipango mingine chini ya awamu ya tatu ni pamoja na lundo la sera mbali mbali za kilimo, mifugo, ushirika, uvuvi na misitu. Baadhi yake ni pamoja na sera ya maendeleo ya kilimo na mifugo ya mwaka 1997 na sera ya taifa ya usalama wa chakula ya mwaka 2004.
Pia ilianzishwa program ya kuendeleza mfumo wa masoko ya mazao ya kilimo (AMSDP - 2002), na Program ya Huduma ya Fedha Vijijni (RFSP-2001).
Lakini pia katika kipindi hiki ulizuka msururu wa asasi za kiraia zaidi ya mia moja zikisaidiana na Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwenye sekta ya kilimo. Baadhi ya asasi hizo ni MVIWATA, Hakiardhi, Maarifa ni Ufunguo, PELUM, ActionAid International Tanzania, KADERES, RUDI, n.k.
Kwa ufupi, kama tulivyoona hapo juu, tunaweza kusema Awamu ya Tatu ya uongozi wa Tanzania chini ya Rais Benjamin Mkapa ilifanyakazi ya kutayarisha mipango ya kuendeleza kilimo ikiwemo program maarufu ya ASDP.
Lakini pia ni katika awamu hii ruzuku ya mbolea ilirudishwa baada ya kuwa imefutwa katika miaka ya 1980 na 1990. Bajeti ya kilimo ilianza kupanda kwa kasi. Vilevile baadhi ya mashamba makubwa yaliyobinafsiswa yalifanyakazi nzuri mfano viwanda vya sukari vya Mtibwa, Kilombera, Kagera, na TPC Moshi.
Pamoja na mafanikio hayo hapakuwepo mabadiliko makubwa katika maisha ya kila siku ya mkulima mdogo. Ukuaji wa sekta ya kilimo uliendelea kuwa chini ya asilimia 4 kwa mwaka.
Awamu ya nne ya uongozi – Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilikuwa na kazi moja kubwa ya kutekeleza mipango ya kuendeleza kilimo iliyopangwa wakati wa Awamu ya Tatu kabla ya kuanzisha mipango yake yenyewe, ambayo naweza kusema ni mingi lakini imetawanyika (fragmented) na hivyo kuwa na hatari ya kutumia fedha nyingi kwa mafanikio kidogo.
Awamu hii bado inaendelea, iko katika mwaka wake wa saba, lakini tumeshuhudia kauli nzuri nzuri zisizo na utekelezaji.
Kauli ya kupanda miti kama kichaa
Mfano, jambo la kwanza lililowapa wananchi matumaini ni Serikali ya awamu hii kutangaza awali kabisa kwamba ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira ingepanda miti kama kichaa. Sisi tunaopata bahati ya kusafiri ng’ambo tulidhani sasa Tanzania inaelekea kupendeza kama nchi za wenzetu ambazo miti ni sehemu ya maisha.
Kwa mfano katika nchi ya Ujerumani unaweza kusafiri kilometa nyingi sana ukisindikizwa na miti pande zote mbili za barabara na wakati mwingine unakatisha misitu minene ya kupanda. Tulidhani hadi kipindi chake cha uongozi kinaisha, tutaweza kuona miti kandokando ya barabara zetu kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma – Songea – Mwanza – Arusha, n.k.
Bila shaka ukiuliza kauli hii imeishia wapi utapewa takwimu ya kutia moyo juu ya mamilioni ya miti iliyokwisha kupandwa tangu 2006! Narudia kusema, watu hawali namba. Namba ambazo haziakisi uhalisia ni kuwafanya watu majuha.
Kama kweli Serikali ilikuwa na nia ya kupanda miti ilishindwa nini kuziagiza Halmashauri zote nchini kupanda na kutunza miti angalau kwa upana wa meta 50 kila katika kipande chote cha barabara ya lami inayopita katika Halmashauri husika.
Baadaye kwa kushirikiana na kitivo cha misitu cha Chuo Kikuu cha Kilimo, SUA, Halmashauri zingewezeshwa kupanda miti bora katika mpango huo inayoweza kuvunwa baada ya kipindi fulani.
Isingeishia hapo tu, serikali ingeagiza Halmashauri kuweka na kusimamia sheria kali za kuzuia moto misituni (bush fire) kwa kutumia uongozi wa vijiji. Haya sio mambo ya kufikirika; mbona jirani zetu hapo Burundi wameweza kuzuia uchomaji ardhi kwa asilimia mia moja. Wenzetu wanaona uchomaji ardhi kama mauaji ya kimbari ya ardhi (land genocide).
Kauli ya kufanya Morogoro kuwa ghala la taifa
Kauli nyingine ya kuvutia ambayo Serikali ilifanya mnamo mwaka 2007 ni kutangaza rasmi mkoa wa Morogoro kuwa ghala la taifa la chakula, katika mpango uliobatizwa jina la ‘Fanya Morogoro kuwa Ghala la Taifa’ (FAMOGATA).
Bila shaka Morogoro ilichaguliwa kuwa ghala la taifa kwa sababu mbalimbali zikiwemo mkoa kubarikiwa ardhi nzuri yenye rutuba, mito mingi, mabonde mazuri ya kilimo, na ardhi kubwa ambayo haijalimwa.
Pia Morogoro iko karibu na Dar es Salaam ambapo ni rahisi kusafirisha bidhaa kwenda nchi za jirani au masoko ya kikanda na kimataifa.
Naweza kusema, pengine FAMOGATA linaweza kuwa wazo la kihistoria katika harakati za kuendeleza kilimo nchini. Hii ni kwa sababu ingeondoa mtawanyiko niliotaja hapo awali. Morogoro ingeanza kama majaribio (pilot) na baadaye kutumia uzoefu huo katika maeneo mengine ya nchi. Yako wapi sasa?
Ugonjwa ni uleule – maneno matamu utekelezaji sifuri. Wanaojua kinachoendelea ni kikundi kidogo cha viongozi wachache walio kwenye hicho kinachoitwa kamati ya FAMOGATA.
Si ajabu kusikia wanaomba bilioni kadhaa, eti kutekeleza mipango ya FAMOGATA! Kama mpango huu ungetekelezwa vizuri kila mkazi wa Morogoro na wapita njia wote wangehisi mawimbi ya FAMOGATA.
Mpango wa ASDP
Pamoja na kauli zisizotekezeka nilizotaja hapo juu nitatumia muda huu kutathmini baadhi ya juhudi za kuendeleza kilimo chini ya Awamu ya Nne kwa kuanzia na ASDP ambayo ni mwendelezo wa shughuli za Awamu ya Tatu.
Kama tulivyoona awali, mkakati mkuu wa kuendeleza kilimo Tanzania uliopangwa wakati wa awamu ya tatu ni Agricultural Sector Development Straregy (ASDS), ambayo utekelezaji wake ni Agricultural Sector Development Program (ASDP) ulioanza kutekelezwa mwaka 2006.
Malengo makuu ya ASDP yaliainishwa kuwa ni kufanya kilimo kukua kwa asilimia 5 kwa mwaka, kugeuza kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa cha kibiashara, kuongeza tija katika uzalishaji, kuongeza faida kwa wakulima, kuongeza vipato vya wakulima kwa kuwawezesha kupata pembejeo na utaalamu unaotakiwa, na kuboresha masoko ya mazao.
Kuna mipango kadhaa ambayo imebuniwa katika utekelezaji wa ASDP. Mifano ya mipango hiyo ni pamoja na mpango wa kusaidia uwekezaji mdogo na wa kati vijijini (Rural Micro, Small and Medium Enterprise Support Programme) ambayo ilianza mwaka 2007 na inatarajiwa kwisha mwaka 2014; mpango wa kuendeleza sekta ya mifugo (Support for Pastoral and Agro-Pastoral Development) ambayo ilianza mwaka 2007 na inatarijia kwisha mwaka 2015; na program ya kusaidia huduma za kilimo (Agricultural Services Support Programme) ambao ni mpango wa miaka 15 kuanzia 2008.
Utekeleza wa mipango iliyoanza 2006 unaendelea na mingine imeanza hivi karibuni, lakini wakulima ambao ndio walengwa wakuu wajiulize kama kwa mambo yanavyokwenda, kuna matumaini ya hali zao za kilimo kuwa zimebadilika sana miaka mitatu au minne ijayo.
Bajeti ya kilimo imeongezeka
Mojawapo ya mambo makubwa katika Awamu ya Nne ni msukumo mpya wa kuendeleza kilimo. Tumeshuhudia bajeti ya sekta ya kilimo ikipanda kutoka asilimia 3 ya bajeti kwa mwaka 2001/2 hadi kufikia asilimia 7.8 mwaka 2010/11. Pia ruzuku imepanuliwa kutoka kwenye mbolea peke yake hadi kwenye bembejeo zingine kama mbegu na zana za kilimo.
Matokeo yake fedha zinazokwenda kwenye ruzuku zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 2 mwaka 2003/4 (sawa na asilimia 1.3 ya bajeti ya kilimo) hadi bilioni 146 mwaka 2010/11 (sawa na asilimia 16.2 ya bajeti ya kilimo).
Lakini tusisahau kwamba kupanga ni kitu kimoja na kutekeleza kwa ufanisi ni kitu kingine, na pia kutenga fedha ni kitu kimoja na kutumia fedha kwa njia inayotakiwa ni kitu kingine kabisa.
Nitatoa ushahidi. Ripoti za kila mwaka za Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) zinaonesha matumizi mengi yenye kutiliwa shaka kwa mtindo wa matumizi yasiyoidhinishwa, matumizi yasiyo kwenye vitabu vya mahesabu, malipo yasiyo ya kawaida, malipo yasiyo na viambatanisho, n.k.
Kwa mfano kati ya mwaka 2001 na 2006, fedha kiasi cha shilingi bilioni 14.5 zilitumiwa vibaya. Pia ripoti ya CAG ya Juni 2008 inaonyesha kwamba kulikuwepo na mashaka sana juu ya matumizi ya shilingi bilioni 2.3 katika programu ya mbolea ya ruzuku.
Dhana ya Kilimo Kwanza
Pia ni katika awamu hii imeanzishwa dhana ya Kilimo Kwanza kwa madai ya kutoa msukumo zaidi katika kuendeleza kilimo. Kama Kilimo Kwanza ni kitu halisi au ni propaganda za kisiasa ni mapema kusema kwa sasa. Lakini lililo wazi ni kwamba dhana yenyewe haieleweki kwa wadau wengi wa sekta ya kilimo.
Hali hii inatoa mwanya kwa kila mtu wakiwemo viongozi kuitafsiri na kuitekeleza kama waonavyo wao inafaa. Tukiachilia mbali mchakato uliozaa Kilimo Kwanza, pamoja na mapungufu yake, dhana yenyewe na andiko lake ni dira muafaka ya kuendeleza kilimo. Nasema hivyo kwa sababu maeneo yote muhimu yameguswa kupitia nguzo zake kumi.
Nguzo hizo ni Dira ya taifa ya Kilimo Kwanza; Kugharamia Kilimo Kwanza, Muundo mpya wa kitaasisi kwa ajili ya usimamizi wa Kilimo Kwanza, Mabadiliko ya mfumo wa kimkakati wa Kilimo Kwanza, Ardhi kwa ajili ya Kilimo Kwanza, Vivutio kwa ajili ya Kilimo Kwanza, Viwanda kwa ajili ya Kilimo Kwanza, Sayansi, teknolojia na rasilimali watu kwa ajili ya Kilimo Kwanza, Miundombinu kwa ajili ya Kilimo Kwanza, Uhamasishaji wa Watanzania kwa ajili ya Kilimo Kwanza.
Katika andishi la Kilimo Kwanza imeonyeshwa waziwazi nini kifanyike lini na nani. Wasiwasi uliopo ni kwamba chapisho la Kilimo Kwanza ni chapisho kama yalivyo machapisho mengi hapa nchini yenye lengo la kuendeleza sekta ya kilimo – mfano Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, MKUKUTA, Mini-Tiger Plan, ASDP, AMSDP, MKURABITA, na sera mbalimbali.
Kama sio mwenyeji wa Tanzania ukisoma ahadi zilizomo katika machapisho haya hasa kuhusu kilimo cha wakulima wadogo utadhani nchi itaendelea kesho. Labda tujipe matumaini kwamba Kilimo Kwanza kitakuwa tofauti kwa vile ni wazo la wafanya biashara tofauti na mipango mingi ya awali.
Lakini hata kama Kilimo Kwanza kitafanikiwa kama kilivyopangwa, kuna mashaka sana kama maisha ya mkulima mdogo yataboreka chini ya Kilimo Kwanza. Sana sana Kilimo Kwanza kinaweza kumuathri mkulima mdogo kutokana na kupoteza ardhi yake chini ya utekelezaji wa dhana hiyo isiyotabirika.
Pamoja na utitiri wa mipango ya kuendeleza sekta ya kilimo, naweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba kiukweli kilimo hakijapiga hatua kubwa kimaendeleo. Bado hali ya chakula siyo ya kuridhisha na umasikini bado umekithiri hasa vijijini.
Hali ya chakula nchini
Ingawa Tanzania sio miongoni mwa nchi zinazojulikana kuwa na tatizo la njaa duniani, bado hali ya upatikanaji wa chakula ina utata katika maeneo mbalimbali ya nchi, jambo ambalo hulazimika kusambaza chakula cha msaada kutoka katika hifadhi ya taifa ya chakula.
Tafiti zinaonyesha kwamba mwaka 2008 mikoa 10 kati ya 21 ya Tanzania Bara, iligundulika kuwa na uhaba wa chakula mara kwa mara, nayo ni Arusha, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mwanza, Mtwara, Shinyanga, Singida na Tabora.
Jumla ya wilaya 20 zinahusika katika uhaba huu. Pamoja na ukosefu huu kuhusishwa na uhaba wa mvua, suala la miundombinu duni ya usafiri linachangia kwa kiasi kikubwa.
Utabiri wa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini unaonyesha kwamba katika kipindi cha 2011/12 Tanzania itazalisha tani milioni 12.8 za chakula. Katika hizo, tani milioni 6.8 zitakuwa za nafaka, na tani milioni 6.0 zitakuwa aina nyingine ya mazao ya chakula. Ukilinganisha na uhitaji, Taifa litakuwa na upungufu wa tani laki 4.1 za nafaka na tani milioni 1.7 za mazao mengine ya chakula.
Utabiri huo unaonesha kuwa pamoja na hayo, mikoa kadhaa ikiwemo Arusha, Pwani, Dar es Salaam, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mwanza, Shinyanga, na Singida itakuwa na ukosefu mkubwa wa nafaka.
Kushindwa kufikia malengo ya milenia
Kutofanya vizuri kwa sekta ya kilimo kuna maana kwamba hali ya umasikini kwa wakazi wa vijijini imeendelea kuwa mbaya. Unaweza kuelewa suala hili ukiangalia suala hili katika mwanga wa malengo ya milenia, na hasa lengo la kwanza (MDG I).
Takwimu zinaonyesha kwamba kwa mwendo wa mambo yalivyo Tanzania haiwezi kupunguza idadi ya masikini vijijini kwa nusu, kutoka asilimia 40.8 mwaka (1992) hadi asilimia 20.4 mwaka 2015 kama inavyotakiwa na malengo ya milenia. Badala yake, kwa kipindi hicho (miaka 23) Tanzania itapunguza umasikini kwa asilimia 4.9 tu.
Kwa hali hii tunatoa wapi ujasiri wa kuwapa watu matumaini ya hali bora katika miaka ya hivi karibuni?
Mpango mpya wa maendeleo wa miaka mitano (2011-2016)
Katika harakati za kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi na hivyo kupunguza umasikini, serikali ya Awamu ya Nne imezuka na mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2011/12-2015/16), kuigiza utaratibu uliokuwa unatumiwa kipindi cha Awamu ya Kwanza ya uungozi wa nchi hii.
Chapisho la mpango huu linaonesha kwamba lengo kuu katika sekta ya kilimo ni kufanya kilimo kuwa cha kisasa, cha kibiashara na chenye tija kubwa.
Ili kufikia lengo hilo mpango utafanya yafuatayo: Kupanua na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji; kurahisisha upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kisasa; kuimarisha shughuli za utafiti na ughani; kuboresha upatikanaji wa masoko; na kuhimiza usindikaji.
Mtu mwenye akili huru akipitia mpango huu kwa makini haraka sana atagundua kwamba hakuna kitu ambacho unaweza kukiita “ubunifu” katika mchakato mzima wa utekelezaji wake ili kuweza kutofautisha mpango huu na mipango mingi iliyotangulia na kushindwa – maneno, ahadi na mbinu ni zilezile.
Kuna mashaka sana kwamba mpango huu utafanikiwa kwa sababu unadai utatekeleza mambo yote kwa miaka mitano ambayo tumeshindwa kuyatekeleza katika kipindi cha miaka 50! Mpango hauelezi tumekuwa tukikosea wapi na umewekwa mkakati gani kukwepa makosa hayo katika kutekeleza mpango huu.
Kwa kifupi hakuna ubunifu katika utekelezaji wa mpango huu. Ubunifu kidogo unajitokeza katika kutafuta fedha za kugharimia mpango wenyewe.
Ikumbukwe kwamba si kweli kwamba Tanzania haiendelei kwa kukosa mipango mizuri, la hasha. Nchi ina ugonjwa sugu wa kushindwa kutekeleza mipango yake kwa dhati.
Machapisho yanaonyesha kwamba mpango huu utagharimu shilingi trilion 37.3, kati ya hizo shilingi trilioni 3.8 sawa na karibu asilimia 10.3 ya bajeti yote zitatumika kwenye sekta ya kilimo.
Hii ni fedha nyingi sana na ni mfano mzuri wa kulenga mbali nilikoongelea mwanzoni mwa mada hii, na sina shaka kwamba fedha hii inaweza kupatikana. Lakini kwa vile mbinu za utekelezaji zitakuwa zilezile zilizozoeleka na watu ni walewale natabiri (hypothesize).
Fedha yote hii itaisha na sekta ya kilimo itakuwa na matatizo yale ya miaka yote, ambayo ni pamoja na: Kutegemea huruma za mbingu kuleta mvua; ukosefu wa miundombinu ya kusaidia uzalishaji na usambazaji; mfumo dhaifu wa utafiti na ughani; matumizi hafifu ya pembejeo na zana za kisasa; kukosa mfumo madhubuti wa mikopo kwa wakulima wadogo; bei kandamizi kwa wakulima wadogo; mfumo duni wa usambazaji wa pembejeo; matumizi ya mbegu duni za mazao na wanyama; kiwango kidogo cha usindikaji wa mazao ya kilimo; kukosekana kwa mfumo madhubuti wa matumizi ya ardhi, na kuathriwa na mabadiriko ya hali ya hewa.
Tunasubiri kwa hamu kuona kama huu hautakuwa mpango wenye ajenda ya siri kwa ajili ya uchaguzi wa 2015 kama ilivyokuwa Kilimo Kwanza katika uchaguzi wa 2010.
Mpango wa kukuza kilimo kanda ya kusini mwa Tanzania
Ninapomalizia kueleza shughuli za kuendeleza kilimo katika Awamu ya Nne ya uongozi wa taifa hili nigusie kidogo mpango wa kukuza kilimo wa kanda ya kusini mwa Tanzania (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT).
Kama nilivyoeleza awali kwa vile mkakati wa utekelezaji Kilimo Kwanza hauko wazi; inategemea na fikra na ubunifu wa mhusika, mpango wa SAGCOT inasemekana kuwa ni kutekeleza Kilimo Kwanza.
SAGCOT ni mpango wa kimataifa wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Mpango ulizinduliwa Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Dunia wa kiuchumi kwa Afrika uliofanyika Mei mwaka huu. Mpango huu utahusisha eneo lenye ukubwa wa karibu theluthi moja ya ardhi ya Tanzania Bara.
Utahusu mikoa yote inayopitiwa au kupakana na reli ya TAZARA, yaani Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Iringa, Mbeya na Rukwa. Utagharimu kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.1 sawa na shilingi trillion 3.5 (kwa sasa) kutoka kwa wadau mbalimbali wapatao 22 yakiwemo mashirika na makampuni maarufu duniani kama USAID, Monsato, Unilever, NMB, Stambic Bank, AGRA, FAO, na CTI. Ni mpango wa miaka 20.
Kulingana na chapisho la SAGCOT, mojawapo ya madhumuni yake ni kutoa fursa kwa wakulima wadogo kushiriki katika kilimo cha biashara na faida. Hili litawezekana kwa kutoa fursa ya wakulima wadogo kuwa na mikataba na wafanya biashara wakubwa kwenye sekta ya kilimo katika ukanda huo.
Mikataba hii itawezesha wakulima wadogo kupata pembejeo, huduma za ughani, usindikaji, na masoko.
Inasemekana pia kwamba SAGCOT itavisaidia vikundi vya uzalishaji vya wakulima wadogo kuingia katika uhusiano wenye faida na wasindikaji wakubwa. Umwagiliaji nao inasemekana utapatikana kwa wazalishaji kupitia utaalamu wa hali ya juu kwenye mashamba.
Baadhi ya mafanikio ya SAGCOT itakuwa kuweka hekta 350,000 kwenye uzalishaji wenye faida, zikihudumia masoko ya ndani na ya kikanda; maelfu ya wakulima wadogo watabadilishwa kuwa wa wakulima wa kibiashara wakiwa na huduma ya umwagiliaji; inatarajiwa kwamba kiasi cha nafasi mpya za kazi 420,000 zitatengenezwa katika mnyororo wa thamani (value chain).
Zaidi ya watu milion mbili wanategemewa kuondolewa moja kwa moja kutoka kwenye umasikini; thamani ya mwaka ya shughuli za kilimo katika ukanda huu itakuwa dola za Marekani bilioni 1.2; na kutakuwepo na usalama wa chakula.
Iwapo hayo yote yatafanyika basi utakuwa mwanzo mzuri wa kuendeleza sekta ya kilimo.
Lakini niseme kwamba kuna maangalizo kadhaa kuhusu mpango huu. Inabidi Serikali iwe macho isije ikawa SAGCOT ni mbinu ya wafanyabiashara kutoka nje ya nchi ya kujipatia ardhi kirahisi kwa ahadi za kilaghai kama walizopewa mababu zetu.
Pia, ili kuwa na manufaa endelevu ingebidi uzalishaji wote kwenye SAGCOT ufanywe na wakulima wadogo baada ya kusaidiwa kujiunga katika vikundi vinavyolima mapande makubwa ya ardhi kwa ushirikiano maalumu (block farming), na wala sio kufanywa wakulima wadogo wenye vishamba vidogo kuzunguka mashamba ya wakulima wakubwa (outgrowers).
Na mwisho, ahadi ya kutengeneza ajira mpya 420,000 kwa miaka 20 (ajira 21,000 kila mwaka) haitii matumaini katika hali ambayo kila mwaka taifa linapata vijana zaidi ya 700,000 wanaoingia kwenye soko la ajira, na ambapo familia masikini ni kama milioni tano Tanzania.
Kama wakulima wadogo ni vigumu kuwaweka pamoja katika mpango huu, basi lingekuwa wazo la hekima kushirikisha wahitimu wa vyuo vikuu, hasa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kupitia mitandao yao kama vile ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa SUA, yaani SUA Graduate Enterpreneurs Cooperative (SUGECO).
Hawa wapewe mapande ya ardhi (block farms) ndani ya SAGCOT na wasaidiwe kuwa wadau muhimu katika mnyororo wa thamani (value chain) katika sekta ya kilimo.
Bado hatujachelewa, haya yanaweza kufanyika kwa manufaa ya kizazi cha leo na baadaye cha taifa hili.
Awamu ya Nne bado inaendelea, kwa hiyo tusubiri tuone hadi 2015 tutakuwa tumesogea umbali gani kutoka kwenye maneno matamu tuliyozoea.
Fursa na machungu ya utandawazi
Mwanzoni mwa mada hii nilisema kwamba nitamalizia kwa kupitia kwa ufupi historia ya ubepari na janga linalosubiri taifa hili iwapo hatutakuwa makini na hiki kinachoitwa utandawazi (globalization). Sasa ni wakati muafaka kufanya hivyo na baadaye nitamalizia kwa kutoa mapendekezo.
Bila shaka neno utandawazi sio geni kwa wasomaji wengi. Ni miongoni mwa maneno yanayotamkwa mara nyingi kwa siku, na mtu anaweza kushinda mabishano kirahisi iwapo atasingizia utandawazi kwenye hoja zake.
Lakini hakuna shaka kwamba utandawazi laweza kuwa miongoni mwa maneno yanayoeleweka kwa kiwango kidogo kwa karne hii.
Katika upande mmoja wa dhana hii kuna kundi la watu wakiwemo wana harakati, vyama vya wafanyakazi na wakulima, na hata watu wa kawaida mtaani ambao wanapinga kwa nguvu zote utandawazi.
Lakini katika upande mwingine, kuna kundi la watu wakiwemo wa uchumi, wafanyabiashara, baadhi ya waandishi wa habari na wanasiasa, ambao waziwazi wanasifu utandawazi kwamba ni shetani wa lazima asiye epukika.
Hakika utandawazi kwa maana ya mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali na chumi za dunia hauepukiki na ni kitu kilichoanza zamani sana. Kimekuwa kikitokea kwa karne nyingi na matokeo yake ulimwengu umezidi kuwa mdogo siku hadi siku; wengine wanasema umekuwa kama kijiji kidogo tu.
Mazao kama pilipili, mahindi, na viazi ambayo zamani yalikuwa yanapatikana Amerika ya Kusini tu sasa hivi ni chakula cha kawaida hapa Afrika, India na Ulaya. Viungo zamani kutoka Indonesia sasa vinalimwa kila mahali duniani.
Hali hii haikuishia katika bidhaa tu, hata hali ya kuwepo kwa watu weusi na weupe katika kila nchi kama matokeo ya utumwa, ukoloni na biashara ni sehemu ya mchakato wa utandawazi.
Kama hali hii ni ya kawaida na imekuwa ikitokea, kwa nini kuna kelele nyingi sasa kuliko zamani?
Tofauti ya utandawazi wa zamani na wa sasa
Tofauti kubwa kati ya utandawazi wa zamani na utandawazi wa sasa ni kasi ambayo utandawazi wa sasa inatokea. Mabadiliko ya haraka ya teknolojia katika tasnia ya elektroniki imebadilisha kabisa mawasiliano ya wanadamu.
Kwa mfano inachukua chini ya saa kumi na sita kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Tokyo, Japan, wakati miaka ya 1970 iliyopita ilikuwa inachukua takribani zaidi miezi mitatu.
Kuwepo kwa intaneti na mapinduzi katika mfumo wa simu kumewezesha watu na biashara kuwasiliana kirahisi kwa ufanisi zaidi. Vilevile njia hizi mpya za mawasiliano zimesaidia kuua tamaduni za dunia na kuwa na utamaduni unaofanana miongoni mwa watu wa rika moja, mfano vijana.
Kwa mfano, aina ya mapishi, mavazi na muziki wa kimagharibi unaonekana kuwavutia mamilioni ya vijana kutoka vijijni hadi majiji makubwa duniani. Tanzania sio kisiwa na hakuna sababu ya kuamini kwamba Tanzania itaepuka utandawazi au mchakato wa utandawazi utasimama kwa miaka ya hivi karibuni.
Swali ni je, utandawazi kama unavyojionesha kupitia uchumi huria, ubinafsishaji, na uwekezaji ni sawa?
Soko huria lisipodhibitiwa hutanua mwanya kati ya walionacho na wasionacho
Kwa njia nyingi utandawazi una fursa ya kuboresha uzalishaji (tija), utundu na ubunifu kupitia matumizi sahihi ya teknolojia, ambayo baadaye yatasababisha kuwepo kwa bidhaa nyingi duniani kuliko kama nchi zingejifungia.
Kama hali ndiyo hiyo, kwanini baadhi ya watu wanapigana usiku na mchana kujaribu kusimamisha mchakato huu wenye neema kwa dunia?
Jibu la swali hili ni kwamba ongezeko la bidhaa au huduma duniani haligawanywi kiusawa miongoni mwa wadau katika mchezo huu wa utandawazi, na hili sio jambo la ajabu – ndivyo uchumi huria unavyofanyakazi.
Sababu mojawapo ni kwamba umiliki wa maliasili na vipaji unatofautiana baina ya mtu na mtu au nchi na nchi. Kwa hiyo iwapo soko huria halitadhibitiwa huwa na tabia ya kupanua mwanya kati ya walio nacho na wasionacho. Walionacho watatumia fursa zinazoletwa na soko huria na kujilimbikizia mali, wasionacho watakuwa watazamaji.
Watawala wa nchi nyingi wanalijua hilo; ndio maana hujishughulisha na sera za kutawanya mafanikio ya kiuchumi (income distribution) kwa njia mbalimbali mfano kodi, ruzuku na njia mbalimbali za kudhibiti mfumo wa uchumi.
Kama soko hupanua mwanya kati ya mtu na mtu katika ngazi ya kitaifa, kwanini lishindwe kufanya hivyo katika ngazi ya kimataifa?
Hakika linafanya tayari. Katika kitabu chake alichokiita “The No-Nonsense Guide to Globalisation” (yaani Mwongozo Makini Juu ya Utandawazi), mtaalamwa uchumi, Wayne Ellwood anasema, kati ya mwaka 1990 na 2000, mgawanyo wa pato la kibiashara ulikuwa kama ifuatavyo: Ulaya (EU) ndiye iliyoibuka na mgao mkubwa ikijipatia dola za Marekani bilioni 80 akifuatiwa na China (Dola bilioni 35), Japan (Dola bilioni 25) na Amerika (USA) (Dola bilioni 20). Nchi zingine zote zilizobaki (isipokuwa Afrika) ziliambulia dola bilioni 10 tu. Afrika ilipoteza dola bilioni 3!
Katika ngazi ya taifa kuna Serikali inayoweza kuweka utaratibu wa kutawanya mapato, bahati mbaya hakuna Serikali ya kidunia ya kufanyakazi kama hiyo. Na hiyo ndiyo changamoto kubwa katika utandawazi wa leo.
Mchumi wa Uingereza, John Maynard Keynes alipendekeza wazo la kuwa na kitu kama hicho mwaka 1944 mjini Bretton Woods, Uingereza wakati wa mkutano wa kutafuta muundo mpya wa kiuchumi duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kuparaganyisha mfumo uliokuwepo. Lakini kwa maslahi na nguvu kubwa za kijeshi za Marekani, wazo hilo lilitupwa kapuni.
Wawekezaji sio mjomba wala shangazi
Ukweli ni kwamba dhana nzima ya nguvu za soko (demand and supply) kuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi imejikita katika kazi ya mkongwe wa uchumi, Adam Smith, katika kitabu chake cha ‘The Wealth of Nations’ (Utajiri wa Mataifa) alichochapisha zaidi ya miaka 250 iliyopita. Kwa hiyo sio dhana mpya.
Fikra za Smith zilikuwa kwamba, kama watu wakipewa uhuru wa kujilimbikizia mali kwa jasho lao, kuna mkono au nguvu zisizoonekana ambazo zitahakikisha kila mwanajamii anafaidi. Mfano kama mtu atanunua basi ili awe tajiri, wananchi watafaidi kwa kuwa na njia bora ya usafiri katika shughuli za maisha yao ya kila siku.
Mara baada ya kusoma mawazo ya Smith, mataifa mengi yalivutiwa na kuijaribu, lakini walishindwa vibaya katika karne ya 19. Dhana hii iliachwa na nafasi yake kuchukuliwa na mfumo wa Serikali kujiingiza katika shughuli za kila siku za kiuchumi ili kuhakikisha uchumi wa taifa unakua kama ilivyopendekezwa na Keynes.
Katika miongo mitatu iliyopita suala la uchumi huria limejitokeza tena, na baadhi ya wanasiasa wamelikumbatia kana kwamba ni muarobaini wa matatizo yote ya uchumi. Wamesahau kwamba tunaishi katika ulimwengu uliotofauti sana na ule Smith alipoanzisha dhana uchumi huria.
Nyakati hizo wamiliki wa biashara waliishi katika jamii zao wakiwa wamezungukwa na ndugu, jamaa marafiki na jumuiya wanayoifahamu vizuri. Kwa sababu hiyo, waliweza kuona madhara ya umasikini unaozunguka biashara zao; na hata hivyo walilazimika kuwasaidia watu wa eneo hilo kwani wengi walikuwa ndugu zao.
Sasa hivi wamiliki wa biashara wanakaa maelfu ya kilomita mbali kabisa na biashara zao zilipo. Hawa mameneja tunaowaona wakiongoza makampuni ya kigeni ni wataalamu tu walioajiriwa kuendesha makampuni kwa niaba ya wamiliki.
Kwa maana hiyo, wamiliki halisi hawajui na hawaoni madhara ya makampuni yao kwa jamii inayozunguka. La muhimu kwao ni faida inayotiririka kwenda waliko.
Na kama hakuna faida wataondoa mitaji yao bila huruma na kuipeleka kwingine, au kuwafukuza mameneja. Hawa sio kina mjomba na shangazi; wako tayari kufanya lolote kuhakikisha wanajilimbikia mali kadiri mazingira yanavyo ruhusu.
Mitizamo ya baadhi ya wawekezaji ni hasi
Hatuwezi kuwa na hakika kama yaliyosemwa na msemaji maarufu wa utawala wa Uingereza mwaka 1890, Cecil Rhodes, wakati mataifa ya magharibi yakihangaika kutafuta makoloni kwamba “We must find new lands from which we can easily obtain raw materials and at the same time exploit the cheap slave labour that is available from the natives of the colonies. The colonies will also provide a dumping ground for the surplus goods produced in our factories”.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, anasema “Lazima tutafute nchi mpya ambazo tutaweza kupata malighafi kirahisi na wakati huo huo tukifaidi nguvukazi ya gharama nyepesi kutoka kwa watumwa wenyeji wa nchi hizo. Makoloni pia yakuwa sehemu ya kutupia bidhaa za ziada zinazotoka katika viwanda vyetu”.
Iweje tuamini kwamba mawazo ya namna hii alikuwa nayo Cecil Rhodes peke yake? Yawezekana kabisa mentality kama hiyo bado wenzetu (wawekezaji) wengi wanayo. Kwa mfano, niliwahi kusikiliza mahojiano ya BBC na Waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani, Marehemu Robert McNamara (Mungu amrehemu) ambapo alitoa matamshi ya kuudhi, lakini yenye kuonyesha mitizamo ya baadhi ya watu wa magharibi juu ya watu masikini.
Alisema (natafsiri) “zinatakiwa dola 600 kumfanya mtoto wa nchi masikini aishi; lakini ni dola 6 tu zinatakiwa kumuua, na isitoshe hazalishi chochote. Kwa hiyo kiuchumi ni jambo la ufanisi kumuua”!
Katika utaratibu kama huu, serikali masikini kama yetu, inatakiwa kuwa makini sana na hicho kinachoitwa uwekezaji kutoka nje ya nchi.
Wakati si rahisi na si busara kuzuia wawekezaji kuleta mitaji yao, ni muhimu Serikali ikawa na mipango ya kuinua wajasriamali wa ndani ili faida ya uchumi huria ibaki hapa nchini kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi yetu.
Suala la kwamba wenyeji hawana mitaji ya kuwekeza lisitumiwe kama kisingizio cha kuwanyang’anya ardhi na kuwanyima fursa ya kufaidi matunda ya utandawazi. Lazima kuwe na sera madhubuti za uwezeshaji sio kwenye makaratasi na propaganda kama ilivyo sasa.
Ukiogopa kuvuja jasho jingi kwenye mazoezi utamwaga damu nyingi wakati wa vita
Wanajeshi wanao msemo kwamba ‘ukiogopa kumwaga jasho jingi wakati wa mazoezi utamwaga damu nyingi wakati wa vita. Sasa hivi tuko kwenye mazoezi na matayarisho ya kuingia kwenye ubepari halisi, hatunabudi kusumbua sana ubongo wetu kuweka misingi ya uchumi sawa ili kuokoa damu ya wajukuu zetu katika vita ya kutafuta usawa wa kiuchumi kwenye nchi yao yenye utajiri mwingi.
Sasa kifanyike nini?
Baada ya tafakuri niliyoifanya kwa muda sasa napenda kumaliza kwa kupendekeza njia ya kujipanga upya ili kurekebisha makosa ambayo tumekuwa tukiyafanya ili kuharakisha mapinduzi ya kijani Tanzania.
Najua wasomaji wanasubiri kusikia mapendekezo yaliyozoeleka mfano kuongeza ruzuku ya pembejeo, kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kuwezesha wakulima kupata masoko, kuimarisha usindikaji, kuongeza miundo mbinu ya usafiri, elimu kwa wakulima, matumizi ya teknolojia kama trekta na zana zingine za kilimo, kuboresha huduma za utafiti na ughani, kuwezesha wakulima kupata mikopo, n.k.
Jamani, haya si kila mmoja wetu anayajua, na yanapatikana karibu katika kila andiko la miradi ya Serikali na tafiti. Tujiulize mbona huwa hayatekelezwi au yakitekelezwa hayaleti mabadiliko yoyote ya maana, zaidi ya kunufaisha wanaofanyakazi katika miradi na tafiti hizo?
Kwa mawazo yangu, kushindwa kwa mipango mingi ya kuendeleza kilimo kunasababishwa na kukosekana kwa mfumo madhubuti wa kuibua na kuratibu mipango ya maendeleo katika sekta ya kilimo. Ukweli ni kwamba hakuna chombo makini chenye jukumu ka kutafakari vya kutosha na kuibua njia za kufuata kueleta mageuzi katika sekta ya kilimo.
Baraza la ushauri la kilimo
Kwa kuzingatia hayo napendekeza liundwe Baraza la Ushauri la Kilimo (National Agricultural Advisory Council - NAAC). Wajumbe wa baraza hilo wateuliwe bila kujali mwelekeo wao wa kisiasa au kazi zao. Wajumbe wa baraza hilo wawe ni wataalam waliobobea kwenye kilimo ambao historia ya matendo yao (track record) inaonyesha mapenzi na uwezo mkubwa wa kuchambua changamoto zinazokabili sekta ya kilimo.
Kuwa na cheo kikubwa serikalini au msomi wa masuala ya kilimo kisiwe kigezo cha kuwa mjumbe wa NAAC. Mjumbe anaweza kuwa mfanyabiashara, mkulima, mfanyakazi wa Serikali, mwanasiasa, au mtu binafsi ili mradi awe na uelewa wa kutosha na rekodi inayoweza kuthibitishwa ya uwezo wake wa kuchambua vikwazo vya sekta ya kilimo.
Usalama wa Taifa unaweza kusaidia upatikanaji wa wajumbe hao kwa mtindo ule ule ambao Mwl. Nyerere alikuwa akitumia kuwapata viongozi.
Baraza hilo lipewe jukumu la kufikiri kwa kina, kwa niaba ya Watanzania wote, changamoto mbalimbali zinazokabili kilimo na kupendekeza mipango ya kukabiliana nazo. Ikiwezekana wajumbe hao wasiwe na kazi nyingine zaidi ya kuwa visima vya fikra (think tank) za maendeleo ya sekta ya kilimo.
Hapa sipendekezi kitu kama mabaraza ya ushauri ya mikoa au wilaya (Regional and District Consultative Councils - RCC and DCC) ambazo ujumbe wa mtu hutegemea cheo cha mtu pale mkoani au wilayani.
Kuwa na cheo hakuna uhusiano wa moja kwa moja na uwezo wa kufikiri kwa kina wa mhusika; mara nyingi hutegemea uhusiano wa mteuliwa na mteuaji.
Bila kuwa na chombo kama hiki, maamuzi magumu kuhusu mwelekeo wa sekta ya kilimo yanaachwa mikononi mwa wanasiasa wakiongozwa na mapenzi yao, ambayo mengine yanaweza kuwa yameathriwa na rushwa.
Mapendekezo ya NAAC yawe yanawekwa hadharani kwa wadau mbalimbali (kwa njia itakayokuwa imependekezwa) ili kujadiliwa na kuwa na umiliki wa mpango wowote utakao tekelezwa.
Kwa njia hiyo Tanzania inaweza kuwa na mipango yake yenyewe kuliko hii ya sasa ya ‘kukata na kubandika’ kutoka kwa wengine.
Kuanzishwa kwa NAAC kwende sambamba na kuanzishwa kwa baraza dogo la mawaziri (mini cabinet) ndani ya baraza kubwa la mawaziri. Mawaziri wa mini cabinet wawe ni wale wanaoongoza wizara zinazohusiana na uzalishaji na kukua kwa uchumi.
Kwa muundo wa baraza la mawaziri la sasa wanaweza kuwa Waziri Mkuu, Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Kilimo Usalama wa Chakula na Ushirika, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Fedha na uchumi, Waziri wa Viwanda na biashara, Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Uchukuzi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, na Waziri wa Nishati na Madini.
Hawa wanaweza kuwa wanakutana kupokea mapendekezo ya NAAC kupanga utekelezaji wa mipango iliyopendekezwa na NAAC.
Lakini yatosha tu kusema pendekezo la kuundwa kwa baraza la ushauri la kilimo linaweza kuzaa matunda iwapo kutakuwepo na utashi wa kisiasa wa kweli na mawazo ya kimapinduzi, ambayo yatatupatia ujasiri wa kukiri kwamba tumethubutu tumeshindwa hivyo ni busara kujipanga upya kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadaye.
Laiti mawazo haya yangetoka kwa mgeni na hasa mwenye ngozi nyeupe naamini yangetiliwa maanani bila kujali kiwango cha elimu na uzoefu wake katika sekta ya kilimo kwenye nchi zinazoendelea. Lakini kwa vile yametoka kwa mwenyeji na mweusi ndio basi tena. Wataishia kusema ‘ametumwa’. Kama ni kutumwa, basi nimetumwa na Mungu.
Asanteni kwa kufuatilia mada hii, MUNGU IBARIKI TANZANIA
Maoni ya Wasomaji
HAKIKA WATANZANIA TUNATAKIWA
HAKIKA WATANZANIA TUNATAKIWA KUFUNGUKA SASA KWAN TUNAPELEKWA SHIMONI NA HAWA WANASIASA WETU!!! MUNGU IBARIKI TANZANIA!!!!!!!!!!
Yote uliyozungumza yana
Yote uliyozungumza yana ukweli kwa asilimia kubwa ila tatizo la watanzania ni ugumu wa kupokea ushauri hasa pale tunaposhauriwa na mtu ambaye tunaamin tumemzidi kwa vitu flan kama umri au madaraka.Nami naamini Mungu ana kusudi maalumu kutuletea watanzania zawadi kubwa ya watu kama nyinyi ambao mtasaidia kubadilisha fikra finyu tulizonazo watanzania ambazo ndizo zinatunyima maendeleo japokua tuna rasilimal za kutosha