Mahojiano
Miaka Mitano ya Mfuko wa Millenia Tanzania
John Daniel
Toleo la 231
21 Mar 2012
  • Mtendaji Mkuu asema matunda yameanza kudhihirika nchini
  • Wakati wengine wakipiga siasa, juhudi za kuunganisha kusini kwa lami yaendelea
  • Peramiho-Mbinga, Tunduma-Sumbawanga, Manyoni-Kigoma ushahidi dhahiri

MFUKO wa Millenia Tanzania (MCA-T) unaodhaminiwa na Serikali ya Marekani kwa bajeti ya dola milioni 678, kupitia mfuko wake maalumu kwa nchi zinazoendelea (MCC), umesukuma kiwango cha maendeleo nchini, kama ambavyo Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Tanzania, Bernard  Mchomvu, anavyoeleza katika mahojiano na Mwandishi Wetu JOHN DANIEL.

Raia mwema:Millenium Challenge Acount -Tanzania (MCA-T) imekuwapo nchini kwa takriban miaka kama mitano sasa, nini historia yake, chimbuko lake na Watanzania wamefaidika nayo vipi kipindi chote hicho?

Mchomvu: Kwanza nianze na historia fupi ya MCA-T. Uanzishaji wake ulitokana na juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutatua vikwazo mbalimbali vya kiuchumi kwa watu wake.

Kwa lugha rahisi naweza kusema juhudi za kushughulikia vikwazo katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kwa mtu mmoja mmoja, yaani kero za wananchi.

Kutokana na juhudi hizo, Tanzania iliiomba  Serikali ya Marekani kuunga mkono juhudi hizo kupitia Mfuko wake wa Kimatiafa ulioanziswa rasmi ili kusaidia nchi zinazoendelea, yaani Millennium Challenge Account (MCA) unaosimamiwa na Millennium Challenge Corporation (MCC).

Nchi zinazopewa fursa ya kufaidika na mfuko huu ni zile zilizoshinda vigezo muhimu vilivyowekwa na Serikali ya Marekani. Hivi ni pamoja na utawala wa sheria na demokrasia, uhuru katika biashara, uwekezaji kwenye rasilimali watu na pia nchi husika kuwa na juhudi dhahiri za kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuondoa umasikini.

Tanzania ilishinda katika vigezo muhimu vilivyowekwa na mwishoni mwaka 2006 ilikubaliwa rasmi na hivyo kutakiwa kuandaa miradi inayoendana na madhumuni ya Mfuko na katikati ya mwaka 2007, miradi ya Tanzania ilipitishwa na Bodi ya MCC na hivyo kutakiwa tuunde chombo maalumu na huru kwa ajili ya  kusimamia utekelezaji wa Miradi iliyokubaliwa na hatimaye kusainiwa na marais wetu Februari 17, mwaka 2008.

Chombo hicho kinajulikana kama Millennium Challenge Account-Tanzania na kiliundwa chini ya kifungu 36 cha Katiba ya Tanzania na uhalali wake unatokana na tangazo la Serikali (GN) namba 2002 la Septemba 21, 2007.

Maana yake ni kuwa mradi huu ni tofauti na miradi mingine ya wafadhili, miradi yote iliyokubaliwa inasimamiwa na chombo kimoja badala ya kila wizara kumegewa sehemu inayoihusu. Kwa ufupi hiyo ndiyo historia ya MCA-T.

Raia Mwema: Ni vigezo vipi muhimu vilivyozingatiwa ili nchi iweze kupata miradi hiyo chini ya MCC?

Mchomvu: Kama ambavyo nimekwisha kuligusia hili, ili nchi iweze kukubalika na kupewa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi husika, kwanza ni lazima serikali ya nchi husika iwe inaendeshwa kidemokrasia na kuzingatia utawala bora.

Pili ni lazima serikali ya nchi husika iwe inaonesha nia ya dhati na ya wazi katika kuwaendeleza watu wake kiuchumi (kuzingatia suala la rasilimali watu na kupewa kipaumbele).

Tatu ni lazima nchi husika iwe imefungua milango ya kibiashara na kuweka mazingira bora ya kuendesha shughuli za uzalishaji mali ikiwemo uwekezaji. Kwa bahati, Serikali yetu ilifanikiwa kukidhi vigezo vyote hivyo muhimu na hivyo kuingizwa rasmi kwenye mradi huu muhimu.

Nieleze pia kuwa vigezo hivi vitatu vinajumuisha viashiria vipatavyo 17 hadi 18 na hupitiwa kila mwaka kuainisha kama bado nchi ni inastahili.

Pia napenda tuelewe kuwa zipo nchi nyingi kadhaa duniani zilizoomba na kukataliwa kutokana na kushindwa kukidhi vigezo hivyo muhimu.

Raia Mwema: Umesema sisi kama taifa tulikidhi vigezo hivyo muhimu, unaweza kunitajia angalau mfano mmoja wa mkakati wa Serikali kuwezesha watu wake kiuchumi?

Mchomvu: Msingi mkuu kwa Tanzania katika hili la kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu ni MKUKUTA (Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza uchumi Tanzania) na MKUZA (Mkakati wa Kukuza uchumi Zanzibar).

Tunayo pia mipango ya utekelezaji kama vile TASAF (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii). Pia Serikali imetumia nguvu nyingi kupambana na rushwa. Rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla. Huyo ni mifano michache tu.

Raia Mwema: Licha ya Tanzania kukidhi vigezo vilivyowekwa ili kupata fedha za miradi chini ya MCA-T, kama taifa tulitumia njia ipi kupata miradi husika hasa kwa kuzingatia kuwa tuna mahitaji mengi kutokana na uchumi wetu kuwa duni?

Mchomvu: Kwanza tuliangalia vipaumbele vyetu kama taifa, lakini pia tuliangalia maeneo yanayohitaji kuangaliwa kwa haraka zaidi hususan maeneo ambayo yanaonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuendelea kutokana na rasilimali zilizopo, lakini yalikuwa yanakabiliwa na vikwazo vingi na hivyo kuendelea kuwa nyuma kimaendeleo. Mikoa ya kusini na mingine ya pembezoni kama vile Kigoma ni mifano hai.

Hivyo, ili kupata maeneo hayo ya kupewa kipaumbele tulirejea kwenye mpango wetu wa maendeleo kama taifa. Kisha kwa kushirikisha wataalamu mbalimbali zoezi la kuandaa miradi lilianza.

Lakini kwa ushirikiano wa karibu na wataalamu wa Marekani, ilibidi kujiridhisha kuwa miradi yote inakidhi vigezo vya muhimu vya kiuchumi kama vile mrejesho wake katika kiuchumi (economic rate of return- ERR) usiopungua asilimia 13.

Kuhusu miradi yetu nataka niweke wazi kuwa tulikuwa na miradi mingi sana katika maeneo ya usafirishaji, maji, kilimo na umeme. Kwa maana hii hata fedha tulizoomba awali zilikuwa ni mara nne ya tulizopata na hivyo hatukuweza kupewa yote yale tuliyotaka.

Kama ambavyo nimekwisha kueleza MCA-T  ilianzishwa kama sharti muhimu na kupewa msaada huu.

Uanzishwaji wa MCA-T umesaidia sana nchi kutekeleza miradi iliyokubaliwa kwa urahisi na kwa wakati, ukilinganisha na wakati kila wizara ilipofanya kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya miradi yake.

Ni vema nikaeleza kuwa wakati wa kuandaa miradi nilikuwa Mratibu (Coordinator) na baada ya kuanzishwa kwa MCA-T ndipo nikateuliwa kama Mtendaji Mkuu ( CEO) tangu Septemba 2007.

Mwanzoni, shughuli za maandalizi ya miradi ilikuwa inaongozwa na kamati maalumu iliyojumuisha wizara za maji, kilimo, miundombinu, nishati, tawala za mikoa na serikali za mitaa, mambo ya nje, mipango, TCCIA, TANGO na wengine chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Hatimaye miradi yetu ilipata baraka za Baraza la Mawaziri na kisha kuwasilishwa kwa Serikali ya Marekani.

Raia Mwema: Hadi sasa ni miradi ipi inayothibitisha mafanikio ya MCA-T?

Mchomvu: Kwa ujumla, miradi yote inakwenda vizuri lakini mingine iko nyuma kulingana na ni lini mjenzi alipatikana. Hata ile ambayo inayoonekana kuwa nyuma, sisi hatuna shaka, tunaamini kuwa itamalizika ndani ya muda tuliopewa.

Hivyo, katika kujibu swali lako ninachoweza kusema tu ni kuwa miradi yote ni mafanikio kwa MCA-T ila kwa hapa nitaelezea tu kuhusu miradi michache tu.

Miradi ya barabara

Tulipokuwa tunaendelea na uchambuzi wa kina wa miradi ya kuombewa fedha kama kamati tulijiridhisha kuwa bila mawasiliano ya barabara, haujamwezesha mwananchi hususan mkulima kusafirisha mazao yake na kupata bei nzuri, pia shughuli nyingi za kiuchumi katika nchi yetu zinategemea sana mawasiliano ya barabara.

Tulizingatia ukweli kwamba bila mawasiliano thabiti ya barabara hakuna maendeleo, kwa lugha nyingine ni kwamba barabara mbovu ni kikwazo kwa maendeleo.

Tulizingatia kwa undani zaidi kwamba wajibu wa Serikali ni kuwawezesha wananchi wake ili kuzalisha kwa urahisi na kwamba hata wawekezaji wanapenda maeneo yenye barabara za uhakika.

Nishati ya umeme

Mradi wa pili muhimu ni umeme, tulijiridhisha kwamba bila umeme hakuna huduma bora za afya kwa maana kwamba upasuaji, vipimo na hata utunzaji wa baadhi ya dawa huhitaji sana umeme kwa kila hatua.

Pia viwanda vinahitaji umeme ili kuendeshwa na kuzalisha mali na inapokosekana nishati hiyo uzalishaji unakuwa ghali hivyo kuwakatisha tamaa wawekezaji huku wananchi pia wakipata adha ya kupanda kwa gharama za maisha.

Huduma ya maji

MCA-Tanzania tuliangalia kwa undani pia umuhimu wa maji katika maisha ya kila binadamu na tukakubaliana kwamba tushughulikie pia eneo hilo kwa kudhamini baadhi ya miradi.

Viwanja vya ndege

Eneo hili pia tuliangalia kwa makini hasa kwa lengo la kuinua sekta ya utalii, na tulianzia na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mafia, eneo ambalo kulikuwa na tatizo kubwa la mawasiliano ya anga huku kukiwa na utajiri mkubwa wa mali asili.

Hadi sasa ujenzi wa kiwanja hicho uko katika maandalizi ya kupeleka zana na watu, lakini ifikapo Agosti, mwaka huu, tunaamini kuwa kazi ya kuweka lami  itaanza. Hii sio tu itapanua shughuli za utalii Mafia bali utakuwa ni ukombozi kwa wananchi wa Mafia.

Kwa ujumla miradi ya MCA-Tanzania inajikita katika ujenzi wa barabara, nishati ya umeme, maji na viwanja vya ndege. Maeneo hayo manne ndio yenye mahitaji makubwa na ambayo yamekuwa kikwazo kikubwa kwa  mafanikioya kila Mtanzania.

Raia mwema: Miradi yenu ya barabara inahusisha maeneo gani?

Mchomvu: Kwanza tulitoa kipaumbele kwa maeneo yaliyoonekana kuwa nyuma katika sekta ya mawasiliano ya barabara huku wakiwa ni wazalishaji wazuri katika shughuli za kiuchumi na kwa kuzingatia hilo, tulibuni ujenzi wa barabara ya Namtumbo hadi Songea yenye urefu wa kilomita 65.

Tunao pia mradi wa Peramiho –Mbinga wenye kilomita 78 na ambao utakamilika Februari mwaka 2013, mradi mwingine mkubwa  wa barabara ni Tunduma -Sumbawanga wenye urefu wa kilomita  224, kwa gharama ya zaidi doa za Marekani milioni nne, eneo ambalo lilikuwa korofi na kikwazo kikubwa kwa maendeleo yetu kama taifa katika ukanda huo wa kusini hususan wakulima.

Raia Mwema: Vipi miradi ya barabara kwa upande wa Zanzibar?

Mchomvu: MCA-Tanzania haijajikita upande mmoja tu wa Muungano kwani tunao mradi wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 35 kule Pemba.

Kinachonifurahisha ni kwamba wakati tunaanza utekelezaji wa miradi ya barabara Namtumbo- Songea, mbunge wa pale hakuamini kama kweli tutafanikisha mradi huo muhimu kwa wananchi wa eneo hilo.

Ieleweke kuwa Tanzania tuliomba ujenzi wa barabara ya Dodoma- Manyoni -Kigoma, Bagamoyo –Tanga hadi Dodoma –Arusha - Serengeti- Mugumu.

Raia Mwema: Vipi kwa upande wa viwanja vya ndege?

Mchomvu: Tuliomba miradi mingi ya ujenzi wa viwanja vya ndege kama vile Kigoma, Musoma, Tabora na Mafia, lakini tulifanikiwa tu Mafia.

Raia Mwema: Miradi ya umeme mmefikia wapi na katika mikoa ipi?

Mchomvu: Kwa upande wa miradi ya umeme pia tumepiga hatua kubwa kwa kujenga miundombinu ya kusambaza umeme katika mikoa saba nchini yaani Tanga, Iringa, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Morogoro na Kigoma. Tunajenga pia vituo 24 vya kuimarisha usambazaji wa umeme (substations).

Kusema kweli tumefanikiwa sana japo kama tunavyojua nchi yetu ni kubwa hivyo si rahisi kufikia lengo kwa muda mfupi lakini wale tuliowafikia wamefurahi na kuona kwa macho yao mafanikio ya MCA-Tanzania.

Raia Mwema: Kwa upande wa maji mafanikio vipi?

Mchomvu: Kama nilivyosema awali, tulikubaliana kwamba bila maji hakuna uhai, tumeanza na mpango wa kupunguza uhaba wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuongeza upatikanaji wake kutoka mita za ujazo 100 hadi 270, tayari tumemaliza ujenzi wa mradi pale Bagamoyo.

Hivi sasa tuko katika hatua ya pili ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kusafirisha maji kuingia Dar es Salaam. Kwa upande wa Morogoro, tunajenga matenki mapya kuanzia milimani hadi kwa wananchi.

Raia Mwema: Ni lini miradi hiyo yote mikubwa ya MCA-T itakamilika na wananchi kuanza kufaidi matunda ya MCA-Tanzania?

Mchomvu: Miradi yote hii tunatarajia ikamilike kabla ya Septemba mwaka 2013 na sehemu kubwa itakamilika Agosti, mwaka huu.

Raia Mwema: Pamoja na hatua mliyofikia ni changamoto zipi zinazowakabili katika shughuli zenu za kila siku?

Mchomvu: Zipo changamoto kubwa zinazotukabili hususan masuala ya usalama kule mikoa ya kusini, baadhi ya makandarasi wanatekwa nyara wakiwa njiani.

Wizi wa vifaa, kama mafuta ni changamoto kubwa kwani makandarasi wanalalamikia tabia hiyo kwa watu mbalimbali, ambapo jirani na kambi zao kuna vituo bubu vya kuuza mafuta ya wizi.

Ukosefu wa huduma muhimu kwa makandarasi ikiwemo hoteli kubwa za kisasa, mfano mtaalamu anatoka kwao katika mazingira mazuri akijua na huku atapata hoteli kubwa za kisasa karibu na maeneo yao ya kazi lakini wanakuta hali tofauti, hivyo kuwalazimu kuishi umbali mrefu na eneo la kazi.

Pia suala la malipo ya fidia kwa wananchi waliovamia hifadhi ya barabara ni changamoto kubwa kwetu.

Wapo baadhi yao wanaoelewa hususan mikoa ya kaskazini ambao wananchi wenyewe wanachangamka kuondoa mali zao ili kupisha mkandarasi, lakini hali ni tofauti sana maeneo mengine ambapo wananchi wakisikia kupisha ujenzi wa barabara wanaona kama ndilo eneo la wao kutajirikia.

Raia mwema: Vipi kuhusu michango ya Serikali kuhusu miradi hiyo?

Mchomvu: Kwanza miradi hii inagharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 698 na Serikali yetu haikuwa nyuma kuunga mkono msaada huo na tayari imetoa Sh. bilioni 20 kati ya 100, kwa upande wa barabara kuonesha ushiriki wake wa moja kwa moja.

Lakini pia Serikali imekuwa mstari wa mbele kwa kutoa misaada ya aina mbalimbali ikiwemo mazingira bora ya kutuwezesha kufanya kazi na mawasiliano kati yetu na Serikali ya Marekani kufanikisha miradi kwa kila hatua.

Raia Mwema: Nini matarajio yenu?

Mchomvu: Kama nilivyoeleza awali, mwisho wa miradi hii ni Septemba mwaka 2013 tunatarajia kufunga virago labda yatokee mabadiliko mengine.

Matarajio yetu ni kufanikisha miradi yote kwa wakati na katika ubora unaotakiwa kwa maslahi ya taifa letu.

Kikubwa ni kwamba ikifika wati huo iwapo mradi wowote utakuwa haujatelekezwa, itabidi fedha zote zirudishwe hivyo nawashauri Watanzania wote tushirikiane kuhakikisha kila kinachoitwa mradi a MCA-Tanzaia, unatekelezwa kwa wakati.

 

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako