Michezo
Mipasho inaposhindwa kuipasha jamii masuala muhimu…
Chesi Mpilipili
Toleo la 050
8 Oct 2008

MWAKA 1975 mwimbaji mashuhuri wa taarabu kutoka mjini Tanga, Shakila Saidi, akiwa na kundi la Lucky Star, aliimba wimbo wa kisiasa katika mahadhi ya taarabu uliotokea kupendwa mno nchini na hata nchi za jirani; 'Viva Frelimo'.

Shakila na Lucky Star walitunga na kuuimba wimbo huo kama mchango wao katika kusherehekea nchi ya Msumbiji kupata uhuru wake tarehe 25 Juni mwaka huo wa 1975.

Wapenzi wa nguli huyu wa muziki wa taarabu wanakubaliana kuwa 'Viva Frelimo' ni miongoni mwa nyimbo ambazo mwimbaji huyo alidhihirisha kipaji na uwezo mkubwa alionao wa kupanga sauti yake alivyopenda, kama anavyoimba katika moja ya beti za wimbo huo:

Leo twakuvika taji mpendwa ndugu Samora,
 Kukomboa Msumbiji si jambo la masikhara,
 Na mreno kafa maji hivi sasa kadorora,
 Viva Frelimo, Viva Samora, Viva Msumbiji,

Katika kipindi hiki ambacho kulikuwa na nyimbo nyingi za mapenzi za taarabu zilizokuwa zikitamba kama 'Kifo cha Mahaba', 'Pete', 'Macho yanacheka Moyo unalia', 'Subalkheri Mpenzi' na kadhalika, usingetegemea wimbo wa 'kisiasa', tena kushangilia uhuru wa nchi jirani, ushike chati miongoni mwa wapenzi wa taarabu nchini.

Lakini ndivyo ilivyokuwa. 'Viva Frelimo' ukawa ni mmoja kati ya nyimbo za taarabu zilizotokea kupendwa sana nchini. Kwa hakika, iwapo sekta yetu ya muziki ingekuwa imeendelea, huu ungeweza kuwa mmoja kati ya zile nyimbo zinazoweza kumpa utajiri mkubwa msanii husika, lakini ndio hivyo tena.

Sio vibaya pia tukadokeza hapa kuwa ni huko huko Tanga na mwaka huo huo wa 1975 ambapo pia kulitoka wimbo bora wa muziki wa dansi kushangilia uhuru wa Msumbiji. Huu ni wimbo wa 'Viva Frelimo' uliopigwa na bendi ya Jamhuri Jazz Band - 'Wanyama Wakali'.

Kama ule 'Viva Samora' wa dada yao Shakila, wimbo wa 'Viva Samora' wa bendi ya Jamhuri Jazz nao ulitokea kupendwa mno kutokana na ubunifu waliofanya wanamuziki hao kwenye korasi ya wimbo huo ambapo kulikuwa na kipande cha dakika tatu hivi ambapo mpiga tumba wa bendi hiyo alipewa nafasi ya kuonyesha umahiri wake wa kupiga tumba hizo katika mapigo ya ngoma ya maarufu ya Wamakonde - Sindimba.

Tukirudi katika taarabu, kulikuwa na nyimbo nyingine za 'kisiasa' ambazo pia zilisisimua kwenye miaka hiyo ya mwanzoni ya 70 na kurudi nyuma.

Wimbo kama 'Wakuu wa Mapinduzi'  uliokuwa unawasifia na kuwaombea dua njema viongozi wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, kwa mfano, uliopigwa na kikundi cha Mila na Utamaduni cha Zanzibar ambacho kilikuwa kikijulikana kama 'Timu ya Taifa' huko Zanzibar kutokana na kukusanya wapigaji wengi mahiri wa taarabu kisiwani humo.

Ulikuwepo pia wimbo wa taarabu uliokuwa unahimiza kilimo ambao ulipigwa na kundi la Egyptian la mjini Dar es Salaam ulioitwa 'Bwana Waziri Kasema' ambapo ndani yake una maneno ya kuwahimiza wananchi kuhusu kilimo;

‘Shambani, shambani mazao bora shambani,
 Bwana Waziri kasema, mazao bora shambani,
 Tusikae mitaani, wanawake kwa waume,
 Haya wananchi shime, mazao bora shambani',

Kimsingi, tofauti na ambavyo wengi wanaweza kusukumwa kudhani kutokana na hali ilivyo sasa hivi, taarabu ya siku za nyuma haikuwa kuhusu mafumbo kati ya wapendanao tu; bali ilijumlisha nyanja zote zinazoizunguka jamii yetu, ikiwemo siasa.

Kwa bahati mbaya, kama ambavyo imekwisha semwa mara nyingi huko nyuma, taarabu imehamishwa kutoka kuwa muziki wa kistaarabu, mapenzi na wa kusikiliza zaidi kuliko kucheza hadi kuwa muziki wa kupigana vijembe, kutambiana, kusutana miongoni mwa akina mama na kucheza zaidi kuliko kusikiliza. Na huko kucheza kwenyewe, basi!

Kwa kutumia kisingizio cha kwenda na wakati na kujali kile mteja anachotaka, muziki wa taarabu umeondolewa kwenye kuwa wa mafumbo ya kiutu uzima ambapo ilibidi mtu aumize kichwa ili kufahamu ujumbe ulio kwenye wimbo husika na kuwa muziki wa 'kusemeana ovyo'.

Katika yote haya, watunzi na waimbaji wa taarabu ya kisasa wameshindwa kutumia umaarufu wa muziki wao miongoni mwa wanajamii wanaoupenda ili kufikisha ujumbe kuhusu masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa yanayotokea nchini na ulimwenguni kwa ujumla.

Kama vile nguli Shakila Saidi alivyoimba 'siasa' kushangilia uhuru wa Msumbiji mwaka 1975, tungetegemea angalau mabingwa wetu wa mipasho watupashe na kutuelimisha juu ya faida ama hasara za siasa za vyama vingi vya siasa kwa mwananchi wa kawaida.

Wakati kundi la sanaa la TOT linalomilikiwa na chama tawala, CCM, lilipoanzishwa zaidi ya miaka kumi na tano iliyopita, pamoja na kuwa na kitengo cha kwaya ambacho kazi yake ni kuimba nyimbo za kukipamba chama na viongozi wake, tulitegemea kitengo cha taarabu cha kundi hilo pia nacho kingekuwa kikiimba nyimbo angalau za kutangaza sera za chama hicho.

Tulitegemea angalau kusikia kutoka kwao aina mpya ya nyimbo za 'Mazao bora shambani' na 'Wakuu wa Mapinduzi dua tunawaombea' zikipigwa katika mtindo mpya wa taarabu ya kisasa. Haikutokea.

Badala yake kundi hilo mashuhuri nalo likajiingiza katika mtego wa kuimba taarabu ya kisasa ya kupigana vijembe na 'madongo' ukiacha nyimbo chache zenye maudhui ya 'kijamii' kama ule wa kumkumbuka hayati Maneti wa Profesa Mrisho na ule wa 'Stahimili' wa Othman Sudi.

Kwa hakika, inashangaza na kuhuzunisha kuona kundi la taarabu lenye wapenzi wengi linaweza likaingiza sokoni albamu mpya yenye nyimbo nane, zote zikiwa kwenye maudhui ya 'Unikome', 'Hakutaki', 'Utajiju', 'Yatakushinda', 'Unalo hilo' na kadhalika bila kuweka angalau wimbo mmoja tu wenye ujumbe wa maana kwa jamii katika kipindi husika.

Haiingii akilini kwa mfano, kwa wapenzi wa taarabu 1,000 kuingia kwenye onyesho la kundi la muziki wa taarabu wakaburudika na taarabu lakini wakatoka bila ujumbe wowote wa maana zaidi ya kusikiliza na kushagilia vijembe vya 'Buzi hakutaki ameni-mind mimi'!

Kama wana mipasho wetu wanakwenda na wakati kweli kama wanavyodai, basi, wanapaswa kufahamu kuwa tungependa kuwaona angalau mara moja moja wakiungana nasi katika kukemea maovu yanayoikabili jamii yetu.

Wanapaswa kufahamu kuwa tutafurahi kuwasikia wakijiunga nasi kwa kurekodi ama kusimama jukwaani na kuwapasha wale 'Paka Mapepe' wanaowatia mimba watoto wetu wa shule na hivyo kuwakatisha masomo yao.

Kwa hakika, furaha yetu itakuwa haina kifani siku tutakapomsikia na kumuona Al-anisa Khadija Omar Kopa akipanda jukwaani na kucheza huku 'akiwapasha' wale 'Vimburu Matari' wote wanaondeleza ukeketaji wa mabinti wadogo, huku sisi wengine tukiinua vidole juu kuunga mkono!

Tutafurahi pia kucheza miondoko ya taarabu ya kisasa iwapo bingwa Mzee Yusuf yupo jukwaani 'akiwachoma msumari kote kote' wale wote wanaowaua ndugu zetu maalbino kwa imani ya kijinga ya kupata utajiri wa haraka haraka badala ya kufanya kazi kwa bidii.

Ma-nguli wetu wa taarabu ya kisasa wanaweza pia kuungana nasi na kuelekeza makombora ya mipasho yao kwa mafisadi badala ya kuendelea kushambuliana wao wenyewe kwa wenyewe kila siku.

Watakapo fanya hivyo, hata sisi wengine ambao bado hatujaikubali sana taarabu ya kisasa, si tu tutajilazimisha kuipenda bali pia hata kuingia ukumbini na kuicheza; huku tukiinua vidole juu kama ishara ya kuiunga mkono!

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Chesi Mpilipili
chesimpilipili@gmail.com

Toa maoni yako