Mizungu ya kisiasa: Leo rafiki, kesho adui

WIKI iliyopita, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alikuwa mgeni wetu kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu. Kwa sasa, si siri tena kwamba anapita katika kipindi kigumu cha urais wake kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili yeye binafsi.

Kwa bahati nzuri, amekuja nchini wakati ndiyo kwanza nimetoka kumaliza kusoma kitabu cha Thabo Mbeki I Know  kilichoandikwa na watu waliowahi kufanya kazi na Mbeki kwa nyakati mbalimbali na kila mmoja kueleza namna alivyomfahamu.

Kuna somo moja la kujiruadia kwenye kitabu hicho; kwamba Zuma na Mbeki walikuwa ni maswahiba wakubwa kwa muda mrefu. Kama kuna watu walikuwa wakijulikana kwa urafiki wao, basi Zuma na Mbeki walikuwa ni mfano.

Hili limeelezwa na wengi ndani ya kitabu hicho; kuanzia Esop na kaka yake Aziz Pahad, mchungaji Frank Chikane, Welile Nhlapo na wengineo. Ni hadithi ya marafiki kabla ya madaraka.

Hivi sasa Mbeki na Zuma wanasalimiana na kuchekeana kinafiki tu. Kila mmoja ana yake ya moyoni kuhusu mwenzake. Thabo anaamini kwamba bila figisufigisu za rafikiye huyo angemaliza urais wake kwa heshima huku Rais huyo wa sasa wa Afrika Kusini akiamini Mbeki alitaka yeye asije kupata nafasi hiyo.

Stori hii ya Zuma na Mbeki inanikumbusha kuhusu hadithi nyingine kati ya Blaise Compaore na Thomas Sankara wa nchi ya Burkina Faso. Hawa walikuwa maswahiba wakubwa kama ilivyokuwa kwa Zuma na Mbeki.

Urafiki huu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba inadaiwa Sankara, aliyekuwa Rais wa Burkina Fasso na kipenzi cha watu wake, aliwakatalia wote waliokuwa wakimwambia kwamba Compaore ana mpango wa kumpindua.

Baadaye, Compaore akaja kumpindua Sankara na kumuua kabisa. Kumbuka, wawili hawa ni watu waliokuwa marafiki kiasi kwamba hata wazazi wao walimuona kila mmoja wao kama mtoto wake wa kumzaa mwenyewe.

Hapa kwetu kuna mfano wa Jakaya Kikwete na Edward Lowassa. Miaka 20 iliyopita, walipachikwa jina la Boyz II Men wakifananishwa na maswahiba waliokuwa wanaunda kundi maarufu la muziki nchini Marekani lililokuwa na jina hilo.

Kimsingi, urafiki wa Kikwete na Lowassa unaweza kuwa na historia ya zaidi ya miaka 30. Hata hivyo, wakati naandika makala hii, watu hawa wawili hawana uhusiano mzuri kama ilivyokuwa huko nyuma.

Matatizo yalianza mara tu baada ya Kikwete kuwa Rais wa Tanzania. Kama yalivyoanza baada ya Thabo na Sankara kuwa marais katika nchi zao.

Kizza Besigye alikuwa daktari binafsi wa Yoweri Museveni wakati wakiwa msituni kama waasi waliotaka kupindua serikali. Kwenye miaka ya kwanza ya urais wa Museveni, familia zao zilikuwa na uhusiano wa karibu.

Wakati naandika makala hii, Yoweri Museveni na Dk. Besigye ni kama paka na panya. Uhasama umefikia kiwango kibaya kiasi kwamba toleo jipya la kitabu cha Rais huyo wa Uganda, Sowing the Mustard Seed, kimeondoa kabisa mambo mazuri aliyoyafanya Kizza wakati wakiwa msituni.

Wapinzani wa Fidel Castro wa Cuba watakwambia wana wasiwasi kama kifo chenye utata cha Camilo Cienfuegos siku chache baada ya mapinduzi hakikuwa na mkono wa El Commandante.

Kwanini hili hutokea? Kuna misemo miwili ambayo naweza kuitumia kueleza hili. Moja ni nukuu maarufu ya William Shakespeare, kwamba madaraka hulevya. Pili ni nukuu nyingine ya Mmarekani, Henry Adams, aliyeandika miaka mingi iliyopita kwamba rafiki aliyepata madaraka ni rafiki uliyempoteza.

Aliye madarakani, kwa sababu ya madaraka aliyoanza kuyapata, huanza kuona watu wenye sifa kama zake kuwa ni kikwazo kwake. Huhofia kwamba wanaweza nao kutamani madaraka na kumpoka nafasi hiyo.

Na wale walio chini ya aliyepata madaraka ya juu, nao huanza kuwa na mawazo ya kusema “kama nimepata hivi tu faida ni kubwa kiasi hiki, vipi kama nikipata madaraka makubwa zaidi?”

Lakini nimewahi kuzungumza na mmoja wa viongozi wastaafu wa vyombo vya dola hapa nchini aliyeniambia wazi kuwa wakati mwingine ugomvi wa marafiki hutengenezwa na vyombo hivyo.

Hili hufanyika kwa sababu kuna wakati kiongozi hujikuta akimsikiliza zaidi swahiba wake kuliko anavyovisikiliza vyombo vilivyowekwa kikatiba kumshauri. Kwa sababu ya urafiki wao, kiongozi anaweza kujikuta ana deni la kumsikiliza mtu anayemfahamu na kumwamini badala ya vyombo.

Hivyo, wakati mwingine, kinachofanyika ni kuwagombanisha tu wakubwa. Wanagombanishwa, iwe kwa ya kweli au ya kutungwa, ili mradi tu wagombane na wasipatane tena.

Kwenye kugombanishwa huko kuna matatu yanaweza kutokea; ama mmoja kuondolewa kabisa duniani, kuondolewa na kuwekwa nje ya duara la ushawishi au kunyamazishwa kwa namna yoyote ile.

Kwa mujibu wa mstaafu huyo, kazi hiyo ya kuchonganisha wakubwa pia ni sehemu ya wajibu wa vyombo hivyo kote duniani. Hilo linafanyika kwa maslahi mapana ya taifa.

Hivyo, kama rafikiyo kapata madaraka leo, usifurahi mpaka jino la mwisho maana kukikucha unaweza kujikuta kuwa mhanga wa kwanza wa mafanikio yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *