Mjadala wa demokrasia haukwepeki, mizengwe ya ‘kiserikali’ haina nafasi

MEI 13, mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilikuwa kimeandaa Kongamano la Demokrasia na Siasa za Ushindani. Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha wadau wa demokrasia ili kujadili, pamoja na mambo mengine, maendeleo na utekelezaji wa demokrasia nchini.

Kwa mujibu wa waandaaji, kongamano hilo lilipangwa kuwashirikisha wawakilishi kutoka vyama vyote vya siasa nchini, wanazuoni, wanasheria, wachumi, wanahabari, taasisi za kiraia na kijamii.  

Waandaaji wa kongamano hilo wanaeleza kwamba majadiliano yalitarajiwa kuegemea zaidi kuhusu dhana na historia ya demokrasia nchini, Katiba ya Jamhuri ya Muungano na demokrasia, demokrasia ya vyama vingi vya siasa, demokrasia na uhuru na haki za raia, demokrasia na uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari, majukumu ya vyombo vya kutoa ulinzi na haki kwa raia katika mazingira ya demokrasia ya sasa hapa nchini, na uhuru wa kufanya siasa za ushindani katika mazingira ya sasa ya demokrasia nchini.

Kinyume cha matarajio ya waandaaji na wadau wengine wa demokrasia nchini, kongamano hilo liliahirishwa dakika za mwisho kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni uamuzi wa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam inadaiwa kuzuia ukumbi wa Arnatouglou uliopangwa kutumika kwa ajili ya kongamano hilo kwa kuwa ukumbi huo, ghafla, ulipangwa kutumika kwa ajili ya shughuli nyingine za serikali hiyo. Zuio hilo linatajwa kuwa la ghafla kwa kuwa, awali, tayari mamlaka husika zilikwishakutoa kibali ili kongamano hilo lifanyike katika ukumbi huo na waandaaji walikwishakukagua ukumbi husika kwa ajili ya matumizi.

Kumekuwa na madai kwamba, zuio hilo la ghafla ni sehemu ya mkakati wa makusudi wa baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuvuruga kongamano hilo. Kwa upande wetu, Raia Mwema, tunaamini kwamba uamuzi wa kuzuia, ghafla, matumizi ya ukumbi huo kwa ajili ya kongamano hilo haukuwa wa busara na hata wale wanaotafsiri kuwa ni uamuzi wenye hujuma dhidi kongamano hilo wanaweza kuwa na sababu za msingi za kuamini hivyo, kwa kuwa, kama mamlaka zilikwishatoa kibali ni kwa nini shughuli hiyo ya ghafla ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Saalam isipangwe katika ukumbi mwingine?

Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ingeweza kupanga ‘kikao’ chake hicho cha ‘ghafla’ katika kumbi nyingine kwa kuheshimu ruhusa iliyotolewa kwa Watanzania wengine kutumia ukumbi huo ambao ni mali ya umma. Kimsingi, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam itambue kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi kubwa, ambazo zinailazimu kutumia muda wake kwa umakini zaidi kutatua changamoto ama kero hizo kuliko kuzuia makongamano ya namna hii.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja Jiji la Dar es Salaam kuendelea kuwa chafu, wafanyabiashara wadogo – maarufu kama wamachinga kutokuwa na uhakika wa maeneo ya kuendeshea biashara zao na miundombinu kama barabara kuwa katika ubora wa kiwango cha chini, nyingi zikiwa na mashimo, na wakati wa mvua zikigeuka mifereji ya maji. Hivyo basi, katika kuchagua matumizi sahihi ya muda na maarifa, tunadhani ni busara serikali hiyo ikatumia muda wake kukabili changamoto hizo kuliko kutumia muda huo kutafakari, kuamua na kutekeleza namna ya kuzuia makongamano ya wananchi. Akili ni nywele, kila mtu ana zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *