- Kiongozi wa Machinga awatolea uvivu
- Asema wanakiua chama kiwapacho kula
MKAKATI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza kuwatumia vijana wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga kurejesha haiba ya chama hicho miongoni mwa vijana umeingia shubiri baada ya vijana hao kuamua kuwapasha viongozi hao jinsi wanavyokibomoa chama chao.
Mpango huo ambao ulihusisha mafunzo ya ujasiriamali kwa wamachinga wapatao 100 yaliyochukua muda wa siku sita, ulikuwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa kwa wamachinga hao wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM katika sherehe zilizofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Katika maadhimisho hayo Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, baada ya vijana hao kusoma risala ya kuonyesha ni jinsi gani sasa wamejitambua na hawatayumbishwa tena na wapinzani, aliahidi kuwapatia vijana hao kiasi cha shilingi milioni 10 ili ziwasaidie katika kuendeleza biashara zao wakiwa katika umoja wao, ambao siku hiyo walitangaza kujiunga na chama hicho na kusema wametambua makosa waliyokuwa wakifanya huko nyuma.
Katika risala yao hiyo ambayo taarifa zilizopatikana zilisema kwa kiasi kikubwa ilikuwa imeandaliwa na wataalam wa propaganda wa CCM, ilieleza kuwa wamachinga wa Mwanza wamegundua kuwa hata wanaowaahidi kuwaletea ukombozi kiuchumi hata wao wanakwenda kuomba kwa Rais Ikulu na kunywa chai na juisi, kwa hiyo wao wameamua kuomba moja kwa moja bila kupitia mtu wa tatu.
Risala hiyo ilitolewa baada ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete kumweleza msimamo wao kuhusu mswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba uliokuwa umepitishwa na Bunge.
Hata hivyo, baada ya kauli hiyo katika maadhimisho hayo, ulitokea mvutano miongoni mwa umoja wa wamachinga hao ambao waliwakana wenzao waliokwenda kusoma risala hiyo mbele ya Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Katika kutekeleza ahadi hiyo ya Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa vijana hao, CCM Mkoa iliratibu mafunzo hayo ya ujasiriamali ambayo yalifikia kilele mwishoni mwa mwezi Mei na yalihitimishwa na hafla fupi iliyofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba ambako pia uogozi wa chama hicho Mkoa ulikabidhi shilingi milioni 10 kama iliyokuwa imeahidiwa na Rais Kikwete.
Ilikuwa ni katika hafla hiyo ambapo Mwenyekiti wa Muungano wa wamachinga Liberatus Kabaila alipoamua kuwatolea uvivu viongozi wa CCM waliohudhuria shughuli hiyo wakiwamo wa kamati ya siasa ya mkoa wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa Clement Mabina na Katibu wa chama hicho Mkoa Joyce Masunga.
Alipopewa nafasi ya kutoa neno la shukrani Kabaila alianza kwa kuwaonya viongozi wa siasa kuacha kuwatumia wamachinga kwa manufaa yao halafu wanawatelekeza, akitoa mfano wa umuhimu wa karai katika ujenzi wa nyumba ya gharofa kuwa, huwa linahitajika sana wakati wa ujenzi lakini baada ya nyumba kukamilika linaonekana uchafu na halitakiwi tena kuonekana katika nyumba lililosadia kuijenga.
Baada ya hapo aliwageukia viongozi wa CCM na kuwataka waache unafiki kwa kuwa wao ndio chanzo cha hali mbaya ya chama sasa hivi. Aliwaonya kuwa kama wanadhani hawawezi kutimiza majukumu yao ni bora waachie ngazi ili wakisadie chama.
“Wana CCM tuache unafiki, ambaye anaona hawezi kujisimamia kwa mujibu wa maadili ya chama ajiondoe mwenyewe, ubovu wa CCM uko mikononi mwenu kwa sababu mmeshindwa kujisimamia, anayezamisha meli yenu ni ninyi wenyewe mnaoongoza meli hii,” alisema.
Alisema bila viongozi hao kuwa na mikakati ya maana katika kuamua kuokoa chama hicho, wasije kutafuta mchawi kwa sababu kama chama hicho kitapoteza hadhi yake mbele ya jamii wao watakuwa wanahusika moja kwa moja, akasisitiza kuwa wanachama wa kawaida hawana shida lakini tatizo la msingi ni viongozi ambao wanakwamisha juhudi za wanachama kuimarisha chama.
“Sisi tunatengeneza halafu ninyi mnaharibu, kwa nini ule kwa raha halafu ujitie kidole utapike, mmefaidika na CCM, mnasomesha watoto wenu na mnapata heshima kwa ajili ya CCM, mnaishi kwa raha kwa ajili ya CCM, mbona sasa mnaisaliti,” aliwahoji viongozi hao wao wakiwa wametulia kimya vitini mwao, wakiwa hawaamini kama shughuli ile ingegeuka kuwa shubiri kwao.
Aliongeza kuwa unafiki na kutoaminiana miongoni mwao ndiko kunakokifanya chama hicho kutotekeleza majukumu yake ya msingi na badala yake viongozi wanakaa kujadili mambo ya majungu huku chama kinaumia.
Akaenda mbali zaidi kiasi cha kuhoji wenyeviti wa UVCCM wa wilaya wanafanya kazi gani kuratibu vijana?
“Wenyeviti wa Umoja wa Vijana wa CCM wanaratibu vijana vipi katika wilaya zao? Maana vijana wapo tu, hawajui nini kinaendelea na ninyi mnajiita viongozi wa chama wa vijana, mnaongoza nini au mnatembelea magari yetu tu,” alihoji Kabaila.
Katika kukomelea msumari wa moto kwenye kidonda, Kabaila aliwaambia viongozi hao kuwa hata kushindwa kwa CCM katika uchaguzi mdogo wa Kata ya Kirumba kuna uhusiano wa moja kwa moja na unafiki wa viongozi na kutotaka kusikiliza ushauri wa watu wanaowaona hawana nguvu kwenye chama.
“Haya tuje kwenye uchaguzi wa Kata ya Kirumba, ushindi mmeupoteza wenyewe kwa ajili ya unafiki. Mtu akiwashauri hivi mnamuona adui, akitaka kuwasema hivi mnapuuza, kama mnaona manusuasua tokeni,” alisema huku akishangiliwa kwa nguvu na wamachinga wenzake waliokuwapo uwanjani hapo.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2010, vijana wamachinga ingawa walikuwa wanapuuzwa kama wafanya fujo na baadhi ya wanasiasa wakubwa walifikia hata hatua ya kuwaita wavuta bangi, kwa kiasi kikubwa ndio walioleta mapinduzi ya kisiasa katika Jiji la Mwanza kwa kukifanya CCM kipoteze majimbo yote mawili ya Nyamagana na Ilemela na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwenda CHADEMA.
Vijana hao ambao wengi wao ssa wanajipambanua wazi kuwa wafuasi wa CHADEMA, na hasa wa mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje au maarufu hapa kama ‘mtoto wa mama ntilie’ kama wanavyomuita wao, kwa kiasi kikubwa ndio wamekuwa waamuzi wa hatma ya siasa za Jiji la Mwanza.
“Ni kweli hawa vijana mwanzoni walionekana kama si watu muhimu sana, wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita hakuna mtu aliyedhani watafanya walivyofanya, hata zile mbwembwe zao za kumsindikiza Wenje kila anakokwenda kila baada ya mikutano ya kampeni zilionekana ni upuuzi wa ujana tu. Lakini sasa liko somo tumejifunza. Hawa si wa kupuuza, ndio wanashika hatma ya siasa za Mwanza,” alisema mjumbe mmoja wa kamati ya siasa ya CCM Mkoa ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Aliongeza kuwa japokuwa chama hicho kimegundua umuhimu wa vijana na hasa wamachinga, katika kuamua mustakabali wa siasa za Mwanza, na hofu kuwa huenda muda ambao wao wameanza kuwasogeza kwao unaweza usiwasaidie sana kwa kuwa mtazamo wa wengi ni kuwa wanaweza kuona kama wanatumiwa kisiasa.
“Tuna mikakati kwa kweli ya kutaka kuwaonyesha vijana hawa umuhimu wa kukikunga mkono CCM kwa kuwa ni kweli kwamba mambo yote mazuri wanayoyaona yamefanywa na CCM, hawa wengine ni wapiga kelele tu, lakini nina shaka na timing yetu, wanaweza wakatutafsiri kuwa tunataka kuwatumia kisiasa lakini kwa kweli malengo yetu si hayo, tutajitahidi kuwaelewesha naamini hatimaye wanaweza kutuelewa” alisema.
Katika hafla hiyo, Mabina aliwakabidhi vijana hao hati ya malipo ya benki ya shilingi milioni 10 zilizowekwa kwenye akaunti ya Muungano wa Wamachinga, na akasema kuwa wako wamachinga walio hai zaidi ya 500 lakini mafunzo hayo yameanza na wamachinga 100 kwa hatua ya awali na wataendelea na wengine kadiri muda unavyosonga mbele ili kuhakikisha kuwa wamachinga wote wanapata elimu ya ujasiriamali ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi.
Aliwakumbusha pia kuwa hata mazingira ya amani na utulivu wanayofanyia biashara zao yameletwa na chama hicho, hivyo wasiruhusu wajanja wachache laghai kuwapotosha na kuwaingiza katika vurugu za siasa kwa sababu watashindwa kufanya kazi zao kwa amani kama ilivyo sasa.
“Jambo jingine la msingi ninalotaka kuwakumbusha ni kuwa tunzeni amani yetu, hii imeletwa na CCM. Ndiyo inayowafanya mfanye kazi zenu katika mazingira ya amani, msikubali kuingizwa katika vurugu za kisiasa, wapo wengine kazi yao kila siku wanataka kuwatumia kisiasa, hili litawafanya mshindwe kufanya kazi zenu za maendeleo, itunzeni hii amani ili mfanye kazi zenu kwa amani,” alisema Mabina.
Toa maoni yako