
SERIKALI ina upungufu wa shilingi bilioni 700 katika Bajeti yake ya sasa inayokwisha baadaye mwezi Juni, mwaka huu, na hali hiyo imeilazimu kupunguza matumizi yake, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, aliwaambia wabunge mjini Dodoma jana Jumanne huku wao wakisema sasa iwe mwisho kupandisha bei za vinywaji kila mwaka.
Kwa mujibu wa Waziri Mkulo, kwa ajili hiyo, wafadhili sasa wameionya Serikali kutokuwa legelege katika kutoa dhamana za mikopo kwa baadhi ya taasisi zake.
Naye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema tayari Baraza la Mawaziri lilikwishakuzuia kutoa dhamana za Serikali kwa muda wa mwaka mmoja maelezo ambayo Waziri Mkulo aliyatumia kuzikumbusha taasisi, idara na wakala za Serikali kutoomba tena dhamana ya Serikali kwa ajili ya mikopo ya miradi mbalimbali ikiwamo ya maendeleo.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea katika hali inayoashiria ugumu kwa Serikali kupitisha bajeti yake kuu ijayo itakayosomwa mwezi Juni, mwaka huu, wabunge wameanza kueleza wazi kuchoshwa kwao na mfumo mkongwe wa Serikali kuwasilisha bajeti inayoongeza bei za bia, soda na sigara kama vyanzo pekee vya uhakika vya mapato.
Kwa sasa, wabunge wameonyesha dalili za kutoendelea kuvumilia migodi na kampuni mbalimbali ya huduma za simu za mkononi nchini wakitaka zitozwe kodi inayostahili ili kupanua wigo wa mapato ya Serikali.
Kilio hicho cha wabunge kimejitokeza wakati wa mjadala wa mapendekezo ya mfumo wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka ujao wa bajeti wa 2012/2013, katika ukumbi wa Msekwa, bungeni mjini Dodoma Jumanne, wiki hii.
Licha ya mapendekezo hayo yaliyowasilishwa kwa wabunge kulenga kupunguza ugumu wa maisha ikiwa ni pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei na kuongeza kasi ya ukuaji uchumi, wabunge walikosoa karibu kila mapendekezo yaliyowasilishwa kwao.
Akichangia mapendekezo hayo, Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, aliwashutumu watalaamu wa uchumi nchini akisema wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na hasa katika maandalizi ya bajeti, wakishindwa kubuni vyanzo vipya vya mapato.
“Kila mara bajeti ikiwasilishwa ni ongezeko la bei za soda na vinywaji vingine, hivi hakuna vyanzo vingine vya mapato? Safari hii hatutaki mazoea hayo katika bajeti ijayo,” alisema Jenista.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nkasi, Ally Kesi alikosoa mapendekezo ya Serikali katika mpango wa bajeti akisema kwa sehemu utekelezaji wake unategemea fedha za mkopo kutoka nje ya nchi, akihoji; “kuna uhakika gani wa kukopeshwa?”
Badala yake, Kesi alishauri Serikali kupanua wigo wa ukusanyaji kodi kwa kuhakikisha migodi nchini na kampuni za simu zinalipa kodi kwa mujibu wa sheria pamoja na kupunguzwa kwa kiwango cha misamaha ya kodi nchini.
Toa maoni yako