Makala
Msuli wa JICA na maboresho serikali za mitaa
Aristariko Konga
Toleo la 010
2 Jan 2008

“Inachukua muda mrefu kwa serikali za mitaa kuwa na madaraka yenye mizizi imara, na kazi ya kuzipa madaraka hayo serikali hizo, kwa hakika, ni ya kubahatisha na ya majaribio tu.”

-Atsushi Hanatani, Mshauri Mwandamizi wa Shirika la Misaada la Japan (JICA), Novemba 14, 2007, Dar es Salaam.

HIVI karibuni Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) liliitisha mkutano wa wadau wa serikali za mitaa kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, ili kujadili mada iliyoitwa: “Mpango wa Maboresho ya Utoaji Huduma katika Afrika Mashariki.”

Kwa ujumla,  jambo ambalo liliwekwa bayana ni kwamba kazi ya kufanya maboresho katika serikali za mitaa ni ya kubahatisha na ya majaribio tu.

Kwamba, hakuna mbinu moja ambayo inaweza kufanikisha kazihiyo, ambayo inaweza kutumiwa katika kila nchi au katika eneo lolote la serikali za mitaa.

“Mbinu mpya za kufikia maendeleo vijijini hazina budi kuendelea kubuniwa na kufanyiwa mabadiliko kila uchao, kwa kupitia majaribio, huku kukiwa na udhibiti wa hali ya juu wa mchakato mzima,” anasema Atsushi Hanatani, Mshauri Mwandamizi wa JICA, mjini Dar es Salaam.

Malengo ya mpango huo, mosi ni kuhamisha madaraka kutoka serikali kuu hadi tawala za mikoa na serikali za mitaa. Pili ni kuhakikisha taasisi za chini za serikali zinapata uwezo wa kujiamulia mambo yanayohusu maisha yao. Kwa maana hiyo, lengo ni kuimarisha mfumo shirikishi katika utawala.

Kwa mujibu wa Dk. Asfaw Kumssa, aliyewasilisha mada katika mkutano huo wa wadau wa serikali za mitaa, ugawaji wa madaraka hayo ni wazo lenye vipengele tofauti.

Kipengele kimojawapo ni kukabidhi madaraka, rasilimali na uwajibikaji wa kiutawala kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa.

Kipengele kingine ni kuhamisha  kazi na rasilimali watu kutoka serikali kuu hadi serikali za mitaa, ambako maofisa walioteuliwa kwenda huko wanakuwa kama wawakilishi wa serikali kuu.

Kukabidhi kazi na wajibu kwa taasisi zinazojitegemea na zile za umma, ni kipengele kingine.

Ubinafsishaji ni kipengele kingine kwenye maboresho ya serikali za mitaa, ambako uuzaji mali za umma kwa sekta binafsi hufanywa.

JICA imekuwa ikitumia msuli wake wa kifedha ili kusaidia kufikia malengo hayo, na ndiyo sababu iliitisha mkutano huo ili kutoa elimu ya kuyatekeleza mambo yote hayo.  

Hata hivyo, Dk. Kumssa anasema kwamba uhamishaji huo wa madaraka ni jambo la lazima, lakini hautoshi kuwa kigezo cha kuwa na utawala bora.

“Uhamishaji wa madaraka pekee kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa hauwezi kuzaa utawala bora, kwa kuwa utawala bora unahitaji taasisi zenye nguvu na zinazofanya kazi kwa umakini, kwa kuzingatia kanuni ya sheria na urasimu wazi,” anasema Dk. Kumssa.

Pamoja na malengo yote hayo, uhamishaji huo wa madaraka umekuwa ukipita katika changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa fedha na rasilimali watu wenye ujuzi kwenye serikali za mitaa, ambao unazifanya ziwe tegemezi kwa serikali kuu.

Udhaifu mwingine ni katika ushirikishi wa watu kwenye shughuli mbali mbali, ukosefu wa ushirikiano baina ya serikali za mitaa zenyewe na hata na serikali kuu.

Kuwa na taasisi dhaifu katika ngazi ya chini pamoja na serikali kuu kuingilia mambo ya serikali za mitaa.

Lakini pia udhaifu mwingine wa uhamishaji huo wa madaraka upo katika serikali kuu, ambayo husita kukabidhi madaraka kwa serikali za mitaa na tawala za mikoa.

Katika Tanzania hatua moja kubwa iliyochukuliwa katika kufanya maboresho katika serikali za mitaa ni “Ajenda ya Mabadiliko ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1996 hadi 2000.” Ajenga hii ilitungwa mwaka 1996. Ajenda hiyo ilikubaliwa kama waraka wa serikali mwaka 1998.

“Waraka huu ulifafanunua kwamba sera ya serikali ya kufanya maboresho ya serikali za mitaa ilikuwa ni kutumia mfumo wa kukabidhi madaraka, raslimali na uwajibikaji wa kiutawala kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa,” anasema Masao Yoshida wa JICA.

Kwa hiyo, mfumo huo unahusu serikali kuu kukabidhi madaraka ya kisiasa, ya kifedha na yale ya kiutawala kwa serikali za mitaa.

Ili kuhakikisha kuwa kuna uhusiano mzuri baina ya serikali kuu na serikali za mitaa, serikali iliunda Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo awali ilikuwa chini ya Ofisi ya Rais, na baadaye ikawekwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Chini ya waraka huo wa mwaka 1998, kuhusu maboresho ya serikali za mitaa, watumishi wote waliokuwa wakijihusisha na masuala ya serikali za mitaa walitakiwa waajiriwe na serikali hizo, yaani Halmashauri ya Wilaya.

Kutokana na mabadiliko hayo, halmashauri za wilaya zilipewa mamlaka ya kuajiri, kupanga majukumu, kupandisha vyeo na hata kufukuza watumishi wa umma.

Masao Yoshida anasema: “Hata hivyo, ilisisitizwa kuwa mishahara, posho na marupurupu vipangwe kwa viwango sawa, na hivyo mambo yote yanayohusu rasilimali watu ikabidi yaangaliwe upya.”

Kabla ya hapo, kulikuwa na taratibu tofauti kwa utumishi wa umma katika serikali kuu na ule wa serikali za mitaa, ingawa serikali kuu ndiyo ilikuwa na jukumu na ajira zote mbili.

Kutokana na mabadiliko ya mwaka 2000 ya Sheria ya Utumishi wa Umma, ajira zote mbili ziliingia katika utaratibu mmoja.

Kukabidhi madaraka ya utawala wa fedha yanajionyesha wazi katika mfumo wa matumizi.

Uhamishaji wa fedha kutoka serikali kuu kwenda serikali za mitaa, kuanzia mwaka 2004, ulikuwa kwenye maeneo sita. Kipaumbele kilikuwa kwa sekta za elimu, afya, maji, barabara, kilimo na malipo kwa mambo ya kiutawala.

Hata hivyo, sekta za elimu na afya ndizo zinachukua sehemu kubwa ya matumizi, ambayo kwa pamoja inafikia asilimia 75. Sababu kubwa ya jambo hilo ni kutokana na uwingi wa walimu wa shule za msingi na watumishi wa afya, kiasi kwamba fungu lao la mishahara linafanya takwimu ya matumizi iwe juu.

Kuna matatizo kadhaa yanayojitokeza kwa upande wa utoaji wa huduma katika serikali za mitaa, kama yanavyoainishwa na Masao Yoshida.

Tanzania imekuwa ikizifanyia maboresho serikali za mitaa tangu miaka mingi. Si jambo lililoanza hivi karibuni. Kutokana na hali hiyo serikali hizo zimekuwa zikipita katika milima na mabonde na migeuko kadha wa kadha.

Pamoja na safari hizo za migeuko, kumekuwa tofauti kati ya siku zilizopita na sasa, kwa kuwa kuna mabadiliko ya jinsi misaada ya kifedha kutoka serikali kuu inavyofanya kazi.

Kuondolewa kwa kodi ya maendeleo kuliziondolewa halmashauri za wilaya vyanzo huru vya mapato kuanzia mwaka 2004. Lakini misaada ya serikali inavyotumiwa kwa njia nzuri inaleta ahueni katika upataji huduma.

Kwa vyovyote vile, JICA ina sehemu yake katika maboresho ya serikali za mitaa. Wametumia misuli yao ya kifedha kuhakikisha ubora unapatikana.

Kwa kuwa jambo hili ni la majaribio na kubahatisha, bado kama kuna mafanikio yamepatikana basi wanastahili pongezi, kwa kuwa hakuna mbinu moja ambayo inaweza kutumiwa kila eneo la serikali ya mtaa.

Bado majaribio ya hapa na pale inabidi yaendelezwe katika kuleta ufanisi wa serikali hizo, ambazo, kwa hakika, ziliwahi kuwa kero kubwa miaka michache iliyopita.

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi

Toa maoni yako