Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi Frank,
VIPI hali yako huko? Ulipenda shairi langu la wiki jana? Nilitarajia na wewe utaniandikia kashairi. Zamani ulikuwa hodari sana lakini naona siku hizi huna muda. Au biashara ni adui wa sanaa? Ubunifu wote kwenye jinsi ya kuuza! Au hali hii ya kuhangaikia kipato ndiyo adui wa kila kitu?
Pole sana lakini laazizi wangu. Najua nalalamika sana ninavyofanyishwa kazi kibao hapa, na hata kuachiwa viporo vya chakula tu baada ya wanene kubugia, lakini angalau najua kwamba nitakula na kushiba mara tatu kwa siku. Dada mmoja alinitania siku moja eti mbwa wa mfalme ndiye mfalme wa mbwa, lakini bado ni mbwa tu na anaweza kupigwa teke siku yoyote, ndiyo maana navaa kufuli ya chuma nisisikie hilo teke hi hi hi!
Lakini bado mpenzi, hata nikikaa na hawa wanene miaka ishirini nitashindwa kuwaelewa. Sijui tatizo ni kichwa changu kibovu au tatizo ni kwamba wamba ngoma wanalewa. Hivyo wanapovutia kwao wanavutia hadi ngozi inapasuka.
Kweli. Iweje kwanza wadai maposho kibao eti hali ya maisha imepaa, tena wadai posho hizi za zidisho (maana si za nyongeza tena) huku tayari wanapokea posho kubwa. Bila aibu! Kisha wengine wakidai kulipwa tu posho ndogo walizopangiwa, wala si nyongeza, wala nini, kulipwa tu posho ndogo walizopangiwa, wanawafukuza kazi. Inayumkinika kweli? Eti wamekiuka kanuni za kazi. Kutowalipa kwa muda unaotakiwa hadi wanashindwa kula na kuvaa sio ukiukwaji wa kanuni za kazi? Basi wafukuzwe kwanza wale ambao walishindwa kuwalipa stahili zao.
Lakini ndio wanene wetu walivyo. Sheria zote ndio hawala zao. Wanalala pamoja kila siku. Na wengine wakijaribu kuwakosoa, wanatafuta kila aina ya kashfa ili wamnyamazishe mtu badala ya kujibu hoja. Yaani mtu akigusia suala la posho nyumbani, bosi anakuwa mbogo hadi anageuka nyati kabisa. Hata Binti Bosi amefyata mkia kuhusu hilo, hafurukuti tena.
‘Watu hawaelewi jinsi mbunge anavyopata maisha magumu. Mateso matupu.’
Yaani ingekuwa mimi mpenzi ningemuuliza kama maisha ni magumu hivyo, kwa nini asiachie ngazi wengine wachukue. Lakini bado wanapata posho ya hiki, na posho ya kile, na baadaye kwenda kufungua kikao au mkutano na kupewa bahasha nono tena juu ya maposho yote mengine. Juzi nililazimika kumsindikiza bosi na Mama Bosi kwenye mkutano fulani kwa sababu baada ya hapo walikuwa wananipeleka kumsaidia kaka yake bosi kwenye sherehe yake. Basi vituko nilivyoviona huko vilinitosha kabisa.
Yaani nakuambia. Baada ya mkutano wema ulizidi uwezo kwa maana kwamba kiasi cha pesa kwenye bahasha ya bosi kilizidi uwezo wa bahasha. Kwanza hata uzito wa maneno ulizidi hali ya hewa kwa maneno kama:
‘Naomba upokee haka kashukrani kadogo kwa furaha ya kuweza kusikiliza maneno yako ya hekima …’
Na maneno mengi-mengi ya aina hiyo. Sasa, wakati wanaendelea kumsifu yeye hadi mababu zake, wakanyanyua bahasha ili wampatie. Wacha bahasha ipasuke. Na kwa kuwa feni ilikuwa inafanya kazi kwa nguvu sana ili mheshimiwa bosi asisumbuliwe na hata tone la jasho, upepo ulianza kupeperusha manoti kila mahali. Basi wacha watu wazipiganie.
‘Neema ya ukubwa huo!’
‘Ada ya shule’
‘Nauli ya feri!’
‘Mboga ya jioni.’
Ikawa vurumai hadi watu wanapigana kabisa na niliona angalau watu wawili wakichana noti kwa sababu hakuna aliyekuwa tayari kumwachia mwenzie. Wakati huo, Bosi alikuwa ameshika bahasha lililopasuka kwa nguvu zote asije akakosa noti zilizobaki.
Lakini zile noti zilikuwa nyingi mpenzi. Mimi sijawahi kushika milioni lakini nilisikia kama zile zilikuwa milioni moja na ushee na nadhani ni ushee tu uliopeperushwa maana milioni moja ilikuwa imefungwa kabisa. Labda ndiyo maana waposholiwa wanadai kuongezewa na wao maana wanaona mawaziri wanafaidi sana. Mgeni rasmi saa za kazi lakini bado anapewa bahasha iliyojaa hadi haiwezi kuhimili. Na sijui sisi tunaogharamia hizi bahasha mwisho wa siku tutahimili hadi lini.
Na hapo BB alinipa stori nyingine ya baba wa taifa, eti alipokuwa anakwenda ng’ambo, mara nyingine alikuwa anaalikwa kutoa mhadhara hapa na pale. Mwisho wa mhadhara walikuwa wanataka kumpa hundi kama malipo yake. Baba daima alikataa lakini waliposisitiza kwamba siyo takrima wala hongo alikuwa anauliza ni shirika gani eneo lile ambalo lilikuwa linafanya kazi nzuri kwa ajili ya watoto yatima au akina nani. Baada ya kuambiwa alielekeza hundi lake la malipo huko huko, siyo kukumbatia bahasha kama vile mpenzi freshi.
Ndiyo maana Baba wa Taifa alikuwa na nguvu na haki ya kukemea uchu wa kutajirika kwa njia yoyote ile ya wanaojidai viongozi wetu. Lakini wengine sijui. Siku mbili-tatu baada ya bosi kukumbatia bahasha yake alirudi akiwa amekasirika kabisa. Akashika glasi yake ya wiski kama vile ni kichwa cha adui wake na anataka kukinyooonga hadi kife kabisa. Lakini hakusema neno hadi taarifa ya habari alipoona mstaafu fulani akiongea.
‘Unamwona huyu? Unamwona huyu? Alipokuwa madarakani alitutetea vizuri sana, kuanzia marupurupu yetu hadi matumizi ya marupurupu. Takrima hoyee! Alipiga marufuku watu hata kuongelea suala la wagombea huru katika uchaguzi kwa wasiwasi kwamba watu wanaopendwa na wananchi kwa kutopendwa na chama watakuja kuwashinda vipenzi vya chama. Lakini tangu aachie ngazi ghafla amekuwa mlokole wa kisiasa na kukemea yaleyale aliyotetea enzi zile, sijui ni ulokole au unafiki lakini ndiyo hivyo.’
BB alishindwa kuvumilia.
‘Lakini baba si anasema ukweli?’
‘Ukweli gani? Kama ni ukweli, mbona hakusema wakati ule?’
‘Ameona madhara ya uamuzi wake huu. Ingawa wengine tunasema siri ya mtungi aijua kata lakini kata inaweza kujua yaliyomo ndani ya mtungi tu. Inabidi kutoka nje ya mtungi kuweza kuona kumbe mtungi una nyufa, au unatambaliwa na nyoka.’
‘Usiniletee ushairi wako hapa. Katetea, kafaidi sasa hataki tufaidi na sisi. Kama anaona uchungu kiasi hicho, basi arudishe hizi za ziada alizotetea wakati ule.’
‘Unajua siyo hivyo baba. Mtu mmoja kurudisha bahasha …’
‘Bahasha … bahasha. Unasema nini?’
Yaani jinsi bosi alivyoonekana kukasirika hapo BB alishindwa hata kuendelea kula. Aisee kugusa suala la bahasha kwa mwanasiasa ni balaa tupu. Hata bosi alikataa kuongea zaidi akatoka na kurudi saa nane za usiku baada ya kushughulikia bahasha moja vizuri sana. Lakini kesho yake, alipoamka na kukuta madaktari wamegoma kufanya kazi hadi walipwe posho zao, wacha akasirike tena.
‘Angalia hawa washenzi sana. Hawajali kabisa maisha ya watu. Kudai posho tu, kudai posho tu, kwani hawapati mshahara’
BB alifikiria kusema lakini naona mwisho aliona akichokoza tena, nyuki watageuka nyoka. Lakini kichekesho ni kwamba bosi wala hakujua kwamba anajipinga mwenyewe. Hadi nimeona kwamba wenye kazi muhimu za watu wanaweza kulipwa kidogo kwa sababu ni kazi muhimu, na wala wasichukue hatua yoyote kwa sababu watawaathiri watu.
Ila wale wasio na kazi muhimu kama wanasiasa wanaweza kujiamulia kujilipia mabilioni. Na wasipopata wanaweza kutishia kuchukua hatua yoyote maana haiwaathiri wengine. Kazi muhimu, malipo adimu. Kazi huoni, malipo bilioni.
Akupendaye kwa moyo wote,
Hidaya
Oh na nilisahau kukupa mchapo wa mwisho.
Unashangaa-shangaa nini. Kashangae feri. Nauli yapanda. Heshima yazama.
Toa maoni yako