Mwenyezi Mungu hahojiwi, lakini hata waumbaji wetu wa duniani? II

WIKI hii mmoja wa wafuatiliaji wazuri wa safu hii alinitumia mwitikio wa mawazo yake akihitimisha kwamba ‘sisi tunaokubali kuumbwa mara ya pili na waumbaji wa duniani’ tunayo matatizo ya msingi ikiwamo “uvivu wa kufikiri”.

Msomaji yule akasema sisi si binadamu pekee duniani tuliotumikishwa na kudhalilishwa na binadamu wengine waliojiona bora zaidi yetu.

Akatoa mfano wa binadamu wa mataifa mengine ambao kwa mujibu wa historia walidhalilishwa, wakakandamizwa, wakatumikishwa na hata kuuawa kinyama lakini ukafika wakati wakasema: “Kamwe, hatutakubali kuonewa tena, kunyonywa tena na kudhalilishwa tena”.

Kama waasisi wa Taifa hili walivyosema wakati wa Azimio la Arusha: “Ni unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na tudhalilishwe”. Na sasa “tunataka ukombozi.”

Yalikuwa maneno ya akina Mwalimu Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Bibi Titi Mohamed na wenzao wa wakati ule ambao waliamua kujilipua kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Congo huru, Patrice Lumumba. Lumumba alizungumza maneneo yenye ladha na lafudhi hii hii ya: “sasa tunataka ukombozi”, na yalimgharimu. Lakini alipaswa kujua kwamba japo alikuwa na jeuri ya kujilipua mbele ya Mfalme wa Ubelgiji siku ya uhuru, bado hakuwa na ubavu wa kuwakoromea waumbaji wake wa duniani (wakoloni). Hili nitalidadisi zaidi katika makala zitakazofuata.

Maneno ya “Sasa tunataka ukombozi” si maneno mazuri hasa kwa binadamu wengine wanaoamini kwamba ujinga wetu ndiyo mtaji wao, salama yao na mafanikio yao na vizazi vyao. Kwa bahati mbaya, kama Patrice Lumumba “alivyopitwa na wakati” mwaka 1960 kwa sababu alishindwa kukariri msahafu unaoainisha maslahi ya waumbaji wetu wa duniani Azimio la Arusha nalo “lilipitwa na wakati” kwa sababu halikutoka kwa miungu wetu wa duniani.

Na kwa mantiki hiyo hiyo hata dhana ya “Sasa tunataka ukombozi” imepitwa na wakati kwa sababu haijaandikwa kokote katika misahafu ya waumbaji wetu wa duniani. Na ningependa kusisitiza hapa kwamba litakuwa kosa la kifikra endapo itahitimishwa kwamba ninaamini Azimio la Arusha tu, kama lilivyokuwa, lingejitosheleza kuleta ukombozi kamili. Pamoja na kwamba lilikuwa ni hatua muhimu, lenyewe tu kama lilivyo halikuwa likijitosheleza kuleta ukombozi kamili. Lakini lilikuwa ni ufunguo.

Na vivyo hivyo, hata Patrice Lumumba tuliyemsoma sana kiitikadi alikuwa na upungufu kadha wa kadha wa kibinadamu ambao huenda ungeliathiri dhamira yake nzuri ya kutaka kuisaidia Congo, na Afrika, kupata ukombozi kamili. Tofauti tu ya akina Lumumba, Nyerere, Kawawa, Bibi Titi na wenzao ilikuwa ni kujitambua na kuthubutu – potelea mbali hata kama walichekwa au kuonekana walipotea.

Ninachokisisitiza zaidi, kama nilivyokwishakufanya katika makala zangu nyingi zilizopita, ni kuona kwamba hata kama wazazi wetu ambao waliishi na ‘kufaidi’ madhila ya wageni bado wanahisi waliyazoea mno kiasi kwamba wanashindwa kuja na msahafu mbadala – na kubaki wakisubiri kupokea kwa wageni – basi hawa vijana waliozaliwa katika Tanganyika huru na Zanzibar huru waanze kutafakari kwa kina kuhusu masuala haya.

Ninapojadili suala la madhila waliyopitia babu na bibi zetu sina maana nimeamua kupanga nyumba moja na historia. Ninaitembelea tu historia kuijulia hali na kuzungumza nayo kisha ninaondoka siku hiyo hiyo nikiwa nimejifunza kitu. Na ninapotumia maneno kama “waumbaji wetu wa duniani” sina maana ya kukashifu binadamu yeyote ambaye naamini anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Ninazungumzia binadamu yeyote anayedhani – na kutenda kama vile – yeye tu ndiye bora kuliko wengine na hivyo mawazo yake ndiyo yanapaswa kuwa msahafu kwa binadamu wengine wote duniani.

Lakini ni dhahiri kwamba kama inavyotarajiwa kuwa yapo mambo ambayo binadamu tunapaswa kuyaiga kutoka kwa Mwenyezi Mungu (imezoeleka kwamba anaishi Mbinguni – au juu ya mbingu), basi hata waumbaji wetu wa duniani wanayo mazuri ya kuiga. Wao wanajitahidi, na kujibidiisha, kujenga mifumo inayoonekana inatoa haki lau kwa watu wao.

Wanajitahidi katika kutoa elimu inayowajenga watoto wao kujitambua, kufikiri zaidi, kubuni zaidi na kuendelea kuiongoza dunia. Wanajitahidi kuhakikisha wanatengeneza fursa kwa wananchi wao ili waishi maisha bora zaidi na waliyoishi babu zao.

Ndiyo maana wao – kama ilivyo hadithi ya biblia kuhusu mchungaji wa kondoo anavyoweza kuacha kundi akamtafuta mmoja aliyepotea – raia wao mmoja akipatwa na masahibu ugenini, wao huwa tayari hata kuingia vitani kumnusuru. Angalau wanaonekana kwa tabia kuwajali na kuwathamini wananchi wao, mmoja mmoja. Wanatambua kwamba sehemu ya wananchi wao ikiishi maisha dhalili basi wanadhalilika wote kama jamii. Pamoja na mifumo ya kiuchumi inayojenga matabaka ya matajiri sana na wengine wakiwa na kidogo, bado wamevuka hali dhalili inayowakumba watu wetu wengi.

Lakini muhimu kuliko yote ambayo tungelipaswa kuiga bila aibu, ni suala la kujitegemea kwa kutumia akili alizotupa Mwenyezi Mungu. Vinginevyo, kutegemea akili za kupewa na waumbaji wa duniani ni kuhitimisha kwamba yeye Mwenyezi Mungu hakutuwekea za kutosha.

Msisitizo wa safu hii ni kwamba umefika wakati sasa watoto wetu, wale ambao hawakuzaliwa katika ukoloni, wabaini, wajitambue na wachukue hatua katika kufikiri na kuhakikisha kwamba uhusiano wetu, ushirikiano wetu, urafiki wetu na binadamu wa mataifa mengine – bila kujali mtindio wa mahusiano yetu kihistoria – unakuwa ni wa watu sawa. Wakatae kuona wanasoma katika historia kwamba tulifanyiwa hivi tukafanyiwa vile lakini wanashangaa hawaoni tofauti.

Kwamba bado uhusiano wetu na wageni tuliohusiana nao, ama kama wafanyabiashara ya kuuza babu zetu mnadani kama ng’ombe au wakoloni waliotukalia kichwani, bado ni ule ule wa sisi kuwamkia: “Shikamoo”; na wao wanaitikia: “Marahaba.” Na watoto wetu wasikubali kabisa kuambiwa kwamba kwa vile kuna Mungu mpya anajitokeza huku Asia basi ati watawasusa Waumbaji wa zamani ambao wameanza kuwa bahili ili wafaidi vya bure kutoka kwa Mungu mpya wa duniani. Na wakatae katakata kumwamkia “Shikamoo” Mungu mwingine yeyote yule, awe na mvi nyingi za busara au ndevu nyingi kama za Wayunani.

Ni jukumu la wakati kuhakikisha watoto wetu si wanaopiga magoti kila wawaamkiapo wageni kwa sababu tu wanahisi wanadaiwa na kwamba kila siku wanaona wageni wakiwa na viongozi wetu wakitia saini makubaliano ya nchi zetu kupewa misaada.

Inapasa watoto wetu waambiwe ukweli kwamba dunia yetu ilivyo hakuna kitu kinaitwa mlo wa bure na kwamba binadamu waliojulikana kama “Wasamaria wema” walikwishafariki dunia wote kule Mashariki ya Kati. Imewapasa watambue hii ni dunia ya biashara na kwamba wanalo jukumu la kutoa majibu kama aliyoyatoa Rais Yoweri  Museveni katika ziara zake za kwanza kule Marekani.

Zipo habari kwamba Rais wa Marekani alipomuuliza Museveni: “Enhe, Rais kutoka Afrika safari hii unataka tukusidie nini?” Museveni alitoa majibu ya kipiganaji: “Rais, mimi sikuja hapa kuomba; nimekuja tuongee biashara. Uganda ni nchi tajiri sana na ninaamini inavyo vingi vya thamani ambavyo tunaweza kufanya biashara na Marekani.”

Na hili linanileta katika hoja ambayo ningelipenda nianze kuidadisi kuanzia wiki ijayo. Maana halisi ya demokrasia na hatma ya nchi zetu. Leo hii nchi zetu nyingi zinaonekana  zinakwama, zinarudi nyuma na, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za hali ya maendeleo barani Afrika, masikini wanazidi kuongezeka. Ni kweli nchi zetu nyingi zimepiga hatua kadhaa, tena hatua nyingine kubwa kweli kweli. Na ni kutokana na ukweli huo ndiyo maana baadhi yetu tunaamini tunaweza kufanya vizuri zaidi.

Ingelikuwa kila kitu kimeborongwa kabisa basi wengine tusingelipoteza muda kuandika makala, hasa za udadisi au uchambuzi; tungelikuwa tunaandika tu hadithi za sungura na fisi.

Ni bora sisi wenyewe tuanze kuitafakari hiyo keshokutwa ya wajukuu zetu kabla wao wenyewe hawajazaliwa. Litakuwa kosa kubwa la wakati kujikuta tunatopea katika siasa za ushindani uliojaa uadui, chuki na fitna huku tukidhani sarakasi za kukanyagana kufikia madaraka zinatosha kushughulikia, kikamilifu, changamoto kubwa za wakati zinazotukabili leo kama watu.

Huenda tungelitafakari kwa makini zaidi tungelibaini kwamba sisi sote – wa vyama vyote vya siasa, wasio na vyama, wa dini zote, wasio na dini, asasi za kiraia, matajiri kwa masikini, wa mijini kwa wa vijijini, – tunahitajiana zaidi katika kukabili changamoto za kizazi chetu, hasa zile zisizoonekana wazi zinazohusiana na uhusiano wetu na waumbaji wetu wa duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *