Mwezi wa Mwanamke: Tano Bora Zangu (2016-2017)

ZAIDI kidogo ya wiki moja iliyopita, sote tulisherehekea Siku ya Mwanamke Duniani. Kila mmoja alisherehekea kwa namna aliyoona inafaa.

Hata hivyo, kimsingi, mwezi Machi sasa unafahamika kama mwezi wa Mwanamke na hivyo si vema kukawa na tukio moja tu na la mara moja tu mwezi mzima.

Leo, nimeona ni vema nikatumia mwezi huu kutambua wanawake watano ambao kwa hakika waliruka vihunzi na kufanya yale ambayo hayakutarajiwa. Mambo yaliyowatokea au kuyafanya yana maana kubwa kwa wanawake wengine na jamii yote ya Watanzania.

Tukumbuke kwamba sote tuko kwenye njia moja ya kuondoa kile ambacho Dk. Asha Rose Migiro (sasa Balozi wetu kule Uingereza), alipata kukisema; kuhusu kuondoa ule uzio wa kioo kwa wanawake.

Uzio ule ni ile mipaka ambayo jamii imeweka kuhusu mafanikio ya wanawake. Kwamba eti mwanamke anaweza kushinda na kufikia hatua fulani tu na haitakiwi kuzidi hapo.

Tunasema ni muhimu kuvunja uzio huo. Ili kwamba sote tuwe na fursa sawa. Maana fursa ni kama mbawa za ndege, kila anayeipata, anaweza kuruka atakavyo.

Wanawake watano hawa, kwa walau mwaka 2016, wamefanya mambo yaliyoonyesha kwamba jinsia hiyo iko tayari kwa nafasi kubwa, kubwa zaidi.

Haya, na tuanze.

 1. Samia Hassan Suluhu (Makamu wa Rais)

   

   

   

   

   

   

  Katika historia ya Tanzania, huyu ndiye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Makamu wa Rais. Ni mtu wa pili kwa madaraka makubwa hapa Tanzania. Ni Rais pekee ndiye aliye juu yake.

  Kuwa kwake Makamu wa Rais kunamaanisha kwamba ndiye pekee ambaye hawezi ‘kutumbuliwa’ na Rais John Magufuli. Yeye na Rais wameingia Ikulu kwa tiketi moja na ni kitu kimoja.

  Alipoteuliwa kuwa mgombea mwenza, si watu wengi walikuwa wakimfahamu. Lakini sasa Mama Samia anajulikana karibu kote nchini.

  Katika mwaka wake wa kwanza kwenye nafasi hiyo, ameonyesha ubunifu, staha, uongozi na utulivu katika mazingira ya kisiasa ambapo mambo hayo ni adimu.

  Amehudhuria mikutano ya kimataifa kwa niaba ya Rais Magufuli na amekaimu Urais wakati Magufuli hayupo na nchi ilikwenda vema pasipo kuyumba wala kujulikana kuna mapungufu.

  Ni ishara tosha kwamba yuko tayari hata kwa nafasi “namba moja”. Na kama Samia yuko tayari hata kwa Urais, maana yake ni kwamba wanawake wa Tanzania wako tayari kwa nafasi yoyote ile iliyopo.

  Mtazamo wangu ni kwamba, kama Samia ataendelea na majukumu yake kama ilivyo sasa, watoto wa kike wanaokua sasa watakuwa na ndoto za juu zaidi kuliko alivyokuwa Samia utotoni kwake.

  Namuweka kwenye nafasi hii kwa sababu ya changamoto kubwa iliyowekwa kwake kwa nafasi hiyo ya kihistoria. Na namuweka hapa pia kwa sababu yeye sasa ni kioo cha wapi mtoto wa kike anaweza kufika kama atapambana.

   

 2. Grace Martin (Mkurugenzi wa Protokali)

   

   

   

  Image result for Grace Martin Mambo ya Nje

   

   

  Miaka saba iliyopita, Grace Martin alikuwa katika mojawapo ya kesi maarufu zaidi hapa nchini. Yeye na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Ricky Mahalu, walikuwa wanatuhumiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.

  Ilikuwa ni kesi iliyodumu kwa muda mrefu, kufuatiliwa kwa karibu na ingeweza kumharibu mtu kisaikolojia na kiakili. Hii ndiyo kesi iliyoweka historia ya kuwa ya kwanza ambayo Rais mstaafu alitoa ushahidi mahakamani.

  Lakini haikuwa hivyo kwa Martini. Aliyakabili mashitaka dhidi yake, akaendelea na kesi hadi mwisho na hatimaye Mahakama kuamua kwamba hakuwa na hatia.

   

  Halafu akaendelea na kazi zake kama kawaida akiwa mmoja wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje. Na mwishoni mwa mwaka jana, Rais John Magufuli, akamteua kuwa Mkuu wa Protokali – mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.

  Hii ni mojawapo ya nafasi nyeti katika serikali. Lakini, namuweka humu kwa sababu ya kuweka historia na pia ujasiri na ustahamilivu wa kupitia kwenye tanuru la moto kama ilivyokuwa kesi ile.

  Ingekuwa rahisi kwa Grace Martin kuacha kazi na kuendelea na mambo mengine baada ya kesi ile ya kuchosha.

  Kwamba ameendelea na kazi yake kiasi cha kuonekana anafaa kwa wadhifa mkubwa zaidi, Grace anaingia kwenye orodha yangu.

 3. Shy-Rose Sadruddin Bhanji (Mbunge EALA)

   

   

   

  Wakati Shy-Rose Bhanji akichaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) miaka mitano iliyopita, Ibara ya 119 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ilisema tu jumuiya hiyo itakuwa na kazi ya kupromoti lugha ya Kiswahili.

  Lakini mwanamke huyu akaingia kwenye Bunge hilo akiwa na azimio moja kwamba; “kwamba wakati namaliza kipindi changu cha kwanza, Kiswahili kiwe na nafasi kubwa zaidi kuliko wakati naingia kwa kukifanya kiwe moja ya lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kufuatilia kwa karibu masuala ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kiswahili kina nafasi nzuri ya kuunganisha wana Afrika Mashariki na itasaidia mtangamano wa Afrika Mashariki kupiga hatua kwa haraka”.

  Hatimaye, Alhamisi ya Agosti 25 mwaka 2016,  kwa kushirikiana na Mbunge mwenzake kutoka Kenya Aboubakar Zein wakawasilisha hoja ndani ya EALA, iliyotaka Kiswahili kiwe lugha rasmi ndani ya Bunge hilo; hoja iliyokubalika kwa kauli moja na bunge hilo na kupitishwa wenzake wote kutoka katika nchi wanachama wake; Tanzania Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. 

  Oktoba mwaka jana, nchi mwanachama wa EAC, Rwanda, ikapiga hatua nyingine mbele kwa kuanza mchakato wa kukifanya Kiswahili kiwe moja ya lugha rasmi nchini huko na hivi karibuni Bunge la nchi hiyo likapitisha Sheria bungeni kuitangaza lugha hiyo kuwa mojawapo ya lugha zake za taifa.

  Shy-Rose, kwa mara nyingine, akawa mbunge wa kwanza kutoa hoja kwa wabunge wote wa EALA kutoa Azimio Rasmi la kuipongeza Rwanda kwa hatua yake hiyo. Azimio hilo likapitishwa na wenzake wote.

  Juhudi hizi za Shy-Rose sasa zinaanza kuzaa matunda kwani wakati Rais Kagame anahutubia kikao cha Bunge la Afrika Mashariki mjini Kigali hivi karibuni alisema kwamba hatua ya Serikali yake kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi imetokana na Azimio la EALA kutaka Kiswahili kiwe moja ya lugha rasmi Afrika Mashariki. 

  Bhanji ameacha alama (legacy) itakayodumu milele kwenye Bunge hilo na historia itamkumbuka kama Mbunge mwanamke kutoka Tanzania aliyepigania Kiswahili kupata hadhi na heshima inayostahili katika Matangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

  Miaka 50 kutoka sasa, wakati watu watakapokuwa wanafanya tafiti kujua ilikuwaje lugha hiyo ikakubalika kutumika Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki jina la mwanamke huyu litaibuka tena. Miaka 50 kutoka sasa!

  Kama EALA itaanza kuonyesha mubashara kupitia luninga kama wabunge wake tena kutoka nchi zote wanachama wanavyopigania sasa, akiwamo Shy-Rose, Watanzania wasiojua lugha ya Kiingereza wataweza kufuatilia mijadala kwa sababu ya juhudi alizofanya mbunge huyu kwa kushirikiana na wenzake.

  Hizi ndizo siasa za wanawake. Siasa zisizo za uongo na porojo. Na ndizo siasa zinazofanya baadhi yetu waamini kuwa dunia inaweza kuwa sehemu salama zaidi endapo wanawake wengi zaidi watapata nafasi kwenye vyombo muhimu vya maamuzi.

  Kwa sababu ya alama hii ya kudumu aliyoweika kwenye EALA mwaka jana, Shy-Rose Bhanji anaingia kwenye tano bora yangu.

   

   

 1. Frannie Leautier (Makamu wa Rais, Benki ya Afrika)

   

   

   

   

  Niseme ukweli kwamba hadi sasa ulimi wangu unapata shida kutamka ubini wake. Sasa sijui ndugu zangu Wachaga wanatamkaje hilo jina kwa lafudhi yao.

  Ugumu huo pembeni, Frannie ni Mtanzania aliyezaliwa Moshi na kukulia Lushoto, Tanga. Ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya Uhandisi lakini pia ni amesoma katika mojawapo ya vyuo vikuu bora zaidi duniani; Massachusetts Institute of Technology (MIT) ambako alibobea katika fani hiyo kwa kiwango cha Shahada ya Uzamivu (PhD).

  Ndiyo, ni Dk. Frannie Leautier ambaye mwezi Mei mwaka jana aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Hakuna Mtanzania aliyewahi kushikilia nafasi hiyo hapo kabla, achilia mbali mwanamke!

  Frannie ananishangaza kitu kimoja tu, kwamba yeye ni mhandisi lakini ametumia zaidi katika taasisi za kifedha. Kabla ya AfDB, alikuwa mmoja wa vigogo katika Benki ya Dunia; wakati mmoja akiwa Mnadhimu Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Benki ya Dunia, wakati huo ikiongozwa na James Wolfensson.

  Kwa mwanamke wa Kitanzania, aliyekulia Lushoto na kuchunga ng’ombe kabla ya kupambana na kufikia alikofika (na pia mashaallah, uzuri upo) na kuruka vihunzi vyote anavyopitia binti wa Kitanzania, Frannie anaingia katika tano bora yangu.

   

 2. Sophia Manguye ( Mwanamke Jasiri)

   

   

  Image result for Mwanamke Jasiri apambana na majambazi

  Kuna dhana imeenea kwamba wanawake ni watu waoga waoga hivi na wasio majasiri. Kwamba ndiyo maana hata mabaunsa wanapendwa na wanawake kwa sababu wanawahakikishia usalama.

  Hiyo ni kabla mtu hajapata habari za mama huyu wa Tarime mkoani Mara. Februari mwaka jana, kuna majambazi walienda kwenye biashara yake ya duka kutaka kupora.

  Walikuwa wanaume watatu walioshiba kwelikweli. Wakiwa na bunduki yao aina ya SMG yenye risasi takribani 27, walivamia maduka kadhaa yaliyopo Sirari, Tarime na kupora fedha. Na halafu wakaingia kwenye duka la mama Manguye. Thubutu!

  Kwa ujasiri uliomfanya aingie kwenye Tano Bora Yangu, mama huyu alimkamata jambazi aliyekuwa ameshika bunduki na kumdhibiti. Jambazi yule alifurukuta kwa kusaidiwa na wenzake walioendelea kumpiga mama huyo. Lakini hakumwachia jambazi yule wala bunduki yake.

  Mwishowe, majambazi wenyewe wakaamua kukimbia mbio. Hii ni kwa sababu Sophia alikuwa akipambana huku akipiga kelele; jambo lililowatisha majambazi hao.

  Matokeo yake bunduki na jambazi yule mmojawa wakabaki mpaka askari walipofika. Sophia akakutwa na majeraha kidogo na wananchi wakampoza kwa shilingi 500.

  Mimi mwenyewe natoka Wilaya ya Rorya, inayopakana na Tarime lakini kwa tukio hili la Sophia, nimewavulia kofia jirani zetu hawa.

  Wanaume waliofuatwa na majambazi kabla ya Sophia walitoa hela. Mama huyu akapambana nao.

  Kwanini asiingie kwenye Tano Bora Yangu?

  0786 722 303

  Mwisho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *