- Maaskofu Timanywa, NiweMugizi walimwadhibu
OKTOBA 26, mwaka 2011, Padri Desidery Kashangaki, aliaga dunia na kuzikwa Rubya-Bukoba, mkoani Kagera, siku mbili baada ya kifo chake. Amefariki akiwa na umri wa miaka 100 na miezi mitano. Mungu amlaze mahali pema peponi.
Kumzika mtu ni bahati, kwa vile bahati hiyo wameipata wengine waliojaliwa kumzika na kumsindikiza Marehemu Padri Desidery Kashangaki, waliobaki tumlilie kwa tanzia hii. Wengi tuliomtunza na kumjali wakati wa kipindi kigumu katika maisha yake na wito wake wa upadri, hatukubahatika kumzika.
Yeye alisema siku zote; “Wananitenga, wananinyanyasa na kunitesa nikiwa hai; Askofu wangu anakataa kunisamehe, nina imani kwamba nikifa watanizika...” Ni kweli wamemzika maaskofu wawili, idadi kubwa ya mapadri na waumini. Sifa walizokataa kumpatia akiwa hai, heshima waliyomnyima na kumtelekeza mitaani, wamempatia akiwa marehemu!
Kuna mambo mengi ya kuandika juu ya padri huyu mzalendo, mpambanaji, mtetezi wa wanyonge na mpenda haki, maana miaka 100 si haba. Ni watu wachache wanaobahatika kufikisha umri huu. Tanganyika ilipojipatia uhuru wake, Marehemu Padri Kashangaki, alikuwa mtu mzima wa miaka 50.
Aliishi kwenye ukoloni na kuishi kwenye uhuru, ni kati ya watu wachache hapa Tanzania ambao walikuwa na bahati ya pekee ya kufanya tathimini yenye kina ya miaka 50 ya uhuru wetu.
Nilipomtembelea kule Karagwe Mei, mwaka huu, aliniambia; “Sherehe za miaka 50 wakati tumelizika Azimio la Arusha na kutupilia mbali mawazo ya Mwalimu Nyerere, ni kupoteza muda. Baada ya Nyerere, taifa letu limepoteza mwelekeo...vyote vinafanana. Taifa limepoteza mwelekeo na Kanisa limepoteza mwelekeo...Kazana kuandika na kuwaelimisha Watanzania, maana naona mnarudi kwenye ukoloni. Sisi siku zetu zimekwisha..”
Jambo la kwanza la kuandika juu ya padri huyu ni kwamba yeye ndiye padri wa kwanza wa Bukoba kufikisha umri wa miaka 100. Alipata upadri hata kabla ya Marehemu Kadinali Rugambwa na hata kabla ya kuzaliwa Askofu Nestory Timanywa, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba. Pili ni kwamba padri huyu alilitumikia kanisa na taifa la Tanzania kwa kipindi cha miaka 60.
Mbali na kazi zake za kiroho, alikuwa mwalimu wa Chuo cha Walimu Butimba, Mwanza. Alifundisha kwa muda mrefu na kwa njia hiyo, amewafundisha walimu wengi nchini. Walimu aliowafundisha nao wamewafundisha wanafunzi wengi.
Maana yake ni kwamba mchango wa Marehemu Padri Kashangaki ni mkubwa katika taifa letu. Kwa tanzia hii basi wanafunzi wake popote walipo wapate habari kwamba mwalimu wao hatunaye tena duniani.
Tatu, ni padri aliyependa elimu. Mbali na masomo yake ya theolojia, alisoma shahada ya elimu ya watu wazima Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiwa na umri wa miaka 60. Kupenda kwake kusoma kulimfanya abaki kijana muda wote. Ingawa alikuwa mtu mzima wa miaka 100, maongezi yake na uelewa wa mambo ulikuwa ni kama wa kijana.
Nilipomtembelea Mei, mwaka huu, wakati alipofikisha miaka 100, nilishangaa sana kuona anavyofahamu dunia inavyokwenda. Alikuwa na redio yake ndogo, akisikiliza habari za dunia. Nne, alikuwa mshauri wa kiroho wa Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hata masomo yake ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alilipiwa na Mwalimu. Wakati akiwa mshauri wa kiroho wa Mwalimu, aliishi na kufanya kazi Dar es Salaam, makao yake yakiwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph. Tano, ni mtu aliyekuwa amejaliwa afya ya pekee. Hakuwahi kuugua katika maisha yake yote.
Anakumbuka kudungwa sindano mwaka wa 1935 kule Katigondo Uganda. Hakukumbuka ulikuwa ni ugonjwa gani. Lakini baada ya hapo yeye hakujua malaria au magonjwa mengine kama shinikizo la damu, kisukari na mengine. Siku zake za mwisho alikuwa na matatizo ya utu uzima, ambayo si magonjwa bali dalili za mwili kuchoka na kuzeeka.
Daima aliuliza dalili za malaria. Hata kifo chake hakikutokana na ugonjwa, tarehe yake ilifika tu akaitika kwa Muumba wake. Sita, alikuwa mtanashati, mtu wa majivuno, mwenye kiburi cha elimu, lakini mwenye kuipenda na kuiheshimu kazi yake ya upadri.
Majivuno yake na kiburi havikuigusa roho yake ya wema, ucheshi na kuwapenda watu. Alipenda sana lugha ya mafumbo na maisha yake lilikuwa ni fumbo la imani. Aliwachukia watu waliotumia lugha ya wazi na kuyachukulia maisha kuwa ni kitu cha wazi.
Alisisitiza umuhimu wa kuyafumba mambo na kuyafumba maisha. Alitaka kuishi kwa staha, alikula kwa staha na kunywa kwa staha, asingeweza kunywa bia zaidi ya mbili na chakula kama hakuna uma na kisu, basi hawezi kula.
Saba, na labda hii ndiyo sehemu mbaya na ngumu sana katika maisha yake; aliadhibiwa na Askofu wake, akiwa na umri wa miaka 80. Inashangaza na kusikitisha, lakini ndio ukweli wenyewe. Askofu wake hakuweza kumsamehe kwa zaidi ya miaka 20, hadi juzi siku mbili kabla ya kifo chake.
Maana yake ni kwamba Askofu, kiongozi wa kiroho, alitunza hasira moyoni mwake zaidi ya miaka 20. Swali la kujiuliza ni je, kama Askofu hawezi kusamehe, Wakristu wengine watafanya namna gani? Je hii ndiyo imani ya Yesu wa Nazareti, aliyetuambia tusamehe saba mara sabini; na kwamba mtu akikupiga shavu la kushoto umgeuzie na la kulia? Ni imani ya Mungu wetu wa upendo na huruma?
Wasomaji wangu wasifikiri nimebadilisha msimamo wangu kwa kuandika tanzia hii. Nilipoandika kitabu changu ya Imani yangu wito wangu, nilitoa ahadi ya kuacha kabisa kuandika masuala ya Kanisa. Na kusema kweli nimeacha, ila leo nimeshikwa ni lazima kushikamana.
Padri Desidery Kashangani, alipotimiza miaka 90, tulimfanyia sherehe kubwa na mimi niliandika makala juu ya maisha yake, baada ya kusoma makala hiyo alisema; “ Priva, natamani uyaandike haya wakati wa kifo changu... nikikutangulia kufa, kumbuka kuandika, maana daima kilichoandikwa kimeandikwa”.
Amenitangulia, sina ujanja wa kukwepa. Na siwezi kuandika juu ya Padri Kashangaki, bila kuligusa kanisa. Hivyo wasomaji wangu mtanisamehe kuvunja ahadi yangu, hata hivyo, nitauma na kupuliza, sitalichokonoa sana kanisa langu nitayagusia yale ambayo hata malaika hawezi kuacha kuyachokonoa.
Chanzo cha adhabu yake ni nini?
Padri Desidery Kashangaki, alipostaafu kazi ya kufundisha Chuo cha Ualimu na kurudi nyumbani kwao Bukoba, akiwa na umri mkubwa, maisha ya Parokiani yalikuwa magumu. Posho aliyokuwa akiipata akiwa mwalimu hakuipata kule parokiani.
Alianza kufuatilia na kuuliza juu ya maisha ya mapadri wanaoishi parokiani na hasa mapadri wazee kama yeye. Baadaye aligundua kwamba Roma kila mwaka inatuma pensheni ya mapadri waliofikisha miaka 60.
Yeye alikuwa na miaka 80, bila kupata pensheni. Ina maana pensheni yake ya miaka 20 ilikuwa inaingia mfuko gani? Alianza mchakato wa kudai pensheni yake kwa Askofu wake. Hiki ndicho chanzo cha mvutano kati yake na Askofu wake, Askofu Nestory Timanywa, wa Jimbo Katoliki la Bukoba.
Mvutano kati ya Padri Desidery Kashangaki na Askofu Timanywa, ulikuwa makubwa kiasi cha Askofu kuomba msaada wa polisi ili kumwondoa Padri Kashangaki kwenye nyumba za kanisa.
Adhabu yake ilikuwa kwenda kuishi nyumbani kwao alikozaliwa. Adhabu hii wanaitumia Maaskofu wengi, hasa wa Afrika, kama njia mojawapo ya kumfanya padri awe mnyenyekevu; ni wazi ni adhabu iliyopitwa na wakati, ya kikatili na ya kudhalilisha.
Mtu mwenye miaka 80, na amelitumikia kanisa miaka 60, kumrudisha nyumbani kwao alikotoka na kuaga kwamba anakwenda kufunga ndoa na kanisa ni kumkosea haki mhusika, hivyo tukio hilo la kumfukuza Padri Desidery Kashangaki, kwenye nyumba za kanisa halikuwa la kawaida.
Iliwashangaza watu wengi, hata kama Padri Desidery Kashangaki, alitumia kiburi na majivuno kudai pensheni yake, umri wake na miaka aliyolitumikia kanisa ilitosha kumchukulia alivyo, kuliko kumfukuza na kumtupa mitaani.
Watu wengi walijitokeza kumwombea msamaha Padri Desidery Kashangaki kwa Askofu wake, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba. Askofu hakutaka kusikia wala kupatanishwa na padri wake. Alikuwa na hasira kubwa ambayo iliibua hata makosa ambayo Padri Desidery Kashangaki, aliyatenda akiwa kijana wa miaka 40.
Sakata hilo lilipotokea, magazeti yaliandika juu ya tukio hilo, lakini kama ilivyo kawaida ya uandishi wetu, mashambulizi yalimwelekea Padri Kashangaki; yalitajwa madhambi ya Kashangaki. Kitendo cha Askofu kumdhalilisha mzee wa miaka 80 na suala lote la kudai pensheni na haki za binadamu, liliwekwa pembeni na waandishi wa habari.
Padri Kashangaki, alipofungua kesi mahakamani, mbinu za “kimafia” zilitumika, alivamiwa na majambazi hotelini Mwanza na kuibiwa nyaraka muhimu za kesi yake. Hivyo hakuweza kuendelea na kesi.
Bahati nzuri, Askofu wa jimbo la jirani la Rulenge, wakati huo, siku hizi linaitwa Rulenge-Ngara, Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, alimwonea huruma Padri Kashangaki na kumkaribisha jimboni kwake. Hivyo Padri Kashangaki, aliishi kama “Mkimbizi” kwenye jimbo la Rulenge.
Waswahili wanasema ng’ombe wa masikini hazai…. Mwaka 1996, Askofu Mwoleka, alistaafu. Roma ilimteua Askofu mwingine, Mheshimiwa sana Askofu Severine NiweMugizi, ambaye kwake maisha ni sheria. Hakuna hekima, busara wala utu – sheria ni msumeno. Ni lazima kufuata sheria. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba hata yeye mwenyewe anashindwa kuzifuata baadhi ya sheria, lakini anataka wengine wazifuate sheria hizo.
Aliposhika utawala wa Jimbo Katoliki la Rulenge, alimfukuzia mbali Padri Desidery Kashangaki, maana hakuwa jimboni Rulenge kisheria. Askofu Mwoleka alimpokea Padri Kashangaki, kiubinadamu maana alikuwa mkimbizi. Kumkatisha mkimbizi hati ya kusafiria, ni uwendawazimu.
Ingawa Padri Kashangaki, alifukuzwa na Askofu wake, mtu aliyefanya dhambi kubwa ni yule aliyemfukuza mara ya pili; aliyemfukuza mkimbizi. Hata sheria za Kimataifa, ukiachia mbali hekima na busara, zinazuia kumfukuza mkimbizi. Hivyo Padri Desidery Kashangaki, alihama kutoka nyumba za kanisa la Jimbo Katoliki la Rulenge na kuishi mitaani. Aliishi maisha magumu.
Watu wengi Wakristu kwa Waislamu walijitokeza kumsaidia na hasa wanafunzi wake. Hata hivyo kipindi kilikuwa ni kirefu kiasi cha wale waliokuwa wakimsaidia kuanza kuchoka. Miaka ya mwisho ya maisha yake, kwa kushirikiana na mapadri waliokuwa na roho ya utu, walimsaidia “kuiteka nyara” parokia ya Bugene Karagwe na kuishi pale.
Lengo lake na matumaini yake ilikuwa ni kurudi kwao Bukoba kudai pensheni yake. Nilipomtembelea mwezi wa tano mwaka huu, aliniambia kwamba atakwenda Bukoba kudai pensheni yake.
Bahati mbaya mauti yamemkuta kabla ya kulipwa pensheni yake. La kumshukuru Mungu ni kwamba, amezikwa nyumbani kwao Bukoba, kama alivyokuwa akitamani. Mungu, amlaze mahali pema peponi rafiki yetu, ndugu yetu na Mtanzania mwenzetu padri Desidery Kashangaki.
Maoni ya Wasomaji
Ndugu yangu,Priva
Ndugu yangu,Priva
MAISHA YETU NDIVYO YALIVYO
BAADHI YETU WAKIWA NA MADARAKA IWE KATIKA SIASA AMA DINI,BASI WANAFIKIRI WAMEFIKA MWISHO WA KONA. HAWAKUMBUKI KUWA MWILI NI HEKARU LA ROHO MTAKATIFU. EBU TU TAZAMA MAISHA WANAYOISHI VIONGOZI WETU WA DINI ULINGANISHE NA HARI ZA WAAMINI WAO...UTACHOKA.
HII LEO WAPO VIONGOZI WA DINI WANAWAOMBEA WAAMINI WAO KUWA NA MAGARI,KWENDA ULAYA, KUPATA UTAJIRI KANA KWAMBA HAYO NDIYO MALENGO YETU KWA MUNGU.WANAFANYA HIVYO ILHALI WENYEWE WAKILIMBIKIZIA SADAKA MATUMBONI MWAO. DINI IMEGEKA BIASHARA NDIYO MAANA HATA VIONGOZI WETU WA KIROHO WANAKWEPA KUWAELEZA UKWELI WANASIASA.
TUMWOMBE MUNGU AWAJALIE ROHO ZA KUWAKUMBUKA WENYE KUHITAJI NA KUWAONDOA KATIKA UBINAFSI