Makala
Nadhani yangu nitaiita Asante Posho Hoteli
Hidaya
Toleo la 217
14 Dec 2011

Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.

 

Frank mpenzi wangu wa moyo,

SIJUI nikushukuru vipi, nikupende vipi.  Sijui nikupe nini.  Yaani baada ya wewe kuja tupate nafasi ya kuongelea yote niliyoyasikia na yaliyokuwa yananisibu moyoni, sasa najiona huru tena.  Naogopa upepo utanipeleka juu angani kwa jinsi ninavyojisikia mwepesi. 

Wacha wanene washerehekee uhuru wao wa kusonga mbele huku sisi twatafuta wa kusonga ugali tu, mimi bila wewe siwezi kuthubutu na sisongi popote. Wacha wao wafurahie uhuru wao wa kutafuna, mimi na wewe mpenzi. 

Tena narudia kuomba msamaha kwa kukuelewa vibaya hivyo, lakini yule Jimi alinipa wasiwasi kweli. Unajua mpenzi wewe ni msingi wa maisha yangu na iwapo msingi unaliwa na vidudu walafi, maisha basi tena.  Ndiyo maana sikuwa na raha kabisa. Na alivyokuwa anaelezea Jimi utadhani alikuwepo kumbe hakuwepo kabisa.

Nakuelewa mpenzi. Kwa biashara yako ya nguo na urembo, lazima warembo watamiminika kwako, na lazima wengi watajishauashaua kwako hivyo waweza kuonekana unawakubali. Ni sawa. Lakini nadhani umenielewa pia. 

Kama mtu amemwamini mtu au kitu kwa nguvu zake zote, kashaka kadogo kakipenya tu, kanaweza kubomoa imani yote. Yale mazuri yote ya nyuma yanageuka vumbi na kusambazwa hadi mwisho wa dunia na upepo wa mashaka. Ndivyo nilivyokuwa mpenzi, na nakushukuru sana kunirudishia imani maana sijui ningeendelea kuishi vipi. 

Na sasa tufanye jitihada kabisa mpenzi. Hidaya wako hataki kuzeekea kuwatumikia wasio na moyo wa kututumikia sisi licha ya maneno kibao. Fanya hima mpenzi.  Mimi niko tayari kulala chini, kwenye kichumba kimoja cha makuti ili mradi tukae pamoja tujenge maisha pamoja. Mwaka mwingine usiishe kabla hatujafunga ndoa yetu. 

Tena nakuambia sihitaji ndoa ya fahari, wala ndoa ya michango. Wacha hawa wanaotuibia pesa zetu washindane kuweka ndoa za kufuru kutambia wizi wao, na wengine wasio na akili kujaribu kuwaiga kwa kuchangisha hadi rafiki zake shemeji wa yule dada anayekaa nyumba ya saba. Ya nini mpenzi? Fahari leo, njaa kesho. Ndoa ni mimi na wewe! Upande wangu nitazidi kudunduliza kila senti ninayoipata kwa ajili ya nyumba yetu.

Lakini mpenzi ungebaki hapa Bongo kidogo ungeona vituko.  Sijui kiherehere cha posho kitatupeleka wapi. Juzi nilikuwa namsikiliza bosi akiongea na simu na rafiki yake mheshimiwa mwingine.

‘Habari za kazi mwenzangu. Habari za kusukuma gurudumu la maendeleo …. Eti nini? Wasukuma mkoko wako tu! Ha ha ha wacha Bwana! Wasikusikie wapiga kura wako … Lakini kweli, wanajua nini, watazibwa mdomo na mnuso wa nguvu kabla ya uchaguzi.  Ha ha ha.  Na wewe nawe Bwana. 

Mimi mzima Bwana. Unajua tulifaidi sana yale maonyesho. Potelea mbali kama walikuja wachache kuona tulichopanga, tumesherehekea sisi au vipi, na kila siku ya kwenda huko tunapewa bahasha ya bashasha, si ndiyo sherehe yenyewe. Ha ha ha! Nakuambia tutajenga mahoteli na hayo mabahasha. Nadhani yangu nitaiita Asante Posho Hoteli ha ha ha!

Enhee, unasemaje?  Posho yetu ya uheshimiwa?  Usiwe na wasiwasi Bwana.  Nakuambia tukiwa watawala, tunaweza kujiamulia lolote tupendalo.  Watatufanyia nini huku tuna zana zote za dola.  Ndiyo posho imepanda.  Watatulaki na malaki ha ha ha! 

Hebu ngoja. Kuna mtu anaongea kwenye luninga. Ah!  Huyu jamaa vipi, anasema hakuna nyongeza ya posho. Ni mtu wetu anawezaje kusema hivi. Atatutambua. Kweli watu wanategemea tulale kwenye vijigesti vya mitaani wakati sisi ni waheshimiwa … nakuambia …

Lakini hebu ngoja tena kuna mama naye ameingia … enhee …. Enhee … ah huyu mama safi sana.   Ndiyo.  Adumu!  Kabisa!  Gharama za maisha zimepanda, za hoteli, za chakula, hata za viblanketi vyetu ha ha ha!  Gharama za kukumbatia nuksi tupu.  Yes! Mama anasema nyongeza ya posho iko palepale.  Sawa mama.   Unastahili kabisa kuwa na cheo chako. Kwa hiyo hamna shida unasikia mzee mwenzangu. Safari hii na vimwana kama kazi na hawa wafanyabiashara uchwara wanaojidai kushindana na sisi watatolewa nje moja kwa moja.  Itakuwaje mfanyabiashara awe na uwezo wa kutupindua huku sisi ni waheshimiwa. Thubutu!

Ha! Hebu ngoja tena. Na mwingine amejitokeza luningani.  Mambo gani hayo? Eti chama kinapinga nyongeza hizo maana italeta picha mbaya kwa wananchi ambao hawana hata harufu ya posho. Nani anajali picha mbaya? Huyu Bwana Mdogo ana wivu kwa sababu si mheshimiwa kama sisi au vipi? Jinga hilo.  Sisi ni wenyewe na lazima tupewe posho ya wenyewe.  Hakuna mjadala. 

Unasemaje mzee mwenzangu. Ha ha ha, usiniambie umeanza kuwa mwoga na wewe. Eti tusiwaamshe waliolala! Mbona dawa yao ya usingizi tunayo. Wewe huwajui watu wetu, watarukaruka na kupiga kelele weeeeeee kisha watatulia na kuendelea kusaka tonge na wao. Na hata kutetea eti ni mpango wa Mungu wengine wale kwa niaba ya wote.  Mungu atupe nini?  Wananchi kama hawa kweli ni zawadi kubwa sana kutoka kwa Mungu.  Waendelee vivyohivyo.  Na hii nyongeza ya posho tutapata, kama si waziwazi basi hata kwa kificho.  Mbona zimeshapangiwa bajeti kabisa. 

Haya Bwana siku njema.  Tungoje kikao kijacho tufaidi.   Lo, naona mama watoto anaingia asije akatusikia tukiongelea habari za vimwana ha ha ha!  Haya na nisalimie waifu wako pia. 

Unasikia mpenzi? Kweli ukiwa juu wala huwaoni wa chini, unapenda kufaidi kukaa juu hukohuko.  Na nasikia dada zetu wanafurika huko midomo wazi kudaka angalau vitonge vya mabonge hao. Nilikutana na mmojawao huko sokoni, ambaye alisoma na sisi. 

‘Wacha kulalamika Hidaya.  Kama matairi yao yamejazwa upepo ni kazi yetu kuwatoa upeo.  Njoo na mimi safari ijayo tuwatoze hawa kodi zetu binafsi.  Mpaka waone kwamba wanatakiwa kudai lakini tano kwa siku.  Watatugawia tu.’

Kwa kweli ilibidi nicheke mpenzi.  Lakini kuwatoa upepo hawa waliojaa pepo kutasaidia nini.  Mimi bado naunga mkono wazo la fyatu wako Makengeza, tuwazomee, tuwasuse, tuwasute hadi washike adabu.  Wamezidi!  Wakianza kuongea tu tuanze kuimba posho … posho … posho … Ingawa walivyo na viburi wanaweza kufikiri tunawaimbia nyimbo za kuwasifu.

Haya Bwana Frank, mume wangu mtarajiwa,
Nakupenda sana
Hidaya

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Hidaya
rmabala@gmail.com

Toa maoni yako