NIANZE kwa kuwashukuru wale wote walionitumia sms za kunipa pole kwa masahibu yaliyotukuta mimi na waandishi wenzangu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ambao tuliponea chupuchupu kukatwa mapanga na wanavijiji wenye hasira katika tindiga la Boluti, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Wasomaji wangu wengi wa ndani na nje ya nchi waliguswa na makala niliyoiandika, toleo lililopita, yenye kichwa kinachosomeka: Siku waandishi wa JET walipoponea chupuchupu kuuawa K’manjaro.
Tulikwenda katika ardhioevu hiyo ya Boloti kujionea jinsi inavyokaribia kukaushwa kabisa na mamia ya mifugo inayolishwa humo, na pia uendeshaji shughuli za kilimo ndani ya tindiga hilo kinyume cha sheria.
Tulidhani tunafanya jambo jema kusaidia kuwaelemisha wanavijiji wale juu ya umuhimu wa kuiokoa ardhioevu hiyo, ambayo maji yake wanayategemea mno kwa matumizi ya nyumbani, lakini wao (wanavijiji) hawakudhania hivyo!
Na kwa sababu hawakuamini kuwa tunalofanya ni jambo jema kwao, wakaamua kututimua kwa mapanga; licha kwamba tulikuwa na ulinzi wa polisi wawili wenye bunduki mbili za SMG. Ni Mungu tu ndiye aliyetunusuru tusiuawe kwa mapanga.
Kwa sababu ya masahibu hayo, wiki nzima iliyopita nimekuwa nikipokea mamia ya sms zenye ujumbe wa kila aina. Wako walioishia tu kutupa pole, lakini wako pia wengine ‘waliowapongeza’ wanavijiji wale kwa kututimua kwa mapanga kwenye ardhioevu hiyo!
Nalichukulia kundi hilo la pili kama ni la aina ya watu katika Tanzania ambao wameanza kukata tamaa na namna mambo yanavyoendeshwa nchini. Hebu soma sms hii ya msomaji wangu mmoja kutoka Mbeya kuhusu suala hilo:
“Mbwambo, pole kwa mkasa wa Boloti. Kaka, mimi binafsi nawapongeza watu wa Moshi pamoja na eneo husika kwa kujua kwamba ardhi ile ni mali yao na wako tayari kufia katika ardhi yao. Nchi hii hakuna wa kumwambia mwenzake akavae nguo wakati yeye yupo uchi. Kuna viongozi hapa nchini wameshajimegea mapande katika migodi ya aina mbalimbali na ardhi zenye rutuba. Viongozi wetu wameshindwa kukemea hayo, itakuwa nyinyi waandishi wa habari?”
Ni dhahiri sms hii inatoka kwa mwananchi ambaye ameanza kukatishwa tamaa na matendo ya viongozi wetu ya kujinyakulia raslimali za nchi bila ya kujali kuwa ni zetu sote.
Kwa hakika, hisia za mkazi huyo wa Mbeya ni sawa na hisia za wanavijiji wanaolizunguka tindiga hilo la Boloti ambao wanaamini kuwa serikali ina mpango wa siri wa kuwaondoa katika ardhioevu hiyo ili auziwe ‘mwekezaji’.
Hawaamini kuwa kuwazuia kulima na kufuga ndani ya tindiga hilo wanalolitegemea kunalenga katika kuliepusha lisikauke kabisa. Wanaamini kuna agenda ya siri ya ama kulitoa eneo hilo kwa ‘mwekezaji’ au kwa kigogo mmojawapo nchini!
Imani hizo (yaweza kuwa ni potofu) zimeanza kuwafanya wakate tamaa na watawala wetu. Wanawaona watawala wetu kuwa ni watu ambao hawana dhamira ya kweli ya kutetea maslahi yao. Wanawaona kuwa ni matajiri wasiosononeshwa na maisha duni ya wanavijiji masikini.
Ukweli ni kwamba tukiuachia ukataji tamaa huu wa wananchi uendelee, matukio kama lile la Boloti ambako wanavijiji wako tayari kumwaga damu ‘kulinda kidogo walichonacho’, yanaweza kuongezeka na kuonekana ya kawaida nchini.
Ni vyema, hivyo basi, watawala wetu wakajitazama upya na kuyachukulia matukio kama hayo kuwa ni kengele ya uamsho na kujirekebisha. Kujisahihisha wanapokosea, ni moja ya sifa za uongozi bora. Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwahi hata kuandika kijitabu cha Tujisahihishe.
Nikirejea katika masahibu yetu ya Boloti, kila ninapoucheza tena kichwani mkanda wa tukio lile; ndivyo ninavyozidi kuamini tena na tena kwamba vita ijayo nchini itakuwa ya kugombea vyanzo vya maji.
Kabla ya masahibu hayo ya Boloti, nimewahi kusoma vitabu kadhaa vinavyohusiana na suala hilo la kuzidi kutoweka kwa raslimali maji katika uso wa dunia kama kile cha mwandishi Steven Solomon kinachoitwa Will The Next War be Fought Over Water? – Vita ijayo itakuwa ya kugombea maji?
Katika kitabu hicho, Steven Solomon anatoa mifano mbalimbali kuthibitisha kwamba maji yanazidi kuwa adimu kote duniani, na kwamba yameanza kuwa adimu kupita hata nishati ya mafuta!
Kama hilo analosema Steven Solomon ni kweli, basi, pengine Serikali ya Tanzania ingetumbukiza mabilioni ya pesa katika miradi ya kuvilinda vyanzo vya maji nchini ikiwa ni pamoja na kupanda miti na kulinda misitu yetu badala ya kuwekeza kwenye utafiti wa nishati ya mafuta!
Lakini pia niliwahi kuingalia documentary ya mtaalamu maarufu wa masuala ya maji wa Columbia, ambaye ni Mkurugenzi wa Columbia Water Centre (CWC), Dk. Upmanu Lall.
Katika documentary hiyo, bwana huyu anabashiri kwamba ifikapo mwaka 2025 dunia itakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, na kwamba itakuwa ni kilio na kusaga meno kwa mataifa 40 ya Afrika ikiwemo Tanzania. Anabashiri kuwa umwagaji damu kugombea vyanzo vya maji hautaepukika.
Je, damu yaweza kumwagika Tanzania kwa sababu ya kugombea vyanzo vya maji? Binafsi, kwa nilichoshuhudia mwenyewe kwa macho yangu huko Boloti wilayani Hai, nina kila sababu ya kuuamini ubashiri huo wa Dk. Lall.
Hebu jenga kichwani mwako picha ya mamia kwa mamia ya mifugo ya vijiji vitatu ikitumbukizwa ndani ya tindiga moja dogo tu kugombea nyasi pekee za kijani zinazopatikana maeneo hayo!
Jenga tena kichwani mwako picha ya makundi ya wanavijiji yakiwaendea na mapanga waandishi saba wa habari bila hata kuhofia kwamba wameandamana na polisi wawili wenye SMG zenye risasi za moto!
Ni dhahiri wanavijiji wale walikuwa tayari damu imwagike kuliko kukubali kuondoka kwenye ardhioevu hiyo. Lakini hata kama wataachiwa waendelee kubaki humo, miaka si mingi watageuziana mapanga wenyewe kwa wenyewe kiasi tindiga hilo linavyozidi kukauka na kuwa dogo zaidi!
Nina hakika ukizijenga picha hizo mbili kichwani mwako, utakubaliana na ile kauli kwamba vita ijayo itakuwa ya kugombea vyanzo vya maji, na kwamba raslimali maji sasa imeanza kuwa adimu kwenye uso wa dunia kuliko ilivyo nishati ya mafuta!
Kwa hakika, kwa tulichojifunza katika ziara hiyo ya hivi karibuni mkoani Kilimanjaro, nami naweza kubashiri kwamba damu ya kwanza (first blood) ya vita ya kugombea maji katika Tanzania itamwagika huko Kilimanjaro.
Kwa maneno mengine, naisikia harufu ya damu ya kwanza itakayomwagika K’manjaro inayohusu vita ya kugombea maji! Tayari mji wa Moshi umeshaanza kuonja mgao wake wa kwanza wa maji ya kunywa katika kipindi cha miaka 20!
Kwenye mazungumzo yetu kati ya JET na maofisa wa Ofisi ya Maji ya Bonde la Pangani (Pangani Basin Water Office – PWBO), ambayo Kilimanjaro ni sehemu ya bonde hilo, tulifahamishwa kwamba kiasi cha maji kinachopatikana kwa sasa kwenye bonde hilo hakilingani kabisa na mahitaji yanayokubalika kimataifa.
Tulifahamishwa kuwa, kwa mujibu wa World Water Index, mtu mmoja anapaswa kutumia mita za ujazo 1,700 za maji kwa mwaka, lakini katika Kilimanjaro na kwingineko kwenye bonde hilo, kiwango kilichopo ni mita za ujazo 1,200 tu kwa mtu kwa mwaka!
Tofauti kati ya mita za ujazo 1,700 (zinazotakiwa) na mita za ujazo 1,200 (zinazopatikana) ni mita za ujazo 500. Hebu jiulize; hiyo nakisi ya mita za ujazo 500 mkazi wa bonde hilo anaiziba vipi? Kama bado huelewi kinachoweza kutokea, jiulize swali jingine: Inatokea nini unapowapa watu wenye njaa 50 chakula kinachotosheleza watu sita tu?!
Hivi sasa mkoani Kilimanjaro; hususan maeneo ya mjini Moshi na vijiji vinavyozunguka mlima Kilimanjaro, watu wameanza kushindana kufyonza maji kwa kutumia pampu kubwa kutoka kwenye vyanzo vichache vya maji vilivyosalia.
Na wengine wameanza kufyonza maji ya ardhini (visima) kwa kutumia pampu kubwa. Hata hivyo, ukweli unabakia pale pale kwamba maji ya juu ya uso wa dunia yakishakauka, hata ya chini ya ardhi hayatachukua muda mrefu nayo pia yatakauka. Ni suala la muda tu, na kwa mkoa wa Kilimanjaro, muda unayoyoma!
Aliye na masikio na asikie. Jukumu letu, kama wanamazingira, ni kupiga kengele ya uamsho ili tuanze kupanda miti ‘kama vichaa’ huku tukiilinda misitu yetu na vyanzo vyetu vya maji hata kwa mitutu ya bunduki. Kama watawala wetu wanaisikia kengele hiyo na kuamka au la, ni suala la muda tu tutaujua ukweli!
Mwisho, ninakusihi msomaji wangu iangalie picha ambayo nimeiambatanisha na makala hii; kwani itakusaidia kuelewa vizuri ninachokizungumzia juu ya suala hili la uadimu wa raslimali maji.
Tafakari.
Maoni ya Wasomaji
Hongera sana Mbwambo katika
Hongera sana Mbwambo katika hili suala la maji kweli tusipochukua hatua za makusudi, kila mtu akapanda miti eneo alilopo na serikali ikatilia mkazo ni dhahiri tutaingia kwenye vita kali sana ya kugombea maji
"wahenga walisema ni bora kinga kuliko tiba"