Nakisi kubwa ya uongozi, utawala nao mbovu

Rai ya Jenerali

NINGEKUWA na uwezo wa kutamka jambo na likawa ningenena kwamba kila anayepita hapa na pale akijipendekeza kuwa mgombea wa urais apigwe marufuku, siyo tu kugombea urais bali nafasi yoyote ya uongozi, kwa sababu hafai.

Ningekuwa na uwezo wa kutaja sifa za kiongozi na hizo sifa zikawa na nguvu katika jamii ningetamka kwamba mojawapo ya sifa hizo si kufanya kampeni za chinichini kutafuta kuungwa mikono ili mtu aweze kupata nafasi ya uongozi. Ningetamka kwamba uongozi ni karama aliyotunukiwa mtu miongoni mwa jamii yake, na kwamba karama hiyo hujitokeza, ikaonekana, ikatambulika ndani ya jamii, wanajamii wakataka kuitumia na wakamuomba mwenye nayo awaruhusu kufanya hivyo.

Hii haina maana kwamba nakubaliana na ile dhana kwamba kiongozi “hana kimbelembele” ambayo nimeisikia ikitamkwa mara nyingi katika matamko ya watawala wetu. Hapana. Kiongozi ana sifa inayofanana sana na “kimbelembele”, kwa sababu siku zote ni mtu wa kuonyesha mambo ambayo wengine hawajayaona. Kiongozi ni yule anayeonyesha njia na haiwezekani kuonyesha njia kama siku zote uko nyuma.

Tunao viongozi wa kila aina, katika kila ngazi, katika kila medani, watu wanaotuonyesha njia. Msomaji atakumbuka kwamba miaka miwili au mitatu niliwahi kutoa mifano ya viongozi ambao watu wengine wangesita kuwaita viongozi kwa sababu tu hawana ofisi za kiutawala. Nilitoa mfano wa Kiongozi Mpeli Nsekela, ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya MultiChoice na akawa anahangaika kutafuta neno la Kiswahili linaloweza kufasiri neno la Kiingereza ‘decorder’ na mwishowe akapata neno ‘king’amuzi’ na akatuachia tulitumie hadi leo. Kiongozi.

Wako wengi wa aina hii, lakini hatutaki kuwatambua kwa sababu tunatafuta uongozi katika utawala. Hauko huko. Ni nadra sana kumpata kiongozi ndani ya utawala, na ukiweza kumpata, ah, ni raha iliyoje! Watawala walio wengi ni watawala tu na hawana chembe ya uongozi kwa sababu nafasi za utawala walizo nazo wamezipata si kwa sababu walionyesha njia mahali, bali kwa sababu walipitia mipangilio ya kimkakati na kimbinu.

Muda ulipita baada ya kuwa nimeandika kuhusu Mpeli kabla hajajitokeza Sugu, mbunge wa Mbeya mjini, ambaye ni msanii wa muziki wa kizazi kipya. Kama ambavyo wasanii wenzake walivyokuwa wameingia katika mabaraza ya uongozi (John Komba bungeni, Hadija Kopa na Mzee Raha (maarufu Mzee Jongo) katika halmashauri kuu ya chama-tawala) huyu naye ni kiongozi kwa wale wanaosikiliza maneno ya muziki wake na falsafa yanayoeleza, na leo ni wengi hawa.

Achia mbali wasanii, ambao binafsi nawatambua kwa mchango wao mkubwa, lakini hata wapiga ramli, katika jamii inayoishi kwa ramli, nao ni viongozi kwa wale wanaowaona kama watu wa msaada mkubwa. Tena hawa ni viongozi kweli kweli kwa sababu hakuna hata chembe ya utawala ndani ya wanachokifanya. Si kama vile waziri, mkuu wa mkoa au rais, ambao wote wanaweza wakawafanya watu wafanye wanavyotaka wao kwa sababu tu watu wanaogopa maguvu ya utawala. Wapiga ramli, wala! Tunajipeleka wenyewe. Viongozi wa watu wanaokwenda gizani, lakini bado viongozi hata hivyo.

Ninachosema ni kwamba hatuna budi kutafuta jinsi ya kuwapata viongozi wa kweli watakaotuongoza ili tujiletee maendeleo. Napenda kurejea kauli yangu ya siku zote: Hakuna kiongozi, hata angekuwa na uwezo au upendo wa aina gani, anaweza kuwaletea watu wake maendeleo. Wananchi watajiletea maendeleo yao wenyewe kwa kufanya kazi kwa akili na bidii, kiongozi wao akiwasaidia kuwaelekeza na kuwawakilisha kule wasikoweza kufika wote. Basi.

Hakuna kiongozi atakayewaletea watu maendeleo, tena kwa sababu tu wamemchagua kuwa kiongozi wao. Kama anajua maendeleo yako wapi na anawapenda watu wake, ni kwa nini asiwaletee maendeleo hayo eti mpaka wamchague? Si angewaletea tu, halafu akajisikia raha kwa kuangalia jinsi watu wake wanavyofurahia maendeleo? Ni kwa nini lazima wamchague kwanza?

Ni mantiki hii iliyopinda inayowafanya watu wazima wakubali kusikika kama majuha kwenye mahojiano wanapotamka kwamba posho haramu wanazozitaka ni kwa sababu ya kuwagawia wananchi wao! Hawatuambii ni lini kazi ya mbunge imekuwa kugawa fedha; hawasemi wameweka mpangilio gani wa kuhakikisha kama kuna mgawo, basi mgawo huo ufanyike kwa urari uliokubaliwa; hawasemi ni nani au asasi gani ina jukumu la kukagua matumizi ya fedha hizo.

Halafu, naaamini kwamba baadhi ya hawa watawala wetu, ambao sasa ni pamoja na wabunge, wanawaona wananchi kama vile hawana akili timamu. Vinginevyo isingewezekana kwamba mtu yule yule aliyepita akimwaga fedha ili achaguliwe hivi majuzi, leo asikike akilalama kwamba posho anayodai ni kwa ajili ya kuwapa watu wake ilhali aliweza kumwaga fedha kwa fujo kabla hajawa mbunge.

Siwasemi wabunge kwa sababu ni wabunge, na wengine wamo. Katika hiki kinyang’anyiro cha kutafuta urais wa muhula ujao tutashuhudia matumizi makubwa ya fedha, watu wakikusanya nguvu za kifedha kununua urais na ‘uongozi’ wa nchi. Hawa, nasema tena, si viongozi, na wakiruhusiwa wakapita hatuna budi kujua kwamba tutakaa bila uongozi kwa muda mwingine mrefu.

Zahama kubwa ya nchi yetu imetokana na kwamba tumeshindwa kuwa na kiongozi wa umma tangu Julius Nyerere afariki. Kwa wakati wote alipokuwa hai, awe madarakani, asiwe madarakani, Nyerere alikuwa kiongozi. Baada yake tumeshindwa kabisa, nasema kabisa, kujenga uongozi, na badala yake tumekuwa tukiishi na utawala, na hata utawala wenyewe umekuwa mbovu kwa sababu hauna uongozi wa kuusimamia.

Tunaweza labda kumlaumu Nyerere mwenyewe kwa kushindwa kuweka misingi ya kupata uongozi wakati akiwa madarakani, sijui, au labda tutajilaumu wenyewe kwa sababu angalau tulikuwa na kiongozi lakini tukashindwa kujifunza kutoka kwake, lakini ukweli ni kwamba tumeshindwa kujenga uongozi, na kwa kushindwa huko tumeiweka nchi yetu katika hatari kubwa. Nchi imekuwa ni kama windo lililo nyikani likifukuzwa na mbweha, mafisi na kila aina ya wanyama wakali. Nchi imekuwa kitoweo cha mafisi, nasi tunaangalia.

Tunayo nchi jirani ambayo imekuwa ikifanya mabadiliko ya viongozi kileleni bila malumbano makubwa, pamoja na kwamba nchi hiyo imepitia misukosuko mikubwa na imemwaga damu nyingi sana. Ikilinganishwa na nchi yetu, ni muujiza kwamba nchi hiyo bado iko kama nchi, na chama-tawala cha nchi hiyo bado kimo madarakani, na viongozi wake bado wako pamoja (wetu hapa wanaongopeana “tuko pamoja” wakati visu viko mifukoni). Ndani ya miaka miwili ijayo nchi hiyo itafanya uchaguzi mkuu mwingine, na rais aliyeko madarakani sasa atakuwa anamaliza muda wake.

Watanzania wanaoishi katika mji mkuu wa nchi hiyo wanaarifu kwamba hakuna kabisa malumbano yanayosikika kuhusu wanachama wanaopigana vikumbo, kutishiana kurogana au kulishana sumu kwa kutafuta urais mwaka 2014. Chama chao kinaendelea na mipango ya maendeleo kiliyowaahidi wananchi, na siku itakapowadia, chama kitampata mgombea wa kupeperusha bendera yake kupambana na wagombea wa vyama vingine. Hivi sasa malumbano ni kuhusu sera na utekelezaji wake.

Rais wa sasa wa nchi hiyo aliingia madarakani baada ya rais aliyekuwapo kuamua kuondoka madarakani kwa hiari, kabla ya muda wake kuisha. Chama kikamkubalia, kisha kikaanza kazi ya kumtafuta mrithi wake miongoni mwa makada wa chama, na hatimaye kikampata mjumbe wa kamati kuu aliyekuwa amejitoa katika utawala na akaingia katika biashara, bado kada na mjumbe wa kamati kuu, kikamuomba agombee urais kukiwakilisha chama chake, akajadili masuala mawili au matatu, mwisho akakubali, chama kikamfanyia kampeni akachaguliwa. Pamoja na utajiri aliokuwa nao, hakutoa fedha zake kununua urais.

Tunayo nchi nyingine jirani. Huko watu walianza kujinadi miaka ishirini iliyopita wakitafuta urais. Mimi, mimi, kabila langu, kabila langu! 2007 kujinadi huko kukafikia kilele. Waliokuwa wakijinadi na makabila yao na wapambe wao wakaingia katika kinyang’anyiro wakiwa na sime na mapanga wameyaficha mikobani. Wakachafua uchaguzi; wakavuruga matokeo; wakapigana, wakachinjana, wakaitia kibiriti nchi yao, wakachungulia kaburi la taifa zima…. na ni kwa bahati tu kwamba sauti za busara ziliingilia kati, pamoja na zile zilizotoka nchini mwetu, kwamba nchi hiyo ilirejea kidogo katika hali ya utulivu… kwa muda.

Sasa wanakinyang’anyiro wale wale wa nchi hiyo hiyo wanataka kurejea mchezo ule ule, wakijua kuwa matokea yatakuwa yale yale… Nasi tunataka kuwafuata katika wazimu wao.

Wiki ijayo nitakuletea simulizi ya meli Titanic na historia yake ya kushangaza.

Add new comment

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.