Namna Magufuli alivyojizamisha

UMPENDE usimpende, Rais Dk. John Magufuli ameendelea kushangaza, kufurahisha na kuchanganya wengi ndani na nje ya nchi.

Kati ya mkanganyiko huo, wiki iliyopita akiwa katika ziara ya chini ya wiki katika Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, Rais Magufuli alitoa kauli ambazo sasa zitakuwa zikiwapeleka mbio watu na watendaji mbalimbali: wamiliki wa kampuni za uwekezaji; wanasiasa; mawaziri hadi watu wa chini kabisa.

Kauli za upendeleo kwa wawekezaji

Katika hatua ya upendeleo wa wazi wa Rais Magufuli kwa baadhi ya wawekezaji nchini, wiki iliyopita akiwa mkoani Mtwara alia aliagiza mfanyabiashara maarufu Alhaj Aliko Dangote anayemiliki kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo mkoani humo apewe sehemu ya mgodi wa makaa ya mawe unaomilikiwa na TanCoal ili aweze kupata rasilimali hiyo kwa ajili ya nishati ya kiwanda chake.

Rais Magufuli aliagiza kuwa Dangote apewe mgodi huo wa makaa ya mawe na akatoa siku saba kwa Wizara ya Nishati na Madini na wahusika wengine serikalini   kuhakikisha kwamba agizo hilo linatimia ndani ya muda huo.

Raia Mwema limeelezwa kwamba agizo hilo sasa linawapeleka puta watu serikalini kuhakikisha taratibu zote, zikiwamo za kisheria, zinatimia ndani ya siku saba, muda ambao kwa ugoigoi uliotamalaki serikalini huenda likakwama.

Pamoja na makaa hayo ya mawe, Rais Magufuli aligiza pia kwamba kufikia wiki hii, Dangote apewe gesi ya kuendeshea mitambo yake kiwandani bila kupitia kwa mtu au kampuni ya kati.

Lakini, kumbukumbu zinaonyesha kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuagiza mfanyabiashara kupewa upendeleo wa aina hiyo.

“ Kama mtakumbuka  Oktoba mwaka jana Rais Magufuli alizuru viwanda vya Said Salim Bakhresa na akamwagiza Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Charles Mwijage kumrudishia mfanyabiashara huyo sukari yake iliyozuiwa bandarini kutokana na kile alichodai kuwa ‘biashara” yake ina tija kwa taifa.

“Magufuli huyo huyo alitoa agizo kwa uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha ndani ya miezi miwili wamefikisha huduma ya umeme katika kiwanda cha kusindika matunda na kuzalisha juisi cha Bakhresa Food Products Ltd kilichopo Mwandege wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, “ anasema ofisa mmoja serikalini akieleza kwamba akiamini kwamba suala husika lina manufaa mapana kwa taifa, Rais Magufuli hasiti kukata shauri.

Katika sakata la sukari, bidhaa hiyo ya Bakhresa ilizuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ya wafanyabiashara wengine miezi michache nyuma wakati Rais Magufuli alipotangaza kusitisha vibali vya kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kwa madai ya kulinda viwanda vya ndani.

Agizo hilo la serikali dhidi ya vibali vya kuagiza bidhaa hiyo lilisababisha uhaba mkubwa wa sukari iliyopanda na kufikia wastani wa Sh 4,500 hadi 6,000 kwa kilo moja katika baadhi ya mikoa nchini.

Kwa wakati huo, mambo matatu yalifanyika yanayoweza kutafsiriwa kuwa ni upendeleo kwa Bakhresa, kwanza, kurejeshewa sukari yake iliyozuiwa sawa na wafanyabiashara wengine, pili, agizo la moja kwa moja la kupatiwa umeme ndani ya miezi miwili, tatu, kupewa eneo la ukubwa wa ekari 10,000 bure ili alime miwa na kufungua kiwanda cha sukari – uamuzi ambao unampa unafuu wa kiuwekezaji Bakhresa ikilinganishwa na wawekezaji wengine watakoamua au waliokwishakuamua kuwekeza kwenye sekta hiyo mahsusi.

Ingawa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bakhresa, Aboubakari Salim, siku hiyo aliweka bayana kwamba kumekuwa na urasimu mwingi katika upatikanaji wa maeneo mapya ya kuanzisha viwanda, lakini bado wapo wawekezaji wanaoamini mwenendo wa Rais Magufuli kwa wawekezaji hautoi fursa sawa kwa wote.

Mtaalamu wa uchumi nchini, Profesa Honest Ngowi, anashauri kwamba serikali ni lazima ijijengee taswira ya kuwaunga mkono kwa usawa wawekezaji wote nchini, na si kuelemea upande mmoja.

“Kimsingi ni vizuri wawekezaji wote wakapata mazingira sawa na ya kuvutia kama Dangote. Wote wakipata uwanja sawa wa kufanya biashara ni bora zaidi,” anasema Profesa Ngowi ambaye katika mazungumzo yake na gazeti hili alikuwa nchini Uswisi.

Pamoja na “upendeleo’ huo wa wazi, Rais Dk Magufuli pia alitoa kauli ambazo zimetafsiriwa kuwa ni tata na huenda nyingine zikazua mijadala ya muda mrefu na ama zisitekelezwe kama alivyoagiza.

Deni la Umeme SMZ

Akiwa bado katika ziara hiyo ya Kusini mwa Tanzania, Rais Magufuli aliliagiza Tanesco kuhakikisha kwamba linawakatia umeme wadaiwa sugu hata kama hao ni serikali, na hata kama ni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Kwa muda mrefu kumekuwa na ukakasi kwa Tanesco kuidai SMZ, na kwa miaka mingi, matamko mengi yamekuwa kama maji machemu yasiyounguza nyumba, kwa vile yalibaki kuwa matamko.

Kwa kauli ya wiki iliyopita ya Rais Magufuli, taarifa kutoka Tanesco zimesema kwamba iko mbioni kuandaa mchakato wa jinsi ya kuidai SMZ limbikizo la deni linalokadiriwa kuwa zaidi ya bilioni 100.

Taarifa zaidi zinasema kwa upande wake SMZ inasema mchakato wa kulipa deni hilo ulikuwa mbioni na kwamba mara kadhaa mazungumzo yamefanyika kati ya SMZ na Bara na Tanesco kufikia muafaka wa ulipaji.

Bila shaka, kama hatimaye Tanesco itaikatia umeme SMZ hatua hiyo itazua changamoto za kisiasa baina ya Bara na Visiwani.

Hata hivyo, wakati Tanesco wakisisitiza utekelezaji wa agizo la Rais, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Mohammed Aboud, amenukuriwa na vyombo vya habari akisema wanaendelea na mazungumzo kati ya mawaziri husika wa pande mbili za Muungano juu ya namna ya kulipa deni hilo.

“Lengo letu ni kulipa deni lote kwa sababu ukidaiwa lazima ulipe. Sisi tupo tayari kulipa ndiyo maana tumeanza kufanya mazungumzo na wenzetu wa Tanzania Bara jinsi gani tunaweza kukubaliana juu ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kulipia hatua kwa hatua ili kumaliza deni,” amenukuriwa akisema Aboud.

Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira wa SMZ Salama Aboud Talib amekaririwa mwanzoni mwa wiki akisema kwamba hadi Januari 2017, ZECO ilikuwa inadaiwa Sh121 bilioni, kwa mujibu wa barua iliyowakilishwa kwake na Tanesco.

Mchanga wa madini

Lakini amri ya hivi karibuni ya kutaka mchanga wa madini kutosafirishwa nje ya nchi nayo imeibua mjadala wa aina yake, na hasa suala la maandalizi ama nchi kujenga uwezo wa kuchenjua mchanga huo wa madini hapa nchini.

Akiwa katika ziara hiyo ya Mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, Rais Magufuli aliamuru mchanga wa madini, maarufu kama makinikia (copper concentrate) kutosafirishwa nje ya nchi.

Kwa Tanzania, kampuni moja tu ya Acacia ambayo inamiliki migodi minne ya dhahabu ndiyo inasafirisha makinikia nje ya nchi wakati Anglo-Gold wanaomiliki mgodi wa dhahabu Geita wakiwa hawafanyi hivyo.

Hatua hiyo sasa, kama anavyoripoti mwandishi wetu FELIX MWAKYEMBE imeigawa serikali katika makundi mawili, kundi la wataalamu wa masuala hayo na kundi la wanasiasa.

Kwa mujibu wa amri ya Rais aliyoitoa akiwa Mkuranga mkoani Pwani, uamuzi huo unelenga zaidi kulinda rasilimli za Taifa.

Tayari Kampuni ya Acacia, ambayo ni muathirika mkuu na zuio hilo, imetangaza kusimamisha usafirishaji wa makinikia ya shaba/dhahabu inayozalisha katika migodi yake miwili ya Buzwagi na Bulyanhulu, ikiwa ni kutii agizo la Rais.

Pamoja na migodi hiyo miwili, Kampuni ya Acacia pia inamiliki mgodi wa North Mara ambao uzalishaji wake wa dhahabu ni tofauti na hiyo migodi miwili.

Wiki iliyopita, Machi 03, 2017, kampuni hiyo ilitoa taarifa rasmi kwa umma inayoelezea kusimamisha usafirishaji wa makinikia ya shaba/dhahabu, muda mfupi baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini kutoa taarifa ya serikali kwa umma kuhusu zuio la usafirishaji makinikia na mawe yenye madini kwenda nje.

Hatua hiyo ilisababisha bei ya hisa za kampuni ya Acacia kwenye masoko ya London na Dar es Salaam kupungua kwa takriban asilimia 18.

Mpaka sasa, bei ya hisa za kampuni hiyo bado hazijaimarika na hiyo imeathiri hata mtaji wa soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) kwani Acacia ndiyo kampuni yenye mtaji mkubwa.

Gazeti la kimataifa ya The Financial Times la Uingereza liliripoti wiki jana kwamba hisa za Acacia zilishuka kwa asilimia 18 kwenye soko la hisa la London, kutokana na kupungua kwa imani ya wawekezaji kwenye kampuni hiyo baada ya kusikia agizo la Rais Magufuli.

Kwa miaka mingi sasa imekuwapo hofu miongoni mwa wananchi kwamba Tanzania inaibiwa kupitia hatua ya kampuni za madini nchini kusafirisha nje ya nchi makinikia kwa ajili ya uyeyushaji kutokana na kukosekana kwa viwanda hivyo nchini.

Lakini wataalamu kwa upande wao wanabainisha kuwa ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha makinikia hayo hautakuwa na faida za kiuchumi kwa Taifa.

Tafiti za kitaalamu zinaonyesha kwamba  makinikia ya shaba (copper concentrate) yanayozalishwa nchini hayakidhi ujenzi wa kiwanda cha kuyeyushia (smelter) kutokana na gharama ya ujenzi kuwa juu ikilinganishwa na kiwango kinachozalishwa kisichokidhi hata mahitaji ya chini ya smelter.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwisho kufanywa kuhusu suala hilo, ipo migodi miwili tu ya dhahabu yenye kulisha makinikia hiyo ya shaba na dhahabu, nayo ni Buzwagi na Bulyanhulu.

Taarifa ya utafiti huo uliofanywa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) inabainisha kuwa kiwango cha makinikia hiyo ya shaba na dhahabu kinachozalishwa na migodi hiyo miwili haifiki hata nusu ya kiwango cha chini kinachohitajika kuyeyushwa na kiwanda hicho.

Miongoni mwa mambo ya msingi yaliyomo kwenye taarifa hiyo ya utafiti ya Februari 2011, ni pamoja na kiwango kinachozalishwa na migodi hiyo miwili, Buzwagi na Bulyanhulu ambacho hakizidi tani 60,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ya chini ya kiwanda cha kuyeyusha makinikia ni tani 150,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya utafiti, mgodi wa Buzwagi huzalisha na kusafirisha makinikia ya shaba kati ya tani 25,000 na 50,000 kwa mwaka wakati ule wa Bulyanhulu huzalisha na kusafirisha tani 10,000 kwa mwaka.

Utafiti huo unaofahamika kama “A Study on Viability to Construct a Copper Concentrate Smelter in Tanzania,” unafichua kuwa takribani wazalishaji wote wa makinikia duniani, sawa na yanayozalishwa nchini, hawana viwanda vyao wenyewe vya kuyeyushia.

Wazalishaji hao nao husafirisha nje, hususan, katika nchi za China, India na Japan kwa ajili ya kutenganisha dhahabu na shaba.

Makinikia ya shaba yanayozalishwa na migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu nchini, husafirishwa kwa ajili ya kuyeyushwa, katika viwanda vya Marc Rich Investment nchini China, Sumitomo Metal Mining Co. Ltd na Pacific Co. Ltd vya nchini Japan au Aurubis AG  nchini Ujerumani.

Raia Mwema inazo taarifa zisizo shaka kwamba TMAA haijafanya utafiti mwingine zaidi ya huo wa mwaka 2011.

“Kimsingi hatujafanya study nyingine, na hatuwezi zungumzia kauli ya Rais,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka TMAA kwa sharti la kutotajwa jina.  

Utafiti huo unabainisha pia kwamba gharama ya ujenzi, kwa kiwanda kilichokamilika, ni kati  ya dola za Marekani milioni 500 hadi 800, zaidi ya shilingi trilioni moja.   

Kiuchumi, inabainishwa kuwa kiwanda cha kuyeyusha kinahitaji mzigo wa makinikia usiopungua tani 150,000 kwa mwaka, lakini uzalishaji wa migodi miwili hapa nchini ya Buzwagi na Bulyanhulu hauzidi tani 60,000 kwa mwaka, kiwango ambacho ni asilimia 40 tu ya uwezo wa kiwanda.

Ili kukidhi mahitaji ya kiwanda, Tanzania italazimika kutegemea zaidi asilimia 60 ya makinikia kutoka kwa wazalishaji wa nje, ama sivyo Tanzania ifungue migodi mingine itakayotumia teknolojia hiyo.

Hata hivyo, hoja ya kufunguliwa kwa migodi mipya itakayotumia teknolojia hiyo inakabiliwa na changamoto moja kuu, kwamba hadi wakati utafiti huo unafanyika, hakukuwa na ugunduzi mpya wa madini ya “copper sulphide” ambayo ingesaidia kuongezea katika mahitaji ya makinikia ya shaba.

Wataalamu hao wa masuala ya madini nchini wanabainisha, katika taarifa yao, kwamba suala la gharama na upatikanaji wa umeme wa uhakika ndiyo mambo ya msingi katika kuamua kujenga kiwanda cha kuyeyushia makinikia.

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe katika maoni yake kuhusu suala hilo la makanikia anasema uamuzi huo wa Rais Magufuli ni sahihi, lakini wakati si sahihi.

Anasema Kabwe Zitto: “…kuweka zuio la kusafirisha mchanga wa dhahabu ni uamuzi sahihi uliofanywa bila kuzingatia kwanza uwezo wa ndani wa kuchenjua( refinery).”

 “Kumekuwa na maneno kuwa hatuna uwezo wa kuchenjua hapa nchini. Haya ni mawazo ya kilofa na kasumba ya hatuwezi. Unahitaji tani 150,000 za mchanga kwa mwaka kuweza kuwa na kinu cha kuchenjua chenye manufaa (economies of scale) lakini sisi tunazalisha tani 40,000 hivi. Pia tunahitaji umeme zaidi ya 1500mw kwa mwaka ambazo kwa sasa hatuna. Tunachoweza kufanya ni kwanza kutazama uwezekano wa eneo letu kuzalisha hizo copper concentrates ili kuingia mikataba na nchi jirani ziweze kuleta mchanga wao hapa na sisi tuwe kituo cha uchenjuaji kwenye ukanda huu.

“Pili tunahitaji uwekezaji mkubwa kwenye uzalishaji wa umeme ili kufikia mahitaji hayo.  Sasa mjadala hapa ni kwa nini tunazuia kabla ya kujenga huo uwezo? Inawezekana zuio alilotoa Rais ndiyo litaweza kuanzisha mjadala wa majawabu hayo kwani ni mjadala wa miaka mingi sana. Kuna nyakati vijana wa Kahama walikuwa wanayapiga mawe magari yaliyobeba mchanga kwa hasira. Sisi wanasiasa tulikuwa tunaibua jambo hili kila mwaka kupinga mchanga kusafirishwa.

Kwa hiyo amri ya Rais iwe ni kuleta mjadala kisha tukubaliane mkakati wa kuhakikisha jawabu la kudumu linapatikana.”

Alisema wataalamu wanaweza kubuni teknolojia yenye uwezo wa kufanya uchenjuaji kwa kiwango cha mchanga tunachozalisha nchini na kusisitiza kuwa, haiwezekani dunia nzima ikawa na teknolojia moja tu ya tani 150,000 la hasha.

“Ushauri wangu ni kwamba serikali ikae na sekta ya madini ili kupata jawabu la kudumu na kuweka azimio la muda maalumu kuendelea kusafirisha mchanga na baada ya muda huo mchanga huo uchenjuliwe nchini kwetu na kuzalisha ajira na kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha. Hii sio zero-sum game (kama si kusafirisha basi hakuna lingine). Hapana. Mjadala unaweza kuleta jawabu lenye faida kwa nchi,” alisema.

Licha ya kutafutwa na gazeti hili, uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini umekuwa kimya kuhusu namna gani agizo hilo la Rais Magufuli ‘litatekelezeka, kwa kuzingatia matokeo ya utafiti uliofanywa na TMAA Februari mwaka 2011.

Mradi wa Maji Lindi

Na katika hatua nyingine, akiwa ziarani mkoani Lindi wiki iliyopita, Rais aliagiza pia kupokonywa hati ya kusafiria ya mhandisi mshauri wa Mradi wa Maji Lindi hadi hapo mradi huo utakapokamilika.

Uamuzi wa kumnyang’anya hati ya kusaifiria raia huyo wa India ulitokana na kusuasua kwa uendelezaji wa mradi ambao utatoa huduma ya maji kwa mamia ya maelfu ya Watanzania hasa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

One thought on “Namna Magufuli alivyojizamisha”

  1. Dennis Bamwenzaki says:

    Mimi naunga mkono anachofanya Rais kuhusu maslahi ya Taifa letu la Tanzania. Mambo yote uanza na mawazo hufuata vitendo. Huo mchanga unaweza kuhifadhiwa wakati mtambo wenye uwezo aidha wa mchanga uliopo au kuongeza kutoka ndani au nje ukifanyika. Tumeumizwa sana na ubeberu. Tunahitaji kuamua hata kama ni kwa kuumia. Wataalamu wanatakiwa kuamka na kudhihirisha utaalamu wao sio kutwambia haiwezekani, haitekelezeki au hailipi. Waamuke wafanye kazi waangalie masuala kizalendo waachane na ugonjwa wa kutawaliwa kifikra na kisaikolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *